Tafuta

Baba Mtakatifu Leo XIV amekubali mwaliko kutoka kwa Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa wa kutembelea Makao makuu ya Shirika hilo mjini Roma Baba Mtakatifu Leo XIV amekubali mwaliko kutoka kwa Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa wa kutembelea Makao makuu ya Shirika hilo mjini Roma  (@Vatican Media)

Papa Leo XIV Kuwahutubia Wajumbe wa Mpango wa Chakula wa Umoja wa Mataifa

Papa Leo XIV amekubali mwaliko kutoka kwa Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa wa kutembelea Makao makuu ya Shirika hilo ili kukuzungumza na wajumbe wa ngazi za juu wa Shirika hili, wafanyakazi pamoja na familia zao, Jumatatu tarehe 22 Juni 2026. Baa la njaa sehemu mbalimbali za dunia linaendelea kusigina utu, heshima na haki msingi za binadamu, mwaliko wa kushikamana ili kuwa na uhakika wa usalama wa chakula duniani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa “World Food Programme WFP” lilianzishwa kunako mwaka 1961 na kuanza shughuli zake rasmi mwaka 1963. Hili ni Shirika linalotoa msaada wa chakula na kwamba, linajishughulisha na mapambano ya kutokomeza baa la njaa duniani sanjari na kukuza uhakika wa usalama wa chakula dunia. Hili ni Shirika linalookoa maisha ya watu wakati wa majanga asilia, vita, migogoro, mipasuko ya kijamii pamoja na athari za mabadiliko ya tabianchi. Baba Mtakatifu Leo XIV amekubali mwaliko kutoka kwa Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa “World Food Programme – WFP” wa kutembelea Makao makuu ya Shirika yaliyoko mjini Roma ili kukuzungumza na wajumbe wa ngazi za juu wa Shirika hili, wafanyakazi pamoja na familia zao, Jumatatu tarehe 22 Juni 2026. Itakumbukwa kwamba, Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa, FAO, tarehe 16 Oktoba 2025 liliadhimisha Kumbukizi ya Miaka 80 tangu kuanzishwa kwake sanjari na Maadhimisho ya Kimataifa ya Siku ya Usalama wa Chakula Duniani kwa Mwaka 2025 yaliyonogeshwa na kauli mbiu: “Tuungane pamoja kupata Chakula Bora Kwa Maisha Bora ya Baadaye.”

Kuna mamilioni ya watu bado wanahitaji msaada wa chakula
Kuna mamilioni ya watu bado wanahitaji msaada wa chakula

Sherehe hii ilihudhuriwa na Baba Mtakatifu Leo XIV ambaye katika hotuba yake elekezi aligusia kuhusu: Mapambano dhidi ya baa la njaa, ili kujenga amani, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. FAO haina budi kutoa kipaumbele cha kwanza kwa uhakika na usalama wa chakula duniani kwa kutumia maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia ya kilimo; ili kuokoa maisha ya mamilioni ya watu wanaoteseka kwa baa la njaa, ambalo wakati mwingine linatumika kama silaha ya vita. Vita, kinzani na mipasuko ya kijamii ni chanzo kikuu cha baa la njaa na umaskini duniani. Kuna umuhimu wa kujenga na kudumisha umoja, mshikamano na udugu wa kibinadamu, ili kutekeleza sera na mikakati ya kuwa na uhakika na usalama wa chakula duniani, kwa kuwawezesha wanawake katika sekta ya kilimo pamoja na kuhakikisha kwamba, watu wengi zaidi wanapata maji safi na salama sanjari na huduma bora za afya. Kuna watu wanapoteza maisha kutokana na vita, changamoto na mwaliko wa kujenga jamii inayosimikwa katika misingi ya haki. Mwishoni aliitaka FAO kuwa ni chombo cha tumaini ambalo halitahayarishi: Spes non confundit" Rum 5:5. Kwa hakika kila binadamu ana njaa na kiu ya: furaha, imani, matumaini na mapendo.

Vita ni kati ya vyanzo vikuu vya ukosefu wa usalama wa chakula
Vita ni kati ya vyanzo vikuu vya ukosefu wa usalama wa chakula   (AFP or licensors)

Mapambano dhidi ya baa la njaa, ili kujenga amani, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Katika kipindi cha miaka 80 ya uhai wake, FAO bado inapambana na baa la njaa na ukosefu wa uhakika wa usalama wa chakula sehemu mbalimbali za dunia na kwamba, hii ni changamoto ya wadau mbalimbali kushiriki kikamilifu ili kuwepo na uhakika wa usalama wa chakula duniani na kwamba, mtu anayeteseka kwa baa la njaa na utapiamlo wa kutisha ni ndugu na kwamba, anapaswa kusaidiwa kwa haraka sana. Ili kufikia lengo hili kuna haja ya kujenga ari na moyo wa mshikamano na udugu wa kibinadamu, ili kuhakikisha kwamba, watu wanapata chakula bora na cha kutosha, ili kukuza na kudumisha, utu, heshima na haki msingi za binadamu. Baa la njaa linazidi kuongezeka kila kukicha kutokana na vita, kinzani na misigano ya kijamii; athari za mabadiliko ya tabianchi bila kusahau majanga asilia. Na matokeo yake ni wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta hifadhi na usalama wa maisha yao. Baba Mtakatifu Leo XIV anasikitika kusema kwamba, licha ya maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia, bado kuna watu milioni sabini na tatu wanasiginwa na baa la njaa sehemu mbalimbali za dunia na watu milioni elfu mbili na mia tatu wanateseka kutokana na utapiamlo pamoja na kukosa uhakika wa usalama na lishe bora. Kuna wanawake wanaoshindwa kuwapatia watoto wao lishe bora na chakula cha kutosha matokeo yake ni madhara makubwa kwa afya na makuzi kwa watoto hawa, kielelezo cha uchumi usiojali; maendeleo tenge na ugawaji wa rasilimali za dunia usio sawa na wala si endelevu. Maendeleo ya sayansi na tekenolojia yasaidie kuleta matumaini ya watu kuishi, ili kukomesha vifo, kielelezo cha ukosefu wa ushirikiano, kanuni maadili na utu wema.

Papa Leo XIV Mpango wa Chakula

 

19 Juni 2026, 15:30