Tafuta

Kanisa limeendelea kusimama kidete kuhusu: Upigaji rufuku utengenezaji, ulimbikizaji na matumizi ya silaha za maangamizi. Kanisa limeendelea kusimama kidete kuhusu: Upigaji rufuku utengenezaji, ulimbikizaji na matumizi ya silaha za maangamizi.  (ANSA)

Papa Leo XIV: Msimamo wa Kanisa Kuhusu Matumizi ya Silaha za Maangamizi

Kanisa katika maisha na utume wake limeendelea kusimama kidete kuhusu: Upigaji rufuku utengenezaji, ulimbikizaji na matumizi ya silaha za maangamizi. Anasema, kama Kiongozi anao wajibu wa kutangaza Injili inayomwilishwa katika Mafundisho Jamii ya Kanisa na wala azungumzi kama Mwanasiasa na mpinzani wa Rais Donald Trump. Tangu mwanzo wa maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro amekazia amani inayobubujika kutoka kwa Kristo Mfufuka!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mtakatifu Yohane XXIII katika Wosia wake wa Kitume, “Pacem in terris” yaani “Amani Duniani” anasema amani inasimikwa katika: ukweli, haki, upendo na uhuru. Kumbe, kuna haja ya kukuza na kudumisha utamaduni wa kuheshimu: utu, heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu sanjari na haki msingi za binadamu na kwamba, kila mtu anapaswa kuwajibika, ili kujenga na kuimarisha mafungamano ya kijamii na mahusiano pamoja na Mwenyezi Mungu. Mtakatifu Yohane wa ishirini na tatu alipoandika Waraka wake wa kitume, Amani Duniani, alikuwa na picha ya kinzani, migogoro na vita mara tu baada ya athari za Vita Kuu ya Pili ya Dunia iliyoleta maafa makubwa na mwendelezo wa vita baridi kati ya Mataifa makubwa duniani. Mtakatifu Yohane XXIII aliona kwamba, amani ilikuwa hatarini kutoweka na kwamba, kulikuwa kuna haja ya kujenga na kuimarisha misingi ya umoja na udugu wa kibinadamu kwa kuaminiana, sanjari na utunzaji bora wa mazingira kama sehemu ya mwendelezo wa kazi ya uumbaji. Kiini cha Wosia huu wa Kitume ni: maisha, utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Haya ni mambo ambayo yanapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza katika sera na mikakati ya maendeleo endelevu na fungamani na kama sehemu ya kanuni msingi katika sheria na ushirikiano wa kimataifa. Huu ndio msimamo ambao Vatican imekuwa ikiupatia msukumo wa pekee katika mikutano ya kimataifa inayojadili masuala ya haki, amani na upigaji rufuku utengenezaji, ulimbikizaji na matumizi ya silaha za maangamizi.

Silaha za maangamizi ni hatari kwa usalama wa Jumuiya ya Kimataifa
Silaha za maangamizi ni hatari kwa usalama wa Jumuiya ya Kimataifa

Kanisa Katoliki kwa upande wake, litaendelea kuhimiza umuhimu wa watu wa Mataifa kudumisha haki na amani. Kanisa linaunga mkono Kanuni na Sheria ya Kimataifa kuhusu Silaha za Nyuklia, ikiwa ni pamoja na Mkataba wa Kimataifa wa Kupiga Rufuku utengenezaji, ulimbikizaji na matumizi ya silaha za kinyuklia duniani kwa kutambua kwamba, amani ni kazi ya haki na matunda ya upendo! Amani inatishiwa sana na mashindano ya silaha; utengenezaji na biashara ya silaha pamoja na mchakato wa ulimbikizaji wa silaha duniani! Ni wajibu wa Jumuiya ya Kimataifa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha amani ambalo ni jina jipya la maendeleo fungamani ya binadamu! Hayati Baba Francisko aliwahi kusema kwamba, dunia bila kuwa na silaha za kinyuklia inawezekana kabisa na ni muhimu sana na kwamba, silaha hizi za maangamizi kamwe haziwezi kuwasaidia viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa kuwa na uhakika wa usalama wa raia na mali zao kitaifa na kimataifa. Kuna haja ya kufanya upembuzi yakinifu kuhusu madhara yake katika maisha ya watu sanjari na mazingira; kwa kuondoa hofu, mazingira ya kutoaminiana, chuki na uhasama vinavyozungumza “dhana ya silaha za nyuklia.”

Madhara ya Silaha za Nyuklia ni makubwa sana kwa Jumuiya ya Kimataifa
Madhara ya Silaha za Nyuklia ni makubwa sana kwa Jumuiya ya Kimataifa   (AFP or licensors)

Jumuiya ya Kimataifa haina budi kujielekeza zaidi katika kubuni sera na mikakati itakayosaidia utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu ifikapo mwaka 2030. Wosia huu wa Kitume wa Amani Duniani una utajiri mkubwa wa Maandiko Matakatifu kuhusu amani, kuwa ni zawadi kubwa ambayo Mwenyezi Mungu amempatia mwanadamu na kwamba, amani ni jina linalomwelekea Mungu mwenyewe. Amani ni neno linalowakilisha ukamilifu na lengo la maisha ya mwanadamu, kama anavyobainisha Yesu Mwenyewe kwa njia ya maisha na utume wake. Ikumbukwe kwamba, amani ni tunda la haki na mapendo. Amani ni sehemu ya mchakato wa kila siku ya maisha ya mwanadamu inayojikita katika utafutaji wa utaratibu wa muafaka kadiri ya mapenzi ya Mungu na kwamba, amani inapatikana ikiwa kila mtu atajitahidi kutekeleza wajibu wake, kwa kuzingatia: ukweli, upendo, upatanisho na utawala wa sheria. Kushindwa kwa mchakato wa amani matokeo yake ni vita!

Kanisa linapinga utengenezaji, usambazaji na matumizi ya silaha za maangamizi
Kanisa linapinga utengenezaji, usambazaji na matumizi ya silaha za maangamizi   (AFP or licensors)

Waraka wa Amani Duniani ni dira na mwongozo makini katika mchakato wa kujenga na kuimarisha haki na amani duniani, hasa wakati huu wa ulimwengu wa utandawazi na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia. Hii ni changamoto ya kudumisha ushirikiano wa kimataifa unaooongozwa na kanuni ya auni kwa ajili ya kutafuta mafao ya wengi, kulinda na kutetea haki msingi, utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Watu wana haki na wajibu wa kujenga na kuimarisha amani kwa kutoa kipaumbele cha kwanza katika haki msingi za binadamu na maendeleo endelevu yanayozingatia mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Rais Donald Trump wa Marekani amerejea tena kutoa shutuma dhidi ya Baba Mtakatifu Leo XIV kuhusu ukimya unaooneshwa na Baba Mtakatifu mintarafu Iran kumiliki silaha za nyuklia, hali ambayo inahatarisha usalama wa Jumuiya ya Kimataifa. Baba Mtakatifu Leo XIV akijibu shutuma hizi, Jumanne, tarehe 5 Mei 2026 wakati akitoka kwenye Ikulu Ndogo ya Castel Gandolfo amesema, ikiwa kama kuna mtu anataka kumshutumu na afanye hivyo kwa kuzingatia ukweli. Kanisa Katoliki katika maisha na utume wake limeendelea kusimama kidete kuhusu: Upigaji rufuku utengenezaji, ulimbikizaji na matumizi ya silaha za maangamizi. Anasema, kama Kiongozi wa Kanisa Katoliki anao wajibu wa kutangaza Injili inayomwilishwa katika Mafundisho Jamii ya Kanisa na wala azungumzi kama Mwanasiasa na mpinzani wa Rais Donald Trump wa Marekani. Tangu mwanzo kabisa wa maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro amekazia amani inayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu Mfufuka.

Papa Leo XIV ni Mjumbe na Shuhuda wa Amani.
Papa Leo XIV ni Mjumbe na Shuhuda wa Amani.   (@Vatican Media)

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Marco Rubio, Alhamisi tarehe 7 Mei 2026 anakutana na Baba Mtakatifu Leo XIV kwa faragha mjini Vatican. Baba Mtakatifu anatumaini kwamba, mazungumzo kati yake na Marko Rubio yatakuwa n ana afya na tija, ili hatimaye kuweza kufikia hali ya kuaminiana inayosimikwa katika ukweli na uwazi. Katika siku za hivi karibuni, Rais Donald Trump wa Marekani amekuwa akimshutumu Baba Mtakatifu Leo XIV juu ya msimamo wake kuhusu Iran, vitendo vya kigaidi, sera na mikakati kwa ajili ya wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta: usalama, hifadhi na maisha bora zaidi nchini Marekani. Baba Mtakatifu Leo XIV daima amejibu kwamba, Mwenyezi Mungu hajibu sala za watu wanaochochea vita. Kama anavyosali Mtakatifu Francisko wa Assisi, kila mtu anapaswa kuwa kweli ni chombo cha amani. Jumuiya ya Kimataifa isimame kidete kuwalinda na kuwatetea maskini kwa kuwa kweli madaraja ya amani na wala si kinzani, migogoro na vita vinavyosababisha maafa makubwa kwa jamii. Watu wajenge na kuimarisha utamaduni wa majadiliano unaosimikwa katika ukweli, uwazi, heshima na mafao ya wengi. Viongozi wa kidini wanapaswa kuonesha utashi wa kufanya majadiliano ya kina, ili amani iweze kutawala na kudumu akili na katika nyoyo za watu.

Msimamo wa Kanisa Kuhusu Silaha
06 Mei 2026, 15:57