Maadhimisho ya Siku ya Vijana Ulimwenguni 2027 Seoul, Corea ya Kusini
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Kardinali Lazzaro You Heung-sik, “Yu Hung Shik” Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Makleri, ambaye katika maisha na utume wake, ameendelea kujipambanua kuwa ni shuhuda na chombo cha haki na amani, Dominika tarehe 14 Juni 2026 ameadhimisha Ibada ya Misa takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Paulo Nje ya Kuta za Roma kwa ajili ya kuombea mchakato wa haki, amani na upatanisho wa Corea ya Kaskazini na Kusini, ambazo bado zimetengana na kwamba, madonda ya utengano huu yanaendelea kuwaathiri watu wa Mungu nchini Corea. Hii ni changamoto kwa watu wa Mungu kuhakikisha kwamba, wanajizatiti kikamilifu katika ujenzi wa haki, amani na upatanisho wa Corea yote katika ujumla wake. Watu wa Mungu nchini Korea wanaweza kutangaza na kushuhudia kwamba, majadiliano katika ukweli na uwazi, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi yana nguvu kuliko malumbano yasiyokuwa na tija kwa watu wa Korea na kwamba, Upatanisho una nguvu zaidi kuliko chuki, uhasama na tabia ya kutaka kulipizana kisasi. Ibada hii ya Misa Takatifu imehudhuriwa pia na Rais wa Corea ya Kusini Lee Jae-myung, wanadiplomasia kutoka nchi mbalimbali duniani pamoja na watu wa Mungu kutoka Korea.
Kardinali Lazzaro You Heung-sik, katika mahubiri yake amekazia kwa namna ya pekee Injili ya matumaini hata pale ambapo watu wamevunjika na kupondeka moyo na kwamba, huruma inapaswa kuchukua nafasi ya vita, kinzani na migogoro isiyokuwa na tifa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Corea. Amesema, amani ya kweli inapata chimbuko lake pale ambapo watu wenye mapenzi mema wanaamua kukutana, kujadiliana na kusikilizana. Mama Kanisa katika maisha na utume wake, katika nafsi ya Baba Mtakatifu Leo XIV ataendelea kusimama kidete kulinda na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu, ili kujenga dunia inayosimikwa katika: haki, udugu wa kibinadamu, amani na upatanisho wa kweli.
Amani ya kweli si ukosefu wa vita, bali inapata chimbuko lake katika majadiliano yanayosimikwa katika ukweli na uwazi; yanayoheshimu na kuthamini utu wa binadamu na haki zake msingi. Lugha ya kisiasa na kidiplomasia inawezekana kuwa na mwelekeo tofauti. Lakini ile kiu ya kulinda na kutunza utakatifu wa maisha; utashi wa kutaka kumhudumia binadamu na kuendelea daima kutafuta, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi ni mambo yanayoweza kupata asili na hatima yake kutoka katika tunu msingi za Kiinjili. Upendo na huruma ni mambo msingi katika jitihada za kuleta upatanisho wa kweli nchini Corea na hivyo kuondokana na kiburi, uchoyo na ubinafsi. Kanisa linapenda kuandamana na waamini wake katika furaha na machungu, ili kuwakirimia imani, matumaini na mapendo wale wote waliovunjika na kupondeka moyo, Kanisa linataka kuwa ni chombo cha huruma, upendo na faraja ya kweli.
Wakati huo huo, Jumatatu tarehe 15 Juni 2026, Baba Mtakatifu Leo XIV amekutana na kuzungumza na Rais Lee Jae Myung wa Corea ya Kusini, ambaye baadaye amebahatika pia kukutana na kuzungumza na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican aliyekuwa ameambatana na Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa Mambo ya Nchi za Nje, Ushirikiano na Mashirika ya Kimataifa. Katika mazungumzo ya Baba Mtakatifu Leo XIV na Rais wa Korea ya Kusini, wameridhishwa na uhusiano mzuri wa kidiplomasia kati ya nchi hizi mbili sanjari na kupongeza mchango wa Kanisa katika ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Korea ya Kusini. Kanisa limeendelea kujipambanua katika huduma ya elimu, afya, maendeleo na ustawi wa jamii.
Itakumbukwa kwamba, baada ya maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo kwa vijana iliyonogeshwa na kauli mbiu: “Vijana mahujaji wa matumaini” Baba Mtakatifu Leo XIV alitangaza kwamba, Maadhimisho ya Siku ya Vijana Ulimwenguni kwa Mwaka 2027 Jimbo kuu la Seoul, Corea ya Kusini, yataanza kutimua vumbi kuanzia tarehe 3 hadi 8 Agosti 2027 na kwamba, maadhimisho haya yananogeshwa na kauli mbiu; “Jipeni moyo; mimi nimeushinda ulimwengu.” Yn 16:33. Matumaini yaliyomo ndani ya nyoyo za waamini ndiyo yanayowapatia nguvu na jeuri ya kutangaza na kushuhudia ushindi wa Kristo Mfufuka dhidi ya dhambi na mauti. Kwa hakika anasema, Baba Mtakatifu Leo XIV vijana wanapaswa kuwa ni mashuhuda wa matumaini hadi miisho ya dunia. Amewakaribisha vijana wengi zaidi huko Seoul, Corea ya Kusini, ili kwa pamoja waweze kuendeleza ndoto na matumaini. Hii pia ilikuwa ni mada nzito katika mazungumzo kati ya Baba Mtakatifu Leo XIV na Rais Lee Jae Myung wa Corea ya Kusini. Wamegusia pia masuala ya kikanda na kimataifa.
