Tafuta

Akiwa njiani kurejea mjini Vatican, Baba Mtakatifu Leo XIV amepata nafasi ya “kuchonga” na waandishi 70 walioko kwenye msafara wake  kuhusu hija yake ya kitume Barani Afrika Akiwa njiani kurejea mjini Vatican, Baba Mtakatifu Leo XIV amepata nafasi ya “kuchonga” na waandishi 70 walioko kwenye msafara wake kuhusu hija yake ya kitume Barani Afrika  (@Vatican Media)

Hija ya Kitume ya Papa Leo XIV Barani Afrika: Mahojiano na Wanahabari

Papa Leo XIV amepata nafasi ya “kuchonga” na waandishi 70 waliokuwa kwenye msafara wake: Dhamana na utume wake wa kwanza ni kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Kamwe hawezi kukaa kimya na kuangalia mateso na mahangaiko ya watoto wasiokuwa na hatia kwenye maeneo ya vita; Msimamo wa Kanisa kuhusu huduma ya wakimbizi na wahamiaji na kwamba, mchakato wa baraka kwa wapenzi wa jinsia moja nchini Ujerumani ni batili.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Leo XIV kuanzia tarehe 13 hadi tarehe 23 Aprili 2026 amefanya Hija ya Kitume ya Siku 10 kwa kutembelea: Algeria, Cameroon, Angola pamoja na Guinea ya Ikweta kama hujaji na shuhuda wa matumaini, amani na upatanisho mkazo ni kwa Familia ya Mungu Barani Afrika kuhakikisha kwamba, inajikita katika mchakato wa kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na upatanisho, ili kweli Afrika iwe ni mahali pazuri zaidi pa kuishi! Baba Mtakatifu Leo XIV amehitimisha Hija yake ya Kitume Barani Afrika akiwa amebeba ndani mwake: Amana na utajiri wa imani, matumaini na mapendo. Hii ni hazina kubwa iliyojumuisha hadithi, nyuso, na shuhuda mbalimbali za furaha na huzuni, ambazo zinaendelea kuboresha maisha, utume na huduma yake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Kama ilivyokuwa kwenye Karne za Mwanzo za maisha na utume wa Kanisa, leo hii Kanisa Barani Afrika linaalikwa kuchangia kwa kiasi kikubwa utakatifu, ari, mwamko na utume wa kimisionari wa watu wa Mungu. Baba Mtakatifu Leo XIV akiwa njiani kurejea mjini Vatican amewatumia wakuu wa nchi za: Guinea ya Ikweta, akiwashukuru kwa mapokezi na ukarimu mkubwa waliomwonesha wakati akiwa nchini mwao, anawaombea umoja, ustawi na maendeleo. Akiwa kwenye anga la Cameroon, amewashukuru na kuwaombea watu wa Mungu nchini Cameroon mshikamano wa udugu wa kibinadamu na furaha; kwa watu wa Mungu nchini Nigeria, Baba Mtakatifu amewatakia utulivu na furaha ya kweli; Kwa wananchi wa Niger, Baba Mtakatifu amewatakia wingi wa baraka na neema kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Amewatakia matashi mema watu wa Mungu nchini Algeria na kuwaombea ukarimu wa Mungu.

Papa Leo XIV akifanya mahojiano na waandishi wa Habari 23 Aprili 2026
Papa Leo XIV akifanya mahojiano na waandishi wa Habari 23 Aprili 2026   (@Vatican Media)

Akiwa kwenye anga la Tunisia, Baba Mtakatifu Leo XIV amewahakikishia sala zake ili waweze kujikita katika mchakato wa ujenzi wa umoja na maridhiano. Baba Mtakatifu Leo XIV alipowasili kwenye anga la Italia, amemwelezea Rais Sergio Mattarella kwamba, anarejea kutoka katika hija yake ya kwanza Barani Afrika ambako kwa furaha kubwa amekutana na watu wa Mungu waliosimika mizizi yao katika mapokeo ya kiimani, huku wakionesha ari na mwamko wa kutaka kusonga mbele katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kwa upande wake Rais Sergio Mattarella, amemkaribisha Baba Mtakatifu Leo XIV kwa moyo mkunjufu na kwamba, kwa hakika amekuwa ni shuhuda na mjumbe wa: amani, matumaini na ujenzi wa udugu wa kibinadamu; majadiliano ya kidini na kiekumene pamoja na ushirikiano wa Jumuiya ya Kimataifa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi; mambo ambayo yamekuwa ni kiini cha ujumbe wa Baba Mtakatifu Leo XIV wakati wa Hija yake ya Kitume Barani Afrika. Hii ni changamoto kwa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, inalisaidia Bara la Afrika kusonga mbele, kwa uwajibikaji uliopyaishwa na unaojikita katika ushirikiano, ili kuendeleza mchakato wa kudumu wa ujenzi wa jamii na uchumi endelevu na shirikishi. Amemtakia kheri na baraka katika utekelezaji wa “Magisterium yake” yaani Mamlaka fundishi ya Kanisa.

Hija ya Kitume Barani Afrika imesheheni imani, matumaini na mapendo
Hija ya Kitume Barani Afrika imesheheni imani, matumaini na mapendo   (@Vatican Media)

Akiwa njiani kurejea mjini Vatican, Baba Mtakatifu amepata nafasi ya “kuchonga” na waandishi 70 waliokuwa kwenye msafara wake na kukazia kwamba, dhamana na utume wake wa kwanza ni kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa. Kamwe hawezi kukaa kimya na kuangalia mateso na mahangaiko ya watoto wasiokuwa na hatia kwenye maeneo ya vita; Msimamo wa Kanisa kuhusu huduma ya wakimbizi na wahamiaji na kwamba, mchakato wa baraka kwa wapenzi wa jinsia moja nchini Ujerumani bado haujaridhiwa na Vatican. Baba Mtakatifu Leo XIV akizungumza na waandishi wa habari amesema katika hija yake ya Kitume Barani Afrika alipenda hasa zaidi kuwafahamu na kuwasindikiza watu wa Mungu Barani Afrika, lakini lengo kuu lilikuwa ni kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu inayochota amana na utajiri wake kutoka kwa Kristo Yesu, ili hatimaye, kuwasaidia watu wa Mungu, kuwajibika katika kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo, katika hali na mazingira yao, ili hatimaye kuimarisha imani yao kwa Kristo Yesu, kwa kukazia toba na wongofu wa ndani; kwa kuendelea kujikita katika mchakato wa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi; kwa ugawanaji sawa wa rasilimali na utajiri wa nchi.

Licha ya mvua kubwa, watu walionesha na kushuhudia imani yao
Licha ya mvua kubwa, watu walionesha na kushuhudia imani yao   (@Vatican Media)

Baba Mtakatifu anasema, Hija yake ya Kitume Barani Afrika imekuwa na mafanikio makubwa, lakini nchini Guinea ya Ikweta imetia fola licha ya mvua kubwa kunyeesha, lakini watu wa Mungu walionesha ushuhuda wa imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake kwa ari na moyo mkuu. Kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kujenga na kudumisha utamaduni wa haki, amani na upatanisho, ili kuondokana na mateso pamoja na mahangaiko ya watu wasiokuwa na hatia kutokana na vita, kama vita inayoendelea kati ya Marekani, Israeli na Iran, hapa kuna haja ya kujenga na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo, kwa kujikita katika mchakato wa majadiliano kwa ajili ya haki, amani na maridhiano sanjari na kutekeleza haki ya Kimataifa. Kama mchungaji na Kiongozi wa Kanisa anasema Baba Mtakatifu Leo XIV anapinga vikali vita na kwamba, anapenda kutoa shime kwa watu wote kujenga na kuimarisha utamaduni wa haki, umoja na amani na hivyo kuondokana na chuki, uhasama na migawanyiko isiyokuwa na tija kwa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Changamoto kubwa ya wakimbizi inahitaji sera za uwekezaji na utu wema
Changamoto kubwa ya wakimbizi inahitaji sera za uwekezaji na utu wema   (AFP or licensors)

Sera na mbinu mkakati wa Kanisa Katoliki katika huduma kwa wakimbizi na wahamiaji inajikita katika mambo makuu manne yaani: “Kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwahusisha wakimbizi na wahamiaji” katika maisha ya jamii inayowapokea na kuwapatia hifadhi na usalama wa maisha! Wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji ni changamoto ya Kimataifa. Kuna Biashara haramu ya binadamu na mifumo yote ya utumwa mamboleo ambayo ni saratani ya kijamii na uhalifu mkubwa unaosigina: utu, heshima na haki msingi za binadamu; mambo ambayo wakati mwingine yanafumbiwa macho na jamii. Wahusika wakuu anasema Baba Mtakatifu Leo XIV ni vijana wanaotafuta fursa, lakini Serikali mbalimbali kwa kukazia utawala wa sheria zinaweza kudhibiti wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji, kwani wakati mwingine watu hawa wanapokuwa vizuizini wanakabiliwa na hali ngumu ya maisha kuliko hata kule walikotoka. Je, nini kinaweza kufanyika ili kudhibiti wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji kutoka sehemu mbalimbali za dunia? Anauliza Baba Mtakatifu Leo XIV. Je, uwekezaji mkubwa wa Makampuni ya Kimataifa unaweza kusaidia kudhibiti wimbi hili? Kuna haja ya kukuza na kudumisha misingi ya haki, usawa, ustawi na maendeleo kwa Bara la Afrika na kwamba, hawa ni binadamu wanapaswa kushughulikiwa kwa kuheshimu utu na ubinadamu wao na wala si kutendewa kama wanyama pori!

Diplommasia ya Vatican inajikita katika utu, heshima na haki msingi
Diplommasia ya Vatican inajikita katika utu, heshima na haki msingi   (@Vatican Media)

Diplomasia ya Vatican na Kanisa Katoliki katika ujumla wake, kimsingi inakazia kwa namna ya pekee kabisa: huduma makini ya maendeleo fungamani ya binadamu; kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha: utu, heshima na haki msingi za binadamu. Mambo mengine msingi ni: amani na maridhiano kati ya watu; huduma makini kwa wakimbizi na wahamiaji duniani; elimu, afya, biashara, mawasiliano, ushirikiano na mshikamano wa Jumuiya ya Kimataifa pamoja na haki miliki ya kiakili. Hizi ni kanuni msingi zinazofumbatwa katika Mafundisho Jamii ya Kanisa yanayotoa dira na mwongozo makini kwa Jumuiya ya Kimataifa katika mchakato wa kukuza na kudumisha utamaduni wa amani, haki, ustawi na maendeleo endelevu ya binadamu. Hii ni sehemu muhimu sana ya utangazaji na ushuhuda wa Habari Njema ya Wokovu miongoni mwa Jumuiya ya Kimataifa. Vatican katika masuala ya kidiplomasia ya Kimataifa inafuata kwa makini sana: Sheria za Kimataifa, taratibu na kanuni za Jumuiya ya Kimataifa sanjari na kuendelea kuwa ni sauti ya kinabii inayojikita katika kanuni maadili na ushirikiano unaosimamiwa na kuratibiwa na kanuni auni. Amani haiwezi kufikiwa mara moja kwa daima, bali inadaiwa kujengwa siku kwa siku. Amani ni matokeo ya haki inayomwilishwa katika upendo, utu, heshima na haki msingi za binadamu. Rej. GS 78. Kumbe, Hija za Kitume za Baba Mtakatifu nje ya Vatican ni fursa kwa Papa kukutana na kuzungumza na watu katika medani mbalimbali za maisha, ili kujenga na kudumisha: haki, amani na maridhiano, ili hatimaye kuhakikisha kwamba, tunu msingi za Kiinjili zinamwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu kama sehemu ya mchakato wa maboresho ya maisha yao. Vatican inapenda kuhakikisha kwamba, inazisaidia nchi mbalimbali ili kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano.

Mkutano na wanadiplomasia na viongozi wakuu wa Serikali ni Uinjilishaji
Mkutano na wanadiplomasia na viongozi wakuu wa Serikali ni Uinjilishaji   (@Vatican Media)

Tamko la Mafundisho Tanzu ya Kanisa “Fiducia supplicans” Yaani “Kuomba Baraka kwa Imani” Maana ya Baraka Kichungaji” lilijadiliwa katika mkutano wa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa, likapelekwa kwa Baba Mtakatifu Francisko na hatimaye, akaridhia lichapwe kwa kuweka saini yake tarehe 18 Desemba 2023. Tamko hili linajadili kwa kina na mapana kuhusu: Baraka katika Sakramenti ya Ndoa, Maana ya baraka katika Maandiko Matakatifu, Uelewa wa baraka kitaalimungu na kichungaji, na nani anaweza kuomba baraka. Baraka kwa watu wenye “ndoa tenge” pamoja na wapenzi wa jinsia moja. Kanisa ni Sakramenti ya upendo wa Mungu. Watu wa Mungu wenye imani thabiti wanaweza kupokea baraka za Mwenyezi Mungu kwa njia ya Kristo Yesu na Kanisa na kwamba, Kristo Yesu ni kielelezo cha baraka kuu kutoka kwa Mungu, baraka ambayo ni chemchemi ya wokovu. Baraka katika Sakramenti ya Ndoa Takatifu: Kiini cha ndoa ya Kikristo ni maagano baina ya mume na mke au ukubaliano wao wa hiari usiotanguka. Muungano huo wa mume na mke na manufaa ya watoto wao huwataka wawe na uaminifu kamili kati yao. Kwa asili yake ndoa na mapendo ya wenye ndoa yamewekwa kwa ajili ya kuzaa watoto na kuwalea; nao ni taji yao. Kwa kweli watoto ni zawadi kuu ya Ndoa na tunu kubwa ya wazazi wenyewe.

Kiini cha Ndoa ya Kikristo ni maagano kati ya mume na mke
Kiini cha Ndoa ya Kikristo ni maagano kati ya mume na mke   (@Vatican Media)

Haya ndiyo Mafundisho tanzu ya Kanisa kuhusu Ndoa na kamwe hayawezi kubadilishwa. Wakati wa kutoa baraka, Kanisa lina wajibu na dhamana ya kuhakikisha kwamba halichanganyi madhehebu ya kutoa baraka, ili kusitokee mkanganyiko na kwamba, Kanisa halina mamlaka ya kutoa baraka kwa wapenzi wa jinsia moja. Tamko hili likapokelewa kwa hisia tofauti na hivyo kuzua mjadala mkali wa: Kiimani, kimaadili, kisheria na utu wema kutoka sehemu mbalimbali za dunia. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, uhusiano wa kijinsia si tema pekee ya kanuni maadili na utu wema katika maisha na utume wa Kanisa. Kuna tema msingi kama vile: Haki, Amani; Usawa pamoja na Uhuru wa kidini mambo yanayopaswa kupewa kipaumbele cha kwanza. Vatican imeonesha msimamo kwamba, haikubaliani na mchakato wa Kardinali Reinhard Marx, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Munich na Freising nchini Ujeruman wa kutoa baraka kwa wapenzi wa jinsia moja. Lengo la Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake, lilikuwa ni kuonesha kwamba, watu wote wanakaribishwa na kupokelewa na Kristo, jambo la msingi ni wao kujikita katika toba na wongofu wa ndani. Baraka kwa wapenzi wa jinsia moja kwa nyakati hizi ni changamoto inayoweza kuvunja umoja wa Kanisa, changamoto kwa waamini kujitahidi kujenga na kudumisha umoja na ushirika wao na Kristo Yesu sanjari na kufuata Mafundisho yake.

Mafundisho Jamii ya Kanisa: Haki, Amani, Usawa na Uhuru wa Kidini
Mafundisho Jamii ya Kanisa: Haki, Amani, Usawa na Uhuru wa Kidini   (AFP or licensors)

Adhabu ya kifo ni kinyume kabisa cha kanuni maadili, utu na heshima ya binadamu. Adhabu ya kifo ni kielelezo cha kutoheshimu zawadi ya uhai. Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Francisko aliridhia kwa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa kufanya marekebisho kwenye Katekisimu ya Kanisa Katoliki, kifungu namba 2267 kinachozungumzia kuhusu adhabu ya kifo na tafsiri mpya inapaswa kuingizwa katika vipengele mbalimbali vya Katekisimu ya Kanisa Katoliki. Kanisa Katoliki limefuta adhabu ya kifo katika Mafundisho na Mapokeo yake kwa kukazia njia zinazotetea na kulinda maisha ya watu, amani na usalama wao dhidi ya adui; kwani hizi ni njia zinazodumisha utu, ustawi na mafao ya wengi. “Kwa kweli leo, kutokana na uwezekano ambao serikali inao siku hizi wa kuweza kufaulu kuzuia uhalifu kwa aliyetenda kosa asiweze kuleta madhara bila kumwondolea kabisa uwezo wa kujikomboa mwenyewe, kesi ambazo kumuua mkosaji ni lazima kabisa kabisa ni chache sana na “kwa kweli karibu haziko kabisa.” Kanisa linafundisha kwa mwanga wa Injili kwamba “Adhabu ya kifo haikubaliki kwa sababu inadhuru haki na utu wa mtu.” Kanisa linaendelea kujizatiti ili kuhakikisha kwamba, adhabu ya kifo inaondolewa duniani kote! Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, analaani vitendo vyote vinavyopandikiza utamaduni wa kifo na mauaji ya watu na kwamba, adhabu ya kifo imepitwa na wakati. Injili ya uhai inapaswa kuheshimiwa tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake hadi kifo cha kawaida kinapomsibu. Pale Serikali inapotoa adhabu ya kifo kwa raia wake, hili ni tukio ambalo linapaswa kulaaniwa!

Papa Leo XIV Mahojiano
24 Aprili 2026, 16:35