Hija ya Kichungaji Pompei na Napoli: Hotuba Kwa Viongozi wa Kanisa na Wananchi
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Leo XIV anaadhimisha Kumbukizi ya Mwaka mmoja tangu alipochaguliwa kuliongoza Kanisa Moja, Takatifu, Katoliki na la Mitume, tarehe 8 Mei 2026 kwa kutembelea Madhabahu ya Bikira Maria wa Pompei, yaliyoko Jimbo kuu la Napoli, Kusini mwa Italia mahali: Pa upendo wa Mungu unaotoa joto kwa wale waliovunjika na kupondeka mioyo; ni mahali ambapo imani na upendo vina tamalaki. Ilikuwa ni tarehe 8 Mei 2025 Baba Mtakatifu Leo XIV alipokabidhiwa dhamana ya: Kuongoza, Kufundisha na Kuwatakatifuza watu wa Mungu kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, Siku ya Sala maalum kwa ajili ya Bikira Maria wa Pompei. Kumbe, hija hii ya kitume inapania pamoja na mambo mengine, kuiweka huduma na utume wa kichungaji unaotekelezwa naye kama Khalifa wa Mtakatifu Petro chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria wa Pompei na kwamba, katika maisha na utume wake, anaendelea kufuata nyayo za Papa Leo XIII, ambaye pamoja na mambo mengine, ni Kiongozi wa Kanisa aliyejibidiisha kuweka msingi wa Mamlaka fundishi ya Kanisa yaani “Magisterium” kuhusu Rozari Takatifu pamoja na yeye mwenyewe kumtangaza Mwenyeheri Bartolo Longo, Mtume wa Rozari Takatifu kuwa ni Mtakatifu.
Baba Mtakatifu Leo XIV baadaye alitembelea Kanisa kuu la Jimbo kuu la Napoli na kutoa heshima yake kwa masalia ya Mtakatifu Gennaro (San Gennaro) Msimamizi na Mwombezi wa Jimbo Kuu la Napoli, Italia, na sherehe zake ni muhimu sana katika amana na urithi wa utamaduni na imani ya watu wa Mungu mjini Napoli na kwamba kila mwaka ifikapo tarehe 19 Septemba Jimbo kuu la Napoli huadhimisha sherehe kubwa ambapo muujiza wa kuyeyuka kwa damu ya Mtakatifu Gennaro hutokea. Chimbuko la imani hii, ni kunako karne 17 wakati kulipotokea janga la Volkano ya Mlima Vesuvius mwaka 1631. Hija hii ya kichungaji ya Baba Mtakatifu Leo XIV ilikuwa ni fupi lakini ilibeba uzito wa pekee katika maisha na utume wa Kanisa Jimbo kuu la Napoli. Huu ni mji ambao una utajiri mkubwa wa sanaa na utamaduni na kwamba watu wake ni mashuhuda wa furaha inayobubujika kutoka katika sakafu ya nyoyo zao licha ya matatizo na changamoto za maisha.
Katika moyo wa urafiki na udugu wa kibinadamu, Baba Mtakatifu Leo XIV amewatia shime Wakleri na Watawa katika safari ya maisha yao sanjari na kuwapatia wosia katika maisha ya kikanisa na katika shughuli za kichungaji. Kama ilivyokuwa kwa wale wanafunzi wa Emau waliokuwa wamevunjika moyo na kukata tamaa, kama ilivyo pia kwa makleri na watawa wanapokumbana na changamoto na matatizo katika maisha na shughuli zao za kichungaji, wakati mwingine wanakata na kukatishwa tamaa, kiasi cha kuhisi uchungu na huzuni moyoni, lakini watambue kwamba, Kristo Yesu anawajali, anatembea na kuambatana nao katika hija ya maisha yao, changamoto na mwaliko kwa wakleri na watawa kutopuuza maisha, bali wajitahhidi kuutunza uzuri na heshima yake kwa kutambua umuhimu wa huduma ya ndani inayogusa mioyo, utu na mahusiano yao na wale wanaowazunguka. Kanisa linapaswa kuwa ni kielelezo cha huduma bora ya uongozi, kwa kuwajali na kuwahudumia maskini; kwa kuendelea kumwilisha ndani mwake tunu msingi za Kiinjili, kama chemchemi ya matumaini kwa wale waliovunjika na kupondeka moyo na hasa vijana wa kizazi kipya wanaopaswa kusindikizwa katika maisha yao: kiroho na kimwili na katika kutafuta na kupata mahitaji yao msingi.
Baba Mtakatifu anawataka viongozi wa Kanisa kujibidiisha kuboresha maisha yao ya ndani, kwa kukuza na kudumisha uhusiano wao na Kristo Yesu kwa njia ya Sala; Utamaduni wa kumsikiliza na kuhojiana na Yesu katika Maandiko Matakatifu na Dhamiri nyofu. Wajitahidi kuboresha maisha na utume wao; kwa kushirikishana katika shughuli za kichungaji, ili hatimaye kushinda kishawishi cha kutumbukia katika uchoyo na ubinafsi, kumbe wanapaswa kujenga utamaduni wa ujirani mwema; udugu wa kibinadamu unaojikita katika utume na mtindo wa maisha ya kimisionari ili kukuza ushirika. Watambue kwamba, Kanisa ni Fumbo la Ushirika na kwa njia ya Ubatizo kila mwamini anapaswa kuwa jiwe hai katika ujenzi wa Kanisa, mtume wa Injili na shuhuda amini wa Ufalme wa Mungu. Maadhimisho ya Sinodi ya Jimbo kuu la Napoli, imekuwa ni fursa ya kutafakari jinsi ya kuwa ni mashuhuda na watangazaji bora wa Injili ya Kristo Yesu.
Huu ni mwaliko wa kuendelea kujikita katika utamaduni wa kusikiliza, ushirikishwaji wa watu wote wa Mungu katika maisha na utume wa Kanisa na kwamba, kwa kudumisha utamaduni wa kusikiliza kwa makini, hapo kunaibuliwa; matumaini ya watu wa Mungu, madonda na machungu ya moyo na hii inakuwa ni fursa kwa Kanisa kufanya wongofu wa ndani katika mtindo wake wa maisha na kujimwilisha katika maisha ya watu wa Mungu, ili kuliwezesha Kanisa kuwa ni mwanga wa matumaini. Huu ni mwaliko wa kujenga utamaduni wa kusikiliza, kutembea kwa pamoja, kwa kuhakikisha kwamba, karama na mapaji mbalimbali yanatumika kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa linalojitambua kuwa ni la Kisinodi na Kimisionari. Jiji la Napoli, linatambulikana kwa ukosefu wa usawa, kiwango kikubwa cha ukosefu wa fursa za ajira miongoni mwa vijana wa kizazi kipya, uwepo wa kiwango kidogo sana cha wanafunzi wanaosoma pamoja na familia zinazokumbana na matatizo na changamoto mbalimbali za maisha. Hali zote hizi zinahitaji kujibiwa na utangazaji wa Injili shirikishi, Ushuhuda wenye mvuto na mashiko unaoweza kuwasaidia watu wa Mungu kuishi kikamilifu tunu msingi za Kiinjili, ili kupyaisha maisha ya Jiji la Napoli. Watambue kwamba, wao ni mashuhuda wa Jiji la Napoli, Mashuhuda wa Kristo Yesu na wapandikizaji wa Injili ya matumaini kwa watu wa Mungu Jimboni Napoli.
Kwa upande wake Kardinali Domenico Battaglia, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Napoli akimkaribisha Baba Mtakatifu Leo XIV kuzungumza na Wakleri na Watawa amesema kwamba: hili ni Kanisa ambalo linajengwa na nyuso za watu mbalimbali wenye historia na waaminifu, kumbe ni Kanisa linalosafiri; Ni Kanisa ambalo limegeuka kuwa ni sauti ya kinabii kwa wale wasiokuwa na sauti; Ni Kanisa linalohudumia na kuendelea kuwa ni mbegu ya matumaini ya Injili na mapendo yanayomwilishwa katika huduma, faraja pamoja na kuganga madonda ya watu wa Mungu; Ni huduma ya upendo inayotolewa kwenye familia, Kanisa dogo la nyumbani; kwa vijana wanaotamani kupata utimilifu wa maisha. Hili ni Kanisa linalotangaza na kushuhudia imani yake kwa Kristo Yesu kwa njia ya: Sala, Ibada na kwamba, imani ni zawadi kutoka kwa Mungu. Uwepo angavu wa Baba Mtakatifu Leo XIV Jimboni mwao ni kielezo cha mchakato wa kutafuta na kuambata amani ya kudumu, kwa kuendelea kushuhudia na kutangaza uwepo angavu wa Kristo Mfufuka kati yao, Kristo anayeendelea kumega Mkate pamoja nao!
Baba Mtakatifu Leo XIV akizungumza na watu wa Mungu Jijini Napoli, Kusini mwa Italia, amesema hili ni Jiji ambalo limesheheni majeraha, umaskini na hofu; watu wake wamechoka na kuchanganyikiwa pamoja na hali ya kukata na kujikatia tamaa. Lakini kama ilivyokuwa kwa Kristo Yesu kuzungumza na kuwaangaza waja wake kwa njia ya Injili ya Wafuasi wa Emau, waliokuwa wamevunjika na kupondeka moyo kutokana na Kashfa ya Fumbo la Msalaba, yaani mateso na kifo cha Kristo Msalabani, hata leo hii, Kristo Yesu anataka kuwaonesha ukaribu wake na kutembea pamoja nao katika hija ya maisha kwa kujikita katika kutenda wema na haki kwa kuondokana na hofu ya maovu sanjari na uponyaji wa majeraha. Ni Jiji ambalo linajengwa katika jiografia ya ukosefu wa haki, na umaskini unaosigina utu, heshima na haki msingi za binadamu; ukosefu wa fursa za ajira hasa kwa vijana wa kizazi kipya pamoja na ukosefu wa miundo mbinu makini kwa ajili ya huduma kwa watu wa Mungu na matokeo yake ni kushamiri kwa uhalifu wa kupangwa unaohusisha mitandao ya uhalifu, matumizi haramu ya dawa za kulevya, rushwa na ufisadi wa mali ya umma. Hizi ni hali zinazoelemea maisha ya watu wengi Jijini Napoli. Kumbe, ni dhamana na wajibu wa Serikali kuhakikisha kwamba, raia wake wanapata usalama wa maisha na mali zao pamoja na kuendelea kuthamini jitihada zinazotekelezwa na Serikali katika medani mbalimbali.
Baba Mtakatifu Leo XIV anawakumbusha watu wa Mungu Jijini Napoli kwamba: haki, ukweli na uzuri ni mambo yanayojengeka katika medani mbalimbali za maisha ya watu, kumbe, kuna haja ya kuwaunganisha watu, ili wafanye kazi kwa njia ya mtandapo, ili kuunda jumuiya. Hayati Baba Mtakatifu Francisko tarehe 15 Oktoba 2020 alizindua Mkataba wa Mfumo Mpya wa Elimu Kimataifa (Global Compact on Education) unaolenga pamoja na mambo mengine: Kupyaisha elimu, ili iweze kusimikwa katika utu, utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Mkataba unahiomiza ushirikiano wa Kimataifa ili kujenga udugu wa kibinadamu, kutoa kipaumbele cha pekee kwa vijana wa kizazi kipya sanjari na kupambana na “janga la elimu makini” kwa kutoa mafunzo yanayo kita mizizi yake katika kanuni maadili na utu wema. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, huu ni mchango mkubwa unaotolewa na Kanisa, changamoto na mwaliko wa kuendeleza Mkataba wa Mfumo Mpya wa Elimu Kitaifa, kwa kuunganisha nguvu kwa kushirikiana Kanisa na Serikali pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo katika sekta ya elimu, ili kuliwezesha Jiji la Napoli kuwa ni mji mkuu wa utu na matumaini.
Napoli inapaswa pia kujikita katika ujenzi wa amani na kwamba, amani ni tunda la haki inayomwilishwa katika huduma. Huu ni mwaliko kwa watu wa Mungu Jijini Napoli kujenga utamaduni wa majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni. Napoli inaendelea kutangaza na kushuhudia utamaduni wake wa ukarimu kwa wageni, wahamiaji na wakimbizi, kielelezo cha Injili ya matumaini. Baba Mtakatifu Leo XIV amesikiliza shuhuda za wenyeji wa Napoli jinsi ambavyo uhalifu unavyoweza kuzima ndoto ya mtu, lakini kwa imani na matumaini, maisha yanaweza kuchipua na kuendelea. Pili ni umuhimu wa kushirikishana matatizo, changamoto na fursa mbalimbali ili kutangaza na kuenzi Injili ya matumaini kwa wale waliovunjika na kupondeka moyo! Baada ya hotuba na shuhuda zote hizi, Baba Mtakatifu Leo XIV alisali Sala ya Kuliweka Jiji la Napoli chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa.
