Tafuta

Baba Mtakatifu Leo XIV katika Nia zake za Jumla kwa Mwezi Juni, 2026 : Tunu Msingi za Michezo Baba Mtakatifu Leo XIV katika Nia zake za Jumla kwa Mwezi Juni, 2026 : Tunu Msingi za Michezo  (Belgaimage)

Nia za Baba Mtakatifu Leo XIV Kwa Mwezi Juni 2026 Tunu Msingi za Michezo!

Baba Mtakatifu Leo XIV katika Nia zake za Jumla kwa Mwezi Juni, 2026 anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kusali ili kwamba michezo iwe ni chombo cha amani, mahali pa watu kukutana, na majadiliano kati ya tamaduni na Mataifa, ili hatimaye, iweze kukuza maadili na utu wema kama vile heshima, mshikamano wa udugu wa kibinadamu na maboresho ya maisha ya mtu binafsi. Michezo ni lugha inayofahamika na watu wengi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Leo wa XIV katika Waraka wake kwa washiriki wa Michezo ya Olympiki kwa Mwaka 2026 amekazia kuhusu: Thamani ya michezo: Michezo na ujenzi wa amani; tunu msingi za michezo katika majiundo na malezi; Mchezo, shule ya maisha na ya kisasa; Michezo na maendeleo binafsi; Mambo yanayohatarisha tunu msingi za michezo; Mashindano na utamaduni wa watu kukutana; Michezo, Mahusiano na mang’amuzi; sanjari na Mpango mkakati wa michezo kwa ajili ya kuwa na maisha tele! Dunia ina kiu ya amani kumbe. Kuna haja ya kutumia nyenzo zitakazo saidia kusitisha matumizi mabaya ya madaraka na hivyo kujikita katika utawala wa haki na sheria. Tunu msingi za michezo katika majiundo ili kuweza kuwa na maisha tele pamoja na utimilifu wake. Rej. Yn 10:10.

Michezo ni chemchemi ya furaha ya kweli
Michezo ni chemchemi ya furaha ya kweli   (ANSA)

Baba Mtakatifu Leo XIV katika Nia zake za Jumla kwa Mwezi Juni, 2026 anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kusali ili kwamba michezo iwe ni chombo cha amani, mahali pa watu kukutana, na majadiliano kati ya tamaduni na Mataifa, ili hatimaye, iweze kukuza maadili na utu wema kama vile heshima, mshikamano wa udugu wa kibinadamu na maboresho ya maisha ya mtu binafsi. Anasema, Mama Kanisa hana budi kutekeleza dhamana na utume wake hapa ulimwenguni, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa binadamu katika michezo kama anavyosema Mtakatifu Paulo, Mtume na Mwalimu wa Mataifa kuhusu utaratibu kwa wanariadha: “Je! Hamjui, ya kuwa wale washindanao kwa kupiga mbio, hupiga mbio wote, lakini apokeaye tuzo ni mmoja? Pigeni mbio namna hiyo, ili mpate. Na kila ashindanaye katika michezo hujizuia katika yote; basi hao hufanya hivyo kusudi wapokee taji iharibikayo; bali sisi tupokee taji isiyoharibika.” 1Kor 9:24-25. Hiki ni kielelezo cha mashindano ya kiroho; na kwamba Binadamu ni umoja wa mwili, roho na nafsi na hivyo Mama Kanisa anakazia umuhimu wa michezo katika maisha ya mwanadamu kama mambo muhimu sana katika kuhubiri na kufundisha.

Wakristi wanahimizwa kushiriki katika michezo
Wakristi wanahimizwa kushiriki katika michezo   (AFP or licensors)

Michezo ni shule ya maisha na ya kisasa mambo ambayo yamepewa kipaumbele cha pekee na walezi katika maisha na kazi; Ustawi na maendeleo ya mtu mzima: kiroho na kimwili na kwamba, Mama Kanisa anaona michezo kama fursa ya kukuza na kudumisha tunu msingi za maisha kama vile: Udugu wa kibinadamu, mshikamano na amani. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema mapumziko yatumike kuimarisha afya ya kiroho na kimwili na kwamba, michezo pia inaweza kuimarisha, kustawisha na kukuza mahusiano ya kidugu kati ya wanadamu wa hali zote, Mataifa na makabila mbalimbali. Kumbe, Wakristo wanahimizwa kushiriki katika michezo, huku ikikolezwa na roho ya kiutu na ya kikristo. Rej. Gaudium et spes, n.61. Katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo, Mama Kanisa amekazia pia umuhimu wa michezo, utamaduni na elimu na kwamba, michezo ni lugha inayofahamika na wengi na kikolezo cha watu kukutana; kujadiliana na kwamba, bado kuna mengi ya kujifunza kutoka katika tamaduni za watu mbalimbali, ili kukuza na kudumisha majadiliano ya kiekumene, kidini na kitamaduni.

Michezo ni nafasi ya kuwakutanisha watu
Michezo ni nafasi ya kuwakutanisha watu   (AFP or licensors)

Michezo na maendeleo binafsi: Michezo ni chanzo cha furaha, mahali mtu anapoweza kujieleza kutoka katika undani wake; ni mahali pa kuonesha umoja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu unaovunjilia mbali uchoyo na ubinafsi, unajielekeza katika mafao ya wengi; michezo inatoa fursa ya watu kukutana na hivyo kukuza na kudumisha udugu; ni mahali pa kuratibu kinzani na migogoro, kwa kusameheana na kusahau. Makocha wanayo kazi na dhamana nyeti katika kujenga umoja kama timu, kati ya wachezaji. Michezo inamwendeleza mtu mmoja mmoja sanjari na kujenga mahusiano na mafungamano ya kijamii; kumbe michezo lazima ijitahidi kuwalenga watu wote ndani ya jamii, kwani ni sehemu muhimu sana ya maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu.Kumbe, michezo inapaswa kuwa ni chemchemi ya umoja katika tofauti zake msingi; zinazopania pamoja na mambo mengine kujenga familia ya binadamu inayosimikwa katika ukarimu, majadiliano na hali ya kuaminiana. Michezo, Mahusiano na mang’amuzi mintarafu ushindi na kushindwa, mambo yanayopaswa kusimikwa katika ukweli na unyenyekevu.

Michezo ina nafasi kubwa katika ustawi na maendeleo ya mtu mzima.
Michezo ina nafasi kubwa katika ustawi na maendeleo ya mtu mzima.

Wanamichezo wajifunze kukubali matokeo, bila kukata wala kukatishwa tamaa; Kukubali ushindi, bila majivuno wala kejeli, bali wapokee ukweli katika hali ya ukomavu, kwa kutambua udhaifu wao na fursa ambazo ziko mbele yao daima. Kamwe michezo isichukue nafasi ya dini katika maisha ya mwanadamu, kwani itapoteza utambulisho wake na kwamba, wanamichezo watambulike kuwa ni watu wenye: mwili, roho na nafsi.Ukaribu na uwepo wa Kanisa katika tasnia ya michezo ukazie kanuni maadili na utu wema; uwiano mzuri kati ya mwili, roho na nafsi katika mchakato wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu. Michezo ni mahali pa kujenga mahusiano ya kijamii, kitamaduni na kimwili; ni chemchemi ya furaha; mahali pa kusaidiana na kwamba, michezo ni fursa ya kujenga na kudumisha maridhiano ya kijamii. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, katika mtazamo wa shughuli za kichungaji, hii ni changamoto kwa Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, anashiriki kikamilifu katika tasnia ya michezo, kwa kuwasindikiza, kuwapatia wanamichezo mang’amuzi na matumaini. Ni katika muktadha huu, michezo kweli inaweza kuwa ni shule ya maisha, mahali pa kushirikishana tunu msingi za maisha; kwa kuheshimiana na wengine na kwa furaha ya kweli ya kutembea bega kwa bega!

Nia Za Papa Mwezi Juni 2026
05 Juni 2026, 15:50