Papa Leo XIV Mwaka Mmoja Tangu Achaguliwe Kuliongoza Kanisa Katoliki: Vipaumbele Vyake!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Leo XIV anaadhimisha Kumbukizi ya Mwaka mmoja tangu alipochaguliwa kuliongoza Kanisa Takatifu, Katoliki na la Mitume, tarehe 8 Mei 2026 kwa kutembelea Madhabahu ya Bikira Maria wa Pompei. Madhabahu ni mahali muafaka pa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wa imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Ni mahali pa toba na wongofu wa ndani, unaomwezesha mwamini kuchuchumilia huruma na upendo wa Mungu katika maisha, kama chachu ya utimilifu na utakatifu. Madhabahu ya Bikira Maria wa Pompei, yaliyoko kwenye Jimbo kuu la Napoli, Kusini mwa Italia ni kitovu cha Ibada kwa Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa. Ibada kwa Bikira Maria imekuwa ni chemchemi na kichocheo kikuu cha waamini kuonesha mshikamano wa upendo na huduma kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Hapa ni mahali muafaka pa kuombea haki na amani, iweze kutamalaki katika uso wa dunia. Madhabahu haya yalianzishwa na Mtakatifu Bartolo Longo aliyetangazwa kuwa Mtakatifu na Papa Leo XIV tarehe 19 Oktoba 2025. Sehemu ya pili ya Siku hii ni kwa Baba Mtakatifu Leo XIV kutembelea Jimbo kuu la Napoli.
Vipaumbele katika maisha na utume wake: Mafundisho Jamii ya Kanisa yanayopata chimbuko lake mintarafu kanuni na muundo wa elimu fahamu, taalimungu, hususan taalimungu maadili ambayo ni dira na mwongozo wa maisha adili ya watu. Yanachota amana na utajiri wake kutoka katika Maandiko Matakatifu na Mapokeo ya Kanisa na imani thabiti ambayo inamwilisha Neno la Mungu katika matendo, kielelezo cha imani tendaji. Mambo msingi katika mchakato wa kudumisha haki msingi za binadamu: Amani katika ukweli, haki, upendo na uhuru. Hizi ni tunu ambazo ni urithi mkubwa kwa binadamu wote kwani zinabubujika kutoka katika asili ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu hivyo, zinapaswa kulindwa, kutetewa na kuheshimiwa na wote; kwa kuzingatia kwamba, haki inakwenda sanjari na wajibu; hakuna haki pasi na wajibu. Hii ni haki ya kuishi, kupata huduma bora ya makazi, afya, elimu, kuabudu, uhuru wa dhamiri, uhuru wa kuchagua mfumo wa maisha; haki za kiuchumi na kisiasa pamoja na uhuru wa kwenda unakotaka kwa kuzingatia sheria na kanuni zilizopo.
Kanisa Katoliki lina amana na utajiri mkubwa wa Mafundisho Jamii ya Kanisa yanayopata chimbuko lake katika Waraka wa Kichungaji wa Papa Leo XIII; Mambo Mapya; “Rerum novarum.” Alisema, kazi ni utimilifu wa utu na heshima ya binadamu, ina thamani na heshima yake ya asili. Aligusia haki msingi za wafanyakazi, mshahara wa haki na wajibu wa wafanyakazi; Umiliki wa binafsi wa mali; wajibu wa Serikali ni pamoja na kuhakikisha haki, sanjari na kuwalinda wanyonge ndani ya jamii; Ustawi na maendeleo ni kwa ajili ya wote, lakini maskini wapewe kipaumbele cha kwanza. Kanuni ya auni inapaswa kuzingatiwa! Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili, katika Waraka wake kuhusu Masuala ya Kijamii “Centesimus Annus,” alifafanua kwa kina kuhusu asili ya haki msingi za binadamu; umuhimu wa kukuza na kudumisha upendo na mshikamano miongoni mwa Jumuiya ya Kimataifa, kama inavyojidhihirisha katika Waraka wake wa “Sollicitudo Rei Socialis” cheche ya uanzishaji wa vyama vya kitume kijamii vilivyokuwa vinapania kulinda na kutetea uhuru, utu na haki msingi za binadamu. Itakumbukwa kwamba, uhuru wa kidini na uhuru wa kuabudu ni muhtasari wa haki zote za binadamu. Dini zisaidie kujenga amani, upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu na kamwe zisiwe ni chanzo cha vurugu, kinzani na vita. Kanuni maadili na utu wema ni sehemu muhimu sana katika maisha ya mwanadamu zinazopaswa kulindwa ili amani na utulivu viweze kushika kasi, bila kusahau nafasi na dhamana ya uwepo wa Mungu katika maisha ya mwanadamu. Waamini wanapaswa kufahamu vyema kweli za imani yao ili wasiyumbishwe, bali wasimame kidete kuilinda, kuitetea na kuishuhudia kwa ajili ya ustawi, mafao na maendeleo ya wengi.
Baba Mtakatifu Leo XIV ambaye anaongozwa na kauli mbiu yake ya Kiaskofu “In Illo unum uno” Yaani “Ingawa sisi Wakristo ni wengi, katika Kristo mmoja sisi ni wamoja.” Huu ni ufafanuzi uliotolewa na Mtakatifu Agostino mintarafu Zaburi ya 127. Papa Leo XIV ni Mtawa wa kwanza wa Shirika la Waagostiniani kuchaguliwa kuwa Khalifa wa Mtakatifu Petro na Mmarekani wa pili kuwahi kuliongoza Kanisa Katoliki kama Khalifa wa Mtakatifu Petro baada ya Hayati Papa Francisko. Katika salam zake kwa mji wa Roma na Ulimwengu katika ujumla wake, “Urbi et Orbi”, Alhamisi tarehe 8 Mei 2025 alikazia pamoja na mambo mengine: Umuhimu wa ujenzi wa amani inayobubujika kutoka kwa Kristo Mfufuka; Mwenyezi Mungu ni mwingi wa huruma na upendo kwa waja wake wote na kwamba, kamwe ubaya hauwezi kushinda. Kuna haja ya kuwa vyombo na wajenzi wa haki na amani; waaminifu kwa Kristo Yesu, tayari kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo, huku wakijitahidi kuwa ni wamisionari. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, kati ya waamini yeye ni Mkristo na kwao yeye ni Askofu. Hii ni changamoto kwa waamini kuhakikisha kwamba, wanajenga Kanisa la: Kisinodi na kimisionari, kwa kujikita katika Injili ya upendo hasa kwa maskini na wahitaji sanjari na majadiliano, ili kujenga madaraja ya kuwakutanisha watu.
Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema kwamba Yesu Kristo, aliye Mchungaji wa milele, alijenga Kanisa takatifu, akawatuma Mitume kama Yeye mwenyewe alivyotumwa na Baba (Rej. Yn 20:21), tena akataka waandamizi wao, yaani Maaskofu, wawe wachungaji wa Kanisa lake hata ukamilifu wa nyakati. Kusudi Uaskofu wenyewe uwe mmoja na usiogawanyika, akamweka Mt. Petro juu ya Mitume wengine, na katika yeye akatia chanzo na msingi udumuo na uonekanao wa umoja wa imani na wa ushirika. Mtaguso Mtakatifu huwatolea tena waamini wote fundisho hilo la uanzishaji, udumifu, nguvu na tabia ya mamlaka tukufu ya Papa na ya Mamlaka fundishi ya Kanisa yasiyoweza kukosa, ili liaminike kwa uthabiti. Tena, katika kuendelea kwa njia hiyohiyo, linaamua kukiri na kutangaza mbele ya wote fundisho juu ya Maaskofu walio waandamizi wa Mitume, ambao pamoja na mwandamizi wa Petro, aliye Wakili wa Kristo na kichwa kionekanacho cha Kanisa zima, waiongoza nyumba ya Mungu aliye hai. Kama vile Mtakatifu Petro na wale Mitume wengine wameunganika, kwa agizo la Bwana, katika urika mmoja tu wa kitume, kwa jinsi iliyo sawa (pari ratione), Baba Mtakatifu aliye mwandamizi wa Petro, na Maaskofu walio waandamizi wa Mitume, wanaungana pamoja. Kuna mambo mawili yaoneshayo tabia na maumbile ya kiurika ya Daraja ya uaskofu: yaani nidhamu ya kale, ambayo kufuatana nayo Maaskofu wa ulimwengu mzima walishirikiana wao kwa wao na pamoja na Askofu wa Roma, katika kifungo cha umoja, upendo na amani.
Urika wa Maaskofu hauwezi kuwa na mamlaka usipounganika na Baba Mtakatifu, aliye mwandamizi wa Petro, naye ndiye kichwa chake, ambaye mamlaka ya ukuu wake hudumu kabisa juu ya wote, wachungaji kwa waamini. Kwa maana Baba Mtakatifu, kwa nguvu ya wadhifa wake kama Wakili wa Kristo na Mchungaji wa Kanisa lote, ana mamlaka katika Kanisa, iliyo kamili, ya juu kabisa na iwahusuyo wote (plenam, supremam et universalem potestatem), ambayo anaweza kuyatimiza kwa uhuru. Urika wa Maaskofu (Ordo Episcoporum) ni urithi wa urika wa Mitume katika kufundisha na katika uongozi wa kichungaji; na ndani yake umoja wa Mitume huendelezwa katika nyakati. [Urika huo wa Maaskofu] pamoja na Kichwa chake aliye Baba Mtakatifu, na kamwe pasipo yeye, una mamlaka ya juu kabisa na kamili juu ya Kanisa lote. [Mamlaka hiyo] yaweza kutekelezwa tu kwa idhini ya Baba Mtakatifu. Bwana alimweka Simoni Petro tu kuwa mwamba na mshika ufunguo wa Kanisa (Rej Mt 16:18-19), akamweka kuwa Mchungaji wa kundi lake zima (Rej Yn 21:15nk); lakini wadhifa wa kufunga na kufungua aliopewa Petro (Rej. Mt 16:19), ulikabidhiwa pia kwa Urika wa Mitume uliounganika na mkuu wake (taz. Mt 18:18; 28:16-20.) Urika huo maadamu umeundwa na wengi, huonyesha hali ya Taifa la Mungu ya kuwa la namna nyingi na la ulimwengu mzima; maadamu ulikusanyika chini ya kiongozi mmoja tu, huonyesha umoja wa kundi la Kristo. Rej. LG 18-22.
Alama za huduma kama Khalifa wa Mtakatifu Petro: Pallio Takatifu na Pete ya Mvuvi: Pallio Takatifu ni kitambaa cha sufi safi kinachovaliwa na Baba Mtakatifu, Maaskofu wakuu wa majimbo ya Kanisa Katoliki pamoja na Mapatriaki. Hii ni alama ya Kristo mchungaji mwema aliyesadaka maisha yake kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Kama ilivyokuwa kwa Kristo Yesu, Mchungaji mwema, hata kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro, Maaskofu wakuu na Mapatriaki wanahamasishwa kuwabeba kondoo wao kama kielelezo cha wachungaji wema; wakumbuke kwamba, wameteuliwa si kwa ajili ya mafao yao binafsi, bali kwa ajili ya kondoo wa Kristo Yesu. Papa mpya na Maaskofu wakuu wanapaswa pia kusadaka maisha yao kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake. Pallio takatifu ni alama ya umoja na mshikamano kati ya Khalifa wa Mtakatifu Petro, Maaskofu wakuu na Mapatriaki, mshikamano unaopata chimbuko lake katika Fumbo la Umwilisho, linalofikia utimilifu wake katika Fumbo la Pasaka. Pallio Takatifu imebarikiwa na Kardinali Mario Zenari, Balozi wa Vatican nchini Siria. Baba Mtakatifu Leo XIV amevishwa pia “Pete ya Mvuvi”: “Anuli Piscatoris” Pete ambayo inamwakilisha Mtakatifu Petro aliyekuwa ni Mvuvi kutoka Galilaya. Pete hii inatumika kama muhuri binafsi wa Baba Mtakatifu; kielelezo cha imani ya Mtakatifu Petro kwa Kristo Yesu na hivyo kuthibitisha uhalisia wake. Pete ya Mvuvi imebarikiwa na Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle, Mwenyekiti Mwenza wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu na Sala kutolewa na Kardinali Fridolin Ambongo, Rais wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM.
Baba Mtakatifu Leo XIV katika mahubiri, yake Dominika tarehe 18 Mei 2025 alipokuwa anauanza utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro wa 267 na Askofu wa Roma, aligusia kuhusu kifo cha Papa Francisko; Umoja na Mshikamano wa Baraza la Makardinali pamoja na sala za waamini; Ujenzi wa Kanisa linalosimikwa katika upendo wa Mungu; Kwa kukuza na kudumisha: Umoja na mshikamano wa Kanisa, chachu ya upatanisho, tayari kujikita katika mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi na Kimisionari. Baba Mtakatifu Leo XIV alitambua uwepo wa umati mkubwa wa watu wa Mungu kutoka sehemu mbalimbali za dunia waliofika kushuhudia anapouanza utume wake rasmi kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Kwa kifo cha Papa Francisko, waamini waligubikwa na huzuni na majonzi makubwa, wakawa kama kondoo wasio na mchungaji. Rej. Mt 9:36. Waamini wakajikita zaidi katika imani kwa Kristo Mfufuka kwa kutambua kwamba, kamwe Kristo hawezi kuwaacha kondoo wake wapotee, atawakusanya, na kuwalinda, kama mchungaji alindavyo kundi lake.Rej. Yer 31:10. Ni katika roho ya Pasaka, Baraza la Makardinali lilikutanika kufanya uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu, Askofu wa Roma, Mchungaji mwenye uwezo wa kulinda na kudumisha amana na utajiri wa imani ya Kikristo, akiwa na mwelekeo mpana zaidi, ili kuweza kukabiliana na matatizo, changamoto na fursa mbalimbali katika ulimwengu mamboleo. Makardinali wakasindikizwa na Sala za waamini, wakashirikiana na kushikamana na matokeo yake wamempata Papa Leo XIV anayekuja mbele ya Kanisa kama ndugu anayetaka kujisadaka katika huduma ya imani, ili aweze kuwa kweli ni chemchemi ya furaha, huku wakitembea kwa pamoja katika njia ya upendo wa Mungu, anayetaka watu wote wawe wamoja kama familia moja.
Kristo Yesu baada ya mateso, kifo na ufufuko wake kwa wafu, alimkabidhi Mtakatifu Petro dhamana ya kuendeleza utume wa upendo na umoja, baada ya kumchagua na kumwimarisha kama mvuvi wa watu, sasa anaitwa na kutumwa kushusha nyavu za matumaini ya Injili, huku akiendelea kuogelea katika bahari ya maisha ya watu wa Mungu, ili wote, hatimaye, waweze kukumbatiwa na Mwenyezi Mungu. Mtakatifu Petro angeweza kutekeleza dhamana na utume huu kwa kuonja na kuguswa na upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka mintarafu nguvu na udhaifu wake wa kibinadamu. Huu ni upendo wa Kimungu, yaani “Agape” unaobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu, tofauti kabisa na ule upendo aliouonesha kwanza Mtakatifu Petro alipokuwa akimjibu Kristo Yesu, kwani kwake upendo huo ulikuwa ni kielelezo cha urafiki kati yao. Lakini Kristo Yesu alikita swali lake katika upendo wa Kimungu “Agape”, tayari kujikita katika kuwachunga kondoo wa Kristo Yesu. Upendo wa Kimungu unamsukuma Mtakatifu Petro kuwapenda zaidi ndugu zake, tayari hata kusadaka maisha yake. Kumbe, Mtakatifu Petro amepewa dhamana ya kupenda zaidi kuliko Mitume wengine wote. Amepewa dhamana ya kuwaongoza watu wa Mungu katika imani, kwa kutembea pamoja, kwani kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo hata waamini wamekuwa ni mawe hai, hivyo wanaitwa na kutumwa kujenga Nyumba ya Mungu katika udugu wa kibinadamu, amani na utulivu katika Roho Mtakatifu, huku wakizingatia tofauti zao msingi zinazojenga umoja na upendo kwa Mungu na jirani. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, ana kiu ya ujenzi wa Kanisa moja, alama ya umoja na ushirika, unaogeuka na kuwa ni chachu ya upatanisho ulimwenguni. Inasikitisha kuona kwamba, Ulimwengu mamboleo umegubikwa na mipasuko ya kijamii, madonda makubwa kutokana na chuki na uhasama, ghasia, maamuzi mbele na woga wa jirani; uchumi tenge unaonyona rasilimali za dunia kwa kuwaacha maskini wakiendelea kutumbukia katika umaskini.
Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, anataka kuwa ni chachu itakayochachua umoja, ushirika na udugu wa kibinadamu, kwa kumwangalia na kumkaribia Kristo Yesu. Kwa hakika Neno la Mungu linaangaza na kufajiri, mwaliko kwa waamini kufuata na kumwilisha ushauri wake wa upendo, ili kujenga familia kubwa ya binadamu na kuendelea kuragibisha majadiliano ya kiekumene na waamini wa Makanisa na Madhehebu mbalimbali ya Kikristo; Majadiliano ya kidini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema ili kwa pamoja wote waweze kujikita katika ujenzi wa Ulimwengu mpya ambamo amani inatawala. Hii ndiyo roho ya kimisionari inayokita mizizi yake katika upendo wa Mungu, ili kweli umoja wa watu wa Mungu kutoka katika jamii na dini mbalimbali uweze kufikiwa. Huu ni wakati wa kumwilisha Injili ya upendo kutoka kwa Mungu unaowafanya wote kuwa ni ndugu wamoja na hivyo kuishi katika amani. Baba Mtakatifu Leo XIV amehitimisha mahubiri yake kwa kuwaalika watu wote wa Mungu kwa mwanga na nguvu ya Roho Mtakatifu, kujikita katika ujenzi wa Kanisa linalosimikwa katika upendo wa Mungu, kama alama ya umoja, Kanisa la Kimisionari, linalofungua malango yake na kuukumbatia ulimwengu; Kanisa linalotangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu na hivyo kugeuka kuwa ni chachu ya amani kwa ajili ya binadamu; watu wote wa Mungu kama ndugu wamoja, watembee kumwendea Mwenyezi Mungu huku wakipendana wao kwa wao.
