Papa Leo XIV: Kristo Yesu Ni Utimilifu wa Sheria Na Unabii: Ushuhuda wa Baba wa Milele
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Tukio la Kung’ara kwa Bwana, kielelezo cha utimilifu wa Sheria na Unabii unaofumbatwa katika Kashfa ya Fumbo la Msalaba, yaani mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu! Kung’ara kwa Bwana ni tukio ambalo Kristo Yesu alilitumia ili kuweza kuwaimarisha mitume wake, ili waweze kukabiliana uso kwa uso na Kashfa ya Msalaba, kielelezo makini cha: hekima ya Mungu, ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu, ili hatimaye, waweze kuwa ni: Vyombo, watangazaji na mashuhuda wa Habari Njema ya Wokovu inayosimikwa katika Fumbo la Msalaba! Mama Kanisa katika maadhimisho haya anaungama kwa dhati kabisa: Ubinadamu na Umungu wa Kristo; Kuzaliwa kwa Mwana wa Mungu na Mkombozi wa dunia sanjari na kuzaliwa kwa Kanisa Sakramenti ya wokovu kwa binadamu! Tukio hili linagusa kwa namna ya pekee, umuhimu wa Kanisa kusimama kidete kulinda na kutunza kazi ya uumbaji kama anavyokaza kusema Mtakatifu Damascene. Kristo Yesu anaufunua Umungu wake kwa njia ya mwili uliotukuka, ndiyo maana Kanisa linamwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na utukufu kwani ukuu una Yeye milele hata na milele! Mababa wa Kanisa wanasema, haikuwa rahisi kwa Mtakatifu Petro kukubali Fumbo la Pasaka, yaani, mateso, kifo na ufufuko kwa Kristo Yesu kutoka kwa wafu; hii ilikuwa ni kashfa ya mwaka. Kwa njia hii, Kristo Yesu anawaandaa Mitume wake kuweza kukabiliana na Kashfa ya Fumbo la Msalaba kwa kugeuka sura, kutokea kwa Musa na Eliya yaani: Utimilifu wa Unabii na Sheria na ushuhuda wa sauti kutoka mbinguni ikisema, “Huyu ni Mwanangu, mteule wangu msikieni Yeye. Rej. Lk 9:31.
Huu ni mwaliko kwa waamini kutafakari utukufu wa Kristo Yesu, Nafsi ya Pili ya Fumbo la Utatu Mtakatifu, ili wanapomwona ametundika Msalabani watambue kwamba, mateso yake yalikuwa ni ya hiari, wawe tayari kutangaza na kushuhudia kwamba, Kristo Yesu ni Mng’ao wa Baba wa milele. Kwa Ubatizo, mwamini anazaliwa mara ya pili na hivyo kushiriki katika Ufufuko wa kristo Yesu kwa njia ya Roho Mtakatifu anayefanya kazi katika Sakramenti za Mwili wa Kristo. Kung’ara sura ni limbuko la ujio mtukufu wa Kristo Yesu, atakaye ubadili mwili wetu wa unyonge, upate kufanana na mwili wake wa utukufu. Waamini wataufikia pia utukufu wa Kristo Yesu kwa njia ya Fumbo la Msalaba. Rej. KKK 554-556. Huu ni ufunuo wa mwanga utakaozima giza la Kashfa ya Fumbo la Msalaba, tayari kutoa nafasi kwa binadamu kumwabudu, kumsifu, kumtukuza na kumwomba Kristo Yesu, Mwana wa Mungu aliye hai. Waamini wanaalikwa kwa namna ya pekee kabisa, kuisikiliza sauti yake na kutekeleza mapenzi yake katika uhalisia wa maisha yao, kwani Neno la Mungu ni dira na mwongozo wa maisha. Neno la Mungu ni Ufunuo wa utambulisho wa Mwana wa Mungu kama siku ile ya Ijumaa kuu atakavyosema yule Akida kwamba, “kwa hakika huyu alikuwa ni Mwana wa Mungu.” Baba Mtakatifu Leo XIV katika tafakari yake Dominika ya Pili ya Kipindi cha Kwaresima, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Dominika tarehe Mosi Machi 2026 amesema kile ambacho Mwenyezi Mungu ameamuru na kunuia kinapata utimilifu wake kwa Neno aliyefanyika Mwili, Kristo Yesu, aliyeshuhudiwa na Baba yake wa mbinguni akisema, “Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye; msikieni yeye.” Mt 17:5.
Huu ni ufunuo wa Mungu kwa njia ya Kristo Yesu anayeng’aa kama jua na mavazi yake meupe kama nuru; Ufunuo unaowashangaza Mitume wa Yesu na kuwawezesha kuutafakari utukufu wa Mungu, kama njia ya kuwaimarisha. Kung’ara kwa Uso, kunatangulia Fumbo la Pasaka, yaani mateso, kifo na ufufuko kwa wafu. Huu ndio mwanga unaowang’aria wote wanaoteseka na kudhulumiwa sehemu mbalimbali za dunia; hii ni miili inayong’ara utukufu wa Mungu. Kristo Yesu Mkombozi wa ulimwengu anang’ara katika madonda ya historia, huku aking’arisha akili na nyoyo za waamini wake, mshangao wa wokovu.Baba Mtakatifu Leo XIV anakaza kusema, ukweli wa Uso wa Mungu unang’ara ndani mwa kila mwamini. Ufunuo wa Baba wa mbinguni kwa wale wasioamini unajidhihirisha kwa zawadi ya Mwanaye mpendwa; wale wapweke na wanaoteseka anajifunua kwa njia ya Roho Mtakatifu, anayewasha moto wake wa mapendo, ili kujenga ushirika na maisha ya uzima wa milele na neema; mbele ya imani haba kama “kiatu cha raba” Kristo Yesu anatangaza Ufufuko, ambao umejidhihirisha kwa Mitume kwa Kristo Yesu kugeuka sura, jambo ambalo litawachukua muda wafuasi wake hadi kuweza kulifahamu. Rej Mt 17:9. Huu ni muda wa ukimya ili kusikiliza Neno la Mungu, Muda wa Toba na Wongofu wa ndani, ili kuweza kufurahia uwepo wa Kristo Yesu kati yao. Haya ndiyo mang’amuzi ya Kipindi cha Kwaresima, mwaliko wa kumwomba Bikira Maria, Mwalimu wa Sala na Nyota ya Asubuhi kuilinda miguu yao katika imani.