Tafuta

Baba Mtakatifu Leo XIV amewashukuru sana watu wa Mungu nchini Guinea ya Ikweta akiwakumbusha kwamba: “Kristo Yesu Mwanga wa Guinea ya Ikweta, kuelekea kwenye matumaini” Baba Mtakatifu Leo XIV amewashukuru sana watu wa Mungu nchini Guinea ya Ikweta akiwakumbusha kwamba: “Kristo Yesu Mwanga wa Guinea ya Ikweta, kuelekea kwenye matumaini”   (@Vatican Media)

Hija ya Papa Leo XIV Guinea ya Ikweta: Ubatizo na Neno la Mungu

Baba Mtakatifu Leo XIV anaondoka Barani Afrika akiwa amebeba amana na utajiri wa imani, matumaini na mapendo. Hii ni hazina kubwa iliyojumuisha hadithi, nyuso, na shuhuda, za furaha na huzuni, ambazo zinaboresha maisha na huduma yake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Kama ilivyokuwa kwenye Karne za Mwanzo za Kanisa, leo Kanisa Barani Afrika linaalikwa kuchangia kwa kiasi kikubwa utakatifu, ari, mwamko na utume wa kimisionari wa watu wa Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Jubilei ya Miaka 170 ya Uinjilishaji nchini Guinea ya Ikweta kuanzia mwaka 1855-2025, inanogeshwa na kauli mbiu “Kristo Yesu Mwanga wa Guinea ya Ikweta, kuelekea kwenye matumaini” ni mwaliko kwa watu watakatifu wa Mungu nchini humo kuyaangalia yaliyopita kwa imani na kuanza kujielekeza katika hija ya imani na matumaini, ni wakati kwa Baba Mtakatifu Leo XIV kuwasha tena moto wa imani kwa kuwaimarisha vijana wa kizazi kipya katika tunu msingi za Kiinjili, ili hatimaye, waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa haki, amani na upatanisho wa Kitaifa, huku wakiendelea kuchangia katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi nchini humo. Baba Mtakatifu Leo XIV kuanzia Jumanne tarehe 21 hadi Alhamisi tarehe 23 Aprili 2026 amefanya Hija ya Kitume nchini Guinea ya Ikweta na hatimaye, kuihitimisha hija hii ambayo imegusa maisha na utume wa Kanisa Barani Afrika kwa kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Uwanja wa Malabo.

Kristo Yesu Mwanga wa Guinea ya Ikweta, kuelekea kwenye matumaini.
Kristo Yesu Mwanga wa Guinea ya Ikweta, kuelekea kwenye matumaini.   (ANSA)

Baba Mtakatifu Leo XIV katika mahubiri yake amekazia kuhusu mchango wa Shemasi Filipo kwa Towashi Mkushi aliyekuwa anarejea kutoka Yerusalemu kwenda Afrika mintarafu Neno la Mungu; Alibahatika kuwa ni mwerevu na aliyeelimika kama inavyoshuhudiwa katika kazi na sala zake, lakini kwa bahati mbaya aliwa ni towashi, hawezi kuzaa na kwamba, uhai wake wote umewekwa katika huduma ya mamlaka inayomdhibiti na kumtawala. Kwa njia ya Ubatizo, mwamini anapata mwanga wa kusoma Neno la Mungu; kutafakari Maandiko Matakatifu kuhusu Manabii, Kusali Zaburi na Sheria na hatimaye kutangaza na kushuhudia Injili inayomwilishwa katika maisha. Maandiko Matakatifu ni amana, utajiri na urithi wa Kanisa; ni ufunuo wa Baba wa milele kwa njia ya Mwanaye Kristo Yesu. Kwa mateso, kifo na ufufuko wake, Kristo Yesu amemkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti, changamoto kwa waamini kuadhimisha mafumbo ya Kanisa kwa furaha. Waamini wanaitwa na kutumwa kujikita katika mchakato wa uinjilishaji wa kina unaopata chimbuko lake kutoka katika Sakramenti ya Ubatizo ambayo: ni nguzo ya umoja wa udugu, inayowatakasa watu kwa Maji na Roho Mtakatifu na kwamba, Sakramenti hii ni kiini cha matumaini. Kwa njia ya ushuhuda, Injili inamwilishwa katika matendo, huduma na msamaha na hivyo kulijenga Kanisa.  

Injili imwilishwe katika matendo, huduma na msamaha
Injili imwilishwe katika matendo, huduma na msamaha   (@Vatican Media)

Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, Liturujia ya Neno la Mungu ni mwaliko kwa waamini kujiandaa kusoma kwa pamoja Kitabu cha historia ya maisha ya kila mmoja wao, kitabu kinachoendelea kuandikwa kila siku na Mwenyezi Mungu. Maandiko Matakatifu yanamwonesha Shemasi Filipo aliyekutana na hatimaye kutanguzana na Towashi Mkushi aliyetoka Yerusalemu na alikuwa anaelekea Afrika. Mkushi huyu alikuwa anatafuta ukweli, uwazi ili hatimaye aweze kuzima kiu ya ndani ya maisha yake. Alikuwa na utajiri mkubwa lakini kwa bahati mbaya alikuwa ni Mtumwa na hivyo nguvu zake ziliwafaidia wengine; alikuwa ni towashi hawezi kuzaa na kwamba, uhai wake wote umewekwa katika huduma ya mamlaka inayomdhibiti na kumtawala. Anarejea Barani Afrika ambako kuligeuzwa kuwa ni mahali pa watumwa, ambako alitangaza na kushuhuidia Habari Njema ya Wokovu, ambalo ilimwezesha kukutana mubashara na Kristo Yesu kwa njia ya Shemasi Filipo aliyetangaza Fumbo la Pasaka, yaani: Mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu, akavutwa na historia hii na hivyo kuanza kutembea katika Njia ya Wokovu, huku akijitahidi kumfahamu Mungu. Kwa njia ya Ubatizo Towashi mkushi anakuwa ni mtoto wa Mungu, anazaliwa katika maisha mapya ya uzima wa milele na hivyo kuwekwa huru na Kristo Yesu.

Waamini kwa njia ya Ubatizo wanapokea mwanga wa imani
Waamini kwa njia ya Ubatizo wanapokea mwanga wa imani   (@Vatican Media)

Waamini kwa njia ya Ubatizo wanapokea mwanga na imani wanaposoma Neno la Mungu, wanapotafakari Maandiko ya Manabii, wanaposali Zaburi, wanapojifunza Sheria na hatimaye kutangaza Habari Njema ya Wokovu kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao. Maandiko Matakatifu ni Neno la Mungu kwa vile limeandikwa kwa uvuvio wa Roho Mtakatifu na kwamba, huu ni ufunuo wa imani, changamoto kwa waamini kama mtu mmoja mmoja, au kama Jumuiya ya waamini kulisoma na kulitafakari. Hii ni hazina takatifu ya imani iliyomo katika Mapokeo na Maandiko Matakatifu na kwamba, waamini wanaweza kulifahamu Neno la Mungu kwa msaada wa wenza katika hija ya maisha. Shemasi Filipo aliweza kumfafanulia Towashi Mkushi Maandiko Matakatifu kutoka katika Kitabu cha Nabii Isaya (Rej. 53:7-8) kuhusu utimilifu wa: Mateso, Kifo na Ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema katika kipindi cha Miaka 40 Waisraeli walitangatanga Jangwani, wakakata tamaa na kupoteza matumaini yao kwa Mungu aliyewakomboa kutoka utumwani Misri, akawalisha manna kutoka mbinguni na kwamba, Kristo Yesu anawakirimia waja wake chakula cha uzima ili kuzima kiu na njaa ya maisha, haki na amani, kwani Kristo Yesu alikubali kuwa ni Mkate na Kinywaji cha maisha ya uzima wa milele katika Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, utimilifu wa maana na maisha; ni chemchemi ya: haki, nguvu na maisha na kwamba, matatizo, fursa na changamoto za maisha hazifutiki wala kukoma, bali zinapata maana mpya kwa mwanga wa Injili.

Papa Leo XIV anakiri kwamba, hija hii imegusa undani wa maisha na utume wake
Papa Leo XIV anakiri kwamba, hija hii imegusa undani wa maisha na utume wake   (@Vatican Media)

Waamini wanaitwa na kutumwa kujikita katika mchakato wa uinjilishaji wa kina unaopata chimbuko lake kutoka katika Sakramenti ya Ubatizo ambayo: ni nguzo ya umoja wa udugu, inayowatakasa watu kwa Maji na Roho Mtakatifu na kwamba, Sakramenti hii ni kiini cha matumaini. Kwa njia ya ushuhuda, Injili inamwilishwa katika matendo, huduma na msamaha na hivyo kulijenga Kanisa. Hayati Baba Mtakatifu Francisko anasema, furaha ya Injili huijaza mioyo na maisha ya wote wanaokutana na Kristo Yesu na pale waamini wanaposhiriki furaha yake, wanapata mang’amuzi juu ya dhana ya ulaji ambao ni fadhaa na mahangaiko yanayotokana na moyo usio na bidii lakini wenye tamaa, utafutaji wa starehe za ovyo na dhamiri iliyofanywa kuwa butu. Sauti ya Mwenyezi Mungu haisikiki tena na haja ya kutenda mema inafifia, hii ni hatari ya wazi kabisa hata kwa waamini. Ni katika muktadha wa changamoto hizi zinazosimikwa katika ubinafsi, upendo wa Mungu unawainua na kuimarisha nguvu zao, hususan katika huduma ya haki na mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Mwishoni mwa mahubiri yake, Baba Mtakatifu Leo XIV amewahimiza watu wa Mungu nchini Guinea ya Ikweta, kuendeleza utume wa wafuasi wa kwanza wa Kristo Yesu kwa furaha, wanaposoma Injili kwa pamoja, waitangaze kwa shauku kubwa kama alivyofanya Shemasi Filipo na wanapoadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu kwa pamoja washuhudie kwa njia ya maisha yao imani inayookoa ili Neno la Mungu liwe ni chachu ya utendaji mema kwa watu wote.

Waamini wanaitwa na kutumwa kuwa ni wainjilishaji kwa vitendo
Waamini wanaitwa na kutumwa kuwa ni wainjilishaji kwa vitendo   (@Vatican Media)

Wakati huo huo, Askofu mkuu Juan Nsue Edjang May wa Jimbo kuu la Malabo, kwa niaba ya watu wa Mungu, ametumia fursa hii kumshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Leo XIV kwa kutangaza na kushuhudia mshikamano wa Kiinjili na upyaishaji wa imani kama kielelezo cha ujenzi wa makazi mapya katika Kristo Yesu, changamoto na mwaliko wa kumpenda Mungu na jirani zao na kwamba, hata katika udogo na uchache wao bado ni sehemu ya Kanisa la Kiulimwengu. Neema na baraka za Baba Mtakatifu Leo XIV ni mwaliko kwa watu wa Mungu kujikita katika upatanisho, haki na amani. Amewashukuru wamisionari wa kwanza waliotangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu takribani miaka 170 iliyopita. Huu ni wakati kwa Kanisa kuendelea kujizatiti katika ujenzi wa jamii inayosimikwa katika misingi ya haki, usawa, udugu wa kibinadamu na upatanisho, kwa kutambua kwamba, Kristo Yesu ni njia, ukweli na uzima. Ni matumaini yao kwamba, Sr. Imelda Makole, Muasisi wa Shirika la Watawa Wamisionari wa Maria pamoja na Katekista Josè watatangazwa kuwa watakatiu katika siku za usoni. Vijana wa kizazi kipya ni matumaini ya Kanisa la leo na kesho iliyo bora zaidi wanapaswa kufundwa na kufundika mintarafu tunu msingi za Kiinjili na kiutu; Kwa Mama Kanisa kuendeleza mchakato wa ujenzi wa jamii inayosimikwa katika misingi ya amani, haki jamii na hivyo kuendelea kuwa ni Mashuhuda wa Injili waliyoipokea.

Papa Leo XIV anaondoka Barani Afrika akiwa amebeba: imani na matumaini
Papa Leo XIV anaondoka Barani Afrika akiwa amebeba: imani na matumaini   (@Vatican Media)

Mwishoni mwa Maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, Baba Mtakatifu Leo XIV amewashukuru sana watu wa Mungu nchini Guinea ya Ikweta akiwakumbusha kwamba: “Kristo Yesu Mwanga wa Guinea ya Ikweta, kuelekea kwenye matumaini” na kwamba, alikuwa anapenda kuagana nao na kutia nanga ya hija ya kitume Barani Afrika. Anawataka watu wa Mungu wawe ni nuru ya dunia na chumvi ya ulimwengu. Amewashukuru viongozi wote wa Serikali waliowezesha kufanisha hija hii ya Kitume katika ubora wake. Anaondoka Barani Afrika akiwa amebeba amana na utajiri wa imani, matumaini na mapendo. Hii ni hazina kubwa iliyojumuisha hadithi, nyuso, na shuhuda, za furaha na huzuni, ambazo zinaboresha maisha na huduma yake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Kama ilivyokuwa kwenye Karne za Mwanzo za Kanisa, leo Kanisa Barani Afrika linaalikwa kuchangia kwa kiasi kikubwa utakatifu, ari, mwamko na utume wa kimisionari wa watu wa Mungu. Baba Mtakatifu Leo XIV ameiweka nia hii chini ya ulinzi, tunza na maombezi ya Bikira Maria. Amehitimisha neno lake la shukrani kwa kuwapongeza watu wote wa Mungu Barani Afrika.

Sakramenti ya Ubatizo
23 Aprili 2026, 15:53