Tafuta

Barcelona: Baba Mtakatifu amekutana na kuzungumza na watu wa kujitolea; Amesali Masifu ya Adhuhuri kwenye Kanisa kuu la Msalaba Mtakatifu na Mtakatifu Eulalia, Jimbo kuu la Barcelona na jioni ameshiriki katika mkesha wa Sala Barcelona: Baba Mtakatifu amekutana na kuzungumza na watu wa kujitolea; Amesali Masifu ya Adhuhuri kwenye Kanisa kuu la Msalaba Mtakatifu na Mtakatifu Eulalia, Jimbo kuu la Barcelona na jioni ameshiriki katika mkesha wa Sala   (@Vatican Media)

Hija ya 4 ya Kitume ya Papa Leo XIV Hispania: Watu wa Kujitolea, Sala Na Mkesha!

Jumanne, tarehe 9 Juni 2026, akiwa mjini Barcelona, Baba Mtakatifu amekutana na kuzungumza na watu wa kujitolea; Amesali Masifu ya Adhuhuri kwenye Kanisa kuu la Msalaba Mtakatifu na Mtakatifu Eulalia, Jimbo kuu la Barcelona na jioni ameshiriki katika mkesha wa Sala kwenye Uwanja wa “Lluis Companys Stadium” kwa kusikiliza shuhuda za watu wa Mungu na hatimaye, akawapatia tafakari yake ya kina! Uwanja huu ulifurika watu wa Mungu kutoka Jijini Barcelona.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Leo XIV kuanzia tarehe 6 hadi 12 Juni 2026 anafanya Hija ya 4 ya Kitume nchini Hispania kwa kunogeshwa na kauli mbiu: "Alzad la mirada" Yaani "Inueni macho yenu.” Yn 4:35. Jumanne, tarehe 9 Juni 2026, akiwa mjini Barcelona, Baba Mtakatifu amekutana na kuzungumza na watu wa kujitolea; Amesali Masifu ya Adhuhuri kwenye Kanisa kuu la Msalaba Mtakatifu na Mtakatifu Eulalia, Jimbo kuu la Barcelona na jioni ameshiriki katika mkesha wa Sala kwenye Uwanja wa “Lluis Companys Stadium” kwa kusikiliza shuhuda za watu wa Mungu na hatimaye, akawapatia tafakari yake ya kina! Uwanja huu ulifurika watu wa Mungu kutoka sehemu mbalimbali za Barcelona. Baba Mtakatifu katika hotuba yake amewapongeza na kuwashukuru watu wa kujitolea kwa kusadaka muda na uwapo wao kwa ajili ya huduma kwa Mungu, upendo kwa Kristo Yesu, Kanisa na kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro na kwamba, kila mmoja wao amejitoa bila ya kujibakiza: kwa mikono, moyo, mawazo, taaluma na  tabasamu la kukata na shoka, Mwenyezi Mungu awakirimie palewalipotoa kwa moyo wa ukarimu na kwamba, Wakristo sehemu mbalimbali za dunia wanaitwa na kutumwa kuwa ni chachu ya sadaka na majitoleo kama ilivyokuwa kwa Mitume wa Kristo Yesu. Rej. Mt 13:33.

Papa Leo XIV amekutana na watu wa kujitolea
Papa Leo XIV amekutana na watu wa kujitolea   (@Vatican Media)

Uzoefu, mang’amuzi na tajiriba yao katika matukio kama haya na kama ilivyokuwa katika Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo ni alama na ishara ya Ujio wa Ufalme wa Mungu, mambo msingi yanayosimikwa katika sadaka. Sadaka na majitoleo anasema Baba Mtakatifu ni chachu ya maboresho ya utu, heshima na haki msingi za binadamu; kanuni maadili na utu wema sanjari na maisha ya kiroho katika jamii na hasa katika ujenzi wa Mji wa Mungu. Mwelekeo huu ni kinyume kabisa cha ukuaji wa kiuchumi unaosimikwa katika kutafuta faida kubwa. Kristo Yesu amekuja ulimwenguni ili kuleta chachu ya Ufalme wa Mungu unaosimikwa katika: kweli na uzima; ni ufalme wa utakatifu na neema; ni ufalme wa haki, mapendo na amani. Katika sadaka yake, Kristo Yesu alipochomwa mkuki ubavuni mara ikatoka damu na maji alama za Sakramenti za Kanisa na baada ya Ufufuko na kupaa kwake mbinguni, akawakirimia waja wake Roho Mtakatifu ili wawe ni vyombo na mashuhuda wa upendo na haki; mambo yanayopata chimbuko lake katika mahubiri, mfumo wa maisha pamoja na kumwilisha tunu msingi za Kiinjili katika maisha. Hata ukuaji wa Jiji la Barcellona ni kwa neema ya Mungu. Kristo Yesu anasema, ni heri zaidi kutoa kuliko kupokea. Huu ni usemi wa busara unaohimiza ukarimu, upendo, na kusaidia wengine katika jamii na kwamba, haya ni maneno yenye msingi mkubwa wa kiroho, kimaadili na kiutu na kwamba, furaha ya kweli inapata chimbuko lake katika kuwashirikisha wengine, kile walicho nacho! Rej. Mdo 20:35. Mwishoni mwa tafakari yake, Baba Mtakatifu Leo XIV amekazia umuhimu wa kujikita katika fadhila ya unyenyekevu na upole; imani inayokita mizizi yake kwenye ukarimu katika huduma.

Wananchi wa Barcellona wakisali pamoja na Papa Leo xiv
Wananchi wa Barcellona wakisali pamoja na Papa Leo xiv   (@Vatican Media)

Baba Mtakatifu Leo XIV Jumanne tarehe 9 Juni 2026 amesali Masifu ya Adhuhuri kwenye Kanisa kuu la Msalaba Mtakatifu na Mtakatifu Eulalia, Jimbo kuu la Barcelona. Mababa wa Kanisa wanasema, Liturujia ya vipindi inapania kuyatakatifuza malimwengu kwa sala ya Kristo Yesu ambaye pamoja na Mwili wake, humwomba Baba wa mbinguni kama Jumuiya ya watakatifu, ili kuonesha upendo; kujenga umoja na ushirika; tayari kutangaza Habari Njema ya Wokovu inayosimikwa katika ujenzi wa udugu wa kibinadamu, mshikamano, tayari kuwa vyombo na mashuhuda wa huruma, upendo wa Mungu na msamaha. Kanisa ni mchumba mwaminifu wa Kristo Yesu, kichwa cha Fumbo la Mwili wake unaowaunganisha watu kutoka katika kila kabila, lugha, jamaa na Taifa katika huduma ya upendo. Rej. Ufu 5:9. Kila mwamini anaitwa kutenda kadiri ya mpango wa Mungu, katika utii na imani thabiti na kwamba, kila mwamini ni muhimu katika maisha na utume wa Kanisa, daima watambue kwamba, wanaunganishwa na nguvu za Roho Mtakatifu, kwa ajili ya wokovu wa wengi. Baba Mtakatifu anawataka watu wa Mungu Jimbo kuu la Barcellona kujikita katika mchakato wa ujenzi wa umoja dhidi ya kinzani, migawanyiko na vita. Waamini wajitahidi kuwa ni mashuhuda manabii wa umoja, ukaribu, amani na utulivu; tayari kuyasadaka maisha yao ikiwa ni lazima ili kujikita katika mambo msingi katika maisha. Umoja na ushirika ni mambo yanayopaswa kuwa ni uitambulisho wa watu wa Mungu katika kutangaza na kushuhudia Injili. Rej. 16: 24-26.

Mkesha wa Sala kwa watu wa Mungu
Mkesha wa Sala kwa watu wa Mungu   (@Vatican Media)

Baba Mtakatifu Leo wa XIV jioni tarehe 9 Juni 2026 ameshiriki katika mkesha wa Sala kwenye Uwanja wa “Lluis Companys Stadium” kwa kusikiliza shuhuda za watu wa Mungu na hatimaye, akawapatia tafakari yake ya kina! Waamini wajitahidi kukutana na Mungu katika furaha inayobubujika kutoka katika imani kwa kutambua uwepo angavu wa Mungu katika uhalisia wa maisha; kwa njia ya sala, tafakari ya Neno la Mungu pamoja na kushirikishana maisha na waamini wengine. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema changamoto ya afya ya akili ni dalili kwamba, kuna mambo katika maisha hayaendi vyema na hivyo baadhi ya watu kujikuta wakitumbukia katika upweke hasi. Mwanadamu katika maisha yake, anakumbana pia na nyakati za giza na upweke, kama ilivyokuwa kwa Kristo Yesu pale Msalabani; kilio chake kikawa ni chemchemi ya sala.

Mambo msingi; utu heshima na haki msingi za binadamu
Mambo msingi; utu heshima na haki msingi za binadamu   (@Vatican Media)

Kwa hakika Mwenyezi Mungu hapendi watu wake wateseke, kumbe anayabeba mateso pamoja na waja wake, ili waweze kudumu katika maisha na kwamba, kwa uwepo wa Mungu, huo unakuwa ni mwanzo mpya wa maisha. Baba Mtakatifu amegusia pia kuhusu msamaha na upatanisho na kwamba, mwanadamu anapaswa kuwajibika kwa matendo yake katika maisha. Utamaduni wa uchoyo na ubinafsi ni chanzo cha maovu mengi ndani ya jamii. Watu wakimwendea Kristo Yesu kwa moyo wa unyenyekevu na unyofu, anaweza kusaidia mchakato wa msamaha na upatanisho, mambo ambayo yanakwenda hatua kwa hatua; mwaliko kwa waamini kukataa tabia ya kinyongo, kutaka kulipiza kisasi na hivyo kuanza kujenga taratibu moyo wa msamaha na upatanisho, ili kupata msamaha, amani na utulivu wa ndani; ili hatimaye, waamini waliosamehewa wanageuka na kuwa ni vyombo na wajenzi wa Ulimwengu unaosimikwa katika msingi wa haki, amani na maridhiano.

Hija ya Kitume Hispania
10 Juni 2026, 14:41