Papa Leo XIV: Wosia Kwa Maaskofu Wasaidizi Jimbo Kuu la Roma!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Mababa wa Kanisa wanasema sifa kuu za Askofu ni: unyenyekevu na huduma; mambo yanayofafanuliwa vyema na Mtakatifu Paulo, Mtume katika Waraka wake kwa Tito, akionesha mambo msingi yanayopaswa kufuatwa na kutekelezwa na Maaskofu, ili kukamilisha yale yanayopungua katika maisha na utume wa Kanisa; kwa kuwachagua na kuwasimika wazee wanaofaa kwa ajili ya uongozi wa Kanisa; watu wema na wenye kiasi, wapenda haki na watakatifu; watu wenye mifano bora ya kuigwa na jamii inayowazunguka. Askofu anayo dhamana ya kusali kwa ajili ya kuwaombea watu wote, kwa kutambua kwamba, kimsingi yeye ni mtu wa Mungu, aliyeteuliwa kati ya watu kwa ajili ya huduma, ili kuhakikisha kwamba, anakuza na kudumisha Ibada na Uchaji wa Mungu, mambo msingi katika kulinda na kudumisha utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Utume huu, umwezeshe Askofu kuwa ni kiongozi mkarimu, akitambua kwamba, Kristo Yesu ndiye anayewaita waja wake na kuwaweka wakfu ili kuendeleza kazi ya ukombozi! Ikumbukwe kwamba, kila Askofu, mbele ya watu watakatifu wa Mungu ni Mwinjilishaji, Mchungaji na Rafiki wa Maskini.
Maaskofu ni waandamizi wa Mitume. Tena, katika kuendelea kwa njia hiyohiyo, linaamua kukiri na kutangaza mbele ya wote fundisho juu ya Maaskofu walio waandamizi wa Mitume, ambao pamoja na mwandamizi wa Petro, aliye Wakili wa Kristo na kichwa kionekanacho cha Kanisa zima, waiongoza nyumba ya Mungu aliye hai. Kama vile Mtakatifu Petro na wale Mitume wengine wameunganika, kwa agizo la Bwana, katika urika mmoja tu wa kitume, kwa jinsi iliyo sawa (pari ratione), Baba Mtakatifu aliye mwandamizi wa Petro, na Maaskofu walio waandamizi wa Mitume, wanaungana pamoja. Kuna mambo mawili yaoneshayo tabia na maumbile ya kiurika ya Daraja ya uaskofu: yaani nidhamu ya kale, ambayo kufuatana nayo Maaskofu wa ulimwengu mzima walishirikiana wao kwa wao na pamoja na Askofu wa Roma, katika kifungo cha umoja, upendo na amani.
Urika wa Maaskofu hauwezi kuwa na mamlaka usipounganika na Baba Mtakatifu, aliye mwandamizi wa Petro, naye ndiye kichwa chake, ambaye mamlaka ya ukuu wake hudumu kabisa juu ya wote, wachungaji kwa waamini. Kwa maana Baba Mtakatifu, kwa nguvu ya wadhifa wake kama Wakili wa Kristo na Mchungaji wa Kanisa lote, ana mamlaka katika Kanisa, iliyo kamili, ya juu kabisa na iwahusuyo wote (plenam, supremam et universalem potestatem), ambayo anaweza kuyatimiza kwa uhuru. Urika wa Maaskofu (Ordo Episcoporum) ni urithi wa urika wa Mitume katika kufundisha na katika uongozi wa kichungaji; na ndani yake umoja wa Mitume huendelezwa katika nyakati. [Urika huo wa Maaskofu] pamoja na Kichwa chake aliye Baba Mtakatifu, na kamwe pasipo yeye, una mamlaka ya juu kabisa na kamili juu ya Kanisa lote. [Mamlaka hiyo] yaweza kutekelezwa tu kwa idhini ya Baba Mtakatifu. Bwana alimweka Simoni Petro tu kuwa mwamba na mshika ufunguo wa Kanisa (Rej Mt 16:18-19), akamweka kuwa Mchungaji wa kundi lake zima (Rej Yn 21:15nk); lakini wadhifa wa kufunga na kufungua aliopewa Petro (Rej. Mt 16:19), ulikabidhiwa pia kwa Urika wa Mitume uliounganika na mkuu wake (taz. Mt 18:18; 28:16-20.) Urika huo maadamu umeundwa na wengi, huonyesha hali ya Taifa la Mungu ya kuwa la namna nyingi na la ulimwengu mzima; maadamu ulikusanyika chini ya kiongozi mmoja tu, huonyesha umoja wa kundi la Kristo. Rej. LG 18-22.
Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Leo XIV, Jumamosi tarehe 2 Mei 2026 amewawekwa wakfu Maaskofu wasaidizi wanne wa Jimbo kuu la Roma hawa ni katika nafsi ya: Askofu Msaidizi Stefano Sparapani, Askofu Msaidizi Alessandro Zenobbi, Askofu Msaidizi Andrea Carlevale pamoja na Askofu Msaidizi Marco Valenti, wote hawa wanabeba ndani mwao tajiriba ya shughuli za kichungaji Jimbo kuu la Roma. Ibada ya kuwaweka wakfu imeadhimishwa kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Laterani, Mama ya Makanisa yote ulimwenguni, “Caput et mater omnium ecclesiarum” na Baba Mtakatifu ndiye Askofu wake mkuu. Kumbe, Kanisa hili pia ni kielelezo cha upendo, msingi wa maisha ya kiroho na mawe hai ni watu wa Mungu wanaolijenga Kanisa hili. Kanisa hili ni alama ya utakatifu wa Kanisa, licha ya watoto wake, wakati mwingine, kuogelea katika dimbwi la dhambi. Kanisa ni moja: lina bwana mmoja, laungama imani moja tu, lazaliwa kwa Ubatizo mmoja, lafanywa mwili mmoja, lahuishwa na Roho mmoja, kwa ajili ya tumaini moja. Rej. Efe 4: 3-5, na katika utimilifu wote migawanyiko yote itashindwa. Kanisa ni takatifu kwa sababu muasisi wake ni Mungu aliye mtakatifu sana. Kanisa ni Katoliki latangaza utimilifu wa imani. Kanisa ni la kitume kwa sababu limejengwa juu ya misingi imara ya Mitume kumi na wawili. Kanisa ni moja, takatifu, katoliki na la Kitume. Rej. KKK 866-870.
Baba Mtakatifu Leo XIV katika wosia wake kwa Maaskofu wasaidizi wa Jimbo kuu la Roma, amewakumbusha kwamba wamewekwa wakfu kwa ajili ya huduma ya Injili ya Kristo, Jiwe walilokataa waashi, lakini limechaguliwa na Mwenyezi Mungu na sasa limekuwa ni Jiwe kuu la pembeni; ufunuo wa Uso wa huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake. Jimbo kuu la Roma linaitwa na kutumwa kutangaza Habari Njema ya Wokovu na kwamba kiini cha maisha na utume wa Kanisa ni kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo Yesu ili kuwaganga na kuwaponya wagonjwa; kuwatakasa na kuwasamehe wadhambi pamoja na kumwilisha Injili ya upendo katika huduma. Huu ni mwaliko kwa Maaskofu wasaidizi na watu wote wateule wa Jimbo kuu la Roma kusimama kidete, kulinda na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu; kipaumbele cha kwanza wakiwa ni maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii.
Maaskofu wasaidizi watambue kwamba, wamepewa zawadi maalum ya kuwatunza watu wa Mungu, mwaliko ni kuendelea kumsaidia Askofu wa Roma, ili aweze kuonekana kama Mchungaji mwema, huku wakiendelea kusimika maisha na utume wao katika Injili ya upendo inayomwilishwa katika huduma kwa watu wa Mungu walionea sehemu mbalimbali za dunia. Wawe ni mashuhuda na wajenzi wa udugu wa kibinadamu na watambue kwamba Kanisa linapaswa kutoka sakristia, ili kuwaendelea watu walioko pembezoni mwa vipaumbele vya maisha ya kijamii, ili kuwaonjesha furaha ya Injili, kwa kutambua kwamba, Kanisa ni kama hospitali iliyoko kwenye uwanja wa mapambano, kumbe, inapaswa kuwa ni alama ya huruma na upendo wa Mungu na kwamba, maskini na watu wa Mungu katika ujumla wao wanapaswa kuwa ni kiini cha Habari Njema ya Wokovu kwa kumwachia nafasi Roho Mtakatifu kutenda kazi ndani mwao. Watambue kwamba, wao ni mashuhuda na mfano wa Kristo Yesu Mchungaji mwema, aliyekuja hapa duniani si kwa ajili ya kutumikiwa bali kutumikia na kutoa uhai wake, ili uwe ni fidia kwa wengi. Rej. Mk 10:45. Ili waweze kuwa ni Manabii katika: Utume na maisha yao, wanapaswa kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa amani na umoja huku wakisimika maisha yao katika neema na huruma; kwa kudumisha utulivu; kwa kuonesha ukarimu, kwa kusikiliza na kutoa msamaha, wawe tayari kwa huduma; wawe ni wasafiri wenza wa watu wa Mungu Jimbo kuu la Roma; vyombo vya matumaini na waragibishaji wa uzuri wa Injili na kwamba, watu wote wa Mungu yaani: Maskini wa Roma, mahujaji na wageni waonje ukarimu wa kimama, kielelezo cha Kanisa la Kristo Yesu.
