Tafuta

Hija ya Papa Leo XIV nchini Angola inanogeshwa na kauli mbiu “Papa Leo XIV, Hujaji wa Matumaini, Upatanisho na Amani, Ibariki Angola. Hija ya Papa Leo XIV nchini Angola inanogeshwa na kauli mbiu “Papa Leo XIV, Hujaji wa Matumaini, Upatanisho na Amani, Ibariki Angola.   (@Vatican Media)

Hija ya Kitume ya Papa Leo XIV Angola: Injili ya Wafuasi wa Emau

Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, Hija ya imani na matumaini inaendelea nchini Angola, ili watu wa Mungu nchini Angola waweze kusimama kidete kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu; kwa kujenga na kudumisha: haki, amani na maridhiano, sanjari na uragibishaji wa udugu wa kibinadamu. Ujumbe mahususi ni kwamba, Kristo Amefufuka. Waamini wajenge uhusiano katika: Sala, Neno sanjari na maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu kiini cha utume!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Hija ya Kitume ya Baba Mtakatifu Leo XIV nchini Angola kuanzia Jumamosi tarehe 18 hadi Jumanne tarehe 21 Aprili 2026, inanogeshwa na kauli mbiu “Papa Leo XIV, Hujaji wa Matumaini, Upatanisho na Amani, Ibariki Angola.” Kristo Yesu ni utimilifu wa Torati na Unabii, mwaliko kwa waamini kuendelea kumtambua Kristo Mfufuka katika: Neno linapotangazwa na kufafanuliwa, Sakramenti za Kanisa na hasa zaidi Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, Sala na katika Matendo ya huruma: kiroho na kimwili, tayari kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, kama walivyofanya wale Wafuasi wa Emau. Hakuna tena hofu wala wasiwasi wa kashfa ya Fumbo la Msalaba. Baraza la Maaskofu Katoliki Angola, Sao Tome na Principe, CEAST, linawaalika waamini na watu wote wa Mungu nchini Angola kuonesha roho ya ushirika, mshikamano, na uwajibikaji na utaratibu wakati wote wa Hija ya Kitume ya Baba Mtakatifu Leo XIV nchini mwao. Baba Mtakatifu Leo XIV, Dominika tarehe 19 Aprili 2026 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu katika eneo la tambarare lililoko Kilamba, nje kidogo ya mji mkuu wa Luanda, Angola. Na katika mahubiri yake amesema, katika utangulizi wa Injili anaona historia ya Angola ikiakisiwa katika uzuri wake na majeraha; nchi ambayo ina njaa na kiu ya matumaini, amani na udugu wa kibinadamu.

Ekaristi Takatifu ni mahali pa kukutana na Mwenyezi Mungu
Ekaristi Takatifu ni mahali pa kukutana na Mwenyezi Mungu   (ANSA)

Habari Njema hata kwa watu katika Ulimwengu mamboleo ni kwamba, Kristo Yesu yu hai, amefufuka na anatembea kando ya waja wake, wanapoendelea kusafiri katika njia ya mateso na uchungu, huku akifungua macho yao, ili kutambua kazi yake na hivyo kuwakirimia neema na baraka za kuanza upya ujenzi wa wakati ujao. Waamini wanapata tajiriba ya ujenzi wa ushirika na Kristo Yesu, katika: Uhusiano, Sala, Kusikiliza, Kutafakari na Kulimwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha ya ona hivyo kuifanya mioyo yao kuwaka kama ilivyokuwa kwa wale wafuasi wa Emau, lakini zaidi katika kuadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu na hapo ndipo wanapokutana na Mwenyezi Mungu. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, katika Maadhimisho ya Liturujia ya Neno la Mungu, Dominika ya tatu ya Kipindi cha Pasaka, Kristo Yesu anazungumza na kuwaangaza waja wake kwa njia ya Injili ya Wafuasi wa Emau, waliokuwa wamevunjika na kupondeka moyo kutokana na Kashfa ya Fumbo la Msalaba, yaani mateso na kifo cha Kristo Msalabani, kiasi kwamba, tukio hili lilizika kabisa matumaini yao. Katika utangulizi wa Injili anaona historia ya Angola ikiakisiwa katika uzuri wake na majeraha; nchi ambayo ina njaa na kiu ya matumaini, amani na udugu wa kibinadamu.

Angola ina kiu na njaa ya haki, amani, maridhiano, ustawi na maendeleo
Angola ina kiu na njaa ya haki, amani, maridhiano, ustawi na maendeleo   (@Vatican Media)

Mazungumzo ya wafuasi wa Emau yanasimikwa katika historia ya machungu kama ilivyo pia Angola ambayo imepitia miaka mingi ya vita ya wenyewe kwa wenyewe, iliyojenga chuki, uhasama, uadui na migawanyiko kati ya watu, kiasi cha kuzalisha umaskini wa hali na kipato pamoja na ukwapuaji wa rasilimali za nchi, kiasi cha kupoteza matumaini na watu wakajikuta wakiwa wamekata tamaa ya maisha, na hivyo kushikwa na “ganzi” la maisha. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, Habari Njema hata kwa watu katika Ulimwengu mamboleo ni kwamba, Kristo Yesu yu hai, amefufuka na anatembea kando ya waja wake, wanapoendelea kusafiri katika njia ya mateso na uchungu, huku akifungua macho yao, ili kutambua kazi yake na hivyo kuwakirimia neema na baraka za kuanza upya ujenzi wa wakati ujao. Wafuasi wa Emau katika kutanguzana na Kristo Mfufuka wakagundua upendo wa Mungu uliokuwa unaambatana nao na alipokuwa ameketeti nao chakulani, yakafumbuliwa macho yao, wakamtambua. Rej. Lk 24: 31.

Jengeni uhusiano na Kristo Yesu katika: Sala, Neno na Ekaristi Takatifu
Jengeni uhusiano na Kristo Yesu katika: Sala, Neno na Ekaristi Takatifu   (@Vatican Media)

Baba Mtakatifu Leo XIV amewaambia watu wa Mungu nchini Angola hii ni fursa ya kuanza tena, kwa kutambua kwamba, Kristo Mfufuka daima ataendelea kuambatana nao na kwamba, anapenda kuwaonesha huruma na upendo wake usiokuwa na mipaka. Waamini wanapata tajiriba ya ujenzi wa ushirika na Kristo Yesu, katika: Uhusiano, Sala, Kusikiliza, Kutafakari na Kulimwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha yao na hivyo kuifanya mioyo yao kuwaka kama ilivyokuwa kwa wale wafuasi wa Emau, lakini zaidi katika kuadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu na hapo ndipo wanapokutana na Mwenyezi Mungu. Huu ni mwaliko wa kuwa makini na dini asili zinazokita mizizi yake katika tamaduni za watu, lakini wawe makini kutochanganya dini asilia na imani za kishirikina, ambazo kimsingi haziwezi kuwasaidia katika ukomavu wa maisha ya kiroho. Baba Mtakatifu Leo XIV anawataka waamini nchini Angola kukita maisha yao katika Mafundisho ya Kanisa, kwa kujiaminisha kwa wachungaji wao wa maisha ya kiroho na kuendelea kumtazama Kristo Yesu anayejifunua kwa njia ya Maandiko Matakatifu na katika Fumbo la Ekaristi Takatifu; mahali ambapo waamini wanaonja na kuhisi uwepo angavu na endelevu wa Kristo Yesu katika maisha yao, huku wakitembea kutoka kwa wafu, ili kuishi katika Fumbo la Ufufuko. Waamini wanapaswa kumtambua Kristo Yesu katika kuumega Mkate, yaani kushiriki kikamilifu katika Fumbo la Ekaristi Takatifu, ili nao kwa upande wao wageuke na kufanywa kuwa ni Mkate unaomegwa kwa ajili ya ukombozi wa walimwengu.

Angola imepitia katika historia ya machungu ya vita, ujinga, umaskini na njaa
Angola imepitia katika historia ya machungu ya vita, ujinga, umaskini na njaa   (@Vatican Media)

Angola bado inaogelea katika hali ngumu ya kijamii ni kiuchumi; umaskini wa hali na kipato na kwamba, uwepo wa Kanisa unapania pamoja na mambo mengine, kusikiliza na kujibu kilio cha watoto wake. Hili ni Kanisa katika mwanga wa Neno la Mungu na Ekaristi Takatifu linafahamu jinsi ya kupyaisha tena matumaini yaliyovunjika; hili Kanisa ambalo lina watu ambao wako tayari kujisadaka na kujimega bila ya kujibakiza, kama kielelezo cha upendo na msamaha kwa pande zote mbili; kwa kuendelea kujizatiti katika upendo, msamaha, tayari kujenga udugu wa kibinadamu, amani, huruma na mshikamano na wale wanaohitaji zaidi. Katika Fumbo la Ekaristi Takatifu, wafuasi wote wa Kristo Yesu watambue kwamba wao ni mwili na roho moja, tayari kujikita katika ujenzi wa nchi yao, kwa kuvuka vikwazo vya utengano wa zamani, vita, chuki na janga la rushwa. Madonda yote haya yatibiwe na kuponywa na utamaduni mpya wa haki na ushirikiano na kwa njia hii, vijana wataweza kupata matumaini mapya waliyopoteza. Huu ni mwaliko wa kutazama ya mbeleni ili kujenga matumaini ya siku za usoni. Baba Mtakatifu Leo XIV anawaalika watu wa Mungu nchini Angola, kamwe wasiogope kuthubutu kutenda hayo, kwani Kristo Yesu anayeambatana kati pamoja nao, katika kuumega Mkate anawahamasisha wawe ni vyombo na mashuhuda wa ufufuko wake na wadau wakuu wa ujenzi wa ubinadamu mpya na jamii mpya na kwamba, anawahakikishia uwepo na sala zake. Mwishoni mwa mahubiri yake, Baba Mtakatifu Leo XIV amewaweka watu wa Mungu nchini Angola chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria wa Muxima, “Mamã Muxima” ili aweze kuwaimarisha katika imani, matumaini na mapendo.

Waamini wamtambue Kristo katika kuumega Mkate
Waamini wamtambue Kristo katika kuumega Mkate   (@Vatican Media)

Kwa upande wake, Askofu mkuu Filomeno do Nascimento Vieira Dias wa Jimbo kuu la Luanda, Angola baada ya maadhimisho ya Misa Takatifu, amemshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Leo XIV kwa uwepo na ujumbe wake maridhiwa, unaowahamasisha watu wa Mungu nchini Angola kushikamana katika wema, ukweli, haki na amani; Waendelee kujikita katika ujenzi wa udugu wa kibinadamu, ili hatimaye, kila mmoja wao, aweze kuwa ni chemchemi ya furaha, ustawi na maendeleo ya wengi, bila kuwabakiza wengine nyuma. Waendelee kujikita katika mchakato wa ujenzi wa haki, amani na maridhiano, ili kupata amani ya kudumu.

Ibada ya Misa Takatifu
19 Aprili 2026, 16:15