Papa Leo XIV:Katikati ya vurugu,huruma ya Mungu inaomba iingie kwa upya mioyoni mwetu!
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Baba Mtakatifu Leo XIV alituma ujumbe wake kwa njia ya video kwa lugha ya Kiingereza huko Vilnius,nchini Lithuania, ambapo Kongamano la Sita la Kitume Ulimwenguni kuhusu Huruma, lililoandaliwa na Baraza la Kipapa la Uinjilishaji kwa ushirikiano na jimbo kuu la eneo hilo, linafanyika kuanzia tarehe 7 hadi 12 Juni 2026. Baba Mtakatifu katika ujumbe huo anaanza kusema kuwa "Wapendwa kaka na dada katika Kristo, ninafurahi kuwasalimu nyote mnaoshiriki katika toleo la sita la Kongamano la Kitume Duniani kuhusu Huruma ambalo lilitamaniwa sana na Mtangulizi wangu Mtukufu, Mtakatifu Papa Yohane Paulo II."
Tumaini pekee liko katika huruma kuu ya Mungu
Katika tukio hili, Papa aliongeza "ningependa kutoa salamu maalum kwa Askofu Mkuu Gintaras Grušas wa Vilnius, ambaye anawakaribisha katika Jimbo lake mahujaji wengi wa huruma kutoka ulimwenguni kote, na pia kwa Mheshimiwa Bwana Gitanas Nausėda, Rais wa Jamhuri ya Lithuania, na hasa kwa Patriaki Bartholomew wa Constantinople, ambaye amekubali kwa neema kuwepo. Baba Mtakatifu alikazia kusema kuwa “Mtakatifu Agostino aliandika katika Maungamo kwamba tumaini lake pekee liko katika huruma kuu ya Mungu (10, 40). Hakika, ni chanzo cha furaha kubwa na tumaini la kweli tunapoona jinsi Mungu alivyo na rehema kwa kila mmoja wetu na jinsi ilivyo vizuri kwetu kufufua imani yetu katika huruma yake.
Ulimwengu unaonesha hitaji la amani mioyoni mwa mtu binafsi
“Ulimwengu wa leo, pamoja na hofu na wasiwasi wake mwingi, mivutano na vita, Papa anabainisha “ unaonesha hitaji kubwa la amani mioyoni mwa mtu binafsi na watu. Katikati ya msongamano wa vurugu unaoharibu mahusiano na kuharibu maisha, huruma ya Mungu inaomba iruhusiwe kuingia mioyoni mwetu kwa nguvu yake ya ajabu ya upya.” Papa alisisitiza tena kwamba “Ni huruma hii inayoweza kubadilisha maisha yetu, ikifungua njia ya upendo na msamaha kama sifa tofauti za uso wa Mungu zinazooneshwa kupitia sisi.”
Msichoke kuonesha upendo
“Wapendwa, Mungu hachoki kuonesha huruma yake. Upendo wake, kama mtunga Zaburi asemavyo (Zaburi 136), unadumu milele, na jinsi ulimwengu wetu unavyolilia huruma katika kila ngazi! Lakini amani tunayoitamani sana haiwezi kupatikana bila huruma.” Kwa hivyo, “tujiunge na imani yetu katika huruma isiyo na kikomo ya Mungu kwa kujitolea kwetu binafsi kujenga jamii inayokaribisha na yenye huruma zaidi, kuanzia na familia zetu.”
Uzoefu wa siku hizi
Kwa kuhitimisha Papa anaonesha tumaini lake na kuwapa baraka: “ Matumaini yangu ni kwamba mtaishi siku hizi huko Vilnius kwa bidii, ili muweze kurudisha katika jumuiya zenu utajiri wa yote mliyoyapata katika mkutano huu wa kimataifa. Kutoka ndani ya moyo wangu, ninawapatia kila mmoja wenu Baraka ya Kitume ya Mungu mwenye huruma nyingi.”
Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku: Just click here.
