Tafuta

kauli mbiu: “Watafua panga zao ziwe majembe na mikuki yao iwe miundu.” Isaya 2:4. kauli mbiu: “Watafua panga zao ziwe majembe na mikuki yao iwe miundu.” Isaya 2:4.   (AFP or licensors)

Kauli mbiu Maadhimisho Siku ya Kuombea Utunzaji wa Mazingira 1 Septemba 2026

Papa Leo XIV anasema, maadhimisho ya Siku ya Kuombea Utunzaji Bora wa Mazingira nyumba ya wote tarehe Mosi Septemba 2026 yananogeshwa na kauli mbiu: “Watafua panga zao ziwe majembe na mikuki yao iwe miundu.” Isaya 2:4. Ujumbe huu unachota utajiri kuhusu uhusiano kati ya migogoro ya vita na uchafuzi wa mazingira nyumba ya wote. Hii ni siku iliyoanzishwa na Papa Francisko Mwaka 2015 kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilei huruma ya Mungu

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Siku ya Kuombea Utunzaji Bora wa Mazingira Nyumba ya Wote kwa upande wa Kanisa Katoliki inayoadhimishwa tarehe 1 Septemba 2026, ilianzishwa rasmi na Baba Mtakatifu Francisko tarehe 10 Agosti 2015 kama sehemu ya mchakato endelevu wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya Huruma ya Mungu, kwa kuwataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kusimama kidete kulinda, kutunza na kudumisha kazi ya uumbaji. Kwa kuthamini na kujali umuhimu wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, maadhimisho haya yakachukua mfumo wa kiekumene na kilele chake ni hapo tarehe 4 Oktoba 2026, Mama Kanisa anapoadhimisha Sikukuu ya Mtakatifu Francisko wa Assisi, aliyejisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya maskini, amani na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Hiki ni kipindi muafaka cha kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa kazi kubwa ya uumbaji sanjari na kujibu kwa vitendo kilio cha Mama Dunia na Maskini, “Akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi.”

Vita ina madhara makubwa katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi
Vita ina madhara makubwa katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi   (AFP or licensors)

Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, maadhimisho ya Siku ya Kuombea Utunzaji Bora wa Mazingira nyumba ya wote tarehe Mosi Septemba 2026 yananogeshwa na kauli mbiu: “Watafua panga zao ziwe majembe na mikuki yao iwe miundu.” Isaya 2:4. Ujumbe huu unachota amana na utajiri kuhusu uhusiano kati ya migogoro ya vita na uchafuzi wa mazingira nyumba ya wote. Uharibifu wa mazingira unakwenda sanjari na ukiukwaji mkubwa wa jukumu la binadamu la kutunza mazingira nyumba ya wote na hivyo hili kuwa ni tishio la muda mrefu kwa maisha ya mamilioni ya watu sehemu mbalimbali za dunia. Baba Mtakatifu Leo XIV anasikitika kusema kwamba, ufahamu ulioenea sasa wa athari za vita dhidi ya maliasili haujasababisha kuundwa kwa taasisi za kutosha au maamuzi ya uwajibikaji yenye lengo la kuzuia migogoro na kutatua migogoro kwa njia ya amani. Kumbe, utabiri wa Nabii Isaya kwamba:“Watafua panga zao ziwe majembe na mikuki yao iwe miundu, yaani zana za kilimo ni mwaliko wa wazi kwa Jumuiya ya Kimataifa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu badala ya kuendekeza vita, vurugu na uharibifu.

Utunzaji bora wa mazingira ni wajibu wa kimaadili wa wote
Utunzaji bora wa mazingira ni wajibu wa kimaadili wa wote   (AFP or licensors)

Kumbe, matukio kuhusu utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote katika kipindi hiki chote, yanapania pamoja na mambo mengine, kufafanua na kumwilisha katika uhalisia wa maisha ya watu taalimungu ya kiikolojia. Lengo ni kudumisha ukweli kuhusu utu, heshima ya binadamu, haki msingi pamoja na uelewa wa kazi ya uumbaji kadiri ya Mafundisho Jamii ya Kanisa. Kazi ya uumbaji iliyokuwa nzuri machoni pa Mwenyezi Mungu na kuikabidhi kwa binadamu kama zawadi imeharibiwa kwa uwepo wa dhambi, ubinafsi na uchoyo unaotaka kuinyonya kwa uchimbaji wa madini na nishati ya mafuta; kilimo cha mashamba makubwa pamoja na uchomaji na ukataji ovyo wa misitu hali ambayo imesababisha kupanda kwa joto duniani pamoja na kuongezeka kiwango cha bahari. Kuna uchafuzi mkubwa wa mazingira unaofanywa kwa kutupa ovyo taka za plastiki; mambo yanayotishia usalama wa maisha ya viumbe hai duniani.

Utunzaji wa mazingira ni wajibu wa wote kimaadili
Utunzaji wa mazingira ni wajibu wa wote kimaadili

Baba Mtakatifu Leo XIV, anaonesha masikitiko yake makubwa kutokana na madhara na ukatili wa vita vinavyoendelea sehemu mbalimbali za dunia. Kwa hakika Kanisa limevunjika na kupondeka moyo kutokana na kilio na maumivu yanayotokea sehemu mbalimbali zilizoathirika kwa vita na hasa: Ukraine, Iran, Israeli pamoja na Ukanda wa Gaza. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, kamwe mwanadamu hapaswi kuzoea vita na kwamba, kuna haja ya kukataa na hatimaye kushinda kishawishi cha kukimbilia silaha zenye nguvu na za hali ya juu. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema kwamba bahati mbaya vita bado havijang’olewa katika maisha ya binadamu. Vita vya hivi karibuni vinaendelea kuleta uharibifu mkubwa: kiroho na kimwili bila kusahau maangamizi makubwa na hasa zaidi, zinapotumika silaha za kisayansi za kila aina, tabia mbaya sana ya vita inatishia kuwapelekea wapiganao kwenye unyama unaozidi wa enzi za zamani. Rej. Gaudium et Spes, 79). Baba Mtakatifu Leo XIV katika jina la utu, heshima na haki msingi za binadamu sanjari na sheria za Kimataifa amerudia tena kuwataka wale wote walio katika nafasi za uwajibikaji, onyo la mara kwa mara la Hayati Baba Mtakatifu Francisko: Vita daima ni kielelezo cha kushindwa!  Na lile la Papa Pius XII: “Hakuna kinachopotea kwa amani. Kila kitu kinaweza kupotea kwa njia ya vita.”

Siku ya Mazingira 2026
04 Juni 2026, 15:48