Hija ya 4 ya Kitume ya Papa Leo XIV Hispania: Bunge, Maaskofu, Maria na Jumuiya
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Leo XIV kuanzia tarehe 6 hadi 12 Juni 2026 anafanya Hija ya 4 ya Kitume nchini Hispania kwa kunogeshwa na kauli mbiu: "Alzad la mirada" Yaani "Inueni macho yenu.” Yn 4:35. Baba Mtakatifu Leo XIV, Jumatatu tarehe 8 Juni 2026 amekutana na Waziri mkuu wa Hispania Pedro Sánchez Pérez-Castejón, ambaye amekuwa madarakani tangu tarehe 2 Juni 2018 na ndiye kiongozi mkuu wa Serikali ya Hispania, Papa pia amekutana na kuzungumza na Bunge la Hispania na baadaye amepata nafasi ya kukutana na kuzungumza na Baraza la Maaskofu Katoliki Hispania na baadaye jioni wakakutana kwa sala na Ibada kwa Bikira Maria Mama wa Almudena “Santa María de la Almudena” ambaye ni Mlinzi na Mwombezi wa Jimbo kuu la Madrid, Hispania na kila mwaka ifikapo tarehe 9 Novemba, anakumbukwa na Mama Kanisa nchini Hispania. Baadaye usiku, Baba Mtakatifu Leo XIV amekutana na kuzungumza na Jumuiya ya Jimbo kuu la Madrid, Hispania, Waswahili wanasema, siku hii ilikuwa “full shangwe.”
Baba Mtakatifu Leo XIV katika hotuba yake kwa Bunge la Hispania, ameitaka Hispania kuendelea kuwa ni mahali pa watu kukutana, katika utamaduni ili hatimaye, kujenga mshikamano wa udugu wa kibinadamu, chemchemi ya Injili ya matumaini. Amekazia utu, heshima, haki msingi za binadamu, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi kwa kuongozwa na kauli mbiu ya Umoja wa Ulaya “In varietate concordia” yaani “Umoja katika Utofauti” kwa kusimikwa katika tofauti za tamaduni, mapokeo na vipaumbele tofauti; mambo ambayo kwa pamoja yanaunda amana na utajiri mkubwa wa watu wa Mungu nchini Hispania. Mama Kanisa anatembea bega kwa bega na binadamu, anashiriki matumaini na madonda yake, anaendelea kusikiliza na kujibu maswali msingi ya binadamu wa kila nyakati na kwamba, kuna tofauti ya utendaji kati ya Kanisa na Serikali; na kwamba, utu, heshima na haki msingi za binadamu ni mambo yanayopaswa kupewa kipaumbele cha kwanza, kwa kuzingatia kwamba, uhuru ni zawadi kubwa ambayo Mwenyezi Mungu amemkirimia mwanadamu.
Kumbe, kuna uhusiano mkubwa kati ya sheria, kanuni maadili na utu wema na kwamba, kimsingi uongozi unabeba dhamana kubwa ya haki na uwajibikaji. Ndiyo maana hata katika ulimwengu mamboleo bado: Utu, heshima, haki msingi za binadamu; ustawi, maendeleo na mafao ya wengi ni vigezo msingi katika kupima mahusiano na mafungamano ya kijamii katika ngazi ya Kitaifa na Kimataifa. Leo hii kuna changamoto mamboleo kutokana na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia, uchumi, tafiti na tiba; ulimwengu wa kidigitali unaogusa maisha ya mtu binafsi na jamii katika ujumla wake na kwamba, maendeleo makubwa ya teknolojia ya akili unde hayana budi kudhibitiwa kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa binadamu, anayepaswa kuongoza maoni na maamuzi mintarafu: kazi, mshikamano, siasa za kijamii; ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Jamii inayosimikwa katika msingi wa haki inatambua na kuthamini utu wa binadamu unaotishiwa na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine.
Kumbe, kuna haja ya kusimama kidete kulinda, kutangaza na kudumisha: tunu msingi za ndoa na familia sanjari na Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo na kwamba, mafao ya wengi kwa namna nyingine ni sehemu ya utu wa binadamu. Vijana wa kizazi kipya wafundishwe kutafuta na kupenda ukweli; watu waondokane na tabia ya ubaguzi na maamuzi mbele, wajitahidi kujenga haki jamii. Sera na mikakati ya Kanisa Katoliki kwa ajili ya wakimbizi na wahamiaji inajikita katika misingi mikuu minne: Kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwahusisha. Mwongozo huu unalenga kutetea utu, kuzuia nyanyaso na kuleta mshikamano kupitia huduma za kiroho na kijamii. Wakimbizi na wahamiaji ni watu waokosa haki, amani na usalama; ni watu wanaosiginwa na umaskini, njaa, maradhi sanjari na athari za mabadiliko ya tabianchi, mwaliko ni ujenzi wa utamaduni wa mshikamano wa dhati.
Ili kukuza na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano anasema Papa Leo XIV kuna haja ya kuheshimiana na kuthaminiana. Ulimwengu umekumbwa na mgogoro wa maisha ya kiroho na kitamaduni; mambo yanayojionesha katika vita, kinzani na mipasuko ya kijamii, kumbe, kuna haja ya kujenga na kudumisha utamaduni wa watu kukutana na kujadiliana; kuheshimiana na kuthaminiana kama binadamu; kwa kujikita katika diplomasia na sheria za Kimataifa na kwamba, kuna haja ya kujenga utamaduni wa amani ya kudumu bila kukimbilia vita kama suluhu ya matatizo na changamoto za maisha ya binadamu. Mwanadamu anapaswa kuwajibika kutokana na matendo yake. Jumuiya ya Kimataifa liwe ni jukwaa la majadiiano ya kina katika ukweli na uwazi. Demokrasia ya kweli inaheshimu: uhuru wa mawazo, uhuru wa dhamiri na uhuru wa kidini na kwamba, waamini wa dini mbalimbali wanapaswa kutangaza na kushuhudia imani yao katika maisha ya hadhara na yale ya binafsi. Siri ya maungamo kwa Kanisa Katoliki ni muhimu sana. Mageuzi ya sheria na teknolojia yanahitaji pia kusimikwa katika kanuni maadili na utu wema, ili kujenga na kudumisha jamii inayosimikwa katika haki na amani.
Baba Mtakatifu Leo XIV akizungumza na Baraza la Maaskofu Katoliki Hispania “Conferencia Episcopal Española (CEE)” lililoanzishwa kunako mwaka 1966 na kwamba, Mwaka huu linasherehekea kumbukizi ya miaka 60 tangu kuanzishwa kwake amekazia ujenzi wa umoja na ushirika wa Kanisa, unaoweza kukusanya karama na zawadi mbalimbali za Roho Mtakatifu na kuzitumia kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa nchini Hispania. Maaskofu wawe ni kiungo makini cha ushirika na nguvu ya kimisionari, kwa kuendelea kutangaza na kushuhudia ukweli, haki na kwamba, waendelee kujikita katika ujenzi wa Kanisa la Kimisionari na Kisinodi kwa kujadiliana, kusikilizana, kuamua na kutekeleza mambo msingi katika umoja, ili kukuza na kudumisha: ukweli, haki, toba, wongofu wa ndani, utakaso na msamaha wa kweli. Kwa wale wote waliojeruhiwa wapate jukwaa la kuwasikiliza, kuwaganga na kuwaponya. Neno la Mungu, Sala na Ekaristi Takatifu ni mambo msingi katika kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, ni mwaliko wa kuendelea kujifunza lugha mpya, kushirikishana tajiriba na kwamba, shughuli za kichungaji kwa ajili ya miito ni ushuhuda wa Injili inayomwilishwa katika furaha, huduma na ujenzi wa umoja na ushirika, kwa kusikilizana na kuthaminiana. Maaskofu wawe ni mashuhuda wa ushirika na Kristo Yesu, kwa kulinda na kudumisha upendo na imani waliyoipokea; wawe wanyenyekevu katika kulisikiliza Neno la Mungu sanjari na kutunza Mapokeo ya Mama Kanisa.
Maaskofu wajenge umoja na ushirika na Khalifa wa Mtakatifu Petro na Kanisa la Kiulimwengu; Askofu ajenge ushirika na Mapadre na waamini wa jimbo lake. Maaskofu wawe ni vielelezo vya umoja na majadiliano, tayari kuwasindikiza waamini walei katika maisha na utume wao na kwamba, Majandokasisi wana haki ya kupata malezi na majiundo makini katika maisha na utume wao, tayari kujenga Jumuiya inayosimikwa katika: Utamaduni wa kusikiliza, ukweli, haki, amani; utakaso, utunzaji pamoja na kuzuia kashfa. Kanisa ni Mama wa ushirika na chemchemi ya matumaini na kwamba, nguvu yake kuu ni utakatifu wa maisha unaopata chimbuko lake kutoka katika Mafundisho yake tanzu; ari na mwamko wa shughuli za kichungaji na upendo kwa shughuli za kitume.
Baba Mtakatifu Leo XIV katika Sala na Ibada kwa Bikira Maria Mama wa Almudena “Santa María de la Almudena” ambaye ni Mlinzi na Mwombezi wa Jimbo kuu la Madrid, Hispania na kila mwaka ifikapo tarehe 9 Novemba, anakumbukwa na Mama Kanisa nchini Hispania ameweka shada la maua ya dhahabu kuonesha upendo wake kwa Mama Bikira Maria na kwamba, uwepo wake ni mwaliko kwa waamini kubomoa kuta za utengano na kwamba, kwa uwepo wake mwanana kuna wahakikishia waamini ulinzi na usalama; anawasikiliza na kuwajibu katika shida, mahangaiko na matumaini yao, changamoto na mwaliko kwa waamini kumtolea ushuhuda wa maisha yao, ili hatimaye, kuweza kutafakari Mpango wa upendo wa Mungu kwa mwanadamu. Upendo kiwe ni kiungo cha watu wa Mungu nchini Hispania, ili kuendelea kupyaisha matumaini sanjari na kuimarisha upendo wao kwa Kristo Yesu pamoja na Kanisa lake. Waamini wawe ni wajenzi wa ushirika, upendo wa kidugu, amani na utulivu.
Baadaye usiku, Baba Mtakatifu Leo XIV amekutana na kuzungumza na Jumuiya ya Jimbo kuu la Madrid, Hispania, Waswahili wanasema, siku hii ilikuwa “full shangwe.” Katika hotuba yake amekazia umuhimu wa watu wa Mungu kujenga na kudumisha Jumuiya ya waamini, kwa njia ya Liturujia, tunu msingi za Kiinjili na kwamba, upendo wa Kristo “Maana, upendo wa Kristo watubidisha.” 2 Kor 5:14. Huu ni mwaliko wa ujenzi wa Jumuiya yao kwa pamoja kwa kujikita katika kusikiliza na kujadiliana; kwa kushiriki ujenzi wa Kanisa la Kisinodi na Kimisionari; kwa kusoma, kulitafakari na hatimaye kulimwilisha Neno la Mungu katika uhalisia na vipaumbele vya maisha; kwa kujenga na kudumisha umoja na ushirika, ili kuondokana na upweke hasi katika maisha na kwamba, Baba Mtakatifu anawahamasisha waamini kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa na kwamba, upendo ni kiungo kinachomfanya kila mtu kujisikia yuko nyumbani!
