Papa Leo XIV: Siku ya Kimataifa ya Uhuru wa Vyombo Vya Habari: Kuna Ukiukwaji wa Haki Hii
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Historia ya Siku ya Kimataifa ya Uhuru wa Vyombo Vya Habari inatokana na mkutano ulioitishwa na Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa, UNESCO huko Windhoek tarehe 3 Mei 1991 na kuhidhinisha Azimio la Windhoek, Namibia kwa ajili ya kukuza na kudumisha taaluma ya uandishi wa habari huru, kutoka kwenye ushawishi, na wenye utofauti wa maoni. Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilitangaza Siku ya Kimataifa ya Uhuru wa Vyombo vya Habari mwezi Desemba 1993, kufuatia mapendekezo ya Mkutano Mkuu wa UNESCO. Tangu wakati huo, kumbukumbu ya Azimio la Windhoek, Namibia huadhimishwa kila mwaka duniani kote tarehe 3 Mwezi Mei kama Siku ya Kimataifa ya Uhuru wa Vyombo vya Habari. Na kwa Mwaka 2026 Maadhimisho haya yananogeshwa na kauli mbiu: “Kuunda Mustakabali wa Amani: Kukuza Uhuru wa Vyombo vya Habari kwa Ajili ya Haki za Binadamu, Maendeleo na Usalama.”
Baba Mtakatifu Leo XIV wakati wa Sala ya Malkia wa Mbingu, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican amewakumbusha waamini na watu wote wenye mapenzi mema kwamba, Dominika tarehe 3 Mei 2026, Jumuiya ya Kimataifa ilikuwa inaadhimisha Siku ya Kimataifa ya Uhuru wa Vyombo Vya Habari iliyoasisiwa na UNESCO. Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, haki ya uhuru wa vyombo vya habari mara nyingi inakiukwa kwa uwazi na wakati mwingine kwa usiri mkubwa. Baba Mtakatifu Leo XIV amewakumbuka waandishi wa habari na wanatasnia ya mawasiliano ambao wameathirika kutokana na vita, kizani na mipasuko ya kijamii.
Tangu kupitishwa kwa Azimio la Windhoek, uhusiano wa kihistoria kati ya uhuru wa kutafuta, kusambaza na kupokea taarifa kwa upande mmoja, na maslahi ya umma kwa upande mwingine, bado umeendelea kuwa ni muhimu sana. Mnamo tarehe Mei 3 ni ukumbusho kwa serikali kuheshimu wajibu wao wa kuhakikisha uhuru wa vyombo vya habari. Pia ni siku ya tafakari kwa wanahabari kuhusu masuala ya uhuru wa habari na maadili ya taaluma yao. Ni fursa ya: Kuadhimisha msingi wa uhuru wa vyombo vya habari. Kutathmini hali ya uhuru wa habari duniani kote. Kutetea vyombo vya habari dhidi ya mashambulizi ya uhuru wake. Ni muda wa kuwakumbuka na kuwaombea waandishi wa habari waliopoteza maisha yao wakitekeleza wajibu wao wa kitaaluma.
Takwimu zilizotolewa na World Press Freedom Index, zinaonesha kwamba, asilimia 52% za nchi wanachama wa UNESCO zinakabiliana na hali ngumu ya uhuru wa vyombo vya habari. Ni asilimia 1% ya watu wanaofaidika na uhuru wa vyombo vya habari na kwamba, taaluma ya uandishi wa habari inapata shinikizo kutoka katika siasa, hali ngumu ya kiuchumi pamoja na sheria kandamizi dhidi ya uhuru wa vyombo vya habari. Irag, Sudan ya Kusini na Yemen ni kati ya nchi ambazo uhuru wa vyombo vya habari uko hatarini. Wadau wa vyombo vya mawasiliano ya jamii wanasema, ili kukuza na kudumisha uhuru wa vyombo vya habari kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kuchukua hatua madhubuti za kuwalinda waandishi wa habari, kwa kuimarisha sheria, taratibu na kanuni zinazowalinda waandishi wa habari pamoja na kuhakikisha kwamba, wale wote wanaohusika na uvunjaji wa sheria hizo wanafikishwa mbele ya vyombo vya sheria, ili haki iweze kutendeka. Ikumbukwe kwamba, uhuru wa vyombo vya habari ni nguzo muhimu sana ya demokrasia na kwamba, uhuru huu kwa siku za usoni unategemea sera na mikakati ya kisiasa kwa nchi husika kwa kulindwa na wananchi wenyewe. Norway ni kati ya nchi ambazo uhuru wa vyombo vya habari unalindwa na kudumishwa na kwamba, hii ni mara ya kumi ikishikilia nafasi ya kwanza.
