Tafuta

Askofu Vincent Cosmas Mwagala,wa Jimbo la Mafinga. Askofu Vincent Cosmas Mwagala,wa Jimbo la Mafinga. 

Ask.Mwagala:Papa anatualika tuogelee katika Bahari ya kidijitali kwa dira ya Injili

Mwanadamu ameanza kuelekea kuwa mnyonge kwa kuamini kwamba akili unde ina nguvu zaidi yake.Lakini katika Waraka huu wa Magnifica Humanitas,Baba Mtakatifu ameonesha kuwa hadhi ya binadamu haiwezi kushushwa na uwezo mkubwa wa akili unde kuchakata taarifa.Ni maoni ya Askofu Mwagala wa Jimbo Katoliki la Mafinga,Tanzania akifafanua juu ya Waraka wa kwanza wa Papa Leo XIV uliochapishwa hivi karibuni.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Waraka wa Kitume wa Papa unaendelea kuchambuliwa kwa ngazi mbali mbali ulimwenguni, kuanzia viongozi wa Kanisa, wa madhehebu mbalimbali ya kikristo na yasiyo ya kikristo, na viongozi wa taasisi za kisiasa na kijamii, kwa sababu Waraka huu wa  "Magnifica Humanitas" ni  wa watu wote, bila kubagua mtu yeyote katika jamii.  Katika uchambuzi wa kina wa  Askofu Vincent Cosmas Mwagala wa Jimbo Katoliki la Mafinga  nchini Tanzania, akizungumza na vyombo vya habari vya Radio Vatican- Vatican News, anasisitiza kuwa, wazo la Papa Leo XIV ni kwamba “Teknologia inabeba sura, tunu na matamanio ya yule anayeibuni, anayeigharimia, anayeiratibu na anayeitumia” na kwamba “wazo hili la Baba Mtakatifu ni la kweli kabisa kwani mabadiliko ya teknolojia yamekuwa na athari chanya na hasi kwa mtu. Ili kupunguza athari hasi, maendeleo ya teknolojia yanapaswa kuongozwa na kanuni za ‘ruzuku’ ‘mshikamano’ na ‘utafutaji wa mema ya pamoja.’ Ufuatao ni uchambuzi wake  wa Askofu Mwagala kuhusu Waraka huu wa Baba Mtakatifu Leo XVI.

Waraka wa Kitume wa Papa Leo XIV
Waraka wa Kitume wa Papa Leo XIV   (@Vatican Media)

"Baba Mtakatifu anataka tuelewe taratibu na taarifa za AI"

Waraka huu wa Kitume wa “Magnifica humanitas” wa Baba Mtakatifu Leo XIV, iliosainiwa tarehe 15 Mei 2026 na kuzinduliwa rasmi tarehe 25 Mei 2026, wakati wa kumbukizi ya miaka 135 ya Waraka wa Kitume wa Papa Leo XIII, wa “Rerum novarum” unalenga kumtetea na kumlinda mtu kwa njia ya mafundisho  Jamii ya Kanisa. Kwa Waraka huu Kanisa linatimiza wajibu wake wa kinabii wa kusoma alama za nyakati katika mwanga wa Injili.  Kwa Waraka huu Kanisa linataka kumlinda mtu dhidi ya tishio la uimla (dictatorship) wa ulimwengu wa kidijitali na akili unde (artificial intelligency). Mwanadamu ameanza kuelekea kuwa mnyonge kwa kuamini kwamba akili unde ina nguvu zaidi yake. Lakini kwa Waraka huu, Baba Mtakatifu  Leo XIV ameonesha kuwa hadhi ya binadamu haiwezi  kushushwa na uwezo mkubwa wa akili unde (AI) kuchakata taarifa.  Baba Mtakatifu ametaka tuelewe kuwa mtu anayeziingiza taratibu taarifa kwenye akili unde ana thamani zaidi kuliko hiyo akili unde inayozichakata kwa kasi kubwa.

"Waraka wa Papa umeganyika katika sehemu 5 msingi"

Kama tunavyoweza kuona, Baba Mtakatifu Leo XIV amegawanya Waraka wake  katika: utangulizi, sura msingi tano na hitimisho. Katika utangulizi akitumia mifano miwili ya kibiblia yaani ujenzi wa mnara wa Babeli na kujengwa upya kwa mji wa Yerusalemu kulikoongozwa na Nehemia, Baba Mtakatifu Leo XIV anatutaka kama Kanisa tuchague kati ya kujenga Babeli kunakolazimisha umoja usioheshimu tofauti na kujenga Yerusalemu kunakoheshimu utofauti wa mawazo; tuchague kati kubaki na mikono safi huku tukishuhudia kudhalilika kwa hadhi ya binadamu na kuwa tayari kuchafuka mikono yetu tukishiriki kuujenga mji unaomweka binadamu katikati ya kila maamuzi.

Waraka wa Kitume wa Papa Leo XIV: Magnifica Humanitas
Waraka wa Kitume wa Papa Leo XIV: Magnifica Humanitas   (@Vatican Media)

Katika sura ya kwanza Baba Mtakatifu anaweka wazi mara moja msimamo wa Kanisa juu ya teknolojia; kwamba si nguvu inayopingana na binadamu na wala kwa yenyewe haipaswi kuchukuliwa kama jambo baya. Hata hivyo, Baba Mtakatifu Leo XIV anakataa kwa nguvu kabisa kwamba, teknolojia inaweza kuwa haina uhusiano na watu. Teknologia inabeba sura, tunu na matamanio ya yule anayeibuni, anayeigharimia, anayeiratibu na anayeitumia. Wazo hili la Baba Mtakatifu ni la kweli kabisa kwani mabadiliko ya teknolojia yamekuwa na athari chanya na hasi kwa mtu. Ili kupunguza athari hasi, maendeleo ya teknolojia yanapaswa kuongozwa na kanuni za ruzuku (subsidiarity), mshikamano (solidarity) na utafutaji wa mema ya pamoja (common good). Katika sura ya Pili, Baba Mtakatifu alipenda kusisitiza juu ya hadhi ya mtu ambayo haiongozwi kwa teknolojia bali kwa Neema. Udhaifu, kutokuwa na ukamilifu na hali ya kufa ya binadamu si kasoro za kiuundaji zinazoweza kurekebishwa, bali ni hali zinazofungamana na ubinadamu wetu ili kutuingiza katika mahusiano na Mungu wetu. Hakuna teknolojia inayoweza kuzalisha au kutoa mbadala wa uzuri wa roho na msukumo wa dhamiri.

Ukuaji wa Teknolojia na uwepo wa AI usimuache mtu nje ya ajira

Katika sura ya Tatu, Baba Mtakatifu anahusianisha akili unde (AI), kazi na heshima ya kijamii. Akianza na Waraka wa  “Rerum novarum” wa  Baba Mtakatifu Leo wa XIII,  mpaka ule wa “Laborem exercens, ”yaani kazi ni wema wa mtu wa Baba Mtakatifu Yohane Paulo II,   Baba Mtakatifu Leo XIV, amedadavua kwa kina athari za akili unde (AI)  juu ya kazi kwamba: Kazi hamsaidii mtu tu kujikimu, bali ni namna pia ya kudhihirisha hadhi na heshima ya mtu huyo. Ukuaji wa teknolojia na hivi uwepo wa akili unde haupaswi kumsukumia mtu nje ya kazi au kudharau uwezo wa kufikiri wa binadamu; Baba Mtakatifu anatahadharisha juu ya hatari iliyopo ya kurundika maarifa na utajiri mikononi mwa wamiliki wa teknolojia wachache na hivi kuwanyang’anya wafanyakazi uhuru wa kimaamuzi na ubunifu wao. Baba Mtakatifu Leo XIV anamtazama binadamu kama ndiye anayetakiwa ayaendeshe maisha yake. Hatakiwi kuingizwa au kuingia kwenye utumwa wa akili unde. Anapaswa aione na aienzi hadhi aliyoumbwa nayo na Mwenyezi Mungu akiamriwa kuvitunza na kuvitiisha viumbe vyote.

Katika sura ya Nne, Baba Mtakatifu Leo XIV  anakemea matumizi ya akili unde kwenye vita. Anaialika jamii ya kimataifa kuondoa silaha kutoka katika akili unde. Kwa hakika hapa Baba Mtakatifu anaiona hatari ya kuishirikisha akili unde isiyo na dhamiri kwenye masuala ya vita. Anasema “hakuna algorithimu(mashine) inayoweza kuifanya vita iwe halali kimaadili.” Hatari nyingine katika hili ni kuwazungumzia wahanga kama namba au takwimu tu badala ya kuwatazama kama watu.  Na hili linaweza kupelekea kufanya operesheni ya kinga bila kujali wahanga hiyo operesheni.

Papa Leo  XIV akiwakilisha Waraka wake
Papa Leo XIV akiwakilisha Waraka wake   (@Vatican Media)

Katika sura ya Tano na ya mwisho Baba Mtakatifu anahimiza juu ya uwajibikaji na ustaarabu wa Upendo. Baba Mtakatifu hataki tujenge Babeli bali, tujenge upya kwa matumaini ya Yerusalemu. Na ili hili lifanikiwe, tunapawa kufanya yafuatayo: Kuyapokonya silaha maneno;  kurudi kuzungumza kwa ukweli, kuachana na taarifa za uongo zinazozalishwa na algorithimu na matamko ya chuki; Kujenga amani katika msingi wa haki  na  hakuna amani ya kweli bila kuzitambua na kuheshimu haki za msingi na usawa wa binadamu; kuwa upande wa wahanga: Baba Mtakatifu anasema mbele ya migogoro na uonevu, hatuwezi kuwa bila upande, ni lazima tuwe upande wa wahanga (wanaoumia).

Kwa “kutenda kwa uhalisia na kuingia kwenye mazungumzo badala ya kutumia nguvu.” Hapa Baba Mtakatifu Leo XIV anakemea kwa nguvu ule uhalalishaji wa ugaidi kwa kutumia dini. Anasema kuwa “anayepigana kwa kutumia jina la dini, anaishambulia dini yenyewe.” Kwa ujumla Baba Mtakatifu Leo XIV katika waraka wake huu Magnifica humanitas(MH), anatupatia mpango wa maisha ya kikristo wenye madai makubwa,  lakini uliojaa matumaini. Anatualika kama Kanisa na Jumuiya nzima ya binanamu kuogelea katika bahari hii ya kidijitali bila kupotea wala kupotezana, tukiongozwa na dira ya Injili.

Hata katika ulimwengu wa AI Binadamu anaitwa kudhihirisha ukuu wake

Hata katika ulimwengu huu wa akili unde, bado binadamu anaitwa kudhihirisha ukuu wake mbele ya viumbe wengine wote. Binadamu hapaswi kuwa wadogo mbele ya mashine zenye uwezo mkubwa  wa kuchakata taarifa kwa kasi. Tofauti ya mashine na binadamu ni kwamba wakati mashine zina uwezo wa kuchakata tu, binadamu ana uwezo wa kufikiri na kuchakata. Na binadamu anapofikiri hahusishi akili pekee bali anasukumwa dhamiri pia. Tunamshukuru sana Baba Mtakatifu Leo XIV, kwa kutupatia zawadi ya waraka wake huu wa Kinabii  katika wakati muafaka.

Askofu Mwagala wa Jimbo la Mafinga Tanzania akidadavua Waraka wa Kitume wa Papa Leo XIV
Askofu Mwagala wa Jimbo la Mafinga Tanzania akidadavua Waraka wa Kitume wa Papa Leo XIV
Askofu Mwagala kuhusu Magnifica Humanitas

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku: Just click here.

02 Juni 2026, 09:39