Papa Leo XIV: Miaka 40 ya Mfuko wa Yohane Paulo II Kwa Ajili ya Sahel
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Mfuko wa Yohane Paulo II kwa Ajili ya Sahel "Fondazione Giovanni Paolo II per il Sahel" na Kwa Kiingereza ni “John Paul II Foundation for the Sahel” unatoa huduma na kuchangia maendeleo fungamani ya wananchi walioko kwenye Ukanda wa Sahel pasi na ubaguzi wa kidini au wa kikabila, kwani wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Mfuko huu ni kielelezo makini cha ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo kadiri ya maelekezo ya Khalifa wa Mtakatifu Petro. Ukanda wa Sahel unakabiliwa na changamoto nyingi za maisha; hapa ni eneo ambalo lina misigano mikali ya kidini na kisiasa; mambo yanayoleta changamoto kubwa katika mchakato wa upatanisho, haki, amani na utulivu. Katika machafuko na kinzani za namna hii katika Ukanda wa Sahel, ushuhuda na mshikamano wa upendo ni mambo msingi sana yanayopewa kipaumbele cha kwanza na Mama Kanisa kama sehemu ya mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili.
Huu ni mwaliko wa kuendeleza majadiliano ya kidini, kwa kutambua kwamba, Kanisa linapenda kuwa ni chombo cha haki, amani na upatanisho kati ya Watu wa Mataifa; ili kwa pamoja waweze kujifunga kibwebwe kupambana na Jangwa ambalo linazidi kutishia: maisha, ustawi na maendeleo ya wananchi wa Ukanda wa Sahel. Hili ndilo lengo kuu lililomsukuma Mtakatifu Yohane Paulo II kuamua kuanzisha Mfuko wa Yohane Paulo II kwa Ajili ya Sahel, ili kusaidia kukoleza mchakato wa maendeleo ya watu katika Ukanda huu tarehe 22 Februari 1980. Mtakatifu Yohane Paulo II aliwataka wajumbe wa Mfuko huu kuhakikisha kwamba, wanajielekeza zaidi katika mafunzo makini kwa wadau ambao watasimama kidete kupambana vyema na: uchafuzi na uharibifu wa mazingira, hali ambayo inachangia kwa kiasi kikubwa kuenea kwa Jangwa la Sahel. Ukame wa kutisha katika Ukanda wa Sahel ni matokeo pia ya mabadiliko ya tabianchi, hali ambayo imesababisha maafa makubwa kwa watu na mifugo yao.
Ni katika muktadha wa maendeleo na ustawi wa Mfuko wa Yohane Paulo II kwa Ajili ya Sahel, Baba Mtakatifu Leo XIV Jumamosi, tarehe 9 Mei 2026 amekutana na kuzungumza na wajumbe wa Mfuko wa Yohane Paulo II kwa Ajili ya Sahel na kukazia umuhimu wa kutafuta na kudumisha Injili ya amani kwa watu wa Mataifa na kwamba, hii ni mara ya kwanza kwake kukutana na kuzungumza na wajumbe wa Mfuko huu kwa kuwapongeza viongozi wakuu wa Mafuko huu kwa kutekeleza dhamana na majukumu yao kwa mtindo wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi na Kimisionari, huku wakishirikiana na Baraza la Kipapa la Maendeleo Fungamani ya Binadamu, Sekretarieti kuu ya Vatican pamoja na Sekretarieti ya Uchumi ya Vatican pamoja na Taasisi nyinginezo, tayari kuanza safari mpya inayokita upyaisho wake katika amana na utume wa Mfuko huu. Mfuko huu unaadhimisha kumbukizi ya Miaka 40 tangu kuasisiwa kwake na Mtakatifu Yohane Paulo II, ni kipindi ambacho Mfuko umekumbana na changamoto za uchumi Kimataifa na ndiyo maana hivi karibuni, kumepitishwa Sheria, Kanuni na Taratibu mpya chini ya usimamizi wa Vatican pamoja na uchaguzi mkuu uliofanyika Mwezi Februari 2026 huko Dakar, Senegal.
Hiki ni kielelezo cha upendo wa Mama Kanisa kwa watoto wake walioko Afrika Magharibi kama alivyosema Mtakatifu Yohane Paulo II mjini Ouagadougou, wakati wa kuzindua Mfuko huu. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, katika Ulimwengu ambao unakabiliwa na changamoto ya mivutano ya kijiografia, ukosefu wa usawa, vita, kinzani na migogoro; Ukosefu wa usalama, vitendo vya kigaidi; Machafuko ya kisiasa na kiuchumi; athari za mabadiliko ya tabianchi matokeo yake ni pamoja na ongezeko la wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani. Kumbe, Mfuko huu pamoja na mambo mengine unapenda kukuza na kudumisha dhamiri yake kuu ya utunzaji wa mazingira nyumba ya wote pamoja na kuendelea kutekeleza wajibu wake wa kijamii, kama Taasisi ya Kipapa mintarafu maono ya Muasisi wake na kadiri ya Katiba mpya.Baraza la Kipapa la Maendeleo Fungamani ya Binadamu litaendelea kuwa ni chombo muhimu cha kisheria kwa ajili ya Mfuko huu na kwamba, ushirikiano na Baraza hili utakita mizizi yake kama sehemu ya ujenzi wa Kanisa la Kisinodi na Kimisionari kwa kuendelea kushirikiana na kushikamana na Mabaraza pamoja na Taasisi nyingine za Vatican, ili kuweza kuchangia katika kulinda na kudumisha utu, heshima na haki msingi za watu waliko katika Ukanda wa Sahel kwa njia ya utekelezaji wa Miradi ya maendeleo fungamani ya binadamu. Mbele yao kuna changamoto nyingi zinazoweza kutatuliwa kwa moyo wa Kisinodi kwa kuendelea kujikita katika utekelezaji wa majukumu yao bila kupoteza Injili ya matumaini.
