Vita Mashariki ya Kati: Majadiliano Katika Ukweli na Uwazi; Diplomasia ya Kimataifa
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Leo XIV amerudia tena kutoa wito kwa Jumuiya ya Kimataifa kujikita katika kutafuta na kudumisha Injili ya amani, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza katika majadiliano yanayofumbatwa katika ukweli na uwazi, ili kuweza kupata suluhu ya changamoto zinazoikabili Jumuiya ya Kimataifa bila kukimbilia “Mtutu wa bunduki” kama suluhu ya matatizo. Majadiliano katika ukweli na uwazi pamoja na diplomasia ya kimataifa vichukue mkondo wake! Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican katika mahojiano maalum na vyombo vya mawasiliano ya jamii vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Vatican chini ya uratibu wa Dr. Andrea Tornielli, Mhariri Mkuu wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano anasema, watu wa Mungu huko Mashariki ya Kati wamegubikwa na majonzi makuu kutokana na vita inayoendelea kati ya Marekani, Israeli na Iran, kiasi kwamba, kuna watu wengi wanaendelea kupoteza maisha, kuzikimbia nchi zao pamoja na uharibifu mkubwa wa miundo mbinu na kwamba, vita hii ina hatari ya kuweza kuenea sehemu mbalimbali za dunia. Haki, amani na utulivu ni mambo yanayopaswa kupewa kipaumbele kwa njia ya majadiliano na diplomasia ya Kimataifa. Marekani inaweza kudai haki yake katika majukwaa mbalimbali chini ya Umoja wa Mataifa. Ikumbukwe kwamba, Vita kuu ya Pili ya Dunia ilipelekea watu milioni 60 kupoteza maisha na huo ukawa ni mwanzo wa uwepo wa Umoja wa Mataifa, ili kudhibiti matukio kama haya yasijirudie tena ulimwenguni. Kwa hakika kuna haja tena kwa Jumuiya ya Kimataifa kujikita katika diplomasia ya Kimataifa itakayosaidia kukuza na kudumisha majadiliano katika ukweli na uwazi, ili kupata amani ya kudumu na kwamba, amani ya kweli kamwe haiwezi kupatikana kwa njia ya mtutu wa bunduki. Vita haina macho na madhara yake ni makubwa katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.
Vita itaendelea kusababisha maafa makubwa kwa maisha ya watu na mali zao. Ni katika mantiki hii, Vatican inapenda kukazia umuhimu wa majadiliano ya kidiplomasia, ili kuweza kupata suluhu ya kudumu na hivyo kuongeza imani kati ya watu wa Mataifa, chachu ya maendeleo fungamani ya binadamu na amani. Vita inayoendelea kati ya Marekani, Israeli na Iran ingeweza kuzuilika, ikiwa kama kanuni na sheria za Kimataifa zingezingatiwa kama chachu ya kutafuta haki badala ya matumizi ya nguvu ambayo inaendelea kusababisha madhara makubwa kwa watu na mali zao, bila kufuata kanuni na sheria za Kimataifa, dunia itaendelea kuwaka moto wa vita. Dhana kwamba, amani inaweza kupatikana tu ikiwa kama mwenye nguvu ataweza “kumshikisha adabu mwenzake.” Kuna haja kwa wakuu wa nchi kusikiliza na kutekeleza matamanio halali ya wananchi wao. Kardinali Parolin anasema, maandamano makubwa yaliyokuwa yakiendeshwa nchini Iran, huku wananchi wa Iran wakitumia haki yao ya uhuru wa kujieleza, yaligonga mwamba na kwamba, hakuna suluhu ya kweli ya amani inayoweza kupatikana kwa njia ya mtutu wa bunduki. Kwa hakika anasema Kardinali Parolin, Sheria ya Kimataifa na Diplomasia ya Majadiliano ni mambo yanayoendelea kupotea kwa kasi kubwa katika medani mbalimbali za Jumuiya ya Kimataifa kutokana na Mataifa yenyewe kutoaminiana pamoja na uhuru usiokuwa na mipaka ya baadhi ya Mataifa duniani. Kumbe, hapa falsafa inayotumika ni kwamba, “mwenye nguvu mpishe.” Sheria ya Kimataifa ya Haki Msingi za Kibinadamu ni jumla ya kanuni ambazo zinajaribu kuzuia athari za migogoro ya silaha kwa raia. Inawalinda watu ambao hawajihusishi au hawaendelei, kushiriki katika mapigano, wakiwemo raia, madaktari, wafanyakazi wa misaada, waliojeruhiwa, wagonjwa na wanajeshi waliopata ajali katika meli yao, wafungwa wa kivita au wengine wanaoshikiliwa.
Sheria ya Kimataifa imeweka mipaka katika njia na mbinu za kivita kwa mfano, matumizi ya aina fulani ya silaha zimepigwa marufuku na Sheria hii ambayo inajulikana kama Sheria ya vita au Sheria ya mzozo wa silaha, imetengenezwa na mikataba kama vile Maazimio ya Geneva na Taratibu zake za ziada. Hivi leo, uhalifu wa kivita unafafanuliwa na Sheria ya Roma ya Mwaka 1998 ya Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu. Panapotokea mgogoro wa Kimataifa wa silaha, vitendo vyovyote kati ya hivyo vya uhalifu dhidi ya watu au mali inayolindwa chini ya vipengele vya maazimio ya Geneva vinachukuliwa kwamba ni ukiukaji wa Sheria ya Kimataifa ya Haki Msingi za Kibinadamu. Uvunjaji wa Sheria ya Kimataifa unaigawa dunia katika makundi ya watu yaani watu walioko Kundi A wenye haki ya kuishi na kutenda wanavyotaka na Kundi B, ni wale wanaopaswa kushikishwa adabu.Kardinali Parolin katika mahojiano haya maalum anakazia umuhimu wa Sheria ya Kimataifa ya haki msingi za binadamu ambayo ni mfumo wa sheria unaoweka wajibu kwa serikali kulinda na kukuza haki za binadamu na uhuru wa kimsingi, ikiwa na msingi mkuu kwenye Azimio la Kimataifa la Haki za Binadamu la mwaka 1948. Sheria hizi zinatambua haki zote kuwa za ulimwengu wote, zisizoweza kubatilishwa, zinazotegemeana, na zisizogawanyika. Ni katika muktadha huu, Vatican inalaani mashambulio yote yanayofanywa dhidi ya raia wasiokuwa na hatia, miundo mbinu ya shule, hospitali, maeneo ya ibada na kwamba, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kusimama kidete kulinda na kudumisha Injili ya uhai, kama sehemu muhimu sana ya nguzo za haki msingi za binadamu na kwamba, maisha ni zawadi kutoka kwa Mungu na ni matakatifu yanapaswa kulindwa na kudumishwa.
Ni matumaini ya Kardinali Pietro Parolin kwamba, wito wa Baba Mtakatifu Leo XIV utaweza kusikilizwa na kwamba, wahusika wa pande zote, wataweza kusitisha mapigano na kuanza kujielekeza katika utekelezaji wa Sheria za Kimataifa na Diplomasia ya Majadiliano katika ukweli na uwazi; katika uvumilivu na kupeana muda ili matokeo chanya yaweze kupatikana. Huu ni wakati muafaka wa kurejea tena na kuangalia ile misingi iliyopelekea kuanzishwa kwa Umoja wa Mataifa. Itakumbukwa kwamba, Katiba ya Umoja wa Mataifa ilitiwa saini tarehe 26 Juni 1945 wakati wa kukunja jamvi la Kimataifa kwa ajili ya kuanzishwa kwa Umoja wa Mataifa na kuanza kutumika rasmi tarehe 24 Oktoba 1945 na huo ukawa ni mwanzo wa Umoja wa Mataifa. Kardinali Parolin anahitimisha mahojiano haya maalum yaliyoratibiwa na Dr. Andrea Tornielli, Mhariri Mkuu wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano kwa kusema, Wakristo wana imani na matumaini kwa Neno aliyefanyika mwili, ambaye katika mateso yake kule Bustanini Gethsemane alimwamuru Mtume Petro akisema: “Rudisha upanga wako alani mwake.” Mt 26:52. Akiwa juu Msalabani alijionea mwenyewe kitisho cha upofu na jeuri isiyokuwa na maana hata kidogo. Kumbe, watu wa Mungu wana matumaini kwa sababu licha ya vita, maafa makubwa na uharibifu kutokana na kutokuwa na uhakika wa maisha pamoja na hali ya kufadhaisha sana, lakini sauti kutoka sehemu mbalimbali za dunia zinaendelea kupazwa kudai haki na amani, watu wanaomba amani. Wito huu unapaswa kutikisa Serikali na wale wote wanaofanya kazi katika mahusiano ya Kimataifa, kujizatiti zaidi na kuongeza juhudi za kuleta amani duniani.
