Tafuta

Mwaka 2026 Idara ya Uchapaji ya Vatican, LEV inamwimbia Mwenyezi Mungu kwa kuadhimisha Jubilei ya Miaka 100 tangu kuanzishwa kwake. Mwaka 2026 Idara ya Uchapaji ya Vatican, LEV inamwimbia Mwenyezi Mungu kwa kuadhimisha Jubilei ya Miaka 100 tangu kuanzishwa kwake.  (@VATICAN MEDIA)

Jubilei ya Miaka 100 Tangu Kuanzishwa Kwa Idara ya Uchapaji Vatican: 1926-2026

Papa Leo XIV amekutana na Familia ya Idara ya Uchapaji ya Vatican, LEV kwa kukazia mambo makuu matatu: Fikara, Kukutana na hatimaye ni Kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema vitabu ni fursa ya kufikiria. Katika Ulimwengu wa kidijitali, vitabu humkumbusha mwanadamu jukumu la mawazo, kutafakari na kusoma, kwani kusoma kunakuza akili, husaidia kustawisha umakinifu zaidi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Idara ya Uchapaji ya Vatican “Libreria Editrice Vaticana” kwa kifupi “LEV” ilianzishwa na Papa Pio XI kunako mwaka 1926 lakini chimbuko lake ni katika mwaka 1587 ikiwa na jukumu na dhamana ya kuchapisha, kusambaza na kuhifadhi: Hati na Nyaraka za Mababa Watakatifu; Mamlaka fundishi ya Kanisa, yaani “Magisterium” ambayo kimsingi ni uwezo na wajibu maalum wa Kanisa Katoliki, uliotolewa na Kristo Yesu: wa kufundisha, kufafanua, na kulinda kweli za imani na maadili. Hii ni Idara inayohifadhi pia hati na nyaraka zinazotolewa na Mabaraza ya Kipapa pamoja na Taasisi za Kipapa. Mwaka 2026 Idara ya Uchapaji ya Vatican inamwimbia Mwenyezi Mungu kwa kuadhimisha Jubilei ya Miaka 100 tangu kuanzishwa kwake na kwamba,  Jubilei ni kipindi maalum cha kiroho na kihistoria, kinachoelezewa kama wakati muafaka wa kuyatafakari yaliyopita kwa moyo wa shukrani, kuyaishi ya sasa kwa hamasa, na kuyakumbatia yajayo kwa moyo wa matumaini.

Jubilei ya Miaka Mia Moja tangu Kuanzishwa kwa LEV
Jubilei ya Miaka Mia Moja tangu Kuanzishwa kwa LEV   (@VATICAN MEDIA)

LEV katika maisha na utume wake kwa Miaka 100, imewahudumia Mapapa tisa kwa kuchapisha, kusambaza na kuhifadhi Mamlaka fundishi ya Kanisa, yaani “Magisterium.” Baba Mtakatifu Leo XIV Alhamisi tarehe 7 Mei 2026 amekutana na Familia ya Idara ya Uchapaji ya Vatican, LEV kwa kukazia mambo makuu matatu: Fikara, Kukutana na hatimaye ni Kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema vitabu ni fursa ya kufikiria. Katika Ulimwengu wa kidijitali, vitabu humkumbusha mwanadamu jukumu la mawazo, kutafakari na kusoma, kwani kusoma kunakuza akili, husaidia kustawisha umakinifu na inayoundwa vizuri; na hulinda dhidi ya mwanadamu kutafuta njia za mkato na za kiitikadi, ndiyo maana Baba Mtakatifu anawahimiza watu wote kusoma vitabu kwani hii ni zana yenye nguvu sana katika kuvunja fikra funge (rigid mindset) na kupunguza mitazamo migumu inayosababisha chuki au maoni ya kupunguza ukweli (bias).

Vitabu ni madaraja ya kuwakutanisha watu; kusoma kunakuza akili
Vitabu ni madaraja ya kuwakutanisha watu; kusoma kunakuza akili   (@Vatican Media)

Baba Mtakatifu Leo XIV anasema vitabu ni fursa ya kukutana na wengine, ni nafasi ya kukutana na Mwandishi na wale waliokisoma kabla au wale watakaokisoma baadaye; ni fursa ya kukutana na kujadiliana, inayokuza na kudumisha utamaduni wa watu kujadiliana na kusikilizana na huu ni mwanzo wa utamaduni wa watu kukutana kama anavyokazia Hayati Baba Mtakatifu Francisko. Kumbe, vitabu ni daraja la kuwakutanisha watu, chanzo cha mijadala yenye kurutubisha, kuchochea na kupanua mitazamo ya watu. Hatimaye, Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, kwa Wakristo vitabu ni fursa ya kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Ni fursa inayotolewa kwa ajili ya kusoma wasifu wa Mtakatifu au tafakari ya maisha ya kiroho kama inavyooneshwa na Mtakatifu Anthony wa Padua katika Fumbo la Umwilisho, akionesha “Nia ya Kusoma Maandiko Matakatifu.” Mtakatifu Anthony wa Padua anashikilia Injili iliyofunguliwa, ambapo Mtoto Yesu amesimama. Mara nyingi tunamwona Mtakatifu Augustino, Askofu na Mwalimu wa Kanisa akiwa ameketi kwenye meza mbele ya kitabu kikubwa, na wakati mwingine anashikilia moyo mkononi mwake kielelezo cha ukweli na upendo. Waamini katika Shule ya Bikira Maria na Watakatifu wajitahidi kulishwa na Neno la Mungu ili kuunda mawazo na matendo yao.  Baba Mtakatifu Leo XIV amewahimiza "kuangalia mbele, kuendeleza mawazo na programu kwa ajili ya siku zijazo." Mwishoni, Baba Mtakatifu Leo XIV amewashukuru wafanyakazi wa Idara ya Uchapishaji kwa kazi kubwa wanayoifanya na ana matumaini kwamba wataendelea kufanya kazi hii kwa juhudi, bidii na maarifa.

Idara ya Uchapaji ya Vatican
07 Mei 2026, 15:23