Maadhimisho ya Siku ya Uhai Kitaifa: Maajabu ya Mtoto Tumboni!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Mtakatifu Yohane Paulo II katika Wosia wake wa Kitume, “Evangelium vitae” yaani “Injili ya uhai” kwa ufupi anakazia kuhusu: Thamani ya maisha, ukuu na utu wa binadamu kama zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Hii ni Injili ya upendo wa Mungu kwa binadamu; Utu na heshima yake, mambo msingi yanayofumbatwa katika Injili. Katika ulimwengu mamboleo kuna mambo ambayo yanaendelea kutishia Injili ya uhai kwa kukumbatia utamaduni wa kifo. Haya ni matokeo ya watu kukengeuka pamoja na kuporomoka kwa kanuni maadili na utu wema. Kuna sera na mikakati mbalimbali ya kisiasa, kiuchumi na kijamii inayotishia Injili ya uhai, ustawi na maendeleo ya wengi. Mtakatifu Yohane Paulo II anawataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kusimama kidete: kuheshimu, kulinda na kuhudumia Injili ya uhai, ili kukuza na kudumisha haki, maendeleo fungamani ya binadamu, uhuru, amani na furaha ya kweli inayobubujika kutoka katika sakafu ya maisha ya mwanadamu. Waamini wanapaswa kujipambanua kuwa ni watu wanaotetea Injili ya uhai kwa ajili ya maisha kwa kupinga utamaduni wa kifo. Hata leo hii bado kuna damu ya watu wasiokuwa na hatia inaendelea kumlilia Mwenyezi Mungu. Haya ndiyo mauaji ya kimbari na vita. Kuna sera za utoaji na uzuiaji mimba; kifo laini pamoja na uzalishaji kwa njia ya chupa. Maendeleo ya sayansi na teknolojia yamepelekea hata mauaji ya watoto wenye ulemavu kuanzia tumboni mwa mama zao. Yote haya ni matokeo ya uhuru unaoshindwa kutambua: utu, heshima na haki msingi za binadamu. Kumbe, kuna haja kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kujenga na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo kwa kutambua uwepo wa Mungu na kuzingatia kanuni maadili na utu wema, kwa kuimarisha matumaini pamoja na maboresho katika huduma ya tiba ya mwanadamu. Jitihada hizi hazina budi kwenda sanjari na mchakato wa kupinga adhabu ya kifo na kwamba, umefika wakati wa kuachana na dhana ya “vita halali na ya haki”, ili kujenga na kudumisha kanuni maadili zinazolenga kukuza na kudumisha misingi ya haki na amani, pamoja na kupambana dhidi ya mauaji ya kimbari.
Mtakatifu Yohane Paulo II anasema, Kristo Yesu ni chemchemi ya utimilifu wa maisha, mwaliko kwa waamini kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya uhai, kwa sababu maisha ni tunu adhimu inayofumbatwa katika maadili na maisha ya kiroho. Ikumbukwe kwamba, utukufu wa Mungu unang’aa katika sura ya mwanadamu kama kielelezo cha hali ya juu kabisa cha ufunuo wa utimilifu wa upendo wake ambao ni zawadi ya maisha ya uzima wa milele. Hii ni changamoto kwa waamini kudumisha upendo kwa Injili ya uhai, kwa kuwajibika barabara kulinda na kudumisha maisha. Utu, heshima na haki msingi za watoto ambao hawajazaliwa zinapaswa kulindwa na wote. Maisha yana thamani hata katika mateso, magonjwa na uzee kama yanavyofafanuliwa katika Amri za Mungu. Huu ni mwaliko wa kuendelea kuwa waaminifu katika Sheria na Injili ya uhai. Kristo Yesu, kwa mateso, kifo na ufufuko wake ameonesha kilele cha ufunuo wa Injili ya uhai. Msalabani, Kristo Yesu alionesha ukuu na utukufu wake, chemchemi ya maisha mapya na mwaliko kwa Wakristo kusimama kidete kulinda Injili ya uhai. Mtakatifu Yohane Paulo II anasema, Usiue kwa sababu maisha ya mwanadamu ni matakatifu na yasioharibika na kwamba, Mwenyezi Mungu ni chanzo na utimilifu wa maisha ya binadamu. Kanisa linalaani vitendo vyote vya utoaji mimba, kifo laini au watu kujinyonga kwa sababu hii ni dhambi dhidi ya utu, heshima na haki msingi za binadamu.
Huruma na upendo ni urithi na amana ya ubinadamu. Mwanadamu anapaswa kuheshimu Sheria na Amri za Mungu, kanuni maadili na utu wema. Upendo kwa Mungu na jirani, usaidie kulinda na kudumisha Injili ya uhai. Mtakatifu Yohane Paulo II analihamasisha Kanisa kujenga na kudumisha utamaduni mpya wa maisha kwa kulinda na kutetea Injili ya uhai; kwa kutangaza na kuadhimisha Injili ya upendo unaomwilishwa katika huduma, ili kuenzi: ukuu na utakatifu wa maisha.Injili ya uhai iwe ni sehemu ya maisha ya sala ya kila siku, maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa pamoja na Liturujia ya Mwaka wa Kanisa. Huu ni mchakato wa ushuhuda wa imani tendaji unaozingatia mpango wa uzazi kwa njia ya asili. Kwa kutambua kwamba, familia ni tabernakulo ya Injili ya uhai; kwa kuwalinda na kuwahudumia watu wanaoteseka kwa uzee na magonjwa ya muda mrefu. Familia, Kanisa dogo la nyumbani linahamasishwa kuwa ni madhabahu ya Injili ya uhai, ambamo zawadi ya maisha inapokelewa na kutolewa. Familia iwe ni mahali pa kujenga na kudumisha tunu msingi za maisha ya mwanadamu kwa njia ya mshikamano na kutembea kama watoto wa mwanga. Lengo ni kuondokana na utamaduni wa kifo kwa kukumbatia na kuambata utamaduni wa uhai. Kila mtu pamoja na taasisi mbali mbali anayo dhamana ambayo anapaswa kuiendeleza, kama shuhuda wa Injili ya uhai na chachu ya mabadiliko ya kweli ndani ya jamii. Amani ya kweli inalinda na kuendeleza Injili ya uhai.
Ni katika muktadha wa kujenga na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo, Baraza la Maaskofu Katoliki Uingereza, Wales, Scotland na Ireland, Dominika tarehe 21 Juni 2026 linaadhimisha Siku ya Uhai Kitaifa kwa kunogeshwa na kauli mbiu: “The Wonder of the Child in the Womb” Yaani “Maajabu ya Mtoto Tumboni.” Siku hii ilianzishwa ili kutetea, kulinda na kudumisha Injili ya uhai tangu pale Mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake hadi kifo cha kawaida kinapomfika. Baba Mtakatifu Leo XIV katika ujumbe ulioandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kwenda kwa Askofu mkuu John Sherrington, Mratibu wa Masuala ya Maisha Baraza la Maaskofu Katoliki Uingereza, Wales, Scotland na Ireland, anasema, tema iliyochaguliwa kwa mwaka 2026 inaakisi maajabu ya Mtoto Tumboni mwa Mama yake, tangu pale mtoto anapotungwa mimba, kwa sura na mfano wa Mungu, anapendwa na kukirimiwa utu. Hivi ndivyo Baba Mtakatifu Leo XIV anavyofafanua katika Waraka wa kwanza wa Kitume wa “Magnifica humanitas” yaani: “Utu wa kupendeza" Juu ya Hifadhi ya Mwanadamu Katika Enzi ya Teknolojia ya Akili Unde” kwa kifupi “MH.” Upendo huu wa kimungu unamwambata kila mtu na kwamba, huu ni mwaliko wa wa kuchuchumilia utimilifu wa maisha. Baba Mtakatifu Leo XIV anaungana na familia ambazo zimewapoteza watoto wao wakiwa wadogo, kwani wanaendelea kuishi mbele ya Mungu. “Naye si Mungu wa wafu, bali wa walio hai; kwa maana kwake wote wanaishi.” Lk 20:38. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Leo XIV kwamba, wazazi hawa wataendelea kupata msaada wanaohitaji kutoka katika Kanisa, ili kwamba, maisha yao yarutubishwe na Sala pamoja na Sakramenti za Kanisa. Baba Mtakatifu anawashukuru waamini na watu wote wenye mapenzi mema wanaoendelea kutangaza na kushuhudia ukuu, utakatifu na maajabu ya maisha, utu na heshima ya binadamu. Baba Mtakatifu Leo XIV yuko karibu nao wote kwa njia ya Sala.
