Papa Leo XIV kwa watoto:Mungu anataka kutazama mioyo yetu na sio simu zetu!
Vatican News
Jumatatu tarehe 22 Julai 2026 Baba Mtakatifu Leo XIV alitembelea kambi ya majira ya joto mjini Vatican na kukutana na watoto na vijana wanaoshiriki katika programu ya kila mwaka ya wakati wa kiangazi kwa Watoto wa wafanyakazi wa Vatican, ambapo mada ya mwaka huu2026 inayowaongoza ni: "Anasafiri yule anayethubutu kusafiri." Kwa njia hiyio mkutano huo umempatia fursa ya kujibu maswali kadhaa na ambayo yalihusu masua ya teknolojia na mahusiano ya familia na shule. Akijibu swali kuhusu ugumu wa kutengana na skrini wakati wa kipindi cha mwaka wa shule, Papa Leo XIV alifafanua juu ya faida za teknolojia lakini pia akasisitiza kwamba haipaswi kuchukua nafasi ya mwingiliano halisi wa kibinadamu.
Tumieni muda kukaa na watu badala ya kupitia muda na vifaa
"Teknolojia inaweza kuwa nzuri sana na yenye manufaa sana kwa mambo mengi. Hata hivyo, tunapokuwa pamoja, si lazima kuwa na simu ya mkononi, simu janja, au kompyuta ya kibao mikononi mwetu kila wakati,” alisema Papa. Kwa hiyo aliwahimiza watoto hao kutumia muda pamoja kama watu badala ya kupitia vifaa. Papa Leo XIV alisema kuwa: “Ni muhimu sana kujenga urafiki, kutumia muda pamoja, kucheza pamoja, na labda hata kujifunza pamoja. Sisi ni wanadamu, watu, na hivyo kuwasiliana na wengine ni muhimu sana." Aliongeza tafakari hiyo hadi kwenye maisha ya kifamilia, ambapo alibainisha kwamba "familia inapokuwa pamoja, siyo vizuri kwa kila mtu kukaa hapo akitazama simu yake. Badala yake, Papa alisema "Ni muhimu sana kujifunza jinsi ya kuzungumza, kufanya mazungumzo, na kufurahia kuwa pamoja."
Mungu anataka kutazama mioyo yetu na sio simu zetu
Baba Mtakatifu aidha alisisitiza umuhimu wa sala, akiwakumbusha watoto kwamba "hata kama tunaweza kuwa na Biblia na sala kwenye simu zetu, Mungu hataki kutazama simu zetu," kwa sababu Mungu anataka kutazama mioyo yetu na maisha yetu," alisisitiza Papa XIV. Kwa utambuzi wa mbinu za kidijitali wakati wa kuwaelekea hasa Watoto wakubwa, alionya kwamba programu nyingi zimeundwa kimakusudi ili kuwaweka watumiaji katika hali ya kujishughulisha kwa muda mrefu. "Wanajaribu kutufanya tutegemee teknolojia hii.” Papa alipendekeza kuweka mipaka ya vitendo katika matumizi ya skrini, kama vile kuweka simu mbali wakati fulani wa siku na kutoa nafasi kwa mazungumzo na shughuli za kifamilia. "Sisi sote hatujaunganishwa kwenye kebo, sisi ni wanadamu."
Kukuza maisha ya kibinadamu na kiroho
Katika hilo Baba Mtakatifu aliwatia moyo watoto kukuza maisha yao ya kibinadamu na ya kiroho kwa kukuza mahusiano, kumtafuta Mungu katika maombi, na kuepuka aina za utegemezi ambazo zinaweza kupunguza uhuru wao. Alisisitiza juu ya kujifunza kufikiria wenyewe badala ya utegemezi.
Utegemezi wa mitandao wakati mwingine inaweza kukupoteza
Kijana mwingine alimuuliza Papa kuhusu uzoefu wake wa kusafiri ulimwenguni kote. Akitumia safari zake mwenyewe, Papa Leo XIV alikumbuka jinsi ambavyo mara kadhaa wakati mifumo ya utumiaji wa GPS ilivyo mwongoza katika mwelekeo mbaya. "Nchini Italia, katika nchi zingine za Ulaya, Peru, na hata mara moja nchini Marekani, nilifuata GPS, na ilinipeleka kwenye njia isiyofaa," alisema. Baba Mtakatifu alieleza kwamba "ni bora zaidi kujifunza kufikiria wenyewe na kukuza uwezo muhimu wa kujua tunakoelekea maishani." Kwa njia hiyo aliwahimiza watoto kutumia kikamilifu uwezo ambao Mungu amewapatia badala ya kutegemea teknolojia kabisa. "Sihitaji simu yangu ikiwa ubongo wangu unafanya kazi," alisema, akiongeza kuwa maandalizi na uamuzi mzuri husaidia watu kukabiliana na matatizo na kupata suluhisho wakati matatizo yasiyotarajiwa yanapotokea.
Mpelelezi Mkuu:Tunataka yesu awe pamoja nasi
Mwishoni mwa mkutano huo, Papa Leo XIV aliitwa "Mpelelezi Mkuu" wa kambi ya majira ya joto na akapewa vifaa vya wapelelezi na bamba la ukumbusho. Aliwaalika watoto wote kusali pamoja naye na kuwatia moyo wawaambie wazazi wao kwamba walikuwa wamesali pamoja na Papa. "Sala ni muhimu sana kwetu. Tunataka Yesu awe hapa pamoja nasi," alisema Papa.
Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku. Just click here
