Tafuta

Baba Mtakatifu alipokuwa njiani kuelekea nchini Angola, alipata nafasi ya “kuchonga” pamoja na waandishi wa habari 70 walioko kwenye msafara wake. Baba Mtakatifu alipokuwa njiani kuelekea nchini Angola, alipata nafasi ya “kuchonga” pamoja na waandishi wa habari 70 walioko kwenye msafara wake.  (@Vatican Media)

Hija ya Papa Leo XIV Nchini Angola: Mazungumzo na Wanahabari

Hija hii ya kitume imekuwa na mafanikio makubwa, anawashukuru watu wa Mungu nchini Cameroon, kwa ukarimu na mapokezi makubwa ya kukata na shoka na kwamba, anayo furaha kwa tajiriba hii anayoifanya Barani Afrika na kwamba, hana haja tena ya kuendeleza malumbano na Serikali ya Rais Donald Trump wa Marekani, kwani tangu siku ile ya kwanza, alifunga ukurasa huu wa malumbano kwani yeye anataka kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo kwa watu wote!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Hija ya Kitume ya Baba Mtakatifu Leo XIV nchini Angola kuanzia Jumamosi tarehe 18 hadi Jumanne tarehe 21 Aprili 2026, inanogeshwa na kauli mbiu “Papa Leo XIV, Hujaji wa Matumaini, Upatanisho na Amani, Ibariki Angola.” Akiwa njiani kuelekea nchini Angola, Baba Mtakatifu Leo XIV amewatumia salam na matashi mema wakuu wa nchi ya Cameroon, akiwashukuru kwa wema, ukarimu na udugu wao alipokuwa nchini Cameroon amewatakia amani na hekima. Akiwa kwenye anga la Guinea ya Ikweta “Equatorial Guinea” amemkumbusha Rais Teodoro Obiang Nguema Mbasogo kwamba, akitoka Angola, itakuwa ni zamu yao kumkaribisha na kwamba, tangu wakati huu anapenda kuwahakikishi sala zake, ili Mwenyezi Mungu aweze kuwakirimia mshikamano, ustawi na maendeleo. Akiwa kwenye anga la Gabon, Baba Mtakatifu amewaombea ustawi, maendeleo na mafao ya wengi pamoja na zawadi ya mshikamano.

Papa Leo XIV anasema, hana haja ya kuendeleza malumbano na Trump
Papa Leo XIV anasema, hana haja ya kuendeleza malumbano na Trump   (@Vatican Media)

Kwa watu wa Mungu nchini DRC, Baba Mtakatifu anawaombea udugu wa kibinadamu na amani. Baba Mtakatifu alipokuwa njiani kuelekea nchini Angola, alipata nafasi ya “kuchonga” pamoja na waandishi wa habari 70 walioko kwenye msafara wake na kusema kwamba, hija hii ya kitume imekuwa na mafanikio makubwa, anawashukuru watu wa Mungu nchini Cameroon, kwa ukarimu na mapokezi makubwa ya kukata na shoka na kwamba, anayo furaha kubwa kwa tajiriba hii anayoifanya Barani Afrika na kwamba, hana haja tena ya kuendeleza malumbano na Serikali ya Rais Donald Trump wa Marekani, kwani tangu siku ile ya kwanza, alifunga ukurasa huu wa malumbano kwani yeye anataka kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo kwa watu wote! Amesema, kiini cha ujumbe wake ni ile siku kwa ajili ya kusali na kuombea haki, amani na upatanisho nchini Cameroon, yaani tarehe 16 Aprili 2026. Anasema, yeye ni shuhuda na mjumbe wa haki, amani na upatanisho. Hii ni changamoto kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kujenga na kudumisha majadiliano ya kidini katika ukweli na uwazi; kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Mkutano wake na wakuu wa dini ya Kiislam nchini Cameroon ni kielelezo cha mchakato wa mwendelezo wa majadiliano ya kidini, katika kuragibisha ujenzi wa udugu wa kibinadamu, haki na amani.

Papa Leo XIV anawashukuru watu wa Mungu nchini Cameroon
Papa Leo XIV anawashukuru watu wa Mungu nchini Cameroon   (@Vatican Media)

Baraka yake kwenye Mnara wa Chuo Kikuu cha Kikatoliki Afrika ya Kati ni kielelezo cha Kanisa Barani Afrika katika mchakato wa kutafuta ukweli, pamoja na kukuza haki, amani na mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Mama Kanisa katika mafundisho yake mintarafu vyuo vikuu pamoja na taasisi za elimu ya juu, anasema kuwa hapa ni mahali pa kuragibisha utamaduni wa watu kukutana, kushirikiana na kushikamana kwa ajili ya ustawi, mafao na maendeleo ya wengi, kwa kujikita katika mchakato wa uinjilishaji unaopania kuleta upyaisho katika maisha ya watu na kama njia ya kutamadunisha Injili ili kuinjilisha tamaduni mintarafu tunu msingi za Kiinjili, wote wakipania kutafuta ukweli na matumaini ili kukabiliana na ukosefu wa haki, usawa, vita na mmong’onyoko wa tunu msingi za maisha ya kiroho; pamoja na mifumo mbalimbali ya umaskini katika ulimwengu mamboleo.

Chuo kikuu cha Kikatoliki ni mahali pa kuragibisha utamaduni wa kukutana
Chuo kikuu cha Kikatoliki ni mahali pa kuragibisha utamaduni wa kukutana   (@Vatican Media)

Kwa hakika, watu wa Mungu nchini Cameroon wanakabiliana na changamoto ya kutokuwepo kwa ugawaji mzuri na wa haki wa rasilimali na utajiri wa nchi. Cameroon ni nchi tajiri ya fursa mbalimbali, lakini pia inakabiliana na matatizo pamoja na changamoto nyingi. Angola ni mahali pa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu; kwa kujenga na kudumisha haki, amani, maridhiano na udugu wa kibinadamu. Baba Mtakatifu Leo XIV amewashukuru tena watu wa Mungu nchini Cameroon kwa mapokezi makubwa, kwa ari, furaha na moyo mkuu, katika kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Kwa hakika, waamini wengi wamejitokeza kuadhimisha imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Hija ya imani na matumaini inaendelea nchini Angola, ili waru wa Mungu nchini Angola waweze kusimama kidete kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu; kwa kujenga na kudumisha: haki, amani na maridhiano, sanjari na uragibishaji wa udugu wa kibinadamu. Baba Mtakatifu Leo XIV anamshukuru Mungu kwa tajiriba hii katika maisha na utume wake. Amewashukuru na kuwapongeza washititi wa tasnia ya mawasiliano kwa kazi kubwa wanayoendelea kuifanya wakati huu wa hija yake ya kitume Barani Afrika.

Hija Papa Nchini Angola
19 Aprili 2026, 15:45