Tafuta

2026.03.21 Papa akutana na washiriki wa Mkutano Mkuu wa Harakati ya wa Focolari. 2026.03.21 Papa akutana na washiriki wa Mkutano Mkuu wa Harakati ya wa Focolari.  (@VATICAN MEDIA)

Papa Leo XIV:Tasaufi ya Wafocolari ni chachu ya mazungumzo ya kiekumeni na kidini

Papa Leo XIV alikutana na washiriki wa Mkutano Mkuu wa Harakati ya Kazi ya Maria ijulikanayo WaFocolari uliofanyika huko Rocca di Papa.Papa aliwahimiza waendelee na karama ya umoja,ya mwanzilishi Chiara Lubich kama ishara ya ulimwengu unaooneshwa na vurugu na ushenzi.Wito wa Papa kwao ni uwazi na ushiriki wa kila mtu ndani ya jumuiya."Muwe ishara ya umoja na kizuizi kwa wapanda chuki duniani.”

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Baba Mtakatifu Leo XIV, Jumamosi tarehe 21 Machi 2026, alikutana mjini Vatican na Washiriki wa Mkutano Mkuu wa Kazi ya Maria wajulikanao Harakati ya Wafocolari, ulioanza tangu tarehe 1 Machi hadi Machi 21, katika Kituo cha Kimataifa huko Rocca di Papa, ambapo Margaret Karram alichaguliwa tena kama rais kwa muhula wa pili na uteuzi wa rais mwenza mpya, Padre wa Italia-Argentina Roberto Eulogio Almada. Hii ni harakati iliyoanzishwa kwa msukumo wa  Mtumishi wa Mungu Chiara Lubich, ambapo ni moja ya harakati kubwa iliyoenea Ulimwenguni.

Papa na Wafocolari
Papa na Wafocolari   (@Vatican Media)

"Nyote mmevutwa na karama ya Mtumishi wa Mungu Chiara Lubich"

Kabla ya kuanza hotuba yake Papa Leo XIV aliwatania kwa sababu, walimsubiri akisema kwamba wamechukua labda chochote cha kula wakati wanamsubiri. Na kuwashukuru wa uvulivu huku akiomba msamaha kwa sababu ya kuchelewa. Kuhusiana na uchaguzi mkuu huo, Papa alisema "Bwana abariki huduma yao." Aliendelea na hotuba yake kwamba “Nyote mmevutwa kwenye karama ya Mtumishi wa Mungu Chiara Lubich, ambayo imeunda uhai wenu binafsi na mtindo wa maisha yenu ya jumuiya. Kila karama katika Kanisa inaonesha kipengele cha Injili ambacho Roho Mtakatifu anakileta mbele katika kipindi maalum cha kihistoria, kwa ajili ya manufaa ya Kanisa lenyewe na kwa ajili ya manufaa ya ulimwengu mzima.” Papa aliendelea kusisitiza kwamba kwao, ni ujumbe wa umoja: umoja miongoni mwa wanadamu ambao ni tunda na tafakari ya umoja wa Kristo na Baba: "Ili Wote wawe wamoja, kama wewe, Baba, ulivyo ndani yangu na mimi ndani yenu" (Yn 17:21).

Kuishi tasaufi ya umoja kwa kushuhudia maisha ya kidugu

Papa Leo XIV alisema kuwa, wao wanaishi tasaufi hiyo ya umoja kwanza kabisa miongoni mwao, na wanaushuhudia kila mahali kama uwezekano mpya wa maisha ya kidugu, ya upatanisho, na ya furaha miongoni mwa watu wa rika tofauti, tamaduni, lugha, na imani za kidini. Ni mbegu, rahisi lakini yenye nguvu, inayovutia maelfu ya wanawake na wanaume, inayohamasisha miito, inayozalisha msukumo wa uinjilishaji, lakini pia kazi za kijamii, kiutamaduni, kisanii, na kiuchumi, na ni chachu ya mazungumzo ya kiekumene na kidini. Chachu hiyo ya umoja inahitajika sana leo hii, kwa sababu sumu ya mgawanyiko na migogoro inaelekea kuchafua mioyo na mahusiano ya kijamii na lazima idhibitiwe kwa ushuhuda wa kiinjili, wa umoja, mazungumzo, msamaha, na amani." Papa Leo XIV alisisitiza kwamba kupitia wao pia, katika miongo iliyopita, Mungu ameandaa watu wakubwa wa amani, ambao, katika wakati huu wa historia, wameitwa kutenda kama kipingamizi na kizuizi kwa wapandaji wengi wa chuki ambao wanarudisha ubinadamu nyuma kwenye aina za ushenzi na vurugu.

Papa na Wafocolari
Papa na Wafocolari   (@Vatican Media)

Ni wakati wa kupambanua pamoja vipengele vipi vya maisha na utume

Mbali na ushuhuda huu muhimu wa umoja na amani, Papa Leo XIV alikazia kusema kuwa wao pia  wamepewa jukumu la kudumisha uhai wa Harakati yao katika awamu ya baada ya kuanzishwa, awamu ambayo haiishii na mpito wa kwanza wa kizazi baada ya kifo cha mwanzilishi, lakini inaendelea zaidi ya hapo. Wakati huu, wanaitwa kupambanua pamoja ni vipengele vipi vya maisha yao ya pamoja na utume wao ni muhimu na kwa hivyo,  lazima vidumishwe, na ni vifaa na mazoea gani ambayo, ingawa yamedumu kwa muda mrefu, si muhimu kwa karama, au yamewasilisha vipengele vyenye matatizo na kwa hivyo lazima yaachwe. Awamu hii pia Papa alisisitiza, inahitaji kujitolea kwa dhati kwa uwazi kwa upande wa wale walio katika nafasi za uwajibikaji, katika ngazi zote.

Uwazi ni sharti la uaminifu 

Kiukweli, kwa upande mmoja uwazi ni sharti la uaminifu, pia ni sharti, na karama ambayo ni zawadi ya Roho Mtakatifu ambayo wanachama wote wanawajibika nayo. Kwa hivyo wana haki na wajibu wa kuhisi hisia ya kuwa sehemu ya Kazi ambayo wamejiunga nayo kwa kujitolea kabisa. Papa Leo XIV alihimiza, "Kumbuka, basi, kwamba ushiriki wa wanachama daima ni thamani ya ziada: huchochea ukuaji, wa watu binafsi na wa Kazi, huleta rasilimali na uwezo  wa kila mtu, na huwezesha na kukuza mchango wa kila mtu." Jukumu la utambuzi wa pamoja, lililokabidhiwa kwao wote, pia linajumuisha jinsi karama ya umoja inavyopaswa kutafsiriwa katika mitindo ya maisha ya kijamii ambayo hufanya uzuri wa upyaishaji wa Injili ung'ae na, wakati huo huo, kuheshimu uhuru na dhamiri ya watu binafsi, wakithamini karama na upekee wa kila mmoja.

Papa Leo XIV na Wafocolari
Papa Leo XIV na Wafocolari   (@Vatican Media)

'Ili wote wawe wamoja:' ni umoja wa juu zaidi kati ya Baba na Mwana

Papa Leo XIV kwa njia hiyo wa Wafocolari alisema tunaweza kutafakari juu ya ukweli kwamba Yesu, katika sala yake ya kikuhani, baada ya kusema "wote wawe wamoja", aliongeza: "nao wawe ndani yetu" (Yn 17:21), hivyo akimaanisha umoja miongoni mwa wanafunzi kwenye umoja wa juu zaidi, ule kati ya Baba na Mwana. Hii ina maana kwamba umoja unaotafuta kuishi na kushuhudia unatimizwa kimsingi "katika Mungu," katika utimilifu wa mapenzi Yake matakatifu, na hivyo katika kujitolea kwa pamoja kwa ushirika na maisha ya kijamii, unaoungwa mkono na kuongozwa na wale waliokabidhiwa huduma hii. Umoja ni zawadi na, wakati huo huo, ni kazi na wito unaowapatia changamoto kila mtu. Wote wameitwa kutambua mapenzi ya Mungu na jinsi ukweli wa Injili unavyoweza kutimizwa katika hali mbalimbali za maisha ya kijumuiya au ya kitume. Na wote, katika safari hii ya utambuzi, lazima watumie udugu, ukweli, uwazi, na zaidi ya yote unyenyekevu, uhuru kutoka kwao wenyewe na mitazamo yao wenyewe. Umoja wa wote katika Mungu ni ishara ya kiinjili ambayo ni nguvu ya kinabii kwa ulimwengu.

Papa Leo XIV na Wafocolari
Papa Leo XIV na Wafocolari   (@Vatican Media)

Umoja si wa mawazo, maoni na mtindo wa maisha 

Umoja, basi, haupaswi kueleweka kama umoja wa mawazo, maoni, na mtindo wa maisha, ambao unaweza kusababisha kushuka kwa thamani ya imani ya mtu mwenyewe, na kuharibu uhuru wake binafsi na uwezo wa kusikiliza dhamiri yake. Chiara Lubich alithibitisha kwamba msingi wa kila kawaida ni upendo (tazama Dibaji ya Sheria). Kwa hivyo ni muhimu kwamba umoja uendelezwe na kudumishwa kila wakati na upendo wa pande zote, ambao unahitaji ukarimu, wema, na heshima; kwamba upendo ambao haujisifu, haujivuni, wala hautafuti maslahi yake mwenyewe, wala hufuatilia makosa yanayopokelewa, bali hufurahi tu na ukweli (rej. 1 Kor 13:4-6).

Tumshukuru Mungu kwa familia kubwa ya kiroho

Kutokana na hilo, Baba Mtakatifu amewaomba Wafocolari: “hebu tumshukuru Bwana kwa ajili ya familia kubwa ya kiroho iliyozaliwa kutokana na karama ya Chiara Lubich. Kwa ajili ya vijana waliopo katika vikundi vyenu, wanaoona kwa macho safi uzuri wa wito wa kuwa vyombo vya umoja na amani duniani. Kwa ajili ya familia, ambazo zimefanywa upya na kuimarishwa na uwepo wa Yesu katikati ya maisha ya familia zao. Kwa ajili ya maaskofu, makuhani, na watu waliowekwa wakfu ambao wameona kipaji cha huduma yao na maisha yao ya wakfu wa kidini yakifanywa upya kupitia mawasiliano na Harakati yenu na hali yenu ya kiroho. Kwa ajili ya WaFocolari wa kike na kiume wengi ambao, mara nyingi kwa kujitolea kwa kishujaa, wanaendelea kuishi maisha ya sala, kazi, mazungumzo, na uinjilishaji  ulimwenguni kote wakifuata mfano wa maisha ya kitume ya vizazi vya kwanza vya Kikristo.”

Papa akiwaaga Wafocolari
Papa akiwaaga Wafocolari   (@Vatican Media)

Kushukuru kwa matunda mengi yasiyohesabika ya utakatifu

Na tunashukuru kwa matunda mengi yasiyohesabika ya utakatifu, yanayojulikana na yasiyojulikana, ambayo kurudi kwa Injili, iliyokuzwa na ninyi, na kuletwa katika  Kanisa kwa miaka hii yote.” Kwa njia hiyo Papa aliwatia moyo waendelea na safari yao na kwa moyo wote waliwabariki huku akiowaombea wote kwa maombezi ya Bikira Maria, ili awalinde na awasindikize kila wakati kwa msaada wake wa kimama. Hata hivyo Papa alieleza alivyosikia kwamba wao wanapenda kuimba na hivyo aliwaomba wasali pamoja Sala ambayo Bwana Yesu alitufundisha ya Baba Yetu, na  wote waliimba kwa kilatino…Pater noster”… Baraka na kuwashukuru tena na kuwatakia mema.

PAPA FOCOLARI

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku bonyeza hapa: Just click here.

21 Machi 2026, 14:20