Papa Leo XIV: Hotuba Kwa Vyama Vya Wasomi na Wanafunzi Wakatoliki Ujerumani
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Vyama vya Wasomi na Wanafunzi Wakatoliki Nchini Ujerumani “Studentenverbindungen” vina historia na desturi ndefu iliyoanza kati kati ya karne ya 19. Kimsingi hili ni Shirikisho kubwa la vyama vya wanafunzi Wakatoliki kutoka Ujerumani, vinavyounganishwa na kushikamanishwa na imani katoliki, mafanikio ya kitaaluma na mshikamano wa maisha na ushuhuda wa imani ya kikatoliki inayosimikwa katika: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu. Vyama hivi vinaongozwa na kanuni zifuatazo: “religio, scientia, amicitia e patria” yaani: “dini, sayansi, urafiki na uzalendo.” Na kauli mbiu yao ni: “In certibus unitas, in dubiis libertas, in omnibus caritas.” Yaani: “Umoja katika mambo msingi, uhuru katika mambo ya mashaka, na upendo katika mambo yote.” Wanachama wa Vyama vya Wasomi na Wanafunzi Wakatoliki Nchini Ujerumani, Ijumaa tarehe 5 Juni 2026, huku wakiwa wamehamasishwa na kujitambulisha kwa imani yao kwa Kanisa Katoliki na ushirika unaowafunga kama Mitume wa Kristo Yesu, pamoja na shughuli zao za kitamaduni, kwa mara ya kwanza, wanafanya mkutano wao mkuu mjini Roma, yaani nje ya Ujerumani. Baba Mtakatifu katika hotuba yake amegusia kuhusu utambulisho wao kama Chama cha Kikatoliki; Ushirika wao katika masuala ya dini, sayansi, urafiki na uzalendo; utafutaji wa ukweli ili kumfahamu Mungu aliyejifunua kwa njia ya Kristo Yesu, Neno wa Mungu aliyefanyika mwili! Baba Mtakatifu anasema, hiki ni Chama kinachoongozwa na kanuni zifuatazo: “religio, scientia, amicitia e patria” yaani: “dini, sayansi, urafiki na uzalendo.”
Imani ya Kanisa Katoliki anasema Baba Mtakatifu Leo XIV ni maisha wanayoshirikisha wengine katika vyuo vikuu na katika medani mbalimbali za maisha yao. Kumbe, huu ni utambulisho wao Barani Ulaya na kwamba, Ujerumani ni kitovu cha ushuhuda huu wa imani. Hawa ni wasomi wanatoa kipaumbele cha kwanza kwa binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu na kwamba, katika mchakato wa maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia, hawana budi kuhakikisha kwamba, wanajikita katika kuragibisha utu, heshima, ustawi na maendeleo ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Mtu katika nafsi yake ni zawadi kwa jirani zake, changamoto na mwaliko kwa watu wa Mungu kujenga na kudumisha jamii inayosimikwa katika misingi ya haki na amani. Baba Mtakatifu Leo XIV amekumbusha kwamba, ushirika wao unasimikwa katika kauli mbiu yao: “In certibus unitas, in dubiis libertas, in omnibus caritas.” Yaani: “Umoja katika mambo msingi, uhuru katika mambo ya mashaka, na upendo katika mambo yote.” Huu ni msingi, kanuni ya majadiliano na uwajibikaji unaotanabaisha Chama chao.
Ni uhusiano unaowafanya kuthaminiana na hivyo kukoleza moyo wa ushirikiano mintarafu tunu msingi za Injili ya Kristo Yesu. Baba Mtakatifu Leo XIV anakaza kusema, imani ya Kanisa Katoliki inaimarishwa kwa njia ya ushirikiano na Mapokeo ya Kanisa Katoliki. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, huku akisukumwa na udugu wa kibinadamu, leo hii imani haina budi kutangazwa, kushuhudiwa na kutamadunishwa kwani huu ni mchakato wa uinjilishaji wa tamaduni na utamadunisho wa Injili unaoiwezesha Habari Njema ya Kristo Yesu kuingia na kupenyeza mizizi yake katika tamaduni mbalimbali, ikiikubali, ikiisafisha, na kuipatia maana mpya bila kuharibu utambulisho wa watu. Lengo ni kufanya Injili ya Kristo Yesu uwe ni ujumbe unaozungumza lugha na tajiriba ya watu mahalia, kwa kuendelea kuwavuta vijana wa kizazi kipya katika Chama chao, kutokana na ushuhuda wa tunu msingi za urafiki wa Kikristo.
Baba Mtakatifu Leo XIV anawapongeza kwa Chama chao kujikita katika taaluma huku wakifuata wito wao, huku wakiendelea kutafuta ukweli unaopaswa kurithishwa kwa vijana wenzao. Huu ni mchakato unaosimikwa katika nidhamu binafsi, toba na wongofu wa ndani; akili na utashi ili kuhakikisha kwamba, wanatekeleza dhamana yao barabara, bila ya kusukumwa na taaluma inayosimikwa katika uchu wa mali na madaraka, mwaliko wa kujenga na kudumisha ikolojia ya binadamu kwa kuheshimu utu wake, kuishi kwa furaha, ukarimu na majitoleo. Huu ni mwaliko wa kuangalia kiini cha utu wa mwanadamu, ili kuzima kiu ya maisha na haki kwa busara na upendo, ili kwa pamoja waweze kugundua ukweli kwa kuufahamu, kutenda na kuamini. Mwanadamu kwa asili yake ni mtu anayemtafuta Mungu ambaye amejifunua kwao kwa njia ya Kristo Yesu, Mkombozi wa Ulimwengu, mwaliko ni kudumisha uhusiano na Mwenyezi Mungu kama njia ya kutafuta utakatifu wa maisha. Mwishoni mwa hotuba yake, Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, dhamira ya kitamaduni ya Wakristo ni kuielekeza jamii na historia kuelekea kilele katika kumtegemea Mwenyezi Mungu. Kwa maombezi ya Mtakatifu Boniface, Mwinjilishaji wa Ujerumani, Baba Mtakatifu anawataka wanachama hawa kuwa ni mashuhuda wa hekima ya Kiinjili katika jamii ya Kijerumani na Bara la Ulaya katika ujumla wake.
