Tafuta

Baba Mtakatifu Leo XIV Ijumaa tarehe 8 Mei 2026 amekutana na kuzungumza na wagonjwa na walemavu waliomiminika kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Pompei Baba Mtakatifu Leo XIV Ijumaa tarehe 8 Mei 2026 amekutana na kuzungumza na wagonjwa na walemavu waliomiminika kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Pompei   (@Vatican Media)

Hija ya Kichungaji Pompei na Napoli: Wagonjwa na Walemavu

Papa Leo XIV tarehe 8 Mei 2026 amekutana na wagonjwa na walemavu waliomiminika kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Pompei kwa wingi bila kujali matatizo na changamoto za maisha yao, kielelezo makini cha nguvu ya imani na upendo kwa Bikira Maria. Baba Mtakatifu Leo XIV ametoa mwaliko kwa wagonjwa na walemavu kumkumbuka na kumwombea kwa ajili ya nia zake mbalimbali na kwamba, kwa hakika wao ni wadau wa Sala na Tafakari ya Rozari Takatifu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kanisa kama Mama na Mwalimu “Mater et magistra” anawakumbusha watoto wake kuwa wakarimu na watu wenye upendo kwa wagonjwa. Wawe mstari wa mbele katika kuwajali na kuwatunza wagonjwa wanaohitaji kuonjeshwa utaalam na weledi; upole, unyoofu na unyenyekevu kwa kujisadaka bila ya kujibakiza, ili wagonjwa waweze kutambua kwamba, wanapendwa na kuthaminiwa! Baba Mtakatifu Francisko anaonya kwamba, maisha ya binadamu kamwe hayawezi kubinafsishwa hasa kutokana na maendeleo makubwa ya sayansi ya tiba ya mwanadamu na teknolojia yanayotoa kishawishi cha watu kutaka kuchezea maisha. Katika ulimwengu wa utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine, ukarimu ni zawadi ambayo inapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza, kwani hii ni asili ya Mungu na kilele cha ukarimu wa Mungu ni katika Fumbo la Umwilisho pamoja na Roho Mtakatifu kuwashukia Mitume. Kila mwanadamu ni maskini, mhitaji na fukara na daima ataendelea kubaki kuwa tegemezi katika hali mbali mbali za maisha, hivyo unyenyekevu uwasaidie watu kukubali udhaifu na hivyo kuwa tayari kushirikiana na kufungamana na wengine kama tendo la fadhila katika maisha. Hali hii itasaidia kukuza mema kwa mtu binafsi na jamii katika ujumla wake pamoja na kuungana ili kukuza umoja unaojali na kuguswa na mahangaiko ya wengine.

Mshikamano wa sala na huduma kwa wagonjwa na maskini
Mshikamano wa sala na huduma kwa wagonjwa na maskini   (@Vatican Media)

Maandiko Matakatifu yanaonesha kwamba, Yesu katika maisha na utume wake alikutana, aliwapokea na kuwakaribisha wagonjwa na wakati mwingine aliwafuata huko walikokuwa ili kukutana nao, kuwaonesha na hatimaye, kuwaonjesha huruma na upendo wake kama mama mzazi afanyavyo kwa mtoto wake. Huu ni mwaliko kwa waamini kuonesha ukaribu, huruma na upendo kwa wagonjwa; kwa njia ya ukimya na sala ili kujenga na kudumisha utamaduni wa ukarimu, kwani waathirika wakubwa wa utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine ni wagonjwa, hali inayoonesha ukatili mkubwa. Kumbe, kuna haja ya kukuza na kudumisha utamaduni wa ukarimu na matendo yanayobubujika kutoka katika tunu msingi za maisha ya Kikristo, upendo wa Kristo Mfufuka na Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa. Huduma kwa wagonjwa inapaswa kufumbatwa katika huruma na mapendo, ili kukua na kukomaa katika utu na kuwafungulia njia ya maisha ya uzima wa milele. Mwamini anayemwilisha matendo ya huruma katika maisha yake, hana sababu ya kuogopa kifo!

Waamini wawe mstari wa mbele kuwajali na kuwahudumia wagonjwa
Waamini wawe mstari wa mbele kuwajali na kuwahudumia wagonjwa   (@Vatican Media)

Ni katika muktadha huu wa huduma na sala kwa wagonjwa, Baba Mtakatifu Leo XIV Ijumaa tarehe 8 Mei 2026 amekutana na kuzungumza na wagonjwa na walemavu waliomiminika kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Pompei kwa wingi bila kujali matatizo na changamoto za maisha yao, kielelezo makini cha nguvu ya imani na upendo kwa Bikira Maria. Baba Mtakatifu Leo XIV ametoa mwaliko kwa wagonjwa na walemavu kumkumbuka na kumwombea kwa ajili ya nia zake mbalimbali na kwamba, kwa hakika wao ni wadau wa Sala na Tafakari ya Rozari Takatifu na kwamba, ushuhuda wa maisha yao, ni chachu inayoweza kuleta mabadiliko makubwa sehemu mbalimbali za dunia. Uwepo wao kwa wingi katika Madhabahu ya Bikira Maria wa Pompei ni chanzo cha neema na baraka, katika kumbukizi ya Jubilei ya Miaka 150 tangu kuwekwa jiwe la msingi la ujenzi wa Madhabahu haya. Amewashukuru kwa uwepo na ushuhuda wao na kwamba, waamini wote wameungana katika Kristo Yesu, kwa njia ya Bikira Maria katika maadhimisho ya Siku hii maalum, ambamo Kristo Yesu anaendelea kuwa karibu na waja wake na kwamba, daima yuko pamoja nao na anaongozana nao katika hija ya maisha yao huku Bondeni kwenye machozi. Amewataka kuunganisha mateso na mahangaiko yao kwa ajili ya toba na wongofu wa ndani, kwa ajili ya haki na amani duniani. Watambue kwamba, Kristo Yesu alipokuwa ametundikwa Msalabani, aliwaweka wafuasi wake wote chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa, aendelee kuwaombea na kuwasindikiza katika hija ya maisha yao huku Bondeni kwenye machozi.

Wagonjwa na Walemavu
08 Mei 2026, 15:15