Papa Leo XIV Adhabu ya Kifo Ni Kinyume Cha Haki Msingi, Utu na Heshima ya Binadamu
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni, kumekuwepo na maendeleo makubwa juu ya tafsiri na uelewa wa Mafundisho ya Kanisa kuhusu utu na heshima ya binadamu kadiri ya mwanga wa Injili, hali ambayo ilimpelekea hata Hayati Baba Mtakatifu Francisko kuamua kufanya mabadiliko kwenye kifungu cha Katekisimu ya Kanisa Katoliki kinachofuta adhabu ya kifo kama sehemu ya Mapokeo na Mafundisho ya Kanisa. Ikumbukwe kwamba, Baba Mtakatifu katika mawazo yake kuhusu adhabu ya kifo anakazia umuhimu wa kulinda uhai wa binadamu na kuuendeleza, changamoto na mwaliko wa kuleta mwono na mwelekeo mpya kuhusu: maisha, utu na heshima ya binadamu. Hii ni hatua kubwa na muhimu katika kutafsiri Mapokeo na Mafundisho hai ya Kanisa kadiri ya Mwanga wa Injili na kwa kusoma alama za nyakati.
Kanisa linatambua uchungu wa watu walioguswa na kutikiswa na matukio ambayo yamepelekea adhabu ya kifo kwa wahusika, lakini, Kanisa linavitaka vyombo vya sheria kutenda haki na kuwajibika barabara badala ya kuendeleza chuki, uhasama pamoja na kudhalilisha utu na heshima ya binadamu kwa njia ya adhabu ya kifo. Kanisa linayasema yote haya kwa kutoa fursa kwa wale waliotenda makosa kama haya yanayostahili kupewa adhabu ya kifo, kupata muda wa toba na wongofu wa ndani, ili kuambata huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao; tayari kuanza kuandika ukurasa mpya kwa kujivika utu mpya na kuanza kutembea katika mwanga wa Kristo Mfufuka. Toba na wongofu wa ndani; msamaha, upatanisho na haki ni mambo msingi yanayozingatiwa na Mama Kanisa katika mchakato wa kufutilia mbali adhabu ya kifo. Hii ni hatua mpya katika mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko!
Ni wakati wa kutangaza na kushuhudia Injili ya furaha na familia inayofumbatwa kwa namna ya pekee kabisa na Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Mauaji ya aina yoyote ile ni jambo ambalo haliwezi kukubalika katika mwanga wa Injili. Adhabu ya kifo ni kinyume kabisa cha kanuni maadili, utu na heshima ya binadamu. Adhabu ya kifo ni kielelezo cha kutoheshimu zawadi ya uhai. Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Francisko aliridhia kwa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa kufanya marekebisho kwenye Katekisimu ya Kanisa Katoliki, kifungu namba 2267 kinachozungumzia kuhusu adhabu ya kifo na tafsiri mpya ilipaswa kuingizwa katika vipengele mbalimbali vya Katekisimu ya Kanisa Katoliki. Kanisa Katoliki limefuta adhabu ya kifo katika Mafundisho na Mapokeo yake kwa kukazia njia zinazotetea na kulinda maisha ya watu, amani na usalama wao dhidi ya adui; kwani hizi ni njia zinazodumisha utu, ustawi na mafao ya wengi.
“Kwa kweli leo, kutokana na uwezekano ambao serikali inao siku hizi wa kuweza kufaulu kuzuia uhalifu kwa aliyetenda kosa asiweze kuleta madhara bila kumwondolea kabisa uwezo wa kujikomboa mwenyewe, kesi ambazo kumuua mkosaji ni lazima kabisa kabisa ni chache sana na “kwa kweli karibu haziko kabisa.” Kanisa linafundisha kwa mwanga wa Injili kwamba “Adhabu ya kifo haikubaliki kwa sababu inadhuru haki na utu wa mtu.” Kanisa linaendelea kujizatiti ili kuhakikisha kwamba, adhabu ya kifo inaondolewa duniani kote! Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, analaani vitendo vyote vinavyopandikiza utamaduni wa kifo na mauaji ya watu na kwamba, adhabu ya kifo imepitwa na wakati. Injili ya uhai inapaswa kuheshimiwa tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake hadi kifo cha kawaida kinapomsibu. Pale Serikali inapotoa adhabu ya kifo kwa raia wake, hili ni tukio ambalo linapaswa kulaaniwa!
Ni katika muktadha wa adhabu ya kifo kupitwa na wakati na kwamba, ni uvunjaji wa haki msingi za binadamu, katika kumbukizi ya Miaka 15 tangu kufutwa kwa adhabu ya kifo Jimboni Illinois, nchini Marekani, Baba Mtakatifu Leo XIV amewatumia ujumbe wa video washiriki waliokuwa wamekutanika kwenye Chuo Kikuu cha “De Paul University of Chicago” kama sehemu ya kumbukizi ya Miaka 15 tangu kufutwa kwa adhabu ya kifo Jimboni humo. Kanisa Katoliki linafundisha kwamba, maisha ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayopaswa kulindwa na kutunzwa tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake, hadi mauti ya kawaida inapomfika kadiri ya mpango wa Mungu. Uhai ni msingi wa haki msingi za binadamu anasema, Baba Mtakatifu Leo XIV na kwamba, haki hii haiwezi kupotea hata pale mtu anapotenda kosa. Kumbe, kuna uwezekano wa kulinda ustawi, maendeleo na mafao ya wengi; kutekeleza haki bila ya kukimbilia adhabu ya kifo ambayo kimsingi ni kinyume cha utu, heshima na haki msingi za binadamu. Baba Mtakatifu Leo XIV ametumia fursa hii kuungana na wale wote wanaosimama kidete kupinga adhabu ya kifo pamoja na Serikali ya Jimbo la Illinois, na nchini Marekani katika ujumla wake ambako kunako mwaka 2011, Jimbo la Illinois liliamua kufuta adhabu ya kifo. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Leo XIV kwamba, mchango na ngvuvu zao zitaweza kuzaa matunda yanayotambua na kuthamini utu, heshima na haki msingi za binadamu na kwamba, hii iwe ni changamoto kwa watu wengine kufanya kazi kwa sababu za kiutu! Mwishoni, amewapatia washiriki wote baraka zake za kitume.
