Tafuta

2026.06.10 Padre Faustine John Mlelwa(OSA)akiwa ameshika Msalaba wakati Papa Leo XIV anaingia katika Parokia ya Mtakatifu Agostino,Barcelona. 2026.06.10 Padre Faustine John Mlelwa(OSA)akiwa ameshika Msalaba wakati Papa Leo XIV anaingia katika Parokia ya Mtakatifu Agostino,Barcelona.  (@Vatican Media)

Barcelona,Pad.F.John Mlelwa:'Ziara ya Papa inatutia moyo kwa ajili ya hudumu ya kichungaji'

Padre Mlewa,Mtawa wa Shirika la Mtakatifu Agostino kutoka Tanzania alielezea safari yake ya upadre na utume wake ulimwenguni hadi Barcelona,Hispania.Papa Leo XIV alitembelea Parokia ya Mtakatifu Agostino Juni 10, ambayo yeye ni Paroko na kufanya mkutano na Mashirika ya Upendo ya Barcelona.Katika Parokia hiyo pamoja na wenzake wanahudumia wakimbizi na wahamiaji kutoka Afrika,Asia na Amerika ya Kusini kupitia huduma ya chakula na misaada ya kijamii.”

Na Sr. Christine Masivo,CPS,Paul Samasumo na Angella Rwezaula–Vatican.

Katika siku yake ya tano ya ziara yake ya kitume nchini Hispania tarehe 10 Juni 2026 alasiri, Baba Mtakatifu Leo XIV alitembelea Kanisa la Mtakatifu Agostino, linalojulikana sana kama "Kanisa Kuu la Maskini," katika kitongoji cha wafanyakazi cha El Raval, katikati ya Ciutat Vella, mji wa zamani wa Barcelona. Baba Mtakatifu alikutana na mashirika ya upendo na ustawi ya Jimbo Kuu  hilo ambapo alisikiliza ushuhuda wa wafanyakazi watatu.

Papa Leo XIV alifanya Mkutano na Mashirika ya Upendo,Barcelona
Papa Leo XIV alifanya Mkutano na Mashirika ya Upendo,Barcelona   (@Vatican Media)

Kabla ya Mkutano huo, vyombo vya Habari vya  Vatican, vilifanya mahojiano na Paroko wa Parokia hiyo, ambaye ni Padre Faustine John Mlelwa, anatoka Tanzania, Parokia ya Mavanga, Jimbo Katoliki la Njombe. Yeye ni miongoni mwa mapadre wa Shirika la Mtakatifu Agostino wanaotoa huduma ya kichungaji katika Parokia hiyo, na amekuwa katika huduma ya upadre kwa takribani miaka thelathini tangu upadrisho wake mwaka 1996.

Akielezea historia yake, alibainisha kuwa baada ya kufanya utume wake nchini Tanzania alihudumu kama misionari nchini Peru, kwa miaka saba na baadaye alihamishiwa Barcelona, Hispania, katika mchakato wa kubadilishana mapadre kati ya majimbo kutokana na changamoto za upatikanaji wa mapadre wazawa, hasa kwa kazi za kichungaji katika mazingira ya mijini na jamii mchanganyiko.

Parokia inahudumia wakimbizi wengi sana
Parokia inahudumia wakimbizi wengi sana   (@Vatican Media)

Huduma kwa Wakimbizi na Jamii ya Wahamiaji

Akiwa Barcelona, Padre Mlelwa alisimulia jinsi alivyoanza kama Paroko msaidizi kabla ya kuteuliwa kuwa Paroko wa Parokia yake ya sasa, na ambapo amehudumu kwa takribani miaka minne. Huduma yake huko Barcelona alisema, “inalenga zaidi wakimbizi na wahamiaji kutoka maeneo mbalimbali duniani. Jumuiya  anayohudumia inajumuisha watu kutoka Amerika Kusini kama vile:  Peru, Bolivia, Paraguay na Ecuador, pamoja na wengine kutoka Afrika Kaskazini na Asia, hasa Pakistan na Ufilipino.”

Watawa wa Mama Teresa wa Kalkuta wanahudumu katika Parokia ya Mt.Agostino
Watawa wa Mama Teresa wa Kalkuta wanahudumu katika Parokia ya Mt.Agostino   (@Vatican Media)

Parokia yake inafanya kazi kwa kushirikiana na mashirika ya kidini na kijamii, likiwemo miongoni mwa hayo Shirika la Masista wa Upendo la Mtakatifu Teresa wa Kalkuta ambao wanapika na kugawa chakula kwa mamia ya watu kila siku. Padre alisimulia kwamba “kila Jumatano, Parokia hupanga ugawaji wa chakula kwa wahitaji kupitia mfumo wa msaada wa moja kwa moja. Huduma hii inalenga kuhakikisha kwamba hakuna mtu anayebaki bila chakula, bila kujali dini au asili yake.”  Kanisa linasisitiza utoaji wa huduma bila ubaguzi, likiwahudumia Wakristo, Waislamu na watu wote wasio na imani sawa.

Padre Faustine John Mlelwa(OSA) akielezea safai yake na utume wake Barcelona

Changamoto na Matarajio ya Kijamii na Kikanisa

Padre Faustine kadhalia  alieleza kuwa “mazingira ya kazi Barcelona yana changamoto kubwa, ikiwemo hali ngumu ya maisha ya wakimbizi, usalama mdogo maeneo fulani, na changamoto za kijamii kama matumizi ya dawa za kulevya na ukosefu wa makazi.” Hata hivyo, alisisitiza kuwa utume wake “ni wa utii na huduma, bila kujali mazingira.”

Papa akiwa katika Parokia ya Mtakatifu Agostino
Papa akiwa katika Parokia ya Mtakatifu Agostino   (@Vatican Media)

Akiendelea kufafanua zaidi alieleza pia matumaini makubwa ya ziara ya Baba Mtakatifu katika eneo hilo, ambayo inalenga kuhamasisha wahudumu wa kijamii na kuwatia moyo “kuendelea na huduma kwa wahitaji. Ni Matarajio ya Padre  Mlelwa  kwamba “Ziara hiyo inatarajiwa kuonesha mshikamano wa Kanisa na watu maskini na wakimbizi, na  kuimarisha wito wa huruma na upendo katika jamii ya Barcelona na Kanisa kwa ujumla.”

Huduma ya Kichungaji kwa wakimbizi katika Parokia ya Mtakatifu Agostino
Huduma ya Kichungaji kwa wakimbizi katika Parokia ya Mtakatifu Agostino   (@Vatican Media)
Padre Faustine John Mlelwa(OSA)-Barcelona

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku. Just click here

 

11 Juni 2026, 09:30