Tafuta

Papa leo XIV: Taalimungu ni kwa ajili ya huduma ya kutangaza na kushuhudia Injili ya kristo Yesu, Papa leo XIV: Taalimungu ni kwa ajili ya huduma ya kutangaza na kushuhudia Injili ya kristo Yesu,   (@Vatican Media)

Papa Leo XIV Taalimungu Isaidie Mchakato wa Kutangaza, Kushuhudia na Kutamadunisha Injili

Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, leo hii imani haina budi kutangazwa, kushuhudiwa na kutamadunishwa kwani huu ni mchakato wa uinjilishaji wa tamaduni na utamadunisho wa Injili unaoiwezesha Habari Njema ya Kristo Yesu kuingia na kupenyeza mizizi yake katika tamaduni mbalimbali, ikiikubali, ikiisafisha, na kuipatia maana mpya bila kuharibu utambulisho wa watu. Lengo ni kufanya Injili ya Kristo Yesu uwe ni ujumbe unaozungumza lugha na uzoefu wa watu mahalia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kitivo cha Taalimungu Puglia (Facoltà Teologica Pugliese - FTP) ni taasisi ya elimu ya juu ya kikatoliki iliyoanzishwa tarehe 20 Juni 2005 na ina Makao yake makuu huko Bari, Kusini mwa Italia. Kitivo hiki ni kituo kikuu cha masomo ya taalimungu katika mkoa wa Puglia, na kinalenga kutoa mafunzo ya Kisayansi katika nyanja za: Falsafa, Taalimungu, Maadili, Maandiko Matakatifu, Historia ya Kanisa, na Sheria za Kanisa. Nayo Taasisi ya Taalimungu ya Calabria: “Istituto Teologico Calabro” inayohusishwa na Seminari ya Kipapa ya Calabria (Pontificio Seminario Teologico Calabro), ina historia ndefu na imepitia mabadiliko kadhaa. Itakumbukwa kwamba, asili yake ni Seminari kuu ya Calabria iliyoanzishwa na Papa Pio X tarehe 4 Januari 1912 kwa ajili ya kuwahudumia wanafunzi wa Falsafa na Taalimungu kutoka Calabria. Kunako tarehe 25 Machi 1914, Seminari hii ilipandishwa hadhi na kuwa ni Taasisi ya Taalimungu ya Calabria kupitia Katiba ya Kitume: “Susceptum inde” yaani: “Imechukuliwa kutoka huko.” Wanajumuiya wa Kitivo cha Taalimungu Puglia pamoja na Taasisi ya Taalimungu ya Calabria, Jumatatu tarehe 2 Machi 2026 walikutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Leo XIV mjini Vatican. Baba Mtakatifu katika hotuba yake amekazia umuhimu wa wanataalimungu kusafiri kwa pamoja, ili kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo Yesu inayokita mizizi yake katika dhana ya upembuzi yakinifu na kinabii; mawazo yenye uwezo wa kutatiza mantiki ya kujikatia tamaa na hali ya kutojali. Taalimungu ni kwa ajili ya huduma ya kutangaza na kushuhudia Injili ya kristo Yesu, changamoto na mwaliko kwa wanataalimungu kufanya kazi kwa umoja na ushirikiano. Huu ndio msingi wa malezi na majiundo yanayopaswa kutolewa katika Taasisi hizi, kwa kuendelea kuogelea katika maji mazito na kwamba, mwamini Mkatoliki hana sababu ya kuogopa machafuko ya bahari na wala kukimbilia kwenye bandari salama.

Taalimungu isaidie mchakato wa kutangaza, kushuhudia na kutakatifuza.
Taalimungu isaidie mchakato wa kutangaza, kushuhudia na kutakatifuza.   (ANSA)

Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, leo hii imani haina budi kutangazwa, kushuhudiwa na kutamadunishwa kwani huu ni mchakato wa uinjilishaji wa tamaduni na utamadunisho wa Injili unaoiwezesha Habari Njema ya Kristo Yesu kuingia na kupenyeza mizizi yake katika tamaduni mbalimbali, ikiikubali, ikiisafisha, na kuipatia maana mpya bila kuharibu utambulisho wa watu. Lengo ni kufanya Injili ya Kristo Yesu uwe ni ujumbe unaozungumza lugha na uzoefu wa watu mahalia. Hii ni changamoto kwa wanataalimungu kuzama zaidi katika Fumbo la Mungu, kwa kuangalia maelekeo mbalimbali ya imani ya kikristo sanjari na kutafuta lugha mpya zitakazosaidia kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa na hivyo kuzamisha mizizi yake katika historia ya mwanadamu. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema Taalimungu ni kwa ajili ya huduma ya kutangaza na kushuhudia Injili ya kristo Yesu, changamoto na mwaliko kwa wanataalimungu kufanya kazi kwa umoja na ushirikiano ili kuendeleza maisha na utume wa Kanisa Ulimwenguni. Malezi na majiundo ya kitaalimungu si kwa ajili ya wateule wachache, bali ni kwa ajili ya watu wote wa Mungu, kwa kuwawezesha waamini kupata nyenzo za kutangaza na kushuhudia Injili katika medani mbalimbali za maisha. Kumbe, kuna haja ya kujenga na kudumisha ushirika, umoja na udugu wa Kikristo kati ya Taasisi na Majimbo mbalimbali yaliyoko Kusini mwa Italia, ili kwa pamoja waweze kukabiliana na changamoto za shughuli za kichungaji sanjari na mahitaji ya mchakato wa uinjilishaji.

Imani inapaswa kutangazwa, kushuhudiwa na kutamadunishwa
Imani inapaswa kutangazwa, kushuhudiwa na kutamadunishwa   (ANSA)

Huu ni mwaliko kwa wanataalimungu kufanya kazi kwa umoja na ushirikiano unaosimikwa katika mchakato wa watu kukutana, kusikilizana, kujadiliana na hivyo kujenga ushirika kati ya Makanisa mahalia yanayoweka rasilimali, amana, utajiri na karama zao kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa la Kristo Yesu. Umoja huu, uwasaidie kuunganisha akili, maisha ya kiroho na shughuli za kichungaji, ili kuwa na mwelekeo wa pamoja unaomwilishwa katika Makanisa mahalia na hivyo kupyaisha mitindo na lugha ya imani katika muktadha wa Makanisa mahalia. Kwa njia hii, wataweza kuwaandaa Mapadre wa leo na kesho, pamoja na wafanyakazi wa shughuli za kichungaji, ili kudumisha ujenzi wa Kanisa la Kisinodi ambapo karama mbalimbali za Kikanisa zinatumika barabara. Kwa kufanya kazi kwa umoja na ushirika, kutawawezesha kubaini na hatimaye, kuzifanyia kazi changamoto mintarafu hali ya kijamii na kitamaduni. Hii ni changamoto pia ya kuendeleza ukarimu wa watu wa Mungu, wanaokabiliana na changamoto ya ukosefu wa fursa za ajira, wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji, mifumo mbalimbali ya utumwa mamboleo inayosigina utu, heshima na haki msingi za binadamu, sanjari na ukosefu wa haki msingi.

Injili ya Yesu ni chemi chemi ya matumaini, imani na mapendo
Injili ya Yesu ni chemi chemi ya matumaini, imani na mapendo   (@Vatican Media)

Changamoto zote hizi ziwasaidie waamini kujenga dhamiri nyofu na kwamba, majiundo ya kitaalimungu yasaidie kujenga uwezo wa upembuzi yakinifu yaani, mawazo yenye uwezo wa kutatiza mantiki ya kujikatia tamaa na hali ya kutojali. Huu ni wakati wa kutekeleza mradi huu mkubwa kwa ari na moyo mkuu, bila kutumbukia katika kishawishi cha kurejea tena nyuma.Ni ndoto ya Baba Mtakatifu Leo XIV ya kutaka kuona kwamba, Majandokasisi wanaojiandaa kwa ajili ya kupewa Daraja Takatifu ya Upadre, watawa na waamini walei, wanafundwa barabara, ili waweze kuzisaidia Jumuiya za Kikristo kuwa kweli ni vyombo, mashuhuda na alama ya Injili ya Kristo, chemchemi ya matumaini. Mwishoni Baba Mtakatifu Leo XIV amewashukuru kwa huduma yao inayosimikwa katika ukarimu, uvumilivu ari na moyo mkuu, kwa ajili ya ujenzi wa ushirika na umoja, ili kuishi kwa uaminifu, kwa kuendelea kujikita katika kipaji cha ubunifu, Mapokeo, upya wa maisha; Umoja na Utofauti, daima wakijenga na kudumisha utamaduni wa kumsikiliza Roho Mtakatifu anataka kuliambia nini Kanisa katika Ulimwengu mamboleo.

Papa Leo XIV Taalimungu
03 Machi 2026, 15:14