Papa Leo XIV: Kumbukizi ya Mwaka Mmoja wa Kifo Cha Papa Francisko 2026
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Ikuwa ni tarehe 21 Aprili 2025 Profesa Andrea Arcangeli, Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Afya na Usafi ya Vatican alipotangaza rasmi kwamba, Baba Mtakatifu Francisko “Jorge Mario Bergoglio” aliyezaliwa tarehe 17 Desemba 1936 aliyekuwa anaishi mjini Vatican na Mwenyeji wa Vatican amefariki dunia saa 1:35 Asubuhi ya tarehe 21 Aprili 2025 katika chumba chake cha “Domus Santa Marta” Hosteli ya Mtakatifu Martha kutokana na ugonjwa wa: “Kiharusi, Kwa kupoteza fahamu, Koma pamoja na Ugonjwa wa Shinikizo la juu la damu. Baba Mtakatifu Francisko pia alikuwa anasumbuliwa na ugonjwa wa: Mkamba, Kisukari pamoja na Shinikizo la damu. Uamuzi wa kifo hiki umeamriwa na rekodi iliyotolewa na chombo kinachojulikana kama “electrocardiothanatographic” na hivyo akatangaza kwamba, sababu za kifo cha Baba Mtakatifu Francisko kulingana na ufahamu wake na dhamiri nyofu ni hizo zilizotangazwa hapo juu anasema Profesa Andrea Arcangeli, Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Afya na Usafi ya Vatican. Ni katika muktadha wa kumbukizi ya mwaka mmoja, tangu Papa Francisko alipofariki dunia, na maadhimisho yake kufanyika kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumanne tarehe 21 Aprili 2026 na kuongozwa na Kardinali Giovanni Battista Re, Dekano wa Baraza la Makardinali, ambaye pia amesoma ujumbe wa Baba Mtakatifu Leo XIV ambaye kuanzia Jumatatu tarehe 13 hadi 23 Aprili 2026 Baba Mtakatifu Leo XIV anafanya hija ya kitume ya Siku 10 kwa kutembelea Algeria, Cameroon, Angola pamoja na Guinea ya Ikweta kama shuhuda na mjumbe wa matumaini, amani na upatanisho.
Baba Mtakatifu Leo XIV katika ujumbe wake kwa watu wa Mungu ambao wamehudhuria Ibada ya Misa Takatifu kama sehemu ya kumbukumbu ya Mwaka mmoja, tangu Baba Mtakatifu Francisko alipoaga dunia anasema, ujumbe wake ni kama ushuhuda na utambuzi wa mchango mkubwa uliotolewa na Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wa Kanisa. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, kifo si ukuta, bali ni mlango unaofungua huruma ya Mungu ambayo Papa Francisko aliitangaza na kuishuhudia katika maisha na utume wake bila kuchoka. Mwenyezi Mungu akamwita kwake tarehe 21 Aprili 2025 katikati ya mwanga wa maadhimisho ya Pasaka ya Bwana. Alihitimisha hija ya maisha yake ya hapa duniani kwa kukumbatiana na Kristo Mfufuka, kwa “furaha ya Injili” ambayo ilikuwa ni kiini cha ujumbe wake katika Nyaraka za Kitume alizowahi kuandika. Papa Francisko alikuwa ni Khalifa wa Mtakatifu Petro na Mchungaji wa Kanisa la Kiulimwengu, katika kipindi ambacho kinaashirikia na kuendelea kuashiria mabadiko makubwa ambayo aliyafahamu fika, akawatolea walimwengu ushuhuda wa ujasiri ambao unaendelea kuwa ni: urithi, amana na utajiri wa Kanisa.
Baba Mtakatifu Leo XIV anaendelea kusema kwamba, mchakato wa Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji msingi ya binadamu: kiroho na kimwili kilikuwa ni kitovu cha “Magisterium” yaani Mamlaka fundishi ya Kanisa mintarafu Hayati Baba Mtakatifu Francisko, ambayo kimsingi yalisimikwa katika maisha kama Mtume mmisionari. Akawa Mfuasi mwaminifu kwa Kristo Yesu tangu alipobatizwa na hatimaye kuwekwa wakfu katika Daraja Takatifu ya Upadre inayopata utimilifu wake kwa kuwekwa wakfu kuwa Askofu, hadi upeo wa maisha. Alikuwa ni Mmisionari aliyetangaza na kushuhudia Injili ya huruma ya Mungu kwa watu wote. Mafao yanayobubujika kutoka katika Injili hii yamewafikia na kugusa “sakafu” ya nyoyo za watu wengi sehemu mbalimbali za dunia, kwa watu wanaoteseka kwa vita, hujaji wa hija za kitume, hadi “hija” yake ya mwisho katika magonjwa hadi kifo chake.
Baba Mtakatifu Francisko kama ilivyokuwa kwa watangulizi wake, ni kiongozi aliyejitahidi kumwilisha Mafundisho ya Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican katika maisha na utume wa Kanisa, kwa kulitaka Kanisa kufungua malango yake, tayari kumtangaza na kumshuhudia Kristo Mfufuka; Hazina na amana ya Injili ya matumaini duniani; Kiongozi aliyekuwa na ari na mwamko wa kutangaza Habari Njema ya Wokovu chemchemi ya utimilifu wa furaha ya ndani. Hata leo hii mwangwi wa maneno ya Hayati Baba Mtakatifu Francisko yanaendelea kusikika kama habari Njema ya Wokovu: Huruma ya Mungu, Amani, Udugu wa kibinadamu, Harufu ya Mwanakondoo, Hospitali katika uwanja wa vita na maneno mengine mengi kama haya. Maneno haya anasema Baba Mtakatifu Leo XIV yanawasaidia waamini kuwa na lugha mpya inayotangaza Injili ya Kristo Yesu. Hayati Baba Mtakatifu Francisko alikuwa na Ibada kwa Bikira Maria na mara nyingi alikwenda kusali na kutafakari kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria mkuu mahali alipozikwa, bila kusahau madhabahu mbalimbali za Bikira Maria duniani. Bikira Maria Mama wa Kanisa awasaidie waamini kila mmoja kadiri ya mazingira yake, Mitume jasiri wa Mwanaye mpendwa Kristo Yesu na Manabii wa upendo wa huruma ya Mungu.
Nembo yake ya Kiaskofu ya Baba Mtakatifu Francisko iliandikwa hivi: “Akamwangalia kwa huruma, akamchagua” “Miserando atque eligendo” ni maneno ya kauli mbiu ya yaliko kwenye Nembo la Kiaskofu ya Hayati Baba Mtakatifu Francisko, kama kumbukumbu endelevu ya maisha ya wito wake alipokuwa kijana, pale Mwenyezi Mungu alipomwangalia kwa huruma na kumchagua. Shughuli za kichungaji kuhusu miito ni mchakato wa kukutana na Kristo Yesu, tayari kumchagua na kumwambata katika maisha. Hayati Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wake wa maisha ya kiroho, aliouandika tarehe 29 Juni 2022, kwanza kabisa alijikabidhi kwa Fumbo la Utatu Mtakatifu. Anasema, kwa kuhisi kwamba, mwisho wa maisha yake ya hapa dunia unakaribia na akiwa na tumaini hai katika uzima wa milele, alipenda kuelezea mapenzi yake kuhusu mahali pa kuzikwa kwake. Hayati Baba Mtakatifu Francisko anasema siku zote amekabidhi maisha na huduma yake ya Kipadre na Kiaskofu chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria Mama wa Bwana wetu Kristo Yesu pamoja na Bikira Maria Mtakatifu. Anaomba kwamba, maisha yake ya kibinadamu yabaki yakipumzika, katika Kanisa kuu la Bikira Maria Mkuu, huku akingojea Siku ya ufufuo wa wafu na maisha ya uzima wa milele. Alitamani kuona safari yake ya mwisho ya hapa duniani inaishia mahali patakatifu pa Bikira Maria, mahali ambapo alienda kwa ajili ya sala mwanzoni na mwishoni mwa kila hija ya kitume, ili kukabidhi nia yake kwa Bikira Maria pamoja na kumshukuru kwa unyenyekevu, kwa ulinzi na tunza yake ya kimama. Hayati Baba Mtakatifu Francisko anaomba kaburi lake liwekwe kwenye Kikanisa cha Bikira Maria Afya ya Warumi “Salus Populi Romani.”
Hayati Baba Mtakatifu Francisko alitaka kaburi lake lichimbwe ardhini, rahisi bila mapambo maalum bali libaki likiwa na maandishi ya pekee “Franciscus.” Gharama ya maandalizi na hatimaye maziko yake, zitagharimiwa na mfadhili ambaye amempanga, safari ya kuhamishiwa kutoka kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, tayari alikwisha kutoa maagizo kwa Kardinali Rolandas Makrikas, Kamishna Maalum wa Kipapa wa Kanisa kuu la Bikira Maria Mkuu. Hayati Baba Mtakatifu anawaombea thawabu stahiki kwa Mwenyezi Mungu wale wote waliompenda na watakaoendelea kumwombea. Anasema, alitolea mateso aliyokumbana nayo katika sehemu ya mwisho wa maisha na utume wake kwa Bwana kwa ajili ya amani na ujenzi wa udugu wa kibinadamu kati ya watu!
