Tafuta

Katika Siku hii ya Kimataifa ya Wanawake Duniani kwa Mwaka 2026 inaongozwa na kaulimbiu Haki, Usawa na Kuchukua Hutua kwa Wanawake na Wasichana Wote Katika Siku hii ya Kimataifa ya Wanawake Duniani kwa Mwaka 2026 inaongozwa na kaulimbiu Haki, Usawa na Kuchukua Hutua kwa Wanawake na Wasichana Wote  

Siku ya Wanawake Duniani 2026: Haki, Usawa Na Kuchukua Hatua Kwa Wanawake Na Wasichana

Siku ya Kimataifa ya Wanawake Duniani, inaongozwa na kaulimbiu Haki, Usawa na Kuchukua Hutua kwa Wanawake na Wasichana inatukumbusha kwamba, usawa wa kijinsia si ndoto bali ni wajibu wa pamoja wa jamii nzima Wanawake na wasichana wengi wanakabiliwa na vikwazo vya kimfumo vinavyowazuia kufikia fursa na haki zao kikamilifu. Changamoto hizi ni pamoja na ukatili wa kijinsia, kutengwa katika mifumo ya kiuchumi, na ukosefu wa fursa sawa katika huduma

Na Mama Evaline Malisa Ntenga, - Dar Es Salaam, Tanzania.

Utangulizi: Katika Siku hii ya Kimataifa ya Wanawake Duniani, inaongozwa na kaulimbiu Haki, Usawa na Kuchukua Hutua kwa Wanawake na Wasichana Wote “Rights, Justice, Action for all Women and Girls" inatukumbusha kwamba, usawa wa kijinsia si ndoto au matarajio tu, bali ni wajibu wa pamoja wa jamii nzima. Wanawake na wasichana wengi bado wanakabiliwa na vikwazo vya kimfumo vinavyowazuia kufikia fursa na haki zao kikamilifu. Changamoto hizi ni pamoja na ukatili wa kijinsia, kutengwa katika mifumo ya kiuchumi, na ukosefu wa fursa sawa katika elimu, huduma za afya, na nafasi za uongozi, licha ya kuwepo kwa ahadi nyingi za Kimataifa zinazolenga kulinda na kukuza haki msingi za binadamu. Kulinda haki kunamaanisha kuhakikisha kwamba kila mwanamke na kila msichana, bila kujali asili yake, hali yake ya kijamii au uwezo wake, anaweza kuishi maisha yenye heshima, uhuru, na usalama. Tunapozungumzia usawa katika sura ya Kimungu hatumaanishi kuwa na mafahali wawili katika familia bali kulinda utu wa kila mmoja na kutambua kuwa sote tumeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu ili kukamilishana. Usaidizi sio unyonge. Leo, utamaduni wetu unaathiriwa zaidi na maendeleo ya kidijitali kuliko mahusiano ya kweli ya kibinadamu. Ingawa teknolojia inatuunganisha kwa urahisi, mara nyingi hututenganisha na ukaribu wa moyo kwa moyo unaojenga huruma, mshikamano na amani ya kweli. Kama wanawake Wakatolili, tunaitwa kujenga tena utamaduni wa kukutana, kusikilizana na kuishi kama ndugu. Katika kuadhimisha siku hii ya Wanawake Duniani, tuwafikie wenzetu wanaopitia changamoto za nyanyaso pamoja na kutelekezwa na familia. Mafundisho ya kijamii ya Kanisa yanatukumbusha kuwa haki ya kweli inahitaji kubadilisha mifumo inayozalisha ukosefu wa usawa, huku tukilenga mema ya wote. Kulinda haki za wanawake na wasichana kunamaanisha kuhakikisha kila mmoja anaishi kwa heshima, kulinda utu wa kila mmoja, usalama na uhuru. Kukuza haki ya kijamii kunahitaji pia kukabiliana moja kwa moja na mifumo na miundo ya kijamii inayozalisha au kudumisha ukosefu wa usawa, pamoja na kuhakikisha kwamba taasisi, mifumo ya uongozi na mamlaka zinawajibika ipasavyo pale kunapotokea ubaguzi au unyanyasaji.

Wanawake na Wanaume wanakamilishana kama kazi ya uumbaji
Wanawake na Wanaume wanakamilishana kama kazi ya uumbaji

Zaidi, ya yote, hatua inatualika sisi sote—serikali, jamii, taasisi za dini na watu binafsi kuacha kubaki katika ahadi na maneno matupu, na badala yake kuwekeza katika suluhisho halisi, jumuishi na endelevu litakalowawezesha wanawake na wasichana kustawi, kujiamini, na kushika nafasi zao katika jamii. Kwa hiyo, wakati huu wa historia ni nafasi muhimu kwa wanawake kuonesha njia ya amani inayotokana na moyo wa kike—njia inayojengwa juu ya kujali, mazungumzo, uwajibikaji na kutetea na kulinda uhai. Tunahitaji mtazamo mpya wa maisha na maendeleo, ambao hautaangalia tu ustawi wa binadamu bali pia utalinda uumbaji wote—wanadamu, mimea, wanyama na mazingira yetu, kama Papa Francisko anavyotukumbusha katika Waraka wake wa Kitume: “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote” kwa kusema kwamba, Wanawake, ambao mara nyingi ni walinzi wa kwanza wa uhai, waalimu wa familia na jamii, wana nafasi muhimu katika kujenga dunia yenye haki, usawa, amani na tumaini. Utakubaliana nami kuwa, wanaohusika kuwanyima wengine haki wamepitia mikononi mwetu- tunabeba mimba miezi 9, kunyonyesha miaka 3 (katika kipindi hiki mtoto anakuwa karibu zaidi na mama) na baadae baba na mama kama walimu wa Imani kwa miaka 9 ya kwanza ya mtoto (natambua siku hizi jukumu hili limeachwa kwa wasichana wa kazi, TV, Mitandao ya kijamii na waalimu wa shule – tutafakari). Kwa hiyo, kama wanawake wa imani, tumeitwa si kuzungumzia haki na usawa tu, bali pia kuchukua hatua za makusudi kwa ujasiri, huruma na imani, ili tuwe mashahidi hai wa tumaini katika familia zetu, jamii zetu na ulimwengu mzima. Tutafakari pia mahusiano baina yetu wanawake kwa wanawake yaanaakisi sura ya Mungu!!

WAWATA katika Ubora wao
WAWATA katika Ubora wao

Mkutano wa Kiekumene na Kidini ulioandaliwa na WUCWO kuelekea siku ya Wanawake Duniani 05/03/2026.Kauli mbiu: "Wanawake wa Imani: Wabeba Amani na Matumaini," "Women of Faith: Bearers of Peace and Hope.” Mkutano huu uliohudhuriwa na zaidi ya watu 250 na viongozi sita wa wanawake wanaowakilisha dini kuu duniani - Wabudha, Waislamu, Wahindu, Wayahudi na Wakatoliki.  Pamoja na kwamba kauli mbiu ya siku ya Wanawake mwaka huu imejikita zaidi katika kutetea haki, usawa wa wanawake na washichana, dunia ilipo sasa inahitaji zaidi amani na matumani kabla hata ya kutazama haki na usawa. Wazungumzaji walishiriki tafakari kuhusu nafasi ya wanawake katika kukuza amani, majadiliano, na ushirikiano wa kidini katika miktadha iliyoangaziwa na changamoto za kijamii. Kardinali George Jacob Koovakad, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini alisisitiza kwamba: Kupokonya silaha huanza katika moyo wa mwanadamu. Wanawake wa imani wanaelewa hili kwa uwangavu kwani: amani haitegemezwi na mikataba pekee, bali kwa kazi ya kila siku ya kumbukumbu za uponyaji, kurejesha utu, heshima na haki msingi za binadamu sanjari, na kupinga mantiki ya hofu. Katika ulimwengu ambao mara nyingi tunajikuta katika njia panda kati ya migogoro na upatanisho, tunaalikwa, kuchagua amani kwani hii ni njia ya amani, na kukutana na ukwel, bidii, ujasiri, na wakati mwingine kujitolea kwa gharama kubwa, ambayo inahitaji kujikita katika, mshikamano, na ulinzi wa utu, heshima na haki msingi za binadamu. Naye Monica Santamarina, Rais wa Umoja wa Wanawake Wakatoliki Duniani (WUCWO- WORLD UNION OF CATHOLIC WOMEN’S ORGANISATION) anasema, kama wanawake wa imani na viongozi wa kimataifa, "amani si neno au matakwa yasiyoeleweka. Ni utume madhubuti, tendo la upendo ambalo tunapaswa kutekeleza kila siku na katika kila mazingira. Tumealikwa kujenga madaraja ya kuwakutanisha watu, kuelimisha kwa amani, kukuza majadiliano ya kidini na ya kiekumene, kujali kazi ya uumbaji, kulinda Injili ya maisha ya watu walio hatarini zaidi, kukuza na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu. Yote haya yanahitaji: Ustahimilivu na ujasiri, hii ni njia madhubuti ya kujenga amani isiyo na silaha na kupokonya silaha ambayo Papa Leo XIV anakazia.

Upendo katika maisha ya ndoa na familia, lakini zaidi kusikilizana
Upendo katika maisha ya ndoa na familia, lakini zaidi kusikilizana   (@Vatican Media)

Tafakari ya Mababa wa Kanisa: Ningependa kurejea maneno ya Askofu Mkuu Yuda Thadei Ruwa'ichi, O.F.M. Cap. wa Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam aliewahi kukumbusha waamini kwamba: Familia yenye amani hujengwa pale mwanamke na mwanaume wanapotambua kwamba wao si wapinzani bali ni washirika katika mpango wa Mungu. Alisisitiza pia kwamba changamoto nyingi katika jamii yetu leo—migogoro ya familia, malezi dhaifu, na kuvunjika kwa mahusiano hutokea pale ambapo ushirikiano wa mwanamke na mwanaume unapodhoofika. Ndiyo maana Kanisa linaendelea kuhimiza familia kurudi kwenye Kanuni maadili, Utu wema, upendo, heshima na uwajibikaji. Naye Baba Mtakatifu Leo XIV, akitoa ujumbe wake kwa maadhimisho ya Jubilei ya Familia Duniani mwezi Juni 2025 alikumbusha Kanisa na dunia kwamba: “Familia ni shule ya kwanza ya upendo. Ndani yake mwanamke na mwanaume wanajifunza kwamba upendo si mamlaka wala mashindano, bali ni kujitoa kwa ajili ya mwingine.” Maneno haya yanatukumbusha jambo la msingi sana: kwamba maisha ya mwanadamu yanaanzia katika ushirika wa upendo kati ya mwanamke na mwanaume. Familia si taasisi ya kijamii tu; ni mpango wa Mungu katika kazi ya uumbaji. Ndani ya familia ndipo mtoto hujifunza maana ya heshima, uaminifu, uvumilivu na kujali wengine. Na msingi wa familia hiyo ni ushirika wa mwanamke na mwanaume ambao wanakamilishana katika wito wao wa maisha. Huu ndio msingi muhimu katika kuleta usawa na haki kwa wote.

Familia ni kitovu cha uinjilishaji na utamadunisho
Familia ni kitovu cha uinjilishaji na utamadunisho   (@Vatican Media)

Mafundisho ya Papa Francisko katika Wosia wake wa Kitume: “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya Upendo ndani ya familia” alisema kwamba: “Upendo wa kweli katika familia hujengwa juu ya kuheshimiana, kuvumiliana na kujitoa kwa ajili ya mwingine.”  Papa Francisko pia alionya kwamba jamii ya leo wakati mwingine husahau uzuri wa tofauti kati ya mwanamke na mwanaume. Alisisitiza kwamba tofauti hizi si chanzo cha mgawanyiko bali ni zawadi ya Mungu kwa ajili ya ukamilishanaji. Katika tafakari zake alisema pia: “Mwanamke na mwanaume wanaposhirikiana kwa heshima na upendo, hapo ndipo uzuri wa mpango wa Mungu katika uumbaji unaonekana wazi.” Kwa hiyo Kanisa halioni tofauti kati ya mwanamke na mwanaume kama tatizo. Kanisa linaiona kama neema na baraka ya Mungu kwa dunia. Msingi wa Biblia kuhusu Uumbaji na Ushirika: Tukirudi katika Neno la Mungu, tunaona wazi kabisa kusudi la Mungu katika uumbaji. Kitabu cha Mwanzo kinatuambia: “Mungu akamwumba mtu kwa mfano wake; kwa mfano wa Mungu alimwumba; mwanamume na mwanamke aliwaumba.” (Mwanzo 1:27) Hii inatufundisha kwamba mwanamke na mwanaume wana hadhi sawa mbele za Mungu, kwa sababu wote wameumbwa kwa mfano wake. Lakini Mungu pia alikusudia ushirika: “Si vema mtu huyu awe peke yake.” (Mwanzo 2:18) Kwa hiyo tangu mwanzo kabisa, mpango wa Mungu haukuwa upweke wala mashindano, bali ushirika wa maisha.

Malezi na makuzi ya watoto ni jukumu la wazazi wote wawili
Malezi na makuzi ya watoto ni jukumu la wazazi wote wawili

Nae Mtume Paulo katika Waraka wake kwa Waefeso anatoa mwongozo muhimu sana kuhusu maisha ya familia. Anasema: “Enyi wake, watiini waume zenu kama kumtii Bwana.” (Waefeso 5:22) Lakini mara nyingi watu husahau kwamba Paulo pia aliwaasa wanaume kwa maneno yenye uzito mkubwa zaidi: “Enyi waume, wapendeni wake zenu kama Kristo alivyolipenda Kanisa akajitoa kwa ajili yake.” (Waefeso 5:25) Upendo ambao Mtume Paulo anaelezea hapa si upendo wa maneno tu. Ni upendo wa kujitoa, wa kulinda, na wa kuwajibika kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya familia. Kwa hiyo Biblia haifundishi ubabe wa mwanaume wala udhaifu wa mwanamke. Inafundisha ushirika wa upendo na heshima. Kuna methali inayosema: “Mkono mmoja hauinui mtoto.” Methali hii yenye tafsiri nyingi ina maana kubwa sana. Inatufundisha kwamba kulea maisha kunahitaji ushirikiano wa mwanamke na mwanaume, familia na jamii. Hakuna anayeweza kujenga familia yenye maadili peke yake. Tujiulize kwa nini Yesu ambae ni Mwana wa Mungu, na Mungu alihitaji malezi ya baba na mama? Uumbaji wa Mungu, Hadhi ya Mwanamke, na Ukamilishanaji wa Mwanamke na Mwanaume. Yapo masuala kadhaa ambayo tunayakosea katika maisha ya ndoa na familia. Naomba niseme na wewe mwanamke, mke mwenye ndoa – Mwanamke (mwanandoa). Ndoa ni faragha (mume na mke). Kwenye ndoa tunawahusisha ndugu wa kiumeni na kikeni, majirani, marafiki na wafanyakazi. Tena tunawaeleza hata ya chumbani na kitandani. Tunapoadhimisha Siku ya Wanawake Duniani kwa Mwaka 2026, sema "NOOO" kwa dhambi hii. Wanawake, hapa niseme midomo yetu inatuponza. Mwambie Jirani yako KAMDOMO!

Siku ya Wanawake Duniani Kwa Mwaka 2026
Siku ya Wanawake Duniani Kwa Mwaka 2026

Naomba niseme na wanandoa pamoja na wanandoa watarajiwa wote KE/ME. Ugomvi wa wanandoa kuvuka kwenda kwa watoto. Kuhitilafiana ni jambo la kawaida sana ila sio jambo la kushirikisha watoto, hasa pale ugomvi unapochukua hatua ya kutengana. Tunakosa baraka za Mungu kwa sababu ni sisi tulitamani kupata watoto na sio watoto kutupata sisi. Kutegeana katika kuitegemeza na kuendesha familia: Suala la kuiendesha familia ni la wawili (baba na mama). Hakuna sababu ya mmoja kuelezea nje kwamba yeye ndio anahangaika wakati mwenzi wake hachangii chochote. Ikiwa ni ndoa, Mungu anaweza kupitisha baraka kwa mmoja wenu kwa kusudi lake! Na hata kama ni tofauti wewe unaeamini unafanya zaidi ya mwenzako – Sema na mwenza wako, usiwaharibu Watoto. Kwani wao kimsingi wanapenda kuwaona mnatabasamu hayo mengine hayawahusu. Kutokuwa na ibada: hapa simaanishi tu kule unakoabudu (kanisani, msikitini, hekaluni au kwenye sinagogi). Kuna ibada za wanandoa – yes hizo hizo hizo! Lakini muhimu pia sana ni ibada za familia za asili; kumbariki mzaliwa wa kwanza maana ni lango ila zaidi kuwabariki watoto kila asubuhi kwa kuzingatia majina yao (maana nusu ya tabia ya mtu inatokana na jina). Shika ardhi kila asubuhi, nena yawafaayo wanao, rejea (Mwanzo 49:1-27.)

Mama  Evaline Malisa Ntenga walipokutana na Papa Francisko
Mama Evaline Malisa Ntenga walipokutana na Papa Francisko   (Vatican Media)

Hitimisho: Katika Siku hii ya Wanawake Duniani kwa Mwaka 2026, tukumbukie kwamba: Mwanamke ameumbwa kwa hadhi na heshima sawa na mwanaume. Mwanaume amepewa wito wa kupenda na kulinda familia kwa kujitoa bila ya kujibakiza. Na wote kwa pamoja wameitwa kujenga jamii yenye haki, amani, upendo matumaini na mshikamano, mwanamke akiwa msaidizi. Mwanamke na mwanaume hawakuumbwa kuwa wapinzani. Waliumbwa kuwa washirika katika mpango wa Mungu wa uumbaji. Na pale ushirika huo unapodumishwa kwa heshima, upendo na imani, hapo ndipo familia inakuwa shule ya upendo, jamii inakuwa mahali pa matumaini, na dunia inaona uzuri wa mpango wa Mungu. Katika kipindi hiki ambacho dunia inapitia changamoto nyingi ya vita kila mahali, mmonyoko wa maadili niwaalike wote tuwekeze katika malezi ya familia kama namna pekee ya kujuenga familia na jamii inayojali utu, haki na usawa wa kila mmoja. Kadiri ile ile tunayowekeza kwenye mambo muhimu ya kiuchumi na kijamii, tuwe pia na mpango Madhubuti wa malezi ya familia ili Watoto wetu wakue wakitambua sote tumeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu na tofauti kati ya mwanamke na mwanaume sio udhaifu bali nguvu yenyewe kutuwezesha kuufikia utakatifu.

Mama Evaline Malisa Ntenga – Mwenyekiti wa WAWATA Taifa na Rais wa Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki Duniani, Kanda ya Afrika.

07 Machi 2026, 18:01