Hija ya Kitume ya Papa Leo XIV Angola: Ibada ya Rozari Takatifu
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Madhabahu kimsingi ni mahali pa: Sala na Ibada kwa Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa, anayetoa machozi ya faraja kwa wale wanaoteseka na kuhuzunika huku Bondeni kwenye machozi. Ni mwombezi wa watu waliovunjika na kupondeka moyo; watu waliokata tamaa na kwamba, Bikira Maria anajaribu kujibu sala ya kila mwamini anayekimbilia ulinzi na tunza yake ya daima. Madhabahu ni mahali ambapo panapaswa kukuza na kudumisha ari na moyo wa Sala ya Kanisa, maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa kama sehemu ya kazi ya ukombozi. Ni mahali pa shuhuda za: imani, matumaini na mapendo, kielelezo cha Kanisa linalokesha na kusali daima! Madhabahu ni mahali pa ukimya unaopaswa kububujika kutoka katika undani wa mahujaji, tayari kuomba: baraka, neema na rehema pamoja na kudumisha upendo kwa Mungu na jirani! Madhabahu ni mahali pa kuonja huruma na upendo wa Mungu unaofumbatwa katika Sakramenti ya Upatanisho, Mahakama ya huruma ya Mungu. Maeneo kama haya yanahitaji wakleri waliofundwa barabara, watakatifu, vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake. Ni matumaini ya Hayati Baba Mtakatifu Francisko kwamba, katika madhabahu, kamwe hawatakosekana Wamisionari wa huruma, mashuhuda wa upendo wa Mungu unaokoa na kuponya! Madhabahu yawe ni mahali pa kumwilisha upendo, kielelezo cha utekelezaji wa Amri ya Upendo kwa Mungu na jirani!
Waamini wanahamasishwa kuendelea kusali Rozari Takatifu, muhtasari wa historia nzima ya kazi ya ukombozi; maisha na utume wa Kristo Yesu. Bikira Maria alipowatokea Watoto watatu wa Fatima yaani Francis, Yacinta na Lucia aliwaagiza kusali Rozari Takatifu kwa ajili ya toba, wongofu wa ndani, maridhiano, haki na amani duniani. Hija ya Kitume ya Baba Mtakatifu Leo XIV nchini Angola kuanzia Jumamosi tarehe 18 hadi Jumanne tarehe 21 Aprili 2026, inanogeshwa na kauli mbiu “Papa Leo XIV, Hujaji wa Matumaini, Upatanisho na Amani, Ibariki Angola. Dominika tarehe 19 Aprili 2026, Baba Mtakatifu Leo XIV amewaongoza watu wa Mungu nchini Angola kusali Rozari Takatifu katika Madhabahu ya Bikira Maria wa Muxima: “Mamã Muxima” yaliyoko mjini Muxima. Baba Mtakatifu alipowasili, amekwenda moja kwa moja kusali kwenye Kikanisa Bikira Maria wa Muxima: “Mamã Muxima” Yaani “Mama wa Moyo Safi” na hatimaye akaweka shada la maua kwa heshima ya Bikira Maria.
Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, Tafakari ya Rozari Takatifu inapyaisha imani na ni nguvu ya Roho Mtakatifu; Mafumbo ya Utukufu ni mwaliko wa kutafakari hatima ya mwamini, utume na upendo wake. Haya ni Madhabahu kwa ajili ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, Sala ya Rozari Takatifu ni chemchemi ya upendo, mwaliko kwa waamini kuwa ni mashuhuda na vyombo vya haki, amani na baraka kwa watu wote. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, Sala na Tafakari ya Rozari Takatifu inapyaisha imani na ni nguvu ya Roho Mtakatifu. Katika Madhabahu haya, watu wa Mungu wamesali katika nyakati mbalimbali, huku miyo yao ikiwa imesheheniu: upendo, majonzi pamoja na nia zao mbalimbali na kwamba, Bikira Maria wa Muxima anawakaribisha na kusikiliza sala za watu wote. Katika Matendo ya Utukufu, waamini wametafakari kuhusu utukufu wa Kristo Yesu na utume wao katika upendo; Ushindi wa Kristo Mfufuka anayewaonesha waja wake njia ya kwenda mbinguni, kwa kuongozwa na Roho Mtakatifu. Kwa furaha kuu, waamini wanamwangalia Bikira Maria kama kielelezo cha utakatifu na kwamba, Rozari Takatifu inawakilisha miito mbalimbali na kwa kila umri. Ni vyema kwa waamini kusali na kutafakari kuhusu Bikira Maria kukingiwa dhambi ya asili, fursa ya kutafakari hatua mbalimbali za maisha ya Kristo Yesu.
Kwa kusali Rozari Takatifu, waamini wanahamasishwa kuwa ni vyombo vya huruma na mapendo hasa kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii. Ni sala inayomwomba Bikira Maria ili aweze kuwakirimia mahitaji yao msingi yaani, chakula bora, huduma bora za afya na elimu, ili hatimaye, waweze kujikita katika ujenzi wa haki, amani; kwa kupambana fika na umaskini wa hali na kipato, unaosigina utu, heshima na haki msingi za binadamu. Tunu msingi za Kiinjili ziwe ni chemchemi ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Waamini na watu wote wenye mapenzi mema, wanaporejea makwao, waendelee kuwa ni wajumbe wa Injili ya uhai inayowakirimia watu wa Mungu neema na baraka kutoka kwa Mungu kwa ajili ya wote na kwamba, watu wa Mungu wanamwendea Bikira Maria wa Muxima, ili aweze kuwaombea neema na baraka, ili hatimaye, hata wao wenyewe waweze kuwa ni baraka kwa wengine.
Kwa upande wake Askofu Emílio Sumbelelo wa Jimbo Katoliki la Viana, Angola, amemshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Leo XIV kwa kukutana na kusali na waamini wa vyama mbalimbali vya kitume nchini Angola. Madhabahu ya Bikira Maria wa Muxima: “Mamã Muxima” yaliyoko mjini Muxima ni kati ya Madhabahu ya Kale nchini Angola na yalianzishwa kunako Mwaka 1833. Hapa kuna bahari ya watu wanaokusanyika kusali; kuomba ulinzi na tunza ya Bikira Maria; neema na baraka kutoka kwa Kristo Yesu kupitia kwa Bikira Maria. Hizi ni sala zinazopata chimbuko lake katika maisha ya waamini. Kwa wale wanaoshindwa kufika katika Madhabahu haya mubashara, wanatuma sala na maombi yao kwa njia ya Posta. Mwaka 2022, Serikali ya Angola na Kanisa Katoliki waliunganisha nguvu ili kujenga Kanisa kuu la Bikira Maria wa Muxima na jiwe la msingi kubarikiwa na Kardinali Alexandre do Nascimento, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Luanda, Angola “1920-2024.” Kanisa hili litajengwa kwa heshima ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, kama utekelezaji wa ahadi iliyotolewa wakati wa hija ya kitume ya Mtakatifu Yohane Paulo II nchini Angola kunako mwaka 1992. Hapa ni mahali ambapo waamini wanataka kutolea ushuhuda wa imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake kwa njia ya Bikira; ni mahali ambapo waamini wanaonesha uaminifu na upendo wao kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Ni matumaini yao kwamba, iko siku, Kanisa hili litaweza kupewa hadhi ya kuwa ni Madhabahu ya Kitaifa nchini Angola.
