Tafuta

Baba Mtakatifu Leo XIV kuanzia Jumanne tarehe 21 hadi 23 Aprili 2026 anafanya Hija ya Kitume nchini Guinea ya Ikweta. Baba Mtakatifu Leo XIV kuanzia Jumanne tarehe 21 hadi 23 Aprili 2026 anafanya Hija ya Kitume nchini Guinea ya Ikweta.  (@Vatican Media)

Hija ya Kitume ya Papa Leo XIV Guinea ya Ikweta: Hotuba Kwa Viongozi wa Serikali

Papa Leo XIV katika hotuba yake amesema, kiongozi wa nchi ni kitovu cha matarajio ya watu wa Mungu kukutana kwa ajili ya ujenzi wa hali ya kijamii ya uhuru, haki, heshima na uendelezaji wa haki za kila mtu au kikundi, na hali bora ya maisha, ambayo inaruhusu watu kujitambua kama wanadamu na kama watoto wa Mungu. Hii ni changamoto kwa viongozi waliokabidhiwa madaraka ya kuwaongoza watu wao. Kwa upande mwingine Kanisa linashiriki furaha na majonzi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Jubilei ya Miaka 170 ya Uinjilishaji nchini Guinea ya Ikweta kuanzia mwaka 1855-2025, inanogeshwa na kauli mbiu “Kristo Yesu Mwanga wa Guinea ya Ikweta, kuelekea kwenye matumaini” ni mwaliko kwa watu watakatifu wa Mungu nchini humo kuyaangalia yaliyopita kwa imani na kuanza kujielekeza katika hija ya imani na matumaini, ni wakati kwa Baba Mtakatifu Leo XIV kuwasha tena moto wa imani kwa kuwaimarisha vijana wa kizazi kipya katika tunu msingi za Kiinjili, ili hatimaye, waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa haki, amani na upatanisho wa Kitaifa, huku wakiendelea kuchangia katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi nchini humo. Baba Mtakatifu Leo XIV kuanzia Jumanne tarehe 21 hadi 23 Aprili 2026 anafanya Hija ya Kitume nchini Guinea ya Ikweta. Akiwa njiani kuelekea nchini humo, Baba Mtakatifu Leo XIV ametuma salamu na matashi mema kwa viongozi wakuu wa Angola, akiwashukuru watu wa Mungu nchini Angola kwa mapokezi makubwa na ukarimu waliomwonjesha wakati wa hija yake ya Kitume nchini mwao na kwamba, anapenda kuwahakikishia sala zake kwa Angola na hatimaye, kuwatakia wingi wa furaha na utulivu. Akiwa kwenye anga la Jamhuri ya Watu wa Congo, amewatakia neema, hekima na ustawi wananchi wote wa Congo, Na alipowasili kwenye anga la Gabon amewatakia amani na ustawi watu wote wa Gabon. Alipowasili kwenye anga la Cameroon, Baba Mtakatifu Leo XIV amewahakikishia sala na sadaka yake kwa ajili ya ujenzi wa umoja, ustawi na maendeleo ya watu wa Mungu nchini Cameroon.  

Papa Leo XIV amepata fursa ya kuzungumza na viongozi wa serikali na diplomasia
Papa Leo XIV amepata fursa ya kuzungumza na viongozi wa serikali na diplomasia   (@Vatican Media)

Baba Mtakatifu Leo XIV Jumanne tarehe 21 Aprili 2026 amepata fursa ya kukutana na kuzungumza na viongozi wa Serikali, Wanadiplomasia wanaowakilisha Nchi zao pamoja na Mashirika ya Kimataifa, Wafanyabiashara maarufu pamoja na wawakilishi wa vyama vya kiraia na kitamaduni. Baba Mtakatifu Leo XIV katika hotuba yake amesema, kiongozi wa nchi ni kitovu cha matarajio ya watu wa Mungu kukutana kwa ajili ya ujenzi wa hali ya kijamii ya uhuru wa kweli, haki, heshima na uendelezaji wa haki za kila mtu au kikundi, na hali bora ya maisha, ambayo inaruhusu watu kujitambua kama wanadamu na kama watoto wa Mungu. Hii ni changamoto endelevu kwa viongozi waliokabidhiwa madaraka ya kuwaongoza watu wao. Kwa upande mwingine: “Furaha na matumaini, huzuni na mahangaiko ya wanaume na wanawake wa siku hizi, hasa wale walio maskini au wanaoteseka kwa njia yoyote ile, hizi ni furaha na matumaini, huzuni na mahangaiko ya wafuasi wa Kristo” Rej. Gaudium et spes (n. 1).

Papa Leo XIV: Utu, heshima na haki msingi za binadamu
Papa Leo XIV: Utu, heshima na haki msingi za binadamu   (@Vatican Media)

Baba Mtakatifu amegusia pia ujenzi wa Makao makuu ya nchi, Mafundisho Jamii ya Kanisa, Changamoto za maisha ya binadamu tangu kuumbwa kwake, Maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia na kwamba, Kanisa litaendelea kuchangia mchakato kwa ajili ya malezi ya dhamiri huru, nyofu na yenye kuwajibika, itakayowawezesha kusonga mbele pamoja kuelekea siku zijazo.  Katika dunia iliyojeruhiwa na kiburi, watu wana njaa na kiu ya haki.  Ni muhimu kuwatia moyo wale wanaoamini katika amani na kuthubutu kujihusisha na siasa za upinzani zinazotoa kipaumbele cha kwanza kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, lengo kuu la hija yake nchini Guinea ya Ikweta ni kuwaimarisha ndugu zake katika imani, kuwafariji watu wa Mungu wanaoendelea kupitia mabadiliko makubwa nchini humo, tayari kusikiliza na kujibu matamanio halali ya watu wa Mungu, katika ujenzi wa mji wa Mungu kwa kuyaelekeza macho yao juu mbinguni, kwakutambua kwamba, mjenzi mkuu ni Mwenyezi Mungu na kwamba, binadamu hapa duniani ni msafiri tu na kwamba, waamini na watu wote wenye mapenzi mema wanapaswa kukita maisha yao katika kanuni maadili na utu wema katika utekelezaji wa masuala ya kijamii na kisiasa.

Papa Leo XIV amepata mapokezi makubwa
Papa Leo XIV amepata mapokezi makubwa   (@Vatican Media)

Baba Mtakatifu Leo XIV anasema kila kizazi kinakumbana na changamoto za maisha zinazotokana na ukosefu wa haki jamii, ukosefu wa ardhi ya kutosha, makazi na pengo kubwa la matumizi ya sayansi na teknolojia kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, changamoto na mwaliko wa kuondoa vikwazo hivi kwa ajili ya maendeleo fungamani ya binadamu yanayokita mizizi yake katika mshikamano na matumizi ya rasilimali za dunia kwa ajili ya mafao ya wengi. Mageuzi makubwa na ya haraka ya teknolojia yameongeza kasi juu ya matumizi makubwa ya malighafi na kwamba, mabadiliko haya yanaonekana kufunika masharti ya kimsingi kama vile ulinzi wa kazi ya uumbaji, haki za jumuiya mahalia, heshima ya kazi na ulinzi wa afya ya umma kama alivyowahi kusema Baba Mtakatifu Francisko kwamba: watu wanapaswa kusema “hapana” kwa uchumi unaobagua na kusababisha kukosekana kwa usawa kwani uchumi wa namna hii unauwa. EG, 53. Kumekuwepo na ongezeko la matumizi makubwa ya silaha za mahangamizi yanayosababisha vita, kinzani na migogoro; uchimbaji na ukwapuaji mkubwa wa nishati ya mafuta na madini, bila kuzingatia wala kuheshimu Sheria ya Kimataifa, ustawi na uhuru wa watu mahalia.

Papa Leo XIV akisali na kutafakari mjini Malebo
Papa Leo XIV akisali na kutafakari mjini Malebo   (@Vatican Media)

Teknolojia hizi mara nyingi huonekana kubuniwa na kutumiwa kimsingi kwa madhumuni kama vita, ndani ya miktadha ambayo inashindwa kupanua fursa kwa wote.  Kinyume chake, hatima ya ubinadamu inahatarishwa na kuathiriwa kwa huzuni bila ya mabadiliko ya mwelekeo katika kuchukua jukumu la kisiasa na bila heshima kwa taasisi na makubaliano na Sheria za Kimataifa.  Kwa hakika hili ni chukizo kwa Mungu. Jina lake takatifu halipaswi kuchafuliwa kwa nia ya kutawala, kwa kiburi au kwa ubaguzi; juu ya yote, halipaswi kuombwa ili kuhalalisha uchaguzi na matendo yanayo chochea utamaduni wa kifo. Changamoto kwa nchi ya Guinea ya Ikweta kuthamini njia zake za maendeleo endelevu na fursa chanya katika ngazi ya Kimataifa kwa kuzingatia huduma na utawala wa sheria na haki. Baba Mtakatifu amegusia pia ujenzi wa Makao makuu ya nchi, Mafundisho Jamii ya Kanisa, Changamoto za maisha ya binadamu tangu kuumbwa kwake, Maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia na kwamba, Kanisa litaendelea kuchangia mchakato kwa ajili ya malezi ya dhamiri huru, nyofu na yenye kuwajibika, itakayowawezesha kusonga mbele pamoja kuelekea siku zijazo.  Katika dunia iliyojeruhiwa na kiburi, watu wana njaa na kiu ya haki.  Ni muhimu kuwatia moyo wale wanaoamini katika amani na kuthubutu kujihusisha na siasa za upinzani zinazotoa kipaumbele cha kwanza kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Elimu iwe ni chachu ya fursa na matumaini kwa vijana wa kizazi kipya. Mji wa Mungu uwe ni kitovu cha amani, upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu.

Papa Leo XIV Diplomasia
21 Aprili 2026, 18:25