Tafuta

Wakurugenzi wa Mashirika ya Kipapa ya Kimisionari kuanzia tarehe 27 Mei hadi tarehe 3 Juni 2026 wanashiriki katikia Mkutano mkuu wa Mashirika haya ya Kipapa. Wakurugenzi wa Mashirika ya Kipapa ya Kimisionari kuanzia tarehe 27 Mei hadi tarehe 3 Juni 2026 wanashiriki katikia Mkutano mkuu wa Mashirika haya ya Kipapa.   (@Vatican Media)

Miaka 100 Tangu Kuanzishwa Kwa Dominika ya Kimisionari Ulimwenguni

Papa Leo XIV, tarehe 1 Juni 2026 amekutana na Wakurugenzi hawa, kwa kugusia kuhusu Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 100 tangu kuanzishwa Dominika ya Kimisionari Ulimwenguni , Kumbukizi ya Miaka 1010 tangu kuanzishwa kwa Umoja wa Wamisionari wa Wakleri wa Kipapa na kwamba, tarehe 24 Septemba 2026, Mtumishi wa Mungu Askofu Fulton J. Sheen atatangazwa kuwa ni Mwenyeheri. Mashirika haya yana mchango mkubwa katika utume wa Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa, (Pontifical Mission Societies-PMS) katika maisha na utume wake, yanapaswa kujikita katika mchakato wa ujenzi wa ushirika, kwa kuongozwa na kipaji cha ubunifu pamoja na ukakamavu, daima yakichota amana na utajiri wake kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu linalofumbatwa katika upendo unaotolewa kwa ajili ya ukombozi wa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Huu ni mwaliko kwa Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa kuendelea kujipyaisha. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, Kanisa linalosafiri duniani, kwa tabia yake ni la kimisionari, sababu limepata asili yake katika kutumwa na Mungu Mwana na kutumwa kwa Roho Mtakatifu, kufuatana na agizo la Mungu Baba Mwenyezi. Ad gentes, 2. Utume huu wa Kanisa unafumbatwa katika kutangaza na kushuhudia kweli za kiinjili zinazofumbatwa katika upendo wa Mungu kwa waja wake; na hivyo kushuhudiwa katika maisha na utume wa Kanisa. Si dhamana wala wajibu wa Kanisa kufanya wongofu wa shuruti, bali watu watakatifu wa Mungu wavutwe na ushuhuda wa upendo, wenye mvuto na mashiko. Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa ni mtandao wenye sura na tamaduni nyingi, changamoto na mwaliko ni kuhakikisha kwamba, imani ya Wakristo inatangazwa na kushuhudiwa sehemu mbalimbali za dunia. Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa ni vyombo vya Injili ya huruma na upendo inayotekelezwa na Khalifa wa Mtakatifu Petro. Kumbe, kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili ni dhamana na utume wa Mama Kanisa unaokwenda kinyume kabisa cha wongofu wa shuruti unaoweza kutekelezwa kwa njia za: kisiasa, kitamaduni, kisaikolojia au kidini. Kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili ni zawadi ya bure ambayo Roho Mtakatifu amelikirimia Kanisa lake na wala si matokeo ya nia au tafakari zinazofanywa na watu binafsi. Kupokea furaha inayobubujika kutoka kwa Roho Mtakatifu ni neema na nguvu ya pekee inayowawezesha waamini kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo Yesu kwa watu wa Mataifa.

Jubilei ya Miaka 100 ya Dominika ya Kimisionari Ulimwenguni
Jubilei ya Miaka 100 ya Dominika ya Kimisionari Ulimwenguni   (@VATICAN MEDIA)

Wokovu ni zawadi ambayo Mwenyezi Mungu anawakirimia waja wake kwa kukutana na ufunuo wa Uso wa Kristo Yesu, anayewaita waja wake, ili hatimaye, waweze kuwa ni mashuhuda wa shukrani na furaha ya Injili. Kimsingi, Injili inatangazwa na kushuhudiwa kama utume kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wake wa Kitume “Evangelii gaudium” yaani “Furaha ya Injili” anafafanua mambo msingi yanayopaswa kupewa kipaumbele cha pekee katika uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Jambo la kwanza kabisa ni kuhakikisha kwamba, Kanisa linakuwa na mvuto na mashiko yanayowahamasisha watu wa Mataifa kujiunga nalo na wala Kanisa haliwezi kukua na kuongezeka kwa wongofu wa shuruti. Watu wanapaswa kuguswa na chemchemi ya furaha inayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Pili, ni moyo wa shukrani na majitoleo pasi na kujibakiza hata kidogo, dhamana na utume unaopaswa kutekelezwa kwa njia ya unyenyekevu kwa kutambua kwamba, mafanikio yanayopatikana si kutokana na jasho au juhudi za wamisionari wenyewe. Kimsingi, Injili inatangazwa na kushuhudiwa kwa njia ya unyenyekevu na wala hakuna sababu ya “kujimwambafai.” Mihimili ya uinjilishaji inapaswa kuwa karibu zaidi na watu wanaoinjilishwa, kadiri ya hali na mazingira yao pamoja na kuzingatia ufahamu wa watu wa Mungu “Sensus fidei” pamoja na kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Kuna haja ya kukuza na kudumisha karama zinazoweza kuboresha ari na mwamko wa kimisionari miongoni mwa wabatizwa. Hiki ndicho kile kinachoitwa “Sensum fidei” yaani “Ufahamu ya waamini” unaofumbatwa katika msingi wa sala na matendo ya huruma. Katika muktadha huu, waamini walei wamekuwa wakiheshimiwa sana na Mama Kanisa, kwa kutambua mchango na ushiriki wao wa kawaida katika maisha na utume wa Kanisa mahalia. Huu ni mtandao unaopaswa kukuzwa na kudumishwa ili kuonesha utajiri unaobubujika kutoka kwa watu wenye mawazo na mitazamo tofauti tayari kujenga na kudumisha Kanisa la kimisionari na la kisinodi.

Wajumbe wakisalimiana na Baba Mtakatifu Leo XIV
Wajumbe wakisalimiana na Baba Mtakatifu Leo XIV   (@VATICAN MEDIA)

Wakurugenzi wa Mashirika ya Kipapa ya Kimisionari ni viongozi walioteuliwa kuratibu shughuli za kimisionari, kuhamasisha uinjilishaji mpya unaosimikwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko, na kusimamia misaada ya kiroho na rasilimali fedha kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Makanisa ya Kimisionari. Wakurugenzi wa Mashirika ya Kipapa ya Kimisionari kuanzia tarehe 27 Mei hadi tarehe 3 Juni 2026 wanashiriki katika Mkutano mkuu wa Mashirika haya ya Kipapa. Baba Mtakatifu Leo XIV, Jumatatu tarehe 1 Juni 2026 amekutana na kuzungumza na Wakurugenzi hawa, kwa kugusia kuhusu Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 100 tangu kuanzishwa kwa Dominika ya Kimisionari Ulimwenguni Kote, Kumbukizi ya Miaka 1010 tangu kuanzishwa kwa Umoja wa Wamisionari wa Wakleri wa Kipapa na kwamba, tarehe 24 Septemba 2026, Mtumishi wa Mungu Askofu Fulton J. Sheen atatangazwa kuwa ni Mwenyeheri na kwamba, Mashirika ya Kipapa ya Kimisionari yana mchango mkubwa katika maisha na utume wa Kanisa sehemu mbalimbali za dunia. Mwaka 2026 Mama Kanisa anaadhimisha Jubilei ya Miaka 100 tangu kuanzishwa kwa Dominika ya Umisionari Ulimwenguni Kote kwa kunogeshwa na kauli mbiu: “Mmoja katika Kristo, Umoja katika Utume,” Rej. Jn 17:20, 21, 26. Hii ni Dominika iliyoanzishwa na Papa Pius XI na kilele cha Maadhimisho haya ni tarehe 18 Oktoba 2026. Ni muda muafaka wa Sala, Tafakari ya kina pamoja na kuchangia ustawi na maendeleo ya Makanisa ya kimisionari; ushiriki mkamilifu wa watu wa Mungu katika maisha na utume wa Kanisa; kwa kukuza na kudumisha ari, mwamko na tasaufi ya kimisionari na waamini kwa kujikita kikamilifu katika azma ya uinjilishaji katika wakati huu wa upyaisho wa shughuli za kimisionari. Mambo msingi ya kuzingatia ni: ukweli wa tasaufi ya kimisionari, umoja na ushirika katika Kristo Yesu sanjari na kuragibisha shughuli za kimisionari.

Mtumishi wa Mungu Askofu Fulton Sheen kuitangazwa Mwenyeheri
Mtumishi wa Mungu Askofu Fulton Sheen kuitangazwa Mwenyeheri

Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, tarehe 24 Septemba 2026, Mtumishi wa Mungu Askofu Fulton J. Sheen atatangazwa kuwa ni Mwenyeheri katika Ibada ya Misa Takatifu itakayoongozwa na Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle, Mwenyekiti Mwenza wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu. Itakumbukwa kwamba, Mtumishi wa Mungu Askofu Fulton J. Sheen alizaliwa tarehe 8 Mei 1895; Akapewa Daraja Takatifu ya Upadre tarehe 20 Septemba 1919 na hatimaye kuwekwa wakfu kuwa Askofu tarehe 11 Juni 1951 akafariki dunia tarehe 9 Desemba 1979, akiwa na umri wa miaka 84. Katika maisha na utume wake, alikuwa ni mhubiri na mwinjilishaji mahiri kwa njia ya Luninga na Radio, kiasi cha kuwagusa mamilioni ya watu kwa Injili ya matumaini; akasaidia kuchangisha rasilimali fedha kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Makanisa ya Kimisionari, mfabo bora wa kuigwa na Wakurugenzi wa Majimbo wa Mashirika ya Kimissionari ya Kipapa. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, Mashirika ya Kimissionari ya Kipapa kwa hakika ndiyo njia kuu ya kuamsha na kupyaisha dhamana na wajibu wa kimisionari wa wabatizwa wote ili kusaidia Jumuiya za Kikanisa katika Makanisa ya kimisionari na kwamba, anawashukuru wote wanaojisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kuragibisha maadhimisho haya. Kuna Majimbo 1, 300 yanayotegemea msaada kutoka katika Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu kwa ajili ya ujenzi wa Makanisa pamoja na kusaidia shughuli mbalimbali za kimisionari, kuchangia gharama za malezi na makuzi ya Majandokasisi wanaosoma mjini Roma, ili wanaporejea Majimboni mwao, waweze kuchangia katika maboresho ya maisha na utume wa Makanisa mahalia. Kumbe mchango wa waamini walei ni muhimu sana katika muktadha huu.

Papa Leo XIV akizungumza na wakurugenzi wa PMS
Papa Leo XIV akizungumza na wakurugenzi wa PMS   (@VATICAN MEDIA)

Katika hotuba yake ya ufunguzi Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle, Mwenyekiti Mwenza wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu, amekazia umoja katika utume. Hii ni kauli mbiu inayochota amana na utajiri wake kutoka katika kauli mbiu ya Kiaskofu ya Baba Mtakatifu Leo XIV: “In Illo unum uno” Yaani: “Ingawa sisi Wakristo ni wengi, katika Kristo mmoja sisi ni wamoja.” Huu pia ni utajiri unaobubujika kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu, Sala ya Kristo Yesu kwa wafuasi wake, ili wawe na umoja; mambo msingi ambayo Mama Kanisa anapenda kukazia kama sehemu ya maandalizi ya Jubilei ya Miaka 100 tangu kuanzishwa kwa Dominika ya Umisionari Ulimwenguni Kote. Umoja unaofumbatwa katika upendo ni kielelezo cha ushuhuda wa kimisionari, katika mchakato wa uinjilishaji wa kina, changamoto inayotolewa na Mababa wa Kanisa. Wakurugenzi hawa katika Maadhimisho ya Fumbo la Utatu Mtakatifu, Dominika 31 Mei 2026 wametembelea Jimbo Katoliki la Aversa mahali ambapo tangu mwaka 2005 Mwili wa Padre Paolo Manna umepumzishwa. Mwenyeheri Paolo Manna,(1872-1952) alizaliwa tarehe 16 Januari 1872 huko Avellino. Akapewa Daraja Takatifu ya Upadre tarehe 19 Mei 1894. Na kunako Mwaka 1916, alianzisha Umoja wa Wamisionari wa Wakleri, ambao Papa Pius XII kunako Mwaka 1956 aliupandisha hadhi na kuwa ni Umoja wa Wamisionari wa Wakleri wa Kipapa. Alifariki dunia tarehe 15 Septemba 1952 na kutangazwa kuwa Mwenyeheri tarehe 4 Novemba 2001 na Mtakatifu Paulo II. Katika maisha na utume wake alikazia sana umuhimu wa majiundo na ushuhuda wa wakleri na watawa katika maisha na utume wa Kanisa kwa njia ya Injili ya upendo inayomwilishwa katika huduma.

Miaka 100 ya Dominika ya Kimisionari Duniani
01 Juni 2026, 15:40