Tafuta

Baba Mtakatifu Leo XIV, Alhamisi tarehe 18 Juni 2026 amewaongoza watu wa Mungu katika Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kumkumbuka na kumwombea Hayati Kardinali Camillo Ruini. Baba Mtakatifu Leo XIV, Alhamisi tarehe 18 Juni 2026 amewaongoza watu wa Mungu katika Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kumkumbuka na kumwombea Hayati Kardinali Camillo Ruini. 

Kardinali Camillo Ruini Mwamba wa Imani na Uongozi 1931-2026

Papa Leo XIV anamkumbuka Kardinali Ruini kwa kipaji cha hekima, busara na akili, mtu aliyejisadaka kwa ajili ya kuhudumia Injili, na Kanisa kwa ajili ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu bila kusahau mchango wake kwa Kanisa la Italia kama Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia. Alikuwa ni chombo cha majadiliano katika ukweli na uwazi katika ulimwengu wa utamaduni. Sasa kwa sala na maombi ya Bikira Maria, Kardinali Camillo Ruini aweze kupokelewa huko mbinguni.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mzaburi anasema, “Basi, utujulishe kuzihesababu siku zetu, tujipatie moyo wa hekima.” Zab 90:2 Haya ni maneno yanayowatia waamini matumaini badala ya kujisikia kuwa wanyonge wanapoyaona maisha yao yana yoyoma na kutoweka mara kama ndoto ya mchana. Kifo kinayaanika maisha ya binadamu na kumwondolea kiburi na kuwahimiza watu kujenga na kudumisha upendo, kutafuta na kuambata mambo msingi katika maisha, ili sadaka na majitoleo yao yaweze kuwapatia amani na utulivu wa ndani wanapokabiliana na Fumbo la Kifo!  Kristo Yesu anapenda kuimarisha matumaini ya waja wake kwamba, Yeye ndiye ufufuo na uzima! Jambo la msingi ni wao kumwamini. Mbele ya Fumbo la Kifo binadamu ni mnyonge na ni “mdogo sana kama kidonge cha piliton.” Mababa wa Kanisa wanasema, maana ya Kikristo ya kifo imefunuliwa katika mwanga wa Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu ambaye ndani yake mna tumaini la Wakristo.

Hayati Kardinali Camillo Ruini 1931 hadi mwaka 2026
Hayati Kardinali Camillo Ruini 1931 hadi mwaka 2026

Mkristo anayekufa katika Kristo Yesu huuacha mwili ili kwenda kukaa pamoja na Mwenyezi Mungu, milele yote! Kwa Mkristo, siku ya kifo huanzisha, mwishoni mwa maisha yake ya Kisakramenti, utimilifu wa kuzaliwa kwake upya kulikoanzishwa na Sakramenti ya Ubatizo, kufanana kamili na sura ya Mwana, kulikotolewa kwa Mpako wa Roho Mtakatifu na ushirika katika karamu ya Ufalme, uliotangulizwa katika Ekaristi, hata kama ana lazima bado kutakaswa zaidi ili kuvikwa vazi la arusi! Mama Kanisa anapenda kuwahamasisha waamini kulitafakari Fumbo la kifo, kama sehemu ya matumaini ya Kikristo kwani, Kristo Yesu mwenyewe anasema, ndiye ufufuo na uzima na kwamba, yeyote anayemwamini ajapokufa atakuwa anaishi na kwamba, heri yao wale wote wanaokufa katika Kristo Yesu. Matumaini ya Kikristo yawasaidie waamini kukabiliana na Fumbo la kifo kwa imani na matumaini na kwamba, hata ustaarabu wa watu wa kale umepitia katika fumbo hili na kwa hakika, ibada ya kifo ni sehemu ya vinasaba vya maisha ya binadamu.

Kardinali Ruini alibahatika kuwa na kipaji cha akili, hekima na busara
Kardinali Ruini alibahatika kuwa na kipaji cha akili, hekima na busara   (ANSA)

Baba Mtakatifu Leo XIV, Alhamisi tarehe 18 Juni 2026 amewaongoza watu wa Mungu kutoka ndani na nje ya Jimbo kuu la Roma katika Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kumkumbuka na kumwombea Hayati Kardinali Camillo Ruini, aliyeitupa dunia tarehe 16 Juni 2026, akiwa na umri wa miaka 95 tangu alipozaliwa yaani tarehe 19 Februari 1931 huko Sassuolo, Jimbo Katoliki la Reggio Emilia, Guastalla. Baba Mtakatifu katika mahubiri yake amegusia mchango wa Kardinali Camillo Ruini katika maisha na utume wake kama Padre, Askofu na Kardinali; katika taalimungu, shughuli za kichungaji, uragibishaji wa maisha ya vijana; katika masuala ya kitamaduni, katika kuhamasisha, kulinda na kutunza miito mbalimbali sanjari na matumizi bora ya uongozi ndani ya Kanisa. Alikuwa ni muasisi wa “Mradi wa Utamaduni”, Maadhimisho ya Sinodi ya Jimbo kuu la Roma; nguzo msingi ya majadiliano katika maisha na utume wa Kanisa; katika masuala ya kisiasa na jamii katika ujumla wake. Alionesha na kushuhudia upendo wa Mungu kwa waja wake katika hali ya unyenyekevu pamoja na kujiaminisha kwa Mungu. Kardinali Ruini alikuwa ni mtu wa sala na tafakari ya kina, aliyasimika maisha yake katika Ibada ya Misa Takatifu. Alikuwa mshirika wa karibu sana wa Mtakatifu Yohane Paulo II katika maisha na utume wake. Kauli mbiu yake ya Kiaskofu ilichota amana na utajiri wake kutoka katika sehemu ya Injili ya Yohane 8:32 “Veritas liberabit nos, “La verità ci renderà liberi” yaani: “Kweli itawaweka huru.” Yn 8:32. Katika maisha na utume wake alitangaza na kushuhudia ukweli unaopata chimbuko lake kutoka kwa Mwenyezi Mungu, chanzo na kiini cha maisha yake. Mwishoni, Baba Mtakatifu Leo XIV amewashukuru na kuwapongeza wale wote waliomsaidia, waliosindikizana naye katika maisha na utume hasa katika miaka ya uzee na ugonjwa wake, wote hawa wapate faraja, amani na utulivu wa ndani.

Papa Leo XIV ameongoza Ibada ya Misa: Kumwombea Kardinali C. Ruini
Papa Leo XIV ameongoza Ibada ya Misa: Kumwombea Kardinali C. Ruini   (@Vatican Media)

Itakumbukwa kwamba, baada ya masomo na majiundo yake ya Kikuhani, akapewa Daraja Takatifu ya Upadre tarehe 8 Desemba 1954. Akateuliwa kuwa Askofu Msaidizi wa Jimbo Katoliki la Emilia na Guastalla na kuwekwa wakfu tarehe 16 Mei 1983. Mtakatifu Yohane Paulo II tarehe 17 Januari 1991 akamteuwa kuwa Makamu wa Askofu Jimbo Kuu la Roma, Katibu mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI na tarehe 28 Juni 1991 akateuliwa kuwa ni Kardinali. Tarehe 27 Juni 2008 akang’atuka kutoka madarakani. Kwa ufupi kabisa Kardinali Camillo Ruini, amelitumikia Kanisa kama Padre kwa muda wa miaka 71, Kama Askofu akiwa na dhamana ya kuongoza, kufundisha na kuwatakatifuza watu wa Mungu kwa muda wa miaka 42 na kama Kardinali kwa muda wa miaka 34. Baba Mtakatifu katika salam zake za rambirambi alizomwandikia Kardinali Baldassare Reina, maarufu kama “Baldo”, Makamu Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Roma, anamshukuru Mungu kwa zawadi, maisha na wito wa Kardinali Camillo Ruini, aliyebahatika kutekeleza utume wake katika medani mbalimbali za maisha na utume wa Kanisa.

Kardinali Camillo Ruini 1931 hadi mwaka 2026
Kardinali Camillo Ruini 1931 hadi mwaka 2026   (@Vatican Media)

 

Baba Mtakatifu Leo XIV anamkumbuka Kardinali Ruini kwa kipaji cha hekima, busara na akili, mtu aliyejisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kuhudumia Injili, na Kanisa kwa ajili ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu bila kusahau mchango wake kwa Kanisa la Italia kama Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia. Alikuwa ni chombo cha majadiliano katika ukweli na uwazi katika ulimwengu wa utamaduni. Sasa kwa sala na maombi ya Bikira Maria, Kardinali Camillo Ruini aweze kupokelewa huko mbinguni. Katika maisha na utume wake, Kardinali Camillo Ruini alijipambanua kuwa ni shuhuda wa tunu msingi za maisha ya ndoa familia katika ulimwengu mamboleo!Kwa upande wake, Kardinali Matteo Maria Zuppi, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI, amemkumbuka Hayati Kardinali Camillo Ruini, kwa sadaka na majitoleo yake alipokuwa Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI. Aliifanya kazi hii kwa hekima, akili na busara, akatangaza na kuonesha moyo wa Kanisa, ili wote waweze kushikamana kwa ajili ya kudumisha umoja kwa kushikamana na Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Kardinali Camillo Ruini
18 Juni 2026, 17:00