Tafuta

2026.06.09 Dom Osório Citora Afonso Askofu Quelimane wa Msumbuji aliyeuawa tarehe 6 Juni 2026 kwa kupigwa risasi 2026.06.09 Dom Osório Citora Afonso Askofu Quelimane wa Msumbuji aliyeuawa tarehe 6 Juni 2026 kwa kupigwa risasi 

Mazishi ya Askofu wa Quelimane nchini Msumbiji,Papa:mchungaji mkarimu

Katika ujumbe uliosomwa Juni 12,katika Kanisa Kuu la Quelimane wakati wa imazishi ya Askofu Osório Citora Afonso,aliyeuawa mnamo Juni 6,Papa Leo XIV alionesha kusikitishwa kwake na kilichotokea na kuelezea matumaini yake kwamba mazingira ya uhalifu huu yatafafanuliwa.Katika mahubiri yake,Balozi wa Vatican nchini Msumbiji,Muñoz Cárdaba, alisema kwamba wamemuua mtu wa amani,mmisionari aliyeamini katika wema wa watu.Rais wa Msumbiji pia alihudhuria misa hiyo.

Federico Piana na Angella Rwezaula- Vatican.

Katika Siku ya mazishi ya Askofu wa Quelimane na Msimamizi wa Kitume wa Jimbo Kuu la Beira, Msumbiji, ambaye aliuawa kikatili katika makazi ya Maaskofu tarehe 6 Juni 2026, Papa Leo XIV alionesha huzuni yake kubwa na ukaribu wa Kanisa Katoliki lote kwa ujumbe ulioelekezwa kwa Askofu Mkuu Inácio Saúre wa Nampula na Rais wa Baraza la Maaskofu wa Msumbiji, ambao Askofu Osório Citora Afonso alihudumu kama Katibu Mkuu.

Baba Mtakatifu aliandika kuwa, "Baada ya kupokea kwa masikitiko makubwa habari za kifo cha kikatili cha Dom Osório Citora Afonso, I.M.C., natamani, katika saa hii ya huzuni, kuungana na maaskofu wote, mama yake na familia yake, wamisionari wa Consolata, mapadre na waamini wengine wa Makanisa mahalia ya  Quelimane na Beira, nikiwahakikishia kwamba wako katika mawazo na maombi yangu." Na "wakati ninaposubiri hali ya uhalifu huu ifafanuliwe kikamilifu, naomba faraja ya matumaini na kuomba kwamba Bwana amkaribishe mchungaji huyu mkarimu na kwamba wakati huu wa maumivu uweze kuishi kwa imani, katika mwanga wa Kristo aliyefufuka, kwa faida ya Kanisa pendwa la Msumbiji, ambalo ninatoa Baraka ya Kitume, ili liendelee kuwa imara katika tangazo la msamaha na maelewano,” Baba Mtakatifu aliandika.

Mazishi ya Askofu Osorio
Mazishi ya Askofu Osorio

Hisia kubwa katika ibada ya mazishi

Misa ya mazishi, iliyoongozwa na Askofu Mkuu Luís Miguel Muñoz Cárdaba, Balozi wa Vatican nchini Msumbiji kwa kushirikiana  na Askofu Mkuu wa Nampula, ilifanyika asubuhi tarehe 12 Juni 2026  katika Kanisa Kuu la Mama Yetu wa Ukombozi huko Quelimane katika mazingira ya ukumbusho mkubwa. Ushiriki na hisia: pamoja na mapadre  wengi, watawa, na watu wa wa  Mungu na wenye mapenzi mema waliotaka kumuaga mtu aliyeheshimiwa na wote na mchungaji aliyezingatiwa kuwa mwangalifu kwa mahitaji ya kiroho na kimwili ya watu waliokabidhiwa kwake, Rais wa Jamhuri ya Msumbiji, Daniel Francisco Chapo, pia alikuwepo, pamoja na wahudumu kadhaa na mamlaka nyingine za kitaifa.

Kujua ukweli

"Hatupaswi kuwa hapa leo, hatupaswi kuadhimisha mazishi haya. Kilichotokea hakipaswi kutokea kamwe. Hakujawahi kutokea katika historia ya Msumbiji kwa Askofu kuuawa," alisema Askofu Mkuu Muñoz Cárdaba katika mahubiri yake, huku akielezea matumaini yake kwamba "sababu zote za kifo hiki cha kikatili zitajulikana kwa uhakika. Hata kama zina uchungu kiasi gani, hatupaswi kuogopa ukweli. Uhuru unatufanya huru."

Mtu wa Amani

Akizingatia sura ya Askofu  Citora Afonso, Balozi wa  Vatican  alikumbuka kwamba "walimuua mtu wa amani, walimuua mtu wa upatanisho, mmisionari aliyeamini katika wema wa watu, mchungaji aliyejitolea kikamilifu kwa huduma hadi mwisho." Kisha Askofu Mkuu akaendelea: "Hatuwezi kuruhusu damu hii isiyo na hatia kutuzamisha katika kukata tamaa. Hapana, huu ni wakati wa uwongofu mkubwa, wa kufanya toba, kwa ajili ya upyaisho wa ndani. Damu ya Askofu Osório itufanye kuwa bora zaidi, ituondolee dhambi, ituongoze kutoka ubaya hadi wema, kutoka gizani hadi nuruni. Kisha kifo chake kitakuwa na matunda, kitasafisha jimbo hili na Kanisa na kutufanya sote kuwa bora zaidi. Nina hakika kwamba kifo hiki cha kikatili hakitakuwa bure. Ninaamini kwamba Mungu, katika Uweza wake mtakatifu na wa ajabu, atafanikiwa kubadilisha ubaya mwingi kuwa mzuri," alisisitiza Askofu Mkuu

Mazishi ya faragha huko Nampula

Mwili wa Askofu uliwasili kwa ndege hadi Nampula, zaidi ya kilomita 500 kutoka Quelimane, ambapo Misa ya mazishi ya faragha iIifanyika tarehe 13 Juni 2026, ambayo iliadhimishwa na Askofu Mkuu wa jiji, Inácio Saúre, katika Kanisa Kuu la Mama Yetu wa Fatima, ambapo Askofu Osório Citora Afonso alibatizwa, akapata kipaimara, na kuwekwa wakfu kuwa Padre. Ibada ya mazishi ilifuatia katika makaburi ya mapadre wa eneo hilo.

Maziko ya Askofu Osorio
Maziko ya Askofu Osorio

Kumbukizi kutoka kwa Makardinali Tagle na Rugambwa

Askofu wa Quelimane, mmisionari wa Consolata, alikuwa na umri wa miaka 54 na kati ya 2017 na 2023, pia alihudumu kama afisa wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji, Kitengo cha Uinjilishaji wa Kwanza na Makanisa Mapya Maalum. Tarehe 11 Juni 2026 katika mahubiri yake wakati wa Misa iliyoadhimishwa katika Kanisa la Wafalme Watatu, katika jengo la Propaganda Fide huko Roma, Kardinali Luis Antonio Tagle, Mwenyekiti wa  Baraza la Kipapa la Uinjilishaji, kwa ajili ya kumkubuka na kumuombea alikumbuka kujitolea kwake bila kuchoka na kwa upendo: “Tulishuhudia shauku na furaha ambayo Osorio alihisi kila aliposhiriki Neno la Mungu. Hakuchoka kuandaa mikutano ya kujifunza Biblia, mafungo ya kiroho, na mafungo. Zawadi aliyopokea bure, aliitoa bure. Hii ndiyo sababu kifo chake cha kikatili kinatuacha sote tukiwa tumechanganyikiwa na kujeruhiwa.”

Kardinali Tagle baadaye aliongeza "“Mtu kama yeye, mkarimu katika kushiriki tabasamu, Neno la Mungu, na Ufalme wa Haki, angewezaje kukutana na mwisho mbaya kama huo? Hatujui bado, na labda hatutawahi kujua. Lakini tunashikilia kwa imani na matumaini maneno ya Yesu katika Injili: "Mnapoingia katika nyumba, semeni amani. Ikiwa nyumba inastahili, amani yenu na ije juu yake; lakini ikiwa haifai, amani yenu na irudi kwenu." Mpendwa Osório, hutanyimwa amani. Zawadi ya Yesu ya amani itarudi kwao. Pumzika kwa amani.”

Maziko ya Askofu Osorio
Maziko ya Askofu Osorio   (©Cremildo Alexandre)

Kwa upnade wa Kardinali Protase Rugambwa, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Tabora, Tanzania, ambaye alikuwa akimjua vizuri sana kwa kuwa walifanya kazi pamoja naye kwenye ofisi moja, pia alizungumzia kuhusu yeye kwamba" alimpenda Mungu na ndugu zake". "Alikuwa mpole, mnyenyekevu, mstaarabu, na msafi. Mfanyakazi mwenye bidii, aliyepatikana kila wakati," alisema. Kisha akaongeza kwamba alikuwa "amekuwa rafiki wa kweli, aliyejaliwa sifa nyingi nzuri kweli."

Rais wa Msumbiji aliudhuria mazishi
Rais wa Msumbiji aliudhuria mazishi
Kifo cha Askofu Osorio,Msubiji

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku. Just click here

13 Juni 2026, 13:26