Hija ya 4 ya Kitume ya Papa Leo XIV Hispania: Wafungwa, Rozari, Huduma na Misa
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Leo XIV kuanzia tarehe 6 hadi 12 Juni 2026 anafanya Hija ya 4 ya Kitume nchini Hispania kwa kunogeshwa na kauli mbiu: "Alzad la mirada" Yaani "Inueni macho yenu.” Yn 4:35. Baba Mtakatifu Leo XIV akiwa Jimbo kuu la Barcelona Jumatano tarehe 10 Juni 2026 amepata fursa ya kukutana na kuzungumza na wafungwa wa Gereza la “Brians wa Kwanza.” Itakumbukwa kwamba, huduma kwa wafungwa ni sehemu ya matendo ya huruma: kiroho na kimwili! Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Fungamani ya Binadamu ndilo ambalo limekabidhiwa dhamana ya shughuli za kichungaji kwa ajili ya wafungwa magerezani, ili kuonesha wasiwasi na ukaribu wa Mama Kanisa kwa wafungwa wanaoteseka magerezani. Baba Mtakatifu anakaza kusema, hii ni dhamana na wajibu wa Kanisa zima kama sehemu ya utekelezaji wa utume wake unaomwilisha matendo ya huruma: kiroho na kimwili katika uhalisia wa maisha ya watu.
Wakati wa hukumu ya mwisho, watu watahukumiwa kadiri walivyowatendea ndugu zake walio wadogo, na kwa kufanya vile, walimtendea Kristo Yesu mwenyewe. (Rej. Mt. 25:40) Kristo Yesu anajitambulisha kuwa kati ya watu wenye njaa, kiu, wageni, watu walio uchi, wagonjwa na wale walioko kifungoni. Gerezani hapo, Baba Mtakatifu amesikiliza shuhuda za wafungwa, wahudumu wa wafungwa pamoja na watu wa kujitolea kutoka Jimbo kuu la Barcellona. Kila mtu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, anapendwa na Mwenyezi Mungu na kwamba, huruma na upendo wa Mungu unadumu milele kwa waja wake. Wafungwa katika shida na mhangaiko yao ya ndani, kamwe wasikate tamaa, bali wanapaswa kuinua vichwa vyao kwa Kristo Yesu, ili waonje huruma, upendo na uwepo wake wa karibu katika maisha yao. Makosa katika maisha, kamwe si utambulisho wa mtu na kwamba, Kristo Yesu ni chemchemi ya: imani, matumaini na mapendo. Watambue kwamba, kila mmoja wao, anapendwa na Mungu, kumbe, anapaswa kuota ndoto ya maboresho ya maisha, tayari kuanza upya kwa toba na wongofu wa ndani; kwa kusamehe na kusahau.
Rozari Takatifu ni muhtasari wa huruma ya Mungu katika maisha ya mwanadamu! Sala ya Rozari ni njia muafaka kabisa ya kutafakari maisha na utume wa Kristo Yesu, ili kumfahamu, kumpenda, kumfuasa na kumtumikia kwa njia ya upendo kwa jirani wenye shida na mahangaiko mbalimbali wanaokumbukwa katika Sala ya Rozari Takatifu. Kwa njia ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, kila mtu ajitahidi kutekeleza dhamana na wajibu wake katika mchakato wa kuponya ulimwengu, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Waamini wanaalikwa kumtaza Kristo Yesu aliyeanzisha Ufalme wa Mungu kwa ujasiri, kwa tafakuri na kwa njia ya ushuhuda wa maisha, ili kwa pamoja waweze kuujenga Ufalme wa Mungu hapa duniani ili kukuza na kudumisha haki, furaha, uponyaji na wokovu kwa wale wote wanaoteseka kwa magonjwa na kifo. Baba Mtakatifu Leo XIV Jumatano tarehe 10 Juni 2026 amesali Rozari Takatifu kwenye Abasia ya Bikira Maria Mama yetu wa Montserrat, ili kukimbilia ulinzi na tunza ya Bikira Maria sanjari na kumkabidhi maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, kwa ajili ya Kanisa na Ulimwengu katika ujumla wake; sanjari na kuombea haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mataifa. Umati wa waamini waliohudhuria ni ushuhuda wa imani yao inayobubujika kutoka katika Damu Azizi ya Kristo Yesu, chimbuko la toba na wongofu wa ndani, kama ilivyotokea kwa Mtakatifu Inyasi wa Loyola; mwanzo wa maisha mapya na huduma kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Huu ni mwaliko wa kusikiliza sauti ya Kristo na kutenda kwa ari na moyo mkuu mintarafu tunu msingi za Kiinjili. Ni mwaliko wa kumwilisha Injili ya upendo, ili kukuza na kudumisha haki, amani na maridhiano; kwa kuendelea kupyaisha maisha na utume kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Waamini katika shule ya Bikira Maria wajifunze kutafuta na kudumisha amani; kukuza upendo kwenye familia, maeneo ya kazi, kwenye mitandao ya kijamii na katika medani mbalimbali za maisha, ili hatimaye chuki na uhasa vitoe nafasi kwa Injili ya matumaini na amani!
Baba Mtakatifu Leo XIV, Jioni Jumatano tarehe 10 Juni 2026 amekutana na kuzungumza na wafanyakazi wa Mashirika ya Misaada na Ustawi wa Jamii wa Jimbo kuu la Barcellona. Katika hotuba yake amekazia umuhimu wa michezo kama sehemu ya maboresho ya akili na mwili na kwamba, waamini wajenge na kudumisha urafiki na Kristo Yesu kwa njia ya: Sala, Tafakari, Sakramenti na matendo ya huruma: kiroho na kimwili, kama njia ya kushiriki utume wa Kristo Yesu katika: kuganga, kuponya, kusamahe na kuwafufua wafu. Waamini wajenge utamaduni wa kusamehe na kusahau, kama sehemu ya mchakato wa kuondoa chuki, hasira na kinyongo kutoka katika sakafu ya nyoyo zao na badala yake yake, wajitahidi kumwilisha Injili ya upendo kwa wote; wajitahidi kutafuta, ustawi na maendeleo kwa jirani, kwa kutambua kwamba, wote ni ndugu wamoja. Upendo wa Kiinjili unapata chimbuko lake kutoka kwa Kristo Yesu, usaidie kupyaisha maisha na utume wa Kanisa katika medani mbalimbali za maisha ya mwanadamu kama alivyojitambulisha mwenyewe Rej. Mt 25:40. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, upendo ndiyo amri kuu ya kijamii inayoheshimu wengine na haki zao msingi; inayotenda haki na kusukuma maisha ya kujisadaka kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengine. Rej. KKK 1889. Huu ni mwaliko kwa waamini kuwa ni vyombo na mashuhuda wa haki na amani upendo na mshikamano; mambo wanayopaswa kuyaboreshwa kwa njia ya: Sala, Neno la Mungu na Sakramenti za Kanisa kama kielelezo cha ukuaji na ukomavu wa imani inayomwilishwa katika matendo mema na adiili.
Kanisa linaadhimisha Jubilei ya Miaka 100 tangu Mtumishi wa Mungu Antoni Gaudì Cornet alipofariki dunia. Kazi yake inayojulikana zaidi ni Kanisa la Malipizi ya Dhambi la “Sagrada Familia.” Antonio Gaudí Cornet, aliyezaliwa tarehe 25 Juni 1852, pengine huko Reus, alikubali kusimamia ujenzi wa Kanisa hili mwaka mmoja mara baada ya kuwekwa kwa jiwe la msingi, kunako mwaka 1883, akiwa na umri wa miaka 31. Tangu wakati huo na kuendelea, alijisadaka maisha yake yote kwa ajili ya ujenzi wa Kanisa hili, Nyumba ya Ibada, ambapo alionesha ujuzi wake wa kisanii, hisia zake za maisha ya kiroho na kidini. Kanisa hili kubwa limebuniwa kama safari ya kiroho inayosimulia maisha, mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu. Jiwe la msingi liliwekwa rasmi tarehe 19 Machi 1882 na kutabarukiwa na Baba Mtakatifu Benedikto XVI mwaka 2010 na kwamba, ujenzi wa Kanisa hili bado unaendelea, ili kuwakumbusha waamini kwamba, maisha ya Kikristo ni safari endelevu kama sehemu ya utekelezaji wa mpango wa Mungu. Ni kielelezo cha umoja, amani na utulivu; Nyumba ya Mungu, mahali pa sala kwa wadhambi, Msalaba unakuwa ni ufunuo wa huruma, upendo na msamaha wa Mungu. Kristo Yesu akishainuliwa juu ya Msalaba, utu na heshima ya binadamu vinang’ara na kwamba, hii ni kazi ya imani na sanaa vinavyosimama pamoja. Kanisa hili ni: “Biblia pauperum” yaani “Biblia ya Maskini” inayobeba amana na utajiri mkubwa katika mchakato wa Uinjilishaji. Hili ni Kanisa refu kuliko Makanisa yote Ulimwenguni, dir ana mwongozo kwa watu wa Mungu wanaofanya hija ya maisha ya kiroho, huku wakiwa na taa zao mikononi wakimsubiri Bwana arusi. Baba Mtakatifu Leo XIV amebariki Mnara wa Kristo Yesu na baadaye aewabariki watu wa Mungu waliohudhuria katika Ibada hii ya Misa Takatifu.
