Tafuta

Maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu, kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaombea wale wote waliofariki dunia kutokana na tetetemeko la ardhi miaka 50 iliyopita kwenye Manispaa ya Friuli Maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu, kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaombea wale wote waliofariki dunia kutokana na tetetemeko la ardhi miaka 50 iliyopita kwenye Manispaa ya Friuli  (©Rhombur - stock.adobe.com)

Papa Leo XIV: Kumbukizi ya Miaka 50 Ya Tetemeko la Ardhi Friuli: Mshikamano!

Papa Leo XIV katika ujumbe ulioandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican na kusomwa na Askofu mkuu Riccardo Lamba wa Jimbo kuu la Udine, anasema, anapenda kuungana na watu wa Mungu katika eneo hili katika maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu, kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaombea wale wote waliofariki dunia kutokana na tetetemeko la ardhi miaka 50 iliyopita kwenye Manispaa ya Friuli, Kaskazini Mashariki mwa Italia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Ilikuwa ni tarehe 6 Mei 1976 majira ya saa 3:00 Usiku kwa Saa za Ulaya, miaka 50 iliyopita, wakati tetemeko la ardhi lenye ukubwa wa 6.5 kwenye kipimo cha Richter, lililochukua sekunde 57 zisizoweza kukatika, na kitovu chake cha kwanza kikiwa chini ya Mlima Simeone, kisha kuenea huko Lusevera. Tetemeko hili liliharibu mji wa Gemona na kusababisha maafa makubwa katika Manispaa ya Friuli iliyoko Kaskazini Mashariki mwa Italia. Takwimu zinaonesha kwamba, watu zaidi ya 1, 000 walifariki dunia, majeruhi walikuwa ni zaidi ya watu 2,500 na kwamba, tetemeko hili liliwaacha watu 60, 000 wakiwa hawana makazi ya kuishi.

Kumbukizi ya Miaka 50 ya Tetetemeko la Ardhi Manisapaa ya Friuli
Kumbukizi ya Miaka 50 ya Tetetemeko la Ardhi Manisapaa ya Friuli   (ANSA)

Kardinali Matteo Maria Zuppi, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI, Dominika tarehe 3 Mei 2026 ameongoza Ibada ya Misa Takatifu kama sehemu ya kumbukizi ya tetemeko la ardhi lililoikumba Manispaa ya Friuli, miaka 50 iliyopita. Ibada hii imeadhimishwa kwenye Kambi ya Goi-Pantanali moja wapo ya maeneo yaliyoathirika vibaya na tetetemeko la ardhi la Mwaka 1976 na Mtakatifu Yohane Paulo II akabahatika kutembelea eneo hili wakati wa hija yake ya kichungaji kunako mwaka 1992. Baba Mtakatifu Leo XIV katika ujumbe ulioandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican na kusomwa na Askofu mkuu Riccardo Lamba wa Jimbo kuu la Udine, anasema, anapenda kuungana na watu wa Mungu katika eneo hili katika maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu, kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaombea wale wote waliofariki dunia kutokana na tetetemeko la ardhi miaka 50 iliyopita.

Kumbukizi ya Miaka 50 ya Tetemeko la Ardhi Friuli: Mshikamano
Kumbukizi ya Miaka 50 ya Tetemeko la Ardhi Friuli: Mshikamano   (ANSA)

Hii imekuwa ni fursa ya kuwashukuru wale wote ambao wameonesha mshikamano wa udugu wa kibinadamu kwa hali na mali na hivyo kuendelea kushirikiana na kushikamana na Jumuiya ya watu mahalia, katika ujenzi wa makazi mapya na upyaisho wa maisha ya kiraia. Baba Mtakatifu Leo XIV amependa kuwahakikishia watu wa Mungu katika eneo hili uwepo wake wa karibu kwa wale wote waliopoteza maisha, ametoa neno la faraja kwa familia ambazo hadi sasa zinaendelea kubeba makovu ya kuondokewa na ndugu, jamaa na marafiki zao. Kumbukizi hii iwe ni chachu ya kujenga na kudumisha mshikamano wa upendo wa kibinadamu na kikristo, kwa wale wote walioguswa na kutikiswa na tukio hili ndani na nje ya Italia. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Leo XIV kwamba, maafa haya makubwa yatasaidia kupyaisha tunu msingi za udugu wa kibinadamu na ujenzi wa Injili ya upendo. Mwishoni mwa ujumbe wake, Baba Mtakatifu Leo XIV amewaweka watu wote wa Mungu walioko kwenye manispaa ya Friuli, chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria pamoja na ya watakatifu Ermacora na Fortunato na hatimaye, akawapatia baraka zake za kitume.

Tetemeko la Ardhi
04 Mei 2026, 14:48