Hija ya 4 ya Kitume ya Papa Leo XIV Hispania: Ekaristi Takatifu, Vijana na Utamaduni
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Leo XIV kuanzia tarehe 6 hadi 12 Juni 2026 anafanya Hija ya 4 ya Kitume nchini Hispania kwa kunogeshwa na kauli mbiu: "Alzad la mirada" Yaani "Inueni macho yenu.” Yn 4:35. Maadhimisho ya Sherehe ya Mwili na Damu ya Kristo, yaani Ekaristi Takatifu: “Corpus Domini” kwa lugha ya Kilatini. Dominika tarehe 7 Juni 2026 imekuwa ni fursa makini kwa waamini kutangaza na kushuhudia imani ya Kanisa kuhusu Fumbo la Ekaristi Takatifu, yaani uwamo wa Kristo katika maumbo ya Mkate na Divai. Mababa wa Kanisa wanathibitisha kwamba, kwa nguvu ya imani ya Kanisa na uwezo wa Neno la Kristo Yesu, na tendo la Roho Mtakatifu, kwamba, mageuzo ya Mkate na Divai yanakuwa ni Mwili na Damu Azizi ya Kristo. Huu ni mwaliko kwa waamini kupyaisha imani yao katika Fumbo hili kuu la Ekaristi Takatifu, kwa kuunganisha sauti za nyimbo kama kielelezo cha moyo wa shukrani, kwa uwepo angavu wa Kristo Yesu katika Kanisa lake.
Ni wito kwa waamini kushiriki kikamilifu katika kazi ya ukombozi, kwani Mwenyezi Mungu kwa wingi wa baraka na neema zake ni Mhusika mkuu, lakini anategemea pia ushiriki wa waamini katika kuganga na kuponya magonjwa ya waamini kiroho na kimwili. Kristo Yesu ni daktari wa roho na mwili! Baba Mtakatifu Leo XIV amesema, Maadhimisho ya Sherehe ya Ekaristi Takatifu ni fursa ya kuzama zaidi katika imani katika Fumbo la Ekaristi Takatifu na hivyo kuendelea kupyaisha upendo kwa Ekaristi Takatifu chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Nchini Hispania Sherehe hii ni kiini cha maisha ya waamini, upyaisho wa upendo wa Mungu na uaminifu kwa Mungu na kwamba, maandamano ya Ekaristi Takatifu ni kielelezo cha imani ya Kanisa juu ya uwamo wa Kristo katika maumbo ya Mkate na Divai, tayari kuwalisha waja wake kwa chakula cha uzima wa milele. Ndiye yule yule Kristo Yesu aliyejitambulisha na maskini, wanyonge na wale waliosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii, ndiye pia chemchemi ya Injili ya upendo, tayari kuleta mageuzi na hivyo kuwafanya kuwa ni wajenzi wa Ulimwengu mpya.
Daima wakumbuke kwamba, kwa muda wa miaka 40 Waisraeli walitangatanga Jangwani, changamoto na mwaliko kwa waamini katika Ulimwengu mamboleo, kutoanguka na kutumbukia katika vishawishi vya watu wa Agano la Kale. Hispania haina budi kubaki katika shule inayotoa kipaumbele cha kwanza kwa uwepo wa Mungu na upendo wa jirani; na shule ya ukarimu tayari kusimama kidete kulinda na kudumisha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kujenga utamaduni wa Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu, kama kielelezo cha shukrani na upendo na matokeo yake, Kristo Yesu anazima: Kiu ya upendo, haki, amani na furaha ya kweli, tayari kuwakirimia wengine Injili ya matumaini, wale wote waliovunjika na kupondeka moyo!
Baba Mtakatifu Leo XIV baada ya kusikiliza shuhuda kutoka katika wajenzi wa mitandao na Ulimwengu wa utamaduni, sanaa, uchumi na michezo: “Building Networks with the Worlds of Culture, Art, the Economy and Sport”, amekazia umuhimu wa wajumbe hawa kujikita katika majadiliano yatakayo dumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu na kwamba, hakuna jambo lililo na hali halisi ya kibinadamu lisiloligusa Kanisa. Gaudium et spes, 1. Utamaduni ni eneo muhimu sana na uwepo wa Kanisa na Wakristo binafsi na kwamba, utamaduni ni kitu ambacho kwa njia yake binadamu, kama binadamu, anakuwa binadamu zaidi, na ana nafsi zaidi ya kukua kuwa binadamu. Ujenzi wa mitandao ni sehemu ya mchakato wa ujenzi wa umoja, ni kuhudumia bila ya kujibakiza na kwamba, wana michezo wanayo dhamana ya ujenzi wa mshikamano na mafungamano ya kijamii; haki, amani na umoja, daima utu, heshima na haki msingi za binadamu vikipewa kipaumbele cha kwanza na kwamba, kazi ni chemchemi ya matumaini kwa watu wengi.
Mwelekeo wa maisha na utume wa Kanisa katika masuala ya: kiuchumi, kijamii, kisiasa na maisha ya kiroho, miongoni mwa vijana yasaidie mchakato wa uinjilishaji mpya miongoni mwa vijana wa kizazi kipya dhidi ya matumizi haramu ya dawa za kulevya; kwa kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini na kiekumene; kwa kushikamana dhidi ya biashara ya binadamu na utumwa mamboleo pamoja na uhamiaji wa shuruti! Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Leo XIV, Jumamosi usiku tarehe 6 Juni 2026 emefanya mkesha na vijana wa kizazi kipya kutoka Hispania pamoja na kusikiliza shuhuda zao! Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wake wa Kitume “Gaudete et exsultate” yaani “Furahini na kushangilia, wito wa utakatifu katika ulimwengu mamboleo” (Mt. 5:12) anasema kwamba, Kristo Yesu anawaalika wote wanaoteseka au kudhulumiwa kwa ajili yake, kufurahi na kushangilia, kwani yeye ni chemchemi ya maisha na furaha ya kweli. Mwenyezi Mungu anataka waja wake kuwa kweli ni watakatifu, mwaliko na changamoto inayojionesha kutoka katika sehemu mbali mbali za Maandiko Matakatifu. Baba Mtakatifu anasema, lengo la wosia huu ni mwaliko wa kuwa watakatifu katika ulimwengu mamboleo; kwa kutambua vizingiti, changamoto na fursa ambazo zinaweza kutumiwa na waamini kufikia utakatifu wa maisha. Kristo Yesu anawaalika waja wake ili wawe watakatifu, watu wasiokuwa na hatia mbele zake katika upendo. (Rej. Ef. 1:4).
Baba Mtakatifu Leo XIV amewaambia vijana kwamba, katika maisha na utume wake, amevutiwa sana na watakatifu watatu: Mtakatifu Yohane Krisostom aliyesema kwamba ili mtu aweze kuondoa utu wa zamani na kuvaa utu mpya, safari ya mtu huyo ya wokovu, inayojumuisha kutubu, kusali, kusamehe, kufanya matendo ya huruma (sadaka) na kuwa na unyenyekevu, mambo ambayo ni endelevu katika maisha. Mtakatifu Thomas wa Villanueva, Askofu kutoka Shirika la Waagustiniani, alijikita katika kupyaisha maisha ya kiroho na mwili ya waamini wake, akajitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya maskini na wahitaji zaidi; alikazia toba na wongofu wa ndani, alitambulikana kwa hekima na utakatifu wa maisha yake kwa kujikita katika maisha ya sala, usafi kamili, utii na ufukara, mambo ambayo yamemtia moyo wakati wa majaribu katika maisha na utume wake. Mtakatifu Toribio Alfonso de Mogrovejo Askofu wa Jimbo Katoliki la Lima, nchini Perù, alitangaza Habari Njema ya Wokovu, akafundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu; akajenga Makanisa, Shule na Hospitali kwa ajili ya kumhudumia mtu mzima: kiroho na kimwili.
Katika maisha na utume wake Papa Leo XIV anasema, ameshuhudia imani ya watu wa Mungu, Habari Njema ya Wokovu ikawa ni chemchemi ya haki, amani na upatanisho na kwamba, ukweli unadumu daima. Vijana wakuze na kudumisha moyo wa sala, kusoma, kutafakari na kumwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha yao; Kuabudu Ekaristi Takatifu pamoja na kushiriki kikamilifu katika Maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa, daima wakijitahidi kumfuasa Kristo Yesu: Mchungaji mkuu, Mwalimu na Rafiki wa kweli. Vijana wawe tayari kuwashirikisha vijana wengine shuhuda za imani yao kwa Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Chumvi ni kielelezo cha utukufu, utakatifu, huruma na upendo wa Mungu unaoganga na kuponya udhaifu na mapungufu ya binadamu. Kumbe, vijana wanaitwa na kutumwa kuwa ni chumvi na nuru ya ulimwengu kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto, kielelezo makini cha imani tendaji.
Vijana wanaalikwa kuwa ni chumvi ya ulimwengu kwa kutambua kwamba kwa kuzaliwa katika Maji na Roho Mtakatifu, Wabatizwa wote wamewekwa wakfu kuwa ni Makuhani, Manabii na Wafalme ili kumtolea Mwenyezi Mungu dhabihu ya sifa na shukrani; kutangaza fadhila za Mungu, ili kuwaita watu watoke gizani na kuingia katika nuru yake ya ajabu, kwa kujitoa wenyewe ili waweze kuwa ni sadaka safi na yenye kumpendeza Mwenyezi na kumshuhudia Kristo Yesu popote pale walipo kama majibu ya habari za tumaini na uzima wa milele lililoko ndani mwao. Rej. Lumen gentium, 9-11. Vijana wanaitwa na kutumwa kumshuhudia Kristo Yesu hata katika Ulimwengu wa Kidigitali, ili vijana waonje na kuguswa na tunu msingi za Kiinjili; wawe ni mashuhuda wa haki, amani na maridhiano katika maisha; Wawe ni mashuhuda na vyombo vya ujenzi wa Ukristo na utu wema; wawe ni wamisionari wa Habari Njema ya Wokovu; watambue vyema imani yao tayari kuitangaza na kuishuhudia miongoni mwa watu wa Mataifa.
Jioni tarehe 6 Juni 2026 Baba Mtakatifu Leo XIV ametembelea Kituo cha “Cedia 24 Horas” Social Project Information and Welcome Center, Madrid”: “Cedia 24 Horas Social Project” kinachoendeshwa na kusimamiwa na Shirika la Misaada la Kanisa Katoliki nchini Hispania, Caritas. Hii ni sehemu muhimu sana ya huduma za kijamii zinazotolewa na Kanisa Katoliki nchini Hispania. Ni mahali pa watu kupata ushauri nasaha, msaada wa kisaikolojia na kwamba, hapa maskini wa Jiji na Madrid wanaweza kupata huduma msingi, ili kukuza na kudumisha utu, heshima na haki zao msingi. Kanisa linajengwa na waamini wanaosimama kidete kulinda, kutetea na kushuhudia tunu msingi za maisha ya Kikristo, kama kielelezo makini cha imani tendaji na sehemu muhimu ya kuyatakatifuza malimwengu kwa chachu ya Injili. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, mradi huu ni kielelezo cha mshikamano wa Kristo Yesu na binadamu dhaifu katika mambo yote isipokuwa dhambi. Kituo hiki ni chemchemi ya maisha mapya yanayosimikwa katika Injili ya matumaini, utu, heshima, haki msingi za binadamu; uhuru pamoja na heshima kwa tunu msingi za utu wa binadamu. Hiki ni kipindi cha neema na baraka, ili kuonja mabadiliko ya ndani yanayobubujika kutoka katika upendo wa Kristo, kama kielelezo cha imani inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili, ushuhuda wa moyo wenye upendo unaosimikwa katika utamaduni wa kusikiliza, kujali na kutenda.
