Tafakari za Kipindi Cha Kwaresima 2026: Toba na Wongofu wa Ndani
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Kipindi cha Kwaresima kwa mwaka huu 2026 kinanogeshwa na ujumbe wa Baba Mtakatifu Leo XIV kwa kauli mbiu: “Kusikiliza na kufunga: Kwaresima kama Kipindi cha Wongofu wa ndani.” Kwaresima ni kipindi ambacho Kanisa kama Mama na Mwalimu, anawaalika watoto wake kutoa kipaumbele cha pekee kwa Fumbo la Mungu katikati ya maisha yao, ili imani ipate tena nguvu na mioyo ya waamini isipotee katikati ya mahangaiko na bughudha za maisha ya kila siku. Kila safari ya wongofu wa ndani huanza pale waamini wanaporuhusu Neno la Mungu liwafikie na kulikaribisha kwa moyo wa unyenyekevu. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, kuna uhusiano kati ya karama ya Neno la Mungu, Nafasi ya Ukarimu na mabadiliko ambayo Neno hili linaleta. Kwa sababu hiyo, safari ya Kwaresima inakuwa ni fursa muafaka ya kusikiliza sauti ya Mungu na hivyo kupyaisha tena maamuzi ya kumfuasa Kristo Yesu, kwa kutembea katika njia ile iendayo Yerusalemu ambako Fumbo la Pasaka yaani: Mateso, kifo na ufufuko vinapata utimilifu wake. Kipindi cha Kwaresima kimsingi kinasimikwa katika nguzo kuu nne: Sala na Kufunga; Tafakari ya Neno la Mungu inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Ni katika muktadha huu, Padre Roberto Pasolini, O.F.M.Cap., Mhubiri wa Nyumba ya Kipapa anasema, tema inayoongoza tafakari za Kipindi cha Kwaresima kwa Mwaka 2026 ni “Ikiwa mtu yuko ndani ya Kristo, amekuwa kiumbe kipya” 2Kor 5:17: Wongofu wa Kiinjili Mintarafu Mtakatifu Francisko wa Assisi.” Hii ni tafakari inayozama katika: Kumbukizi ya miaka 800 tangu Mtakatifu Francisko wa Assisi alipofariki dunia, kielelezo makini cha hija ya toba na maisha yanayosimikwa katika tunu msingi za Kiinjili. Katika Kanisa Katoliki maadhimisho ya Jubilei ni mwaka wa toba na maondoleo ya dhambi; upatanisho, na wongofu wa ndani unaojikita katika Sakramenti ya Kitubio.
Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo yalinogeshwa na kauli mbiu: “Peregrinantes in spem” yaani: “Mahujaji wa Matumaini.” Huu ukawa ni muda muafaka wa kusoma na kutafakari Neno la Mungu; Kusali na kumwilisha sala hii katika matendo ya huruma kiroho na kimwili, ili kuwaonjesha matumaini wale waliopondeka na kuvunjika moyo! Tafakari hizi zitajikita katika: Uhuru wa ndani, utume na udugu wa kibinadamu mintarafu changamoto mamboleo za kujenga na kudumisha haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mataifa, changamoto na mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kujenga Ufalme wa Mungu unaosimikwa katika kweli na uzima; ni ufalme wa utakatifu na neema; ni ufalme wa haki, mapendo na amani. Ni katika nguvu ya unyenyekevu wa upendo matunda ya haki na amani yanaweza kuchanua na kustawi. Neno la Mungu linapania kuleta toba na wongofu wa ndani, ili kujenga utamaduni wa upendo, haki, amani na udugu wa kibinadamu. Huu ni mwaliko wa kufanya toba na wongofu wa ndani. Ujumbe wa Baba Mtakatifu Leo XIV wa Siku ya 59 ya Kuombea Amani Duniani tarehe Mosi, Januari 2026 umenogeshwa na kauli mbiu: "Amani iwe nanyi nyote: Kuelekea amani "Isiyo na Silaha na inayopokonya Silaha."
Padre Roberto Pasolini, O.F.M.Cap., Mhubiri wa Nyumba ya Kipapa anasema, haitoshi kufunga maneno makali yanayoumiza, bali pia huu ni mwaliko wa kujenga nia njema, utamaduni wa kusikilizana na uchaguzi wa maneno na kuendelea kujikita katika ujenzi wa utamaduni wa majadiliano, katika ukweli na uwazi, kwa kuthaminiana. Katika Ulimwengu mamboleo unaoendelea kutopea katika hali ya kukengeuka; kuporomoka kwa kanuni maadili na utu wema sanjari na ukanimungu; tajiriba ya toba na wongofu wa ndani mintarafu maisha ya Mtakatifu Francisko wa Assisi inawaelekeza waamini kutafuta na kuambata mambo msingi katika maisha; kwa kujikita katika Injili inayopaswa: Kusoma, Kutafakariwa na hatimaye, Kumwilishwa katika uhalisia wa maisha ya waamini. Mtakatifu Francisko wa Assisi ni mtu anayezungumza na walimwengu ili kujenga na kudumisha: amani na utulivu wa ndani; udugu wa kibinadamu na maisha ambayo yanajipatanisha na Mungu, ili watu waweze kutambuana kuwa ni ndugu wamoja licha ya tofauti zao msingi.
Padre Roberto Pasolini, O.F.M.Cap., katika tafakari yake ya kwanza ya Kipindi cha Kwaresima, Ijumaa tarehe 6 Machi 2026 imenogeshwa na kauli mbiu: Wongofu wa Kiinjili Mintarafu Mtakatifu Francisko wa Assisi. Huu ni mwaliko wa kuendelea kutunza amana na utajiri ulioibuliwa katika Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo, kielelezo cha toba na wongofu wa ndani. Tafakari hii imehudhuriwa na Baba Mtakatifu Leo XIV, Makardinali, Maaskofu, Wakuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume sanjari na wafanyakazi wa Sekretarieti kuu ya Vatican pamoja na watu wenye mapenzi mema, waliotaka kushiriki mafungo haya. Katika tafakari hii, Padre Roberto Pasolini, O.F.M.Cap., amejikita zaidi katika: Wongofu wa ndani kama njia ya kumfuasa Kristo Yesu katika unyenyekevu. Wongofu wa ndani unaoleta mabadiliko akilini na nyoyoni na hivyo kuwa na mtazamo na mang’amuzi tofauti ya maisha, kwa kuondokana na dhambi pamoja na nafasi zake, tayari kuambata huruma na upendo wa Mungu kama alivyofanya Mtakatifu Francisko wa Assisi. Huu ni mwaliko kwa waamini kuwa na huruma kwa jirani zao na hasa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii na kwamba, wongofu wa ndani ni nyenzo inayomwezesha mwamini kupima, kuamua na kutamani mintarafu kanuni maadili na utu wema unaokita mizizi yake katika maisha mapya ndani ya Kristo Yesu. Wongofu wa ndani umwezeshe mwamini kuona aibu mbele ya Mungu kutokana na dhambi alizotenda, kama ilivyokuwa kwa Adami na Hawa. Rej. Mwa 3:9-10. Aibu ni matunda ya dhambi. Leo hii dhana ya “Dhambi” inaendelea kutoweka taratibu na hivyo kuathiri ukuu wa uhuru wa binadamu na uwajibikaji wake kimaadili. Kumbe, toba na wongofu wa ndani ni hija ya maisha ya kiroho inayotambua ukuu wa Mungu kwamba ni Muumbaji na Mkombozi, jambo la msingi ni kukuza na kudumisha mahusiano na mafungamano mema, matakatifu na adili kwa uhuru kamili na furaha ya ndani.
Mtakatifu Francisko wa Assisi alipokutana na wakoma, akaanza hija ya toba na wongofu wa ndani, akafanywa upya katika roho na nia zake na kuanza kuuvaa utu mpya: “ulioumbwa kwa namna ya Mungu katika haki na utakatifu wa kweli.” Efe 4:24. Tangu hapo Mtakatifu Francisko wa Assisi akakita maisha yake katika fadhila ya unyenyekevu “Humilitas” na ufukara wa Kristo Yesu aliyejifunua katika Fumbo la Umwilisho linalopata utimilifu wake katika Fumbo la Pasaka, yaani mateso, kifo na ufufuko uletao maisha na uzima wa milele. Akajitambua kwamba, ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, changamoto na mwaliko kwa waamini kuishi fadhila hii ya unyenyekevu kama Kristo Yesu anavyowataka: “Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu” Mt 11:29. Kwa hakika, huu ni ukweli wa mwanga wa Kiinjili unaokumbatia imani ya Kikristo na hivyo kumwinua mwanadamu katika ukuu wake. Kumbe toba na wongofu wa ndani ni safari ya kurejea katika ukuu wa mwanadamu uliopotea kutokana na dhambi ya asili, iliyomfanya mtu kukataa fadhila ya unyenyekevu na kutaka kujikweza na kuwa kama Mungu. Unyenyenyekevu ni mwaliko kwa waamini kuwa wadogo kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Francisko wa Assisi alipoinama na kuwahudumia wagonjwa wa Ukoma, kwa huruma na upendo mkuu, ndiyo maana Mtakatifu Francisko na wanashirika wake wakajiita “Ndugu wadogo” tayari kumwilisha Injili katika uhalisia wa maisha na vipaumbele vyao, wakarimu na watu wazi kwa jirani zao na kwamba, Ufukara wa Kiinjili ukawa ni utambulisho wao; katika udogo wao, wakabahatika kuwa ni watu wakubwa, alama muhimu sana kama Wafuasi wa Kristo Yesu, wakajisikia kupendwa na kuthaminiwa na Mungu, katika utu wao mpya, ambao waamini wanakirimiwa tena upya kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo.
Padre Roberto Pasolini, O.F.M.Cap., Mhubiri wa Nyumba ya Kipapa, anakaza kusema, toba na wongofu wa ndani ni mchakato endelevu katika maisha ya mwamini na hatima yake ni utakatifu wa maisha, kazi inayofanywa na Roho Mtakatifu: “Naye akaniambia, Neema yangu yakutosha; maana uweza wangu hutimilika katika udhaifu. Basi nitajisifia udhaifu wangu kwa furaha nyingi, ili uweza wa Kristo ukae juu yangu. Kwa hiyo napendezwa na udhaifu, na ufidhuli, na misiba, na adha, na shida, kwa ajili ya Kristo. Maana niwapo dhaifu ndipo nilipo na nguvu.” 2 Kor 12:9-10. Huu ni mwaliko kwa waamini anasema Baba Mtakatifu Leo XIV kujifunza vyema Injili ya Msalaba inaofumbatwa katika ushirika na Kanisa kwani ni katika muktadha huu, Utakatifu wa Kanisa unajionesha, Kristo Yesu anaendelea kujisadaka bila ya kujibakiza kwa njia ya udogo na udhaifu wa waja wake na kwamba, huu ndio “Mtindo wa Mungu” anayeendelea kujifunua na kutenda kwa njia ya udhaifu wa viumbe vyake. Kwa hakika amani ya kweli inaundwa na watu wanyenyekevu, wanaofanya shughuli zao kwa ujasiri, huku wakijizua kutumia mifumo mbalimbali ya nguvu, tabia ya kutaka kulipiza kisasi na badala yake, wanaamua kufuata majadiliano katika ukweli na uwazi; mambo yanayopaswa kumwilishwa kila siku katika maisha na vipaumbele vya watu. Huu ni mwaliko kwa waamini kutenda mema kwa niaba ya Mwenyezi Mungu, na kadiri inavyo mpendeza, huku wakiwa wamesafishwa na kuangazwa kutoka katika undani wa maisha yao na moto wa Roho Mtakatifu tayari kufuaata nyayo za Kristo Yesu, kwa msaada wa neema ili waweze kufikia katika umoja na Fumbo la Utatu Mtakatifu, anayeishi na kutawala katika utukufu, daima na milele. Amina.
