Tafuta

Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, kuwasikiliza waathirika wa vitendo vya nyanyaso za kijinsia ni kitendo cha haki na ukweli. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, kuwasikiliza waathirika wa vitendo vya nyanyaso za kijinsia ni kitendo cha haki na ukweli.  

Papa Leo XIV: Ulinzi wa Watoto Amerika ya Kusini: Kusikiliza Ni Tendo La Haki Na Ukweli

Papa Leo XIV: Kuwasikiliza waathirika wa vitendo vya nyanyaso za kijinsia ni kitendo cha haki na ukweli. Hii ni sehemu ya ujumbe kwa Kongamano la Tano la Kituo cha Utafiti na Mafunzo kati ya Taaluma mbalimbali kwa ajili ya Ulinzi wa Watoto Amerika ya Kusini (CEPROME), Lililonogeshwa na kauli mbiu: “Ulipaji fidia kati ya imani inayowatunza, huduma inayowasindikiza na haki inayotendeka. Kuna haja ya kujikita katika ukweli na uwajibikaji wa shughuli za kichungaji!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo ni kielelezo madhubuti cha kumong’onyoka kwa kanuni maadili na utu wema, ni matumizi haramu ya madaraka na kwamba, hii ni kashfa kubwa dhidi ya utu na heshima ya binadamu; maisha na utume wa Kanisa. Kashfa hizi ni tendo la aibu sana katika maisha na utume wa Kanisa. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, kuwasikiliza waathirika wa vitendo vya nyanyaso za kijinsia ni kitendo cha haki na ukweli. Hii ni sehemu ya ujumbe wa Baba Mtakatifu Leo XIV kwa wajumbe wa Kongamano la Tano la Kituo cha Utafiti na Mafunzo kati ya Taaluma mbalimbali kwa ajili ya Ulinzi wa Watoto Amerika ya Kusini (CEPROME), lililofunguliwa tarehe 3 na kuhitimishwa tarehe 5 Machi 2026 huko San Josè de Costa Rica, nchini Costa Rica, kwa kunogeshwa na kauli mbiu: “Ulipaji fidia kati ya imani inayowatunza, huduma inayowasindikiza na haki inayotendeka. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema ulipaji fidia unahitaji toba na wongofu wa kweli, uwajibikaji wa kichungaji na usikivu wa dhati kwa wale ambao wamekumbwa na nyanyaso na ukatili huu. Ujumbe wa Baba Mtakatifu umesomwa na Askofu mkuu Mark Gerard Miles, Balozi wa Vatican nchini Costa Rica na kwamba, Baba Mtakatifu anawatia shime wajumbe kuendelea na safari hii ya uwajibikaji kichungaji, inayogusa moja ya madonda yenye uchungu mkubwa katika maisha na utume wa Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa. Hii ni safari ya upyaishaji wa maisha na utume wa Kanisa kwa ajili ya waathirika na kwa ajili ya Kanisa. Huu ni mwelekeo mpana wa utume wa Kanisa katika muktadha wa uinjilishaji wa kina unaomgusa mtu mzima: kiroho na kimwili.

Ulinzi wa watoto dhidi ya nyanyaso za kijinsia Amerika ya Kusini
Ulinzi wa watoto dhidi ya nyanyaso za kijinsia Amerika ya Kusini

Huu ni uwajibikaji unaopaswa kutekelezwa na wahusika, kwa kuambata na kukumbatia utamaduni wa huduma itakayowezesha kashfa ya namna hii isijitokeze tena katika maisha na utume wa Kanisa na kama ushuhuda wa huruma na upendo wa Kristo Yesu kwa waja wake, unaowezesha kugeuza madonda haya kuwa ni chemchemi ya matumaini mapya. Baba Mtakatifu Leo XIV anakaza kusema, tajiriba na mang’amuzi ya miaka ya hivi karibuni yanaonesha kwamba, Maaskofu mahalia pamoja na Wakuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume, wakitekeleza dhamana na wajibu wao barabara, Kanisa linaendelea kuwa ni mahali pa matumaini, kwa kuonesha ile sura ya kibinadamu na hivyo kuweza kujikita zaidi katika mchakato wa uinjilishaji. Baba Mtakatifu XIV katika ujumbe wake, anakazia zaidi utamaduni wa kuwasikiliza waathirika kama kielelezo cha haki, ukweli na uwajibikaji wa kichungaji. Ndani ya Kanisa ulipaji wa fidia unakwenda sanjari na huruma na upendo wa Mungu; Utekelezaji wa sheria, kanuni maadili na utu wema; jambo linalohitaji umakini mkubwa na mtazamo mpana wa Kanisa.

Uwajibikaji wa kichungaji ni muhimu sana katika ulinzi wa watoto.
Uwajibikaji wa kichungaji ni muhimu sana katika ulinzi wa watoto.

Mchakato wa kuwasindikiza waathirika wa ukatili na nyanyaso za kijinsia unahitaji maamuzi yenye ujasiri kutoka kwa Askofu mahalia na kwamba, uamuzi wowote unaofanywa katika ukweli ni hatua muhimu inayoweza kuamsha matumaini kwa ajili ya Kanisa na Ulimwengu katika ujumla wake. Katika muktadha huu, Kituo cha Utafiti na Mafunzo kati ya Taaluma mbalimbali kwa ajili ya Ulinzi wa Watoto Amerika ya Kusini (CEPROME), kinaweza kuwa ni kituo muhimu cha utafiti, mahali muafaka pa kukutania ndani ya Kanisa Amerika ya Kusini na hivyo kuendelea kukomaa na hivyo kuna umuhimu kwa Kituo hiki kushirikiana na kufungamana na Baraza kuu la Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Amerika ya Kusini na Caribbean CELAM pamoja na Shirikisho la Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume Amerika ya Kusini CLAR. Hapa inawezekana kuunganisha uwajibikaji wa kichungaji wa Maaskofu, amana, utajiri wa Karama za Mashirika pamoja na tajiriba ya mwingiliano wa taaluma.

Kuwasikiliza waathirika wa nyanyaso ni kitendo cha haki na ukweli
Kuwasikiliza waathirika wa nyanyaso ni kitendo cha haki na ukweli

Kongamano la Tano la Kituo cha Utafiti na Mafunzo kati ya Taaluma mbalimbali kwa ajili ya Ulinzi wa Watoto Amerika ya Kusini (CEPROME), linapania pamoja na mambo mengine kuwa ni mahali ambapo: tafakari, malezi, majiundo makini na majadiliano katika ukweli na uwazi yanafanyika kama shemu ya utekelezaji wa haki na kulipa fidia kwa kujikita katika taalimungu ya kulipa fidia; Dhamana ya Kanisa kuwasindikiza walezi, faraja ya kichungaji; dhamana na wajibu wa wanataalimungu pamoja na Maakimu; Waathirika, Wataalam wa Sheria za Kanisa na Kiraia pamoja na kuangalia mchango wa jumuiya pamoja na mtandao wa kusaidiana pamoja na kuwahusisha Maaskofu mahalia.

Ulinzi wa Watoto
05 Machi 2026, 14:28