Tafuta

Papa Leo XIV Jumatatu tarehe 20 Aprili 2026 Ametembelea nyumba ya wazee na kuwafariji. Papa Leo XIV Jumatatu tarehe 20 Aprili 2026 Ametembelea nyumba ya wazee na kuwafariji.   (@Vatican Media)

Hija ya Kitume ya Papa Leo XIV Angola: Nyumba ya Wazee Saurimo!

Huduma kwa wanyonge ndani ya jamii ni kielelezo cha ubora wa maisha ya kijamii katika Taifa lolote. Papa Leo XIV anasema, wazee wanahitaji kusikilizwa, kwa sababu hawa wanatunza ndani mwao hekima na busara ya jamii. Hija hii ya Kitume kwenye nyumba hii, anasema Papa Leo XIV imeacha kumbukumbu ya kudumu katika akili na moyo wake. Nyumba hii inawahudumia wazee 62 na kati yao kuna wanaume 26 na wanawake 36, waliotelekezwa na familia zao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Hija ya Kitume ya Baba Mtakatifu Leo XIV nchini Angola kuanzia Jumamosi tarehe 18 hadi Jumanne tarehe 21 Aprili 2026, inanogeshwa na kauli mbiu “Papa Leo XIV, Hujaji wa Matumaini, Upatanisho na Amani, Ibariki Angola.” Baba Mtakatifu kabla ya kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu, Jumatatu tarehe 20 Aprili 2026 ametembelea na kuzungumza na wazee wanaotunzwa na Jimbo kuu la Saurimo, lililoko Kusini mwa Angola. Kituo hiki cha kutunzia wazee kinaitwa “Nyumba” ambamo wazee wanaishi katika mazingira ya kifamilia, kama ilivyokuwa kwa Kristo Yesu alivyopenda kuwatembelea rafiki zake kama ilivyokuwa nyumbani mwa Mtakatifu Petro, Mtume na kwa rafiki zake Maria, Martha na Lazaro, hapo akakaribishwa kama Mwalimu. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Leo XIV kwamba, Kristo Yesu anaishi pamoja na hawa wazee, kila mara wanapojitahidi kupendana na kusaidiana kama ndugu wamoja; wanaposamehena na kuendelea kujikita katika mchakato wa upatanisho; wanaposali pamoja katika hali ya unyenyekevu, hapo Kristo Yesu yuko pamoja na kati yao.

Wazee wanapaswa kusikilizwa na kuhudumiwa
Wazee wanapaswa kusikilizwa na kuhudumiwa   (AFP or licensors)

Baba Mtakatifu Leo XIV ametumia fursa hii kuishukuru na kuipongeza Serikali ya Angola, kwa kusimama kidete kwa ajili ya huduma kwa wahitaji zaidi ndani ya jamii, hasa wazee, amewashukuru wahudumu pamoja na watu wote wa kujitolea. Huduma kwa wanyonge ndani ya jamii ni kielelezo cha ubora wa maisha ya kijamii katika Taifa lolote. Baba Mtakatifu anasema, wazee wanahitaji kusikilizwa, kwa sababu hawa wanatunza ndani mwao hekima na busara ya jamii. Hija hii ya Kitume kwenye nyumba hii, anasema Baba Mtakatifu Leo XIV imeacha kumbukumbu ya kudumu katika akili na moyo wake. Mwishoni amewatakia kheri na baraka tele, kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria katika Familia Takatifu iliyosheheni imani na mapendo, aendelee kuwasimamia na kuwalinda, kwa tunza yake ya kimama.

Mama akitoa ushuhuda wa huduma ya upendo mbele ya Papa Leo XIV
Mama akitoa ushuhuda wa huduma ya upendo mbele ya Papa Leo XIV   (@Vatican Media)

Kwa upande wao, wazee wanaohudumiwa Kituoni hapo, wamemwonesha baba Mtakatifu Leo XIV furaha na basheshe kubwa, kwani uwepo wake kati yao ni chemchemi ya furaha inayoendelea kukuza na kuboresha matumaini katika maisha na kwamba, uwepo wake unasaidia sana kuimarisha imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Hii ni nyumba inayowahudumia wazee 62 kati yao kuna wanaume 26 na wanawake ni 36, wengi wao ni wale ambao wametelekezwa na familia zao; watu waliokuwa wananyanyaswa na kudhulumiwa; wengine walishutumiwa kwa kuhusika na imani za kishirikina. Kuna baadhi yao wanaokabiliwa na changamoto ya afya ya akili.

Nyumba ya Wazee
20 Aprili 2026, 17:04