Tafuta

2026.06.23 Kardinali Koovakad akiwa Angelicum katika Mkutano wa Kidini. 2026.06.23 Kardinali Koovakad akiwa Angelicum katika Mkutano wa Kidini. 

Kard.Koovakad:dhana ya udugu si wazo la utopia

Katika hotuba yake ya ufunguzi wa mkutano katika Kanisa Kuu la Malaika kuhusu mada "Kujenga udugu kupitia mazungumzo na ushirikiano,"Kardinali George Koovakad, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini,aliakisi jukumu la tamaduni tofauti za kidini katika kutetea na kukuza amani katika ulimwengu unaozidi kugawanyika na kusambaratika

Vatican News

Majadiliano na mazungumzo, kubadilishana uzoefu, na kuelekea lengo moja: kuwa kaka na dada waliojitolea kujenga na kuimarisha vifungo vya udugu. Hii ndiyo maana ya mkutano uliopewa mada ya: "Wabudha, Wakristo, Wahindu, Wajaini, na Wasikh barani Ulaya: Kujenga udugu kupitia mazungumzo na ushirikiano," unaofanyika kuanzia, tarehe 23  hadi 24 Juni 2026, katika Chuo Kikuu cha Kipapa cha Mtakatifu Thomas Aquinas jijini Roma.

Katika salamu yake, Kardinali George Jacob Koovakad, Mwenyekiti wa  Baraza la Kipapa la Mazungumzo ya Kidini, mmoja wa waandaaji wa mpango huo, alisisitiza kwamba "dhana ya udugu mara nyingi huchukuliwa kama wazo la ndoto," hasa wakati ambapo "umedhoofishwa sana na uhalifu dhidi ya ubinadamu, vita, vurugu, migogoro, mgawanyiko, ubaguzi na chuki katika sehemu mbalimbali za dunia." Kardinali alikumbuka "Roho ya Assisi," kabla ya maadhimisho ya miaka 40 ya Siku ya Maombi ya Amani Duniani iliyoitishwa na Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili mwaka  1986, na maadhimisho ya miaka 800 ya kifo cha Mtakatifu Francis, "mtume wa udugu wa ulimwengu wote," ambaye aliongoza waraka wa Papa Francis kuhusu udugu wa binadamu Fratelli tutti.

Kujenga madaraja

Kardinali Koovakad pia alitafakari maneno ya Papa Leo XIV kuhusu hitaji la kujenga madaraja kati ya waamini na watu wenye mapenzi mema "kupitia mazungumzo na ushirikiano." Kwa Papa, Kardinali Koovakad aliongeza, udugu ni "ukweli ulio hai, wenye nguvu kuliko migogoro, tofauti, na mivutano," unaobadilisha "tamaduni, hisia, na mila kuwa fursa ya kutajirishana."

Bara lenye utofauti mwingi

Akirejeea Ulaya, alibainisha kuwa linahifadhi "urithi wa kiutamaduni na kidini unaoshuhudia kwa fahari kustawi kwa makundi mbalimbali na ujumuishaji wao katika historia, ambayo alipendekeza, imekuwa na alama ya uhamiaji, utandawazi, mabadiliko ya idadi ya watu, na kupungua kwa nguvu kazi. Kutokana na hilo , alibainisha kwamba, kumeibuka mabadiliko ya bara hilo kuwa "sufuria kubwa ya mchanganyiko" wa makabila, lugha, na tamaduni za kidini. Kardinali Koovakad aliendelea kusema, urithi huu lazima uthaminiwe ili kuunda "jamii jumuishi, yenye mshikamano, na yenye usawa," ikihamaisha udugu na urafiki kwa heshima kamili ya kila mwanadamu na haki zake, "ikiwa ni pamoja na haki ya kukiri na kutekeleza dini yake."

Kufanya Kazi kwa Manufaa ya Wote

Kardinali aliwasihi wale wanaoishi Ulaya na wale ambao wameifanya kuwa makazi yao kufanya kazi pamoja kwa manufaa ya wote, "kwa imani kwamba utofauti wa kiutamaduni, kidini, na kijamii ni utajiri wa binadamu na si tishio." "Kadiri sisi, watu wa tamaduni  tofauti za kidini," Kardinali Koovakad alisema, "tunavyokutana na kubadilishana mawazo huku tukiheshimu upekee wa miktadha, tamaduni na dini za kila mmoja, ndivyo tutakavyokua,  si tu katika upendo wa kidugu na kuheshimiana, bali pia katika kujitolea kwetu kufanya kazi na kuchangia pamoja kwa manufaa ya wote katika jamii."

Kuhamasisha amani

Kwa kuhitimishaa, Kardinali Koovakad akirudia maneno ya Papa Leo XIV, alisema kuwa alitaka kuunganisha nguvu "ili kutetea na kuhamasisha amani, haki, na udugu wa kibinadamu kupitia mazungumzo, ushirikiano, na urafiki wa kijamii. Alisisitiza kwamba vipengele hivi ni "vipengele vya msingi vya kujenga udugu wa kibinadamu katika wakati wetu, wakati dunia imegawanyika zaidi na kusambaratika kuliko hapo awali. Kardinali alielezea matumaini kwamba siku hizi za kutafakari na kubadilishana zitawasaidia washiriki "kupata njia na njia za kuimarisha mahusiano ya pande zote kulingana na heshima, udugu, mshikamano, na uaminifu."

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata taarifa mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku. Just click here

23 Juni 2026, 16:27