Papa Leo XIV: Gazeti la "Corrierre Della Sera: Kumbukizi ya Miaka 150 ya Uhai Wake
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko anasema kwamba, mintarafu Maandiko Matakatifu, Jubilei ni muda muafaka wa kufanya toba na wongofu wa ndani, tayari kukimbilia huruma na kuambata msamaha unaobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa ajili ya waja wake. Ni kipindi cha kushukuru na kuomba tena neema na baraka za kuweza kujizatiti zaidi katika maisha na wito, tayari kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya Mungu na jirani, kama mashuhuda na vyombo vya huruma na upendo wa Mungu. Ni wakati murua sana wa mapumziko; muda wa kujichotea nguvu pamoja na kufurahia matunda ya kazi ya uumbaji. Ni wakati wa kuyatafakari yaliyopita kwa moyo wa shukrani, kuyaishi ya sasa kwa moyo wa hamasa na kuyakumbatia ya mbeleni kwa moyo wa matumaini.
Ni katika muktadha wa Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 150 tangu kuanzishwa kwa Gazeti la “Corriere della Sera”, huko Milano na Eugenio Torelli kunako tarehe 5 Machi 1876. Baba Mtakatifu Leo XIV katika salam zake za pongezi kwa Mhariri mkuu wa Gazeti hili anasema, katika kipindi cha Miaka 150 kila kukicha wamesimulia historia ya Italia, anawataka kuangalia changamoto za maendeleo makubwa ya teknolojia na hasa matumizi ya akili unde na hatimaye, anawatakia heri na baraka katika safari yao ya huduma kwa watu wa Mungu nchini Italia.
Baba Mtakatifu Leo XIV katika Makala maalum iliyochapishwa kwenye Gazeti la “Corriere della Sera”, anasema kwamba, historia ya Gazeti hili inakwenda sanjari na historia ya Italia kwa kuonesha umuhimu wa magazeti kama chombo cha kusambaza habari, mawazo na utamaduni na kwamba, Gazeti hili limechangia sana katika utekelezaji wa majukumu haya na ujenzi wa jamii. Katika miaka 150 Gazeti limewashirikisha wasomaji wake kuhusu: Matukio ya Vita Kuu ya Dunia, Kupanda na Kuanguka kwa utawala wa Kifashisti kuanzia kwaka 1922-1945; kutoka katika Utawala wa Kifalme hadi utawala wa Kijamhuri; Ugaidi wa ndani hadi Ugaidi wa Kimataifa, Kuanguka kwa Ukuta wa Berlin pamoja na hali tete inayoendelea kujitokeza kwa sasa.
Katika ulimwengu mamboleo wenye maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia ya matumizi ya akili unde wana wajibu mkubwa na kwamba, kati ya historia na teknolojia, mwelekeo wa mwanadamu lazima ulindwe na kukuzwa na hasa na magazeti makubwa kama hili. Wahakikishe kwamba, wanazingatia ukweli asili wa vyanzo vyao vya habari, dhamana na wajibu wa wanahabari; utu na heshima ya wasomaji wao, ambao unaweza kusimuliwa na tajiriba ya siku nyingi kama ilivyo kwa Gazeti la “Corriere della Sera.”
