Tafuta

Baba Mtakatifu Leo XIV anaadhimisha Kumbukizi ya Mwaka mmoja tangu alipochaguliwa kuliongoza Kanisa Moja, Takatifu, Katoliki na la Mitume, tarehe 8 Mei 2026 kwa kutembelea Madhabahu ya Bikira Maria wa Pompei, Baba Mtakatifu Leo XIV anaadhimisha Kumbukizi ya Mwaka mmoja tangu alipochaguliwa kuliongoza Kanisa Moja, Takatifu, Katoliki na la Mitume, tarehe 8 Mei 2026 kwa kutembelea Madhabahu ya Bikira Maria wa Pompei,   (@Vatican Media)

Hija ya Kichungaji Pompei na Napoli: Madhabahu ya Bikira Maria wa Pompei

Papa Leo XIV anasema, Madhabahu ya Bikira Maria wa Pompei: Ni mahali ambapo watu wa Mungu wanaonja nguvu ya ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu kwa njia ya upendo, unaopyaisha maisha kwa chemchemi ya Injili; Maisha ya sala yanayomwilishwa katika ukarimu na huduma ya upendo kwa wale wote wanaokimbilia huruma na tunza ya Bikira Maria wa Pompei. Ni kituo cha elimu, maisha ya kifamilia na faraja kwa wale wote wanaoteseka kiroho na kimwili.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Madhabahu ni mahali pa kuonjeshana: huruma, upendo na ukarimu, ili kila hujaji anapofika mahali hapa aweze kujisikia kuwa yuko nyumbani anakaribishwa, kuthaminiwa na kupendwa. Madhabahu kimsingi ni mahali pa: Sala na Ibada kwa Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa, anayetoa machozi ya faraja kwa wale wanaoteseka; ni mwombezi wa watu waliovunjika na kupondeka moyo; watu waliokata tamaa na kwamba, Bikira Maria anajaribu kujibu sala ya kila mwamini anayekimbilia ulinzi na tunza yake ya daima. Madhabahu ni mahali ambapo panapaswa kukuza na kudumisha ari na moyo wa Sala ya Kanisa, maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa kama sehemu ya kazi ya ukombozi. Ni mahali pa shuhuda za imani, matumaini na mapendo, kielelezo cha Kanisa linalokesha na kusali daima, tayari kujielekeza katika ujenzi wa Kanisa la Kisinodi na Kimisionari. Madhabahu ni mahali pa ukimya unaopaswa kububujika kutoka katika undani wa mahujaji, tayari kuomba: baraka, neema na rehema pamoja na kudumisha upendo kwa Mungu na jirani! Madhabahu ni mahali pa kuonja huruma na upendo wa Mungu unaofumbatwa katika Sakramenti ya Upatanisho, Mahakama ya huruma ya Mungu. Maeneo kama haya yanahitaji wakleri waliofundwa barabara, watakatifu, vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake. Baba Mtakatifu Leo XIV anaadhimisha Kumbukizi ya Mwaka mmoja tangu alipochaguliwa kuliongoza Kanisa Moja, Takatifu, Katoliki na la Mitume, tarehe 8 Mei 2026 kwa kutembelea Madhabahu ya Bikira Maria wa Pompei, yaliyoko Jimbo kuu la Napoli, Kusini mwa Italia mahali: Pa upendo wa Mungu unaotoa joto kwa wale waliovunjika na kupondeka mioyo; ni mahali ambapo imani na upendo vina tamalaki.

Madhabahu ni mahali pa sala, tafakari na matendo ya huruma
Madhabahu ni mahali pa sala, tafakari na matendo ya huruma   (@VATICAN MEDIA)

Ni mahali ambapo watu wa Mungu wanaonja nguvu ya ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu kwa njia ya upendo, unaopyaisha maisha kwa chemchemi ya Injili; Maisha ya sala yanayomwilishwa katika ukarimu na huduma ya upendo kwa wale wote wanaokimbilia huruma na tunza ya Bikira Maria wa Pompei. Ni kituo cha elimu, maisha ya kifamilia na faraja kwa wale wote wanaoteseka kiroho na kimwili. Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Baba Mtakatifu Leo XIV wakati wa hija yake ya kichungaji kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Pompei, tarehe 8 Mei 2026. Anasema, Mtakatifu Bartolo Longo alipofika eneo hili kwa mara ya kwanza, alikutana na watu wachache, ambao utu na heshima yao vilikuwa vinasiginwa na umaskini, magonjwa na mashambulizi ya majambazi, lakini Mtakatifu Bartolo Longo aliona ndani mwao Uso wa Kristo Yesu, hasa miongoni mwa yatima, watoto wa wafungwa magerezani, akawafanya kuhisi ndani mwao huruma na upendo wa Mungu; kwa hakika ni upendo wa Mungu uliokuwa unamsukuma kutenda yote haya, leo hii Madhabahu ya Bikira Maria wa Pompei yamekuwa ni Kituo muhimu sana cha ushuhuda wa imani, kiini cha maisha ya Kikristo, Ibada na heshima kwa Bikira Maria; Madhabahu ambayo yanafahamika na watu wengi kutoka sehemu mbalimbali za dunia!

Madhabahu ya Bikira Maria wa Pompei ni Mahali ya Sala ya Rozari
Madhabahu ya Bikira Maria wa Pompei ni Mahali ya Sala ya Rozari   (@Vatican Media)

Rozari Takatifu ni muhtasari wa upendo na huruma ya Mungu katika maisha ya mwanadamu! Sala ya Rozari ni njia muafaka kabisa ya kutafakari maisha na utume wa Kristo Yesu, ili kumfahamu, kumpenda, kumfuasa na hivyo kumtumikia kwa njia ya upendo kwa jirani wenye shida na mahangaiko mbalimbali wanaokumbukwa katika Sala ya Rozari Takatifu. Kwa njia ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, kila mtu ajitahidi kutekeleza dhamana na wajibu wake katika mchakato wa kuponya ulimwengu, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, Madhabahu ya Bikira Maria wa Pompei ni mahali pa Sala ya Rozari Takatifu na msingi wa Ibada na heshima kwa Bikira Maria, mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kuendeleza Ibada na heshima kwa Bikira Maria, kwa kutafakari maisha na matendo ya Kristo Yesu, yanapenyeza na hatimaye kuleta mabadiliko katika maisha ya waamini. Hii ni changamoto kwa watu wote wa Mungu kuwa ni watu wa sala, inayowawezesha kuwa ni watu wanaokita maisha yao katika huduma, majadiliano na imani inayomwilishwa katika matendo mema: kiroho na kimwili. Vijana wamkimbilie Kristo Yesu, kama rafiki yao mpendwa asiyewatelekeza na kwamba, wanayo dhamana ya kumtangaza na kumshuhudia kwa watu wa Mataifa. Mwishoni mwa hotuba yake, Baba Mtakatifu Leo XIV amewapatia baraka zake za kitume, akiwataka watu wa Mungu kuendelea kujikita katika ukarimu na imani.

Sala ya Rozari Ni Njia Muafaka ya kutafakari safari ya Ukombozi
Sala ya Rozari Ni Njia Muafaka ya kutafakari safari ya Ukombozi   (@Vatican Media)

Kwa upande wake, Askofu mkuu Tommaso Caputo, Mwakilishi wa Kitume kwa ajili ya Madhabahu ya Bikira Maria wa Pompei amesema, haya Madhabahu yanapata chimbuko lake kunako tarehe 8 Mei 1887, yalipozunduliwa kama Madhabahu ya imani, na tangu wakati huo Mashirika, vyama mbalimbali vya kitume na watu wa kujitolea wametoa huduma ya upendo kwa watu waliovunjika na kupondeka moyo. Kwa hakika, hili ni tukio la neema na kilele chake ni maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu na Sala kwa Bikira Maria wa Pompei. Baba Mtakatifu Leo XIV amepata fursa ya kusikiliza shuhuda mbalimbali zilizotolewa na waamini walionja tunu msingi ya upendo na maisha ya kifamilia; watoto waliokuwa wametupwa na kutelekezwa, wakapata hifadhi na upendo wa kifamilia. Hapa ni mahali ambapo vijana wamejifunza kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa jirani zao.

Bikira Maria wa Pompei
08 Mei 2026, 15:36