Tafuta

Ujumbe wa Baba Mtakatifu Leo XIV kwa Kipindi cha Kwaresima 2026: “Kusikiliza na kufunga: Kwaresima kama Kipindi cha Wongofu wa ndani.” Ujumbe wa Baba Mtakatifu Leo XIV kwa Kipindi cha Kwaresima 2026: “Kusikiliza na kufunga: Kwaresima kama Kipindi cha Wongofu wa ndani.”   (@Vatican Media)

Ujumbe wa Papa Leo XIV Kipindi Cha Kwaresima 2026: Kusikiliza Na Kufunga

Papa Leo XIV: “Kusikiliza na kufunga: Kwaresima kama Kipindi cha Wongofu wa ndani.” Kwaresima ni kipindi ambacho Kanisa kama Mama na Mwalimu, anawaalika watoto wake kutoa kipaumbele cha pekee kwa Fumbo la Mungu katikati ya maisha yao, ili imani ipate tena nguvu na mioyo ya waamini isipotee katikati ya mahangaiko na bughudha za maisha ya kila siku. Kila safari ya wongofu wa ndani huanza pale waamini wanaporuhusu Neno la Mungu liwafikie na kulikaribisha.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kipindi cha Kwaresima kwa mwaka huu 2026 kinanogeshwa na ujumbe wa Baba Mtakatifu Leo XIV: “Kusikiliza na kufunga: Kwaresima kama Kipindi cha Wongofu wa ndani.” Kwaresima ni kipindi ambacho Kanisa kama Mama na Mwalimu, anawaalika watoto wake kutoa kipaumbele cha pekee kwa Fumbo la Mungu katikati ya maisha yao, ili imani ipate tena nguvu na mioyo ya waamini isipotee katikati ya mahangaiko na bughudha za maisha ya kila siku. Kila safari ya wongofu wa ndani huanza pale waamini wanaporuhusu Neno la Mungu liwafikie na kulikaribisha kwa moyo wa unyenyekevu. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, kuna uhusiano kati ya karama ya Neno la Mungu, Nafasi ya Ukarimu na mabadiliko ambayo Neno hili linaleta. Kwa sababu hiyo, safari ya Kwaresima inakuwa fursa muafaka ya kusikiliza sauti ya Mungu na hivyo kupyaisha tena maamuzi ya kumfuasa Kristo Yesu, kwa kutembea katika njia ile iendayo Yerusalemu ambako Fumbo la Pasaka yaani: Mateso, kifo na ufufuko vinapata utimilifu wake. Baba Mtakatifu Leo XIV katika safari ya Kwaresima anakazia utamaduni wa kusikiliza Neno la Mungu kama njia muafaka ya kujenga na kudumisha mahusiano na mafungamano na Mwenyezi Mungu pamoja na jirani, kama ilivyotokea kule Jangwani, Mwenyezi Mungu alipomtokea Mtumishi wake Musa kwenye kijiti kilichokuwa kinawaka moto na Mwenyezi Mungu akamwambia: “Hakika nimeyaona mateso ya watu wangu walioko Misri, nami nimekisikia kilio chao kwa sababu ya wasimamizi wao.” Kut 3:7. Huo ukawa ni mwanzo wa historia ya ukombozi inayomshirikisha hata Musa, kwa kumtuma ili awe ni mjumbe atakayesaidia kuwaletea watoto wa Mungu waliokandamizwa katika kongwa la utumwa, hata leo hii, Mwenyezi Mungu anapenda kuwashirikisha watu katika ulimwengu mamboleo. Ndio maana Liturujia ya Neno la Mungu ni sehemu muhimu sana inayowafundisha waamini kujenga utamaduni wa kusikiliza na kulimwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha ya mtu binafsi na yale ya kijamii.

Kwaresima: Neno la Mungu liwe ni dira na mwongozo wa maisha
Kwaresima: Neno la Mungu liwe ni dira na mwongozo wa maisha   (@VATICAN MEDIA)

Neno la Mungu linawawezesha waamini na watu wote wenye mapenzi mema kutambua ndani mwao ile ladha ya chumvi ya mateso na ukosefu wa haki, ili hatimaye, kuyapatia majibu muafaka. Kilio cha maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii, ni mwaliko kwa waamini kujifunza kusikiliza kama Mwenyezi Mungu anavyofanya, ili waamini nao kwa upande wao, waweze kuwa wasikivu na hatimaye kutoa majibu muafaka kadiri ya maisha yao, jamii inayowazunguka, katika mifumo ya kisiasa na kiuchumi na hata ndani ya Kanisa lenyewe! Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, Kufunga kunawawezesha waamini kujiweka katika mazingira ya kulipokea Neno la Mungu na kwamba, kufunga na kujinyima chakula ni zoezi la maisha ya kiroho, ambalo limekuwepo tangu zamani za kale, ni tendo muhimu sana katika mchakato wa toba na wongofu wa ndani, kwa kumjengea mwamini njaa ya mambo msingi katika maisha na hivyo kuiratibu njaa hii, ili kuwasaidia kukesha kwa ajili ya kujizatiti katika kutekeleza njaa na kiu ya haki; mambo yanayomwilishwa katika sala na huduma kwa jirani mhitaji zaidi. Mtakatifu Augustino Askofu na Mwalimu wa Kanisa anasema, watu katika maisha yao ya hapa duniani wanalazimika kujizatiti katika mapambano ya njaa na kiu ya haki, lakini watalipwa huko juu mbinguni, kwani watalishwa na kushibishwa na Malaika wa Bwana. Kwa mfungo wa chakula, unampatia mwamini nidhamu ya kudhibiti hamu yake, inamtakasa na hivyo kumwezesha kuwa mtu huru zaidi, kwa kumshirikisha Mwenyezi Mungu katika safari ya maisha yake na hivyo kujielekeza katika kutenda mema.

Kwaresima ni Maandalizi ya Sherehe ya Fumbo la Pasaka
Kwaresima ni Maandalizi ya Sherehe ya Fumbo la Pasaka

Hata hivyo, anasema Baba Mtakatifu Leo XIV “Funga ya chakula” inapaswa kumwezesha mwamini kujikita katika kweli za Kiinjili, kukwepa au kukimbia vishawishi; kwa kuepuka majaribu ya kuifanya mioyo ya waamini kuwa na kiburi bali funga ya chakula iwawezeshe kuendelea kuishi katika imani na unyenyekevu kwa kuwa na ushirika na Kristo Yesu kwa njia ya Neno lake kwani wale wasioweza kujilisha wenyewe kwa Neno la Mungu hawafungi ipasavyo. Funga ni kama ishara inayoonekana ya majitoleo ya waamini kutoka katika undani wao ili kutubu na kuongoka kutoka katika dhambi na maovu na kwamba, kwa msaada wa neema kufunga lazima kujumuishe namna nyingine za kujikana kwa lengo la kuwasaidia waamini kuwa na maisha ya kiasi na utulivu wa ndani unaoyafanya maisha ya Kikristo kuwa imara na ya pekee zaidi. Baba Mtakatifu Leo XIV anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kufunga na kujiepusha na maneno ambayo yanaudhi na kuumiza jirani zao; ni maneno yanayoivunjilia heshima lugha inayotumika; waamini waepuke maneno makali na hukumu za haraka haraka, wajiepushe na kashfa sanjari na kuwateta na kuwasema vibaya wale ambao hawapo na hawawezi kujitetea. Baba Mtakatifu Leo XIV anawaalika waamini kujitahidi kupima maneno yao na kusitawisha wema na heshima katika familia zao, miongoni mwa marafiki zao, maeneo ya kazi, kwenye mitandao ya kijamii, katika mijadala ya kisiasa, kwenye vyombo vya mawasiliano ya jamii na katika jumuiya za Kikristo. Kwa njia hii, maneno ya chuki na uhasama yatatoa nafasi kwa maneno ya matumaini na amani.

Kufunga si kukimbia vishawishi
Kufunga si kukimbia vishawishi

Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, Safari ya Kwaresima pamoja na mambo mengine inatoa kipaumbele cha pekee kwa Jumuiya kusikiliza, kulitafakari, kulimwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha yao pamoja na kufunga. Kwa mfano, Kitabu cha Nabii Nehemia kinasimulia jinsi watu walivyokusanyika ili kusikiliza usomaji wa Sheria hadharani, wakijitayarisha kukiri imani na ibada yao kwa njia ya kufunga, ili kupyaisha agano na Mwenyezi Mungu (Rej. Neh 9:1-3). Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Leo XIV anawaalika wanafamilia, parokia, vyama na mashirika ya kitume, pamoja na jumuiya mbalimbali kufanya safari ya pamoja wakati huu wa Kwaresima: Kwa kusikiliza Neno la Mungu pamoja, Kilio cha Dunia Mama na Kilio cha Maskini, ili kuwa ni sehemu ya maisha ya waamini na kwamba, kufunga kunakuwa ni msingi wa toba ya kweli. Kwa njia hii toba na wongofu wa ndani unagusa dhamiri ya mtu inaboresha mahusiano na mazungumzo ya watu wa Mungu. Jambo hili linamaanisha waamini kujiruhusu wenyewe kupingwa na ukweli kwa kutambua kile kinachoongoza tamaa zao, ndani ya jumuiya na Kanisa katika ujumla wake kwa kujielekeza zaidi katika kutelekeza kiu ya mwanadamu ya haki, amani na upatanisho. Baba Mtakatifu Leo XIV anahitimisha ujumbe wake wa Kwaresima kwa mwaka 2026 unaonogeshwa na kauli mbiu: “Kusikiliza na kufunga: Kwaresima kama Kipindi cha Wongofu wa ndani” kwa kuwaalika waamini kumwomba Mwenyezi Mungu neema ya kumsikiliza zaidi Mwenyezi Mungu sanjari na kusikilizana wao kwa wao, hasa kwa kutoa kipaumbele cha pekee kuwasikiliza wale walio wadogo zaidi miongoni mwao. Waombe neema ya nguvu itokanayo na aina ya funga ambayo itaboresha matumizi ya lugha, ili maneno ya kuumiza yapungue na kutoa nafasi kubwa kwa sauti ya wengine iweze kusikilizwa. Waamini wajitahidi kuzifanya Jumuiya zao kuwa ni mahali ambapo kilio cha wale wanaoteseka kinakaribishwa na kusikilizwa; Funga iwe ni njia ya kuelekea ukombozi na hivyo kuwafanya kuwa tayari na shauku ya kuchangia katika ujenzi wa ustaarabu wa upendo.

Papa Leo XIV Kwaresima 2026
12 Machi 2026, 14:57