Tafuta

2026.03.26 Kanisa Kuu la Kianglikani Canterbury. 2026.03.26 Kanisa Kuu la Kianglikani Canterbury. 

Papa Leo XIV:'Tofauti haziwezi kutuzuia kutambuana kama kaka na dada katika Kristo'

Papa Leo XIV alituma ujumbe wa matashi mema kwa Sarah Mullally,Askofu Mkuu Mpya wa Kianglikani wa Canterbury nchini Uingereza,wakati wa kuanza na kusimikwa rasmi tarehe 25 Machi 2026.Mjumbe wa Papa alikuwa Kardinali Koch,aliyewasilisha barua mwishoni mwa sala ya pamoja ya kusherehekea kumbukumbu ya miaka 60 ya mkutano kati ya Mtakatifu Papa Paulo VI na Askofu Mkuu Ramsey, uliofanyika mjini Roma mnamo 1966.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Baba Mtakatifu Leo XIV alituma Ujumbe katika fursa ya kusimikwa rasmi kwa Askofu Mkuu Mpya Kianglikani  wa Canterbury nchini Uingereza. Barua ya matashi mema ilikabidhiwa katika Kanisa Kuu la Canterbury, mara baada ya hitimisho la Sala ya pamoja iliyoongozwa na Askofu Mkuu mpya mwenyewe wa Canterbury na mkuu wa Umoja wa Kianglikani, Sarah Mullally, na Mwakilishi wa Baba Mtakatifu Kardinali Kurt Koch, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Umoja wa Wakristo. Liturujia ilifanyika katika kumbukumbu ya miaka 60 tangu kufanyika mkutano wa kihistoria kati ya Mtakatifu Papa Paulo VI na Askofu Mkuu wa Kianglikani wa Canterbury, Michael Ramsey, uliofanyika mjini Roma mnamo tarehe 24 Machi 1966.

Tarehe 25 Machi 2026 alisimikwa rasmi Askofu Mkuu wa Kianglikani nchini Uingereza
Tarehe 25 Machi 2026 alisimikwa rasmi Askofu Mkuu wa Kianglikani nchini Uingereza   (PA Wire/PA Images)

Ujumbe wa Baba Mtakatifu Leo XIV unaanza: “Neema, huruma, na amani iwe pamoja nasi, kutoka kwa Mungu Baba, na kutoka kwa Yesu Kristo, Mwana wa Baba, katika ukweli na upendo” (2 Yh 1:3). Kwa uhakikisho huu wa uwepo wa kudumu wa Mungu, ninatuma salamu, wakati wa kusimikwa  kwako kama Askofu Mkuu wa Canterbury.” Papa aliendelea kuwa “Ninajua kwamba huduma ambayo umechaguliwa ni nzito, yenye majukumu, si tu katika Jimbo la Canterbury, bali pia katika Kanisa la Uingereza na Usharika wa Kianglikani kwa ujumla. Zaidi ya hayo, unaanza majukumu haya katika wakati historia ya familia ya Kiangilikani.” Kwa njia hiyo Papa aliomba Bwana amwimarishe kwa kipaji cha hekima, na aliomba kwamba ataongozwa na Roho Mtakatifu katika kuhudumia jumuiya yake na atapata msukumo kutoka kwa  mfano wa Maria, Mama wa Mungu.

Sura mpya ya uwazi na eshima imezaa matunda

Papa Leo XIV akitafakari kuhusu tukio la kihistoria alisema: “Miaka sitini iliyopita, wakati wa mkutano wao wa kihistoria,  Roma, watangulizi wetu, Mtakatifu Paulo VI na Askofu Mkuu Michael Ramsey, waliwaweka Wakatoliki na Waanglikani katika "awamu mpya katika maendeleo ya mahusiano ya kidugu, kulingana na upendo wa Kikristo" (Tamko la Pamoja, Machi 24, 1966). Papa aliongeza “Sura hiyo mpya ya uwazi wa heshima imezaa matunda mengi katika miongo sita iliyopita na inaendelea kufanya hivyo leo hii." Katika tukio hilo hilo, Papa Paulo VI na Askofu Mkuu Ramsey, pia walikubaliana kuanzisha mazungumzo ya Kitaalimungu. Hakika, Tume ya Kimataifa ya Kianglikani na Kikatoliki(ARCIC) imetoa mchango mkubwa katika ukuaji wa maelewano ya pande zote tangu kuanzishwa kwake. Matunda ya kazi hii muhimu yametuwezesha kushuhudia pamoja kwa ufanisi zaidi (rej. Tume ya Kimataifa ya Kianglikani-Katoliki kwa ajili ya Umoja na Utume, Kukua Pamoja katika Umoja na Utu, 93). "Hili ni muhimu hasa kutokana na changamoto nyingi zinazoikabili familia yetu ya kibinadamu leo hii.”

Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiangliani nchini Uingereza
Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiangliani nchini Uingereza   (TOBY MELVILLE)

Umoja unaotafutwa na Wakristo si mwisho wenyewe

Kwa hivyo, Papa Leo XIV aliwashukuru kwamba mazungumzo haya muhimu yanaendelea. Wakati huo huo, “tunajua pia kwamba safari ya kiekumeni haikukosa vikwazo kila wakati. Licha ya maendeleo mengi, watangulizi wetu wa karibu, Papa Francisko na Askofu Mkuu Justin Welby, walikiri waziwazi kwamba "hali mpya zimeleta kutokubaliana kati yetu." Hata hivyo, tumeendelea kutembea pamoja, kwa sababu tofauti "haziwezi kutuzuia kutambuana kama kaka na dada katika Kristo kwa sababu ya Ubatizo wetu wa pamoja" (Tamko la Pamoja, Oktoba 5, 2016).”

"Kwa upande wangu, Baba Mtakatifu Leo XIV alibainisha - ninaamini kabisa kwamba lazima tuendelee kuzungumza katika ukweli na upendo, kwani ni katika ukweli na upendo pekee tunapojua pamoja neema, huruma, na amani ya Mungu (taz. 2 Yh 1:3) na hivyo kuweza kutoa zawadi hizi za thamani kwa ulimwengu.”  Zaidi ya hayo, Papa Leo XIV alisisitiza “umoja ambao Wakristo wanatafuta kamwe si mwisho wenyewe, bali unalenga kumtangaza Kristo, ili, kulingana na sala ya Bwana Yesu mwenyewe, "ulimwengu upate kuamini"(Yn 17:21.”

"Itakuwa kashifa Wakristo kuwa na migawanyiko"

“Akiwahutubia Mapadre wa Usharika wa Kianglikani mwaka 2024, Baba Mtakatifu Leo XIV, alisisitiza kwamba, “Papa Francisko alisema, "itakuwa kashfa ikiwa, kwa sababu ya mgawanyiko, hatutatimiza wito wetu wa pamoja wa kumtangaza Kristo" (Hotuba kwa Washiriki katika Mkutano wa Mapadre wa Ushiraka wa Kinglikani, 2 Mei 2024). Papa Leo XIV alibainisha: “Dada mpendwa, kwa hiari yangu nayafanya maneno haya kuwa yangu, kwani ni kupitia ushuhuda wa jumuiya ya Kikristo iliyopatanishwa, ya kidugu, na yenye umoja ndipo kutangazwa kwa Injili kutasikika wazi zaidi (taz Ujumbe wa Dominika ya 100 ya Utume Duniani, nambari 2). Kwa kuhitimisha Baba Mtakatifu Leo XIV alimtakia matashi mema anapoanza utume wake mpya katika Kanisa hilo la Uingereza kwamba: "Kwa hisia hizi za kidugu, ninakuombea baraka za Mwenyezi Mungu unapochukua majukumu  yako ya juu. Roho Mtakatifu akushukie na kukufanya uzae matunda katika huduma kwa Bwana.”

Katika sherehe hiyo Ujumbe wa Wakatoliki Pamoja na Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Umoja wa Kikirsito, uliundwa pia na Katibu wake, Askofu Mkuu Flavio Pace, Afisa Martin Brown, Makardinali: Vincent Nichols na Timothy Radcliffe, Askofu Mkuu wa Birmingham Bernard Longley, Rais Mwenza wa Tume ya Mazungumzo ya Kiangliakani-Katoliki (ARCIC), Askofu Mkuu wa Westminster Richard Moth, Askofu Mkuu wa Southwark John Wilson, Askofu Mkuu wa Mtakatifu Andrew na Edinburgh, Leo William Cushley, Askofu wa Kanisa Katoliki la Kigiriki la Ukraine nchini Uingereza, Kenneth Anthony Adam Nowakowski, na Ante Vidović, Kaimu Balozi wa Ubalozi wa Vatican jijini London.

MATASHI MEMA KWA KIANGLIKANI

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata taarifa mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku:Just click here.

26 Machi 2026, 17:02