Tafuta

Sherehe za kuapishwa kwa walinzi 28 wa Kikosi cha Ulinzi cha Papa mjini Vatican zimeanza kwa Ibada ya Misa Takatifu Sherehe za kuapishwa kwa walinzi 28 wa Kikosi cha Ulinzi cha Papa mjini Vatican zimeanza kwa Ibada ya Misa Takatifu   (@Vatican Media)

Walinzi 28 wa Kikosi cha Walinzi wa Papa Wamekula Kiapo cha Utii

Sherehe za kuapishwa kwa walinzi 28 wa Kikosi cha Ulinzi cha Papa mjini Vatican zimeanza kwa Ibada ya Misa Takatifu iliyoongozwa na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican na kuadhimishwa kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Jioni walinzi wapya wakala kiapo cha utii mbele ya Baba Mtakatifu Leo XIV ambaye, Alhamisi tarehe 7 Mei 2026 amekutana na kuwapongeza kwa wito na utume huu: Huduma ya unyenyekevu na busara na utakatifu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kikosi cha Walinzi wa Papa kutoka Uswiss, maarufu kama “Swiss Guards” kina dhamana na utume unaojikita katika wito, uaminifu, umakini na sadaka inayotekelezwa kwa ari na moyo wa unyenyekevu pasi na makuu kwa kuongozwa na kauli mbiu “Acriter et fideliter” yaani Ujasiri na Uaminifu na kilianzishwa na Papa Giulio wa Pili tarehe 22 Januari 1506. Jumatano tarehe 6 Mei 2026 Wanajeshi 28 wa Kikosi cha Ulinzi wa Papa kutoka Uswisi, wamefanya kumbukumbu ya Askari 189 kutoka Uswisi waliofariki dunia kunako mwaka 1527 wakati wa kumlinda Khalifa wa Mtakatifu Petro, wakati huo katika nafsi ya Papa Clement VII dhidi ya Mfalme Charles V. Tangu wakati huo, hawa wamekuwa ni walinzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro mjini Vatican. Ni Askari wakakamavu, nadhifu, wapole na waungwana wanaotekeleza dhamana na wajibu wao kwa: Ari, weledi, uadilifu na uwajibikaji mkubwa kwa ajili ya Papa, Kanisa na Vatican katika ujumla wake; wanatoa huduma kwa waamini na mahujaji wanaofika mjini Vatican kwa shughuli mbalimbali! Walinzi hawa kila mwaka hula kiapo cha utii kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Maadhimisho yameanza kwa Ibada ya Misa Takatifu
Maadhimisho yameanza kwa Ibada ya Misa Takatifu   (@VATICAN MEDIA)

Sherehe hizi zimeanza kwa Ibada ya Misa Takatifu iliyoongozwa na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican na kuadhimishwa kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Jioni walinzi wapya wakala kiapo cha utii mbele ya Baba Mtakatifu Leo XIV ambaye, Alhamisi tarehe 7 Mei 2026 amekutana na kuzungumza nao. Siku hii kwa Baba Mtakatifu Leo XIV imekuwa ni fursa ya kutoa shukrani kwa Taifa la Uswisi ambapo vijana walioajiriwa na Vatican kutoka Uswisi wanaonesha ile furaha ya kutoa huduma ya unyenyekevu na busara inayotekelezwa usiku na mchana. Amezishukuru familia za vijana hawa, kwa kuwashirikisha furaha na majaribu ya maisha sanjari na kuwasindikiza, kielelezo cha urafiki unaowazunguka, heshima na wajibu wanaouonesha kwa njia ya zawadi ya uhai kwa ajili ya huduma na ulinzi kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro ambaye kwa sasa ni katika nafsi ya Baba Mtakatifu Leo XIV.

Kristo Yesu ni Mzabibu wa kweli na wao ni matawi yake
Kristo Yesu ni Mzabibu wa kweli na wao ni matawi yake   (@Vatican Media)

Maaskari hawa wanatoa huduma yao mjini Vatican na kwenye Makanisa makuu ya Kipapa yaliyoko mjini Roma. Haya ni maeneo yenye amana na utajiri mkubwa wa maisha ya kiroho na kiimani, yanayowasaidia waamini kuzama katika tafakari na sala, kwa kushangaa uzuri wa kazi ya uumbaji inayowapeleka kwa Muumba wao! Baba Mtakatifu Leo XIV amewakumbusha walinzi hawa kwamba, wito wao wa kwanza ni huduma ya kijeshi inayopaswa kusimikwa katika utakatifu wa maisha, unaopata chimbuko lake katika Sakramenti ya Ubatizo. Hii ni huduma inayokita mizizi yake katika maisha ya kiroho, kwa kuwahudumia zaidi waamini, mahujaji na watalii wanaofika kwa wingi mjini Vatican na kwamba, wanapaswa daima kukumbuka maneno ya Kristo Yesu anayesema: “Amin, nawaambia, kadiri mlivyomtendea mmojawapo wa hao ndugu zangu walio wadogo, mlinitendea mimi.” Mt 25:40.

Wamekula Kiapo mbele ya Papa Leo XIV
Wamekula Kiapo mbele ya Papa Leo XIV   (@Vatican Media)

Katika huduma yao, daima wanapaswa kuwa makini, wakiendelea kuboresha maisha yao kwa sala na tafakari ya kina, ili kuweza kukutana na Kristo Yesu kutoka katika undani wa maisha yao, tafakari zitakazowaongoza hadi kwake, ili waweze kuwa wake milele yote. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, hiki ni Kikosi cha Ulinzi wa Papa kutoka Uswisi kinachosimikwa katika sifa, utofauti pamoja na haiba zao. Kambini ni mahali pa kukuza na kudumisha fadhila za: Kiutu na kibinadamu, za huduma kwa jirani, ukarimu na unyenyekevu; kwa kujenga na kudumisha mshikamano wa udugu wa kibinadamu, ili kujenga maelewano, chemchemi ya furaha ya ndani inayojionesha kwa wale wote wanaokutana nao katika utekelezaji wa majukumu yao. Huu ni mwaliko kwa walinzi hawa kuendelea kujikita katika njia hii, ambayo mara nyingi ina changamoto zake, lakini inayoweza kuzaa matunda mengi. Mwishoni, Baba Mtakatifu Leo XIV amewashukuru walinzi wote kwa huduma hii inayosimikwa katika bidii na ukarimu unaotangazwa na kushuhudiwa kila kukicha na hatimaye, akawaweka chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria Mama wa Mungu na Kanisa, Mtakatifu Martin wa Tours, Mtakatifu Sebastian, na Mtakatifu Nikolai wa Flüe, pamoja na Watakatifu walezi na wasimamizi wao; na mwishoni akawapatia baraka zake za kitume.

Walinzi 28 wa Kikosi cha Ulinzi wa Baba Mtakatifu wamekula kiapo
Walinzi 28 wa Kikosi cha Ulinzi wa Baba Mtakatifu wamekula kiapo   (@Vatican Media)

Katika mahubiri yake Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican amewakumbusha wanajeshi hawa kwamba, Kristo Yesu ni Mzabibu wa kweli: “Mimi ni mzabibu; ninyi ni matawi, akaaye ndani yangu nami ndani yake, huyo huzaa sana; maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya neno lo lote.” Yn 15:5. Huu ni uhusiano unaosimikwa katika sadaka ya maisha na hivyo inakuwa ni chemchemi ya furaha katika huduma kwa Kristo Yesu, Khalifa wa Mtakatifu Petro na Kanisa katika ujumla wake. Kumbe, wanapaswa kujenga na kudumisha mahusiano na Kristo Yesu kwa njia ya: Sala, Sakramenti za Kanisa, Tafakari ya kina ya Neno la Mungu inayomwilishwa katika huduma makini na hivyo kujenga urafiki na udugu na Kristo Yesu. Neno la Mungu li hai, linasafisha, linatakasa na kutenda kazi, mwaliko kwa waamini kuendelea kusimika maisha na utume wao katika Kristo Yesu, ambaye kimsingi ndiye Mzabibu wa kweli na hivyo kuendelea kuwa huru, waaminifu na watoto watiifu wa Mungu. Huu ni mwaliko kwa wanajeshi hawa kusoma, kulitafakari na kulimwisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha yao, baada ya kumfahamu Kristo Yesu kupitia Maandiko Matakatifu, kielelezo cha upendo na kwamba, Mwenyezi Mungu anawatambua jinsi walivyo, yuko daima pamoja na kati yao na hivyo wataendelea kumtukuza na hatimaye kuzaa matunda mengi kwa ajili ya huduma kwa jirani zao.

Walinzi wa Papa kutoka nchini Uswisi tangu mwaka 1527
Walinzi wa Papa kutoka nchini Uswisi tangu mwaka 1527   (@Vatican Media)

Hii ni huduma inayopaswa kutolewa kama sadaka inayokita mizizi yake katika furaha ya kutoa kwani Maandiko Matakatifu yanasema: “Katika mambo yote nimewaonesha ya kuwa kwa kushika kazi hivi imewapasa kuwasaidia wanyonge, na kuyakumbuka maneno ya Bwana Yesu, jinsi alivyosema mwenyewe, Ni heri kutoa kuliko kupokea.” Mdo 20:35. Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican amehitimisha mahubiri yake kwa kuwataka wanajeshi wapya kamwe wasiogope, bali waendelee kukita maisha yao katika fadhila ya unyenyekevu na imani; mambo msingi yanayowaunganisha na Kristo Yesu katika huduma na hivyo wataweza kuzaa matunda mengi. Baada ya Sherehe ya Kula Kiapo cha Utii kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro, katika nafsi ya Baba Mtakatifu Leo XIV aliwashukuru wanajeshi, familia na viongozi waliofika mjini Vatican kutoka Uswisi kuhudhuria sherehe hizi nzuri, zinazosisimua na kukata na shoka. Sherehe za kula kiapo ni ishara inayothibitisha sadaka na majitoleo yao ya uaminifu kwa kuchochewa na ari pamoja na shauku ya ujana inayosimikwa katika fadhila ya imani kwa Mungu mmoja na upendo kwa Kanisa.

Papa Leo XIV amewashukuru walinzi wake kwa kazi nzuri
Papa Leo XIV amewashukuru walinzi wake kwa kazi nzuri   (@Vatican Media)

Kwa upande wake Kanali Christoph Graf, Mkuu wa Kikosi cha Walinzi wa Papa kutoka Uswiss, amewashukuru wote waliohudhuria katika sherehe hizi ambamo wanajeshi wapya wamekula kiapo cha utii kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro kwa kutumainia kwa uaminifu, ukweli na kwa heshima na hivyo kuthibitisha nia yao ya kuweza kuishi kiapo hiki kwa uangalifu na uaminifu kwa kutambua kwamba, huduma ni sehemu muhimu sana ya utambulisho wao kama binadamu na kama wakristo unaosimikwa katika unyenyekevu. Hii ni fursa ya kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa Baba Mtakatifu, Vatican na kwa Kanisa katika ujumla wake. “Kwa maana Mwana wa Adamu naye hakuja kutumikiwa, bali kutumika, na kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi.” Mk 10:45.

Kikosi cha Walinzi wa Papa wakutana na Papa Leo XIV
Kikosi cha Walinzi wa Papa wakutana na Papa Leo XIV   (ANSA)

Itakumbukwa kwamba, Rais wa Shirikisho la Uswisi Bwana Guy Parmelin pamoja na ujumbe wake, Jumatano, tarehe 6 Mei 2026 amekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Leo XIV, Kardinali Pietro Parolin aliyekuwa ameambatana na Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa Mambo ya Nchi za Nje, Ushirikiano na Mashirika ya Kimataifa. Viongozi hawa kwa pamoja wamesifu uhusiano wa kidiplomasia uliopo kati ya nchi hizi mbili; bila kusahau huduma ya uaminifu inayotekelezwa na Kikosi cha Walinzi wa Papa kutoka Uswiss. Baadaye katika mazungumzo yao wamegusia masuala ya Kimataifa na Kikanda, hususan vita inayoendelea kati ya Urussi na Ukraine; vita huko Mashariki ya Kati na kutaka watu wenye mapenzi mema kushirikiana, ili kuweza kuragibisha amani.

Kikosi cha walinzi wa Papa
07 Mei 2026, 15:43