Tafuta

Baba Mtakatifu Leo XIV amerudia tena kutoa wito kwa Jumuiya ya Kimataifa kujikita katika kutafuta na kudumisha Injili ya amani duniani. Baba Mtakatifu Leo XIV amerudia tena kutoa wito kwa Jumuiya ya Kimataifa kujikita katika kutafuta na kudumisha Injili ya amani duniani.  (AFP or licensors)

Papa Leo XIV Jengeni Utamaduni wa Amani, Acheni Chuki, Uhasama na Kulipizana Kisasi

Baba Mtakatifu Leo XIV amerudia tena kutoa wito kwa Jumuiya ya Kimataifa kujikita katika kutafuta na kudumisha Injili ya amani, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza katika majadiliano yanayofumbatwa katika ukweli na uwazi, ili kuweza kupata suluhu ya changamoto zinazoikabili Jumuiya ya Kimataifa bila kukimbilia “Mtutu wa bunduki” kama suluhu ya matatizo. Majadiliano katika ukweli na uwazi pamoja na diplomasia ya kimataifa vichukue mkondo wake!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Leo XIV anasema kwamba, Injili ya amani inahitaji uvumilivu, kuanzia chini kwenda juu, kuanzia mahali pa chini sana, kuendelea katika jumuiya na hatimaye katika taasisi mahalia, kwa kujenga tabia ya kusikiliza; ili kutatua changamoto za kutokubaliana kwa kukubali uwepo wake, kujitahidi kuzielewa na hatimaye, kuzishughulikia kwa kujikita kwenye majadiliano katika ukweli na uwazi na kwamba huo ni mwanzo wa kuchipua kwa utamaduni na Injili ya amani inayowawezesha wadau mbalimbali kujielekeza katika huduma, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Na kwa hakika hii inakuwa ni chemchemi ya matumaini. Katika ulimwengu unaosimikwa katika: vita na machafuko; vitendo vya kigaidi, biashara haramu ya binadamu pamoja na mifumo ya utumwa mamboleo, uvunjifu wa haki, watoto na vijana wa kizazi kipya wanapaswa kupata tajiriba na mang’amuzi ya Injili ya maisha, majadiliano pamoja na tabia ya watu kuheshimiana na kuthaminiana kama binadamu.

Diplomasia ya Kimataifa ichukue dhamana na wajibu wa kimaadili.
Diplomasia ya Kimataifa ichukue dhamana na wajibu wa kimaadili.   (AFP or licensors)

Kimsingi ni watu wanaopaswa kushuhudia utamaduni wa amani katika ngazi mbalimbali za maisha na kwamba, wale ambao wamekoseshwa haki na amani, wasitumbukie katika ombwe la kutafuta kulipiza kisasi na kwa njia hii, watakuwa kweli ni mashuhuda wa Injili ya amani, kama mbinu mkakati na mtindo wa maisha unaowapambanua kwa maamuzi, mahusiano, mafungamano pamoja na matendo yao! Ikumbukwe kwamba, amani ni tunda la haki Rej Yak 3:18; kazi ya haki ni kuleta amani Rej. Isa 32:17 na kwamba, pasipo haki hakuna amani. Ni katika muktadha wa vita inayoendelea kati ya Marekani, Israeli na Iran, Baba Mtakatifu akiwa kwenye Ikulu Ndogo ya Castel Gandolfo, nje kidogo ya mji wa Roma, wakati wa mapumziko ya kikazi, Jumanne 3 Machi 2026 amerudia tena kutoa mwaliko kwa Jumuiya ya Kimataifa kujikita katika kutafuta na kudumisha Injili ya amani, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza katika majadiliano yanayofumbatwa katika ukweli na uwazi, ili kuweza kupata suluhu ya changamoto zinazoikabili Jumuiya ya Kimataifa bila kukimbilia “Mtutu wa bunduki” kama suluhu ya matatizo.

Vita ina madhara makubwa kwa watu: mali na maisha yao
Vita ina madhara makubwa kwa watu: mali na maisha yao   (AFP or licensors)

Huu ni mwaliko kwa viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa kuchukua na kutekeleza wajibu wa kimaadili, kwani amani ya kweli haijengwi kwa “mtutu wa bunduki” kwani vita ina madhara makubwa katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Diplomasia ichukue mkondo wake. Jumuiya ya Kimataifa inapaswa kuwa mstari wa mbele kukuza na kudumisha mafao ya wengi, amani na utulivu unaosimikwa katika haki. Baba Mtakatifu Leo XIV anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuendelea kusali kwa ajili ya kuombea amani duniani. Wachunguzi wa mambo ya kiuchumi wanasema, kufungwa kwa Mlango wa Bahari wa Hormuz kuna madhara makubwa katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, kwani huu ni Mlango wa kimkakati kiuchumi. Kufungwa kwake kutapelekea kupanda kwa bei ya nishati ya mafuta na gesi; kuanguka kwa uchumi wa Kimataifa; Mfumuko wa bei ya chakula, bidhaa na huduma utaongezeka maradufu. Masoko ya hisa yatapomoka, Deni la Taifa litaongezeka na kwamba, Mataifa ya Asia yataathirika sana sanjari na vitega uchumi na uzalishaji wa gesi asilia na mafuta utaathirika.

Injili ya Amani Duniani
04 Machi 2026, 16:08