Papa Leo XIV Mwezi Mei: Ibada na Heshima Kwa Bikira Maria Mama wa Mungu na Kanisa
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Mama Kanisa ameuanza Mwezi Mei uliotengwa kwa heshima na Ibada kwa Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa. Ibada kwa Bikira Maria na Ibada ya huruma ya Mungu ni nyenzo muhimu sana katika hija ya kuutafuta na kuukumbatia utakatifu wa maisha pamoja na kuendelea kuwa wafuasi aminifu wa Kristo sanjari na kuwa mashuhuda wa huruma ya Mungu hapa duniani. Huu ni mwaliko kwa waamini kumwomba Roho Mtakatifu ili aweze kuwasaidia kutambua na kuthamini dhamana na nafasi ya Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa katika ufuasi wao. Bikira Maria ni Tabernakulo ya kwanza ya Neno wa Mungu, Mtumishi mwaminifu na mwalimu mkuu katika shule ya huruma na upendo wa Kristo kwa waja wake. Ni nyota angavu inayowasindikiza waamini katika hija ya kumwendea Baba wa milele kwa njia ya Kristo Yesu!
Bikira Maria ni mfano bora wa kuigwa katika mapambano ya maisha ya kiroho, kwani ni kielelezo cha Eva mpya, Sanduku la Agano, Mlango wa huruma ya Mungu na mbingu; Nyota angavu ya alfajiri na Mama wa mchakato wa Uinjilishaji mpya unaojikita katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Bikira Maria alikingiwa dhambi ya asili, kielelezo makini cha upendeleo wa Mungu katika maisha yake, akamkinga na dhambi pamoja na mauti, ili aweze kuwa ni Mama wa Mungu na Kanisa, tayari kuwasaidia waamini kumfuasa Kristo Yesu kwa ujasiri na moyo mkuu. Huu ni mwaliko wa kuingia katika shule ya upendo inayoongozwa na kusimamiwa na Bikira Maria.
Hapa waamini wanapaswa kukubali kuona kwa jicho la imani: mateso na mahangaiko ya Bikira Maria tangu siku ile alipopashwa habari kwamba, atakuwa ni Mama wa Mungu hadi aliposimama chini ya Msalaba na kushuhudia Mwanaye mpendwa akiinamisha kichwa na kukata roho! Waamini wajitahidi kumchukua Bikira Maria katika maisha yao kwa kujiweka wakfu kwa Bikira Maria; kwa kusali na kutafakari Rozari Takatifu ambayo kimsingi ni muhtasari wa Injili, yaani: maisha, utume na historia ya kazi nzima ya ukombozi na kwamba, hii ni Biblia ya waamini wa kawaida! Waamini wajenge na kudumisha Ibada kwa Moyo Safi wa Bikira Maria pamoja na kufanya mapilizi kwa ajili ya dhambi za walimwengu. Ili kukuza na kudumisha moyo na ari ya Ibada kwa Bikira Maria kuna haja ya kujikita katika fadhila ya: imani, utii, unyenyekevu, huruma, uwajibikaji pamoja na kujiaminisha kwa Kristo Yesu!
Baba Mtakatifu Leo XIV mara baada ya Sala ya Malkia wa Mbingu, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Dominika tarehe 3 Mei 2026, katika Mwezi Mei, Kanisa zima kwa furaha linakusanyika kwa pamoja chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, ili kuweza kupyaisha, lakini zaidi kwa kusali Rozari Takatifu kwa pamoja kama familia, jumuiya na Kanisa na hata kwa mtu binafsi. Hii ni kumbukumbu hai na endelevu inayowawezesha waamini kujichotea mang’amuzi na tajiriba ya uzoefu waliokuwa nao wanafunzi wa Kristo Yesu, kati ya Sherehe ya Kupaa Bwana Mbinguni sanjari na Sherehe ya Pentekoste, Roho Mtakatifu alipowashukia Mitume, wakatoka kifua mbele kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Katika kipindi chote hicho, Bikira Maria Mama wa Mungu na Kanisa alikuwa kati kati yao, kule kwenye Chumba cha juu, ili kumwomba Roho Mtakatifu; Moyo wake usiokuwa na doa ulishikilia moto ambao ulipyaisha sala ya kila mtu. Katika kipindi hiki cha Mwezi Mei, uliotengwa na Mama Kanisa kwa Ibada na heshima kwa Bikira Maria, Baba Mtakatifu Leo XIV anapenda kuwakabishi waamini na watu wote wenye mapenzi mema nia zake maalum haswa katika kukuza ushirika ndani ya Kanisa na amani duniani.
